Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niungane na wachangiaji waliotangulia katika kutoa mchango wangu kwenye kujadili Kamati zote zilizowasilisha hoja. Pamoja na kwamba, hoja hizi zimekuwa zikijirudia kila wakati, lakini bado tunaona kuna jitihada za Serikali kwenye baadhi ya maeneo tunaona yanaboreshwa na lazima tu-acknowledge kwa baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo sekta ambazo zinafanya vizuri na ni muhimu sasa nikazitaja. Mathalani, sekta ya nishati inafanya vizuri, Sekta ya Maji inafanya vizuri, vilevile Sekta ya Afya inafanya vizuri pamoja na Sekta ya Ujenzi, changamoto tu ni rasilimali fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la kukosekana kwa mipango madhubuti ya Halmashauri zetu katika kukusanya mapato ya ndani. Tumeambiwa hapa na Kamati kwamba, kwa Mwaka wa Fedha 2020/2023, Serikali kuu imepeleka fedha takribani shilingi trilioni 7.6 kwenye halmashauri zetu nchini, shilingi trilioni 2.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi trilioni 5.2 ni fedha za matumizi ya mishahara na matumizi mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kueleza hapa kwamba, bado tuna changamoto kubwa kama Taifa kwenye halmashauri zetu. Bado halmashauri zetu zimekuwa zikitegemea kwa 90% Serikali Kuu na hii inakwenda kinyume na Sera yenyewe ya Ugatuzi wa Mamlaka au Madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki, nitazitaja, kama Kenya, Uganda, Rwanda na nyinginezo, Serikali za Mitaa zinajitegemea zenyewe kwa mapato ya ndani. Changamoto ipo wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kupeleka fedha kwenye halmashauri zetu siyo jambo baya, ni jambo jema, lakini yapo maeneo Serikali Kuu haina sababu ya kupeleka fedha. Ukipeleka fedha maana yake unakwenda kuzifanya halmashauri hizi zikose kuwa na fikra mbadala au kuwa na ubunifu wa vyanzo vingine vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa Jiji la Ilala, Jiji la Ilala linakusanya bilioni 130, lakini bado linapelekewa fedha za matumizi mengineyo na mishahara ya watumishi na bado linapelekewa fedha za maendeleo, sikatai kwenye sekta ya maendeleo, zinaweza kupelekewa, lakini siyo kwa maana zifanane na Halmashauri zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali Kuu imepata mzigo mkubwa wa utegemezi kutoka Serikali za Mitaa? Ni kwa sababu tuna changamoto kubwa ya Halmashauri zetu kuwa wabunifu katika kukusanya mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kushauri, kwa changamoto hii ili tuweze kuzijengea uwezo Halmashauri zetu ziwe na uwezo wa kukusanya mapato ya ndani na wakati mwingine ziweze kujitegemea kwa sehemu fulani na siyo 90% kwa Serikali Kuu, nashauri jambo la kwanza ni kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani ili Wakurugenzi na Menejimenti wanavyopeleka mapendekezo yao ya vyanzo vingine kuhusu mikakati mbalimbali ya kukusanya mapato ya ndani waweze kuwaelewa na wawaunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo kimsingi lingefanywa ni lazima sasa Serikali iwape Wakurugenzi wote wa Halmashauri vigezo mahsusi vya utendaji kazi KPI – Key Performance Indicators na wapimwe kila baada ya kipindi cha miezi sita. Hii itasaidia Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa wabunifu. Watakuwa wabunifu kwa sababu wanaamini baada ya miezi sita atapimwa kwa KPI aliyopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ambayo tunayo na ninadhani hili ni jambo ambayo kimsingi linatekelezeka. Wakipewa na wapimwe kwa maana ya namna gani wanaweza wakawa wabunifu wa vyanzo vya mapato, kukusanya mapato, lakini pia na matumizi yao yawe yenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze hapa bayana, kwa nini tumekuwa na changamoto mara kwa mara kwenye taasisi zetu za umma? Ninaamini kwamba ukiona taasisi yoyote haifanyi vizuri, changamoto siyo watumishi wa kada ya chini, mara nyingi tunakosea sana, yaani tunamwacha Mkurugenzi wa taasisi hapa juu halafu tuna-deal na wale anaowasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utamaduni wa utawala wowote ule kuna kitu kinaitwa utamaduni wa utawala. Maana yake, utamaduni wa utawala unajengwa na kiongozi wa taasisi. Kwa hiyo, ukiona taasisi yoyote inatuhumiwa kwa rushwa, maana yake anayekula rushwa ni Mkuu wa Taasisi. Wale wasaidizi wanafuata boss alivyo. Kwa hiyo, sioni sababu ya ku-deal na watu wa chini halafu tunawaacha Wakurugenzi wa taasisi pale wanatamalaki. Kwa hiyo, ushauri wangu ni muhimu sasa badala ya kumwajibisha mtumishi wa kawaida, wawajibishwe wakuu wa taasisi, hii itasaidia kwa sababu mkuu wa taasisi ndiyo anayejenga utamaduni wa taasisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijielekeze kwenye eneo moja ambalo linahusu Halmashauri zetu kudaiwa. Tumeambiwa na Kamati hapa, baadhi ya Halmashauri zinadaiwa kiasi cha fedha takribani bilioni 21.85. Kuna fedha ambazo Wizara ya Ardhi ilipeleka kwenye Halmashauri kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha, madeni wanayodaiwa mpaka sasa ambayo fedha hazijarejeshwa ni bilioni 21.85.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nishauri hapa kwa Halmashauri hizi ambazo zina changamoto hii. Wakati huo huo Halmashauri hizo zinadai fedha 42,536,221,960, fedha ambazo hazijalipwa kutokana na mauzo ya viwanja. Sasa, mimi sioni kwa nini wanashindwa kulipwa hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwa hawa wakurugenzi wenye hii kadhia, kimsingi ushauri wangu hapa, wana viwanja vipo. Kwa sababu wangeweza kushusha bei ya hivyo viwanja, vingenunulika. Mfano, kiwanja kinachouzwa 1,000,000 ukimwambia leo mtu ambaye ameshindwa kulipa 1,000,000 akulipe 500,000 na ukampa notice ya mwezi mmoja analipa. Tena atakimbia atakopa fedha, atalipa haraka sana kwa sababu anajua hiyo umempa fursa ya yeye kupata kiwanja chake. Ni hesabu ndogo sana. Kwa hiyo, nawashauri wakurugenzi wote wenye viwanja ambao kimsingi wana kadhia ya kutorejesha fedha hizi bilioni 21, washushe bei, hivyo viwanja vitakimbiliwa na hiyo fedha itapatikana na wataweza kulipa mkopo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la makusanyo kwa kutumia POS (Point of Sales). Labda nieleze changamoto za makusanyo au kukusanya tozo kwa kutumia POS. Kwanza, POS inaruhusu mjadala kati ya mtoza ushuru na anayetoa ushuru. Wana-compromise, kwa sababu kama mtu alitakiwa alipe laki sita tozo anamwambia nipe 200,000 nakusamehe. Sasa nadhani kwa sasa umepitwa na wakati. Tunaweza kuutumia kwa maeneo ambayo hayana fursa au hayana mtandao kwa maana ya internet hasa kule vijijini, lakini hadi Dodoma, Arusha Mjini na Dar es Salaam hadi Ilala Jiji bado POS zinatumika kwa ajili ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mfumo mzuri ni wa kutumia control number. Hakuna nafasi ya watu ku-compromise na hakuna mazingira ya kujadiliana alipe kiasi gani, lakini POS bado zinatoa nafasi ya mtoza ushuru na mtoa ushuru ili wakubaliane apate kidogo, Serikali ikose kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), nadhani wapo hapa watusaidie. POS siyo kwamba ziache kutumika, ila zitumike kwa maeneo ambayo hawana access ya internet na TRA wanafanya hivyo nchi nzima. Kwa sababu control number inamlazimisha mtu alipe kiasi anachopaswa kulipa na huu ndiyo mfumo utakaotusaidia kudhibiti mianya ya rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye eneo lingine la riba zinazotokana na ucheleweshwaji wa madai au malipo kwa wakandarasi. Jambo hili linaweza kuepukika. Waswahili wanasema, heri kinga kuliko tiba. Tunafahamu zipo changamoto kadhaa kwenye kuwalipa wakandarasi lakini zipo ambazo zinaweza kuepukika mathalani, miradi ya ujenzi wa barabara. Karibu miradi mingi ina changamoto hii ya kulipwa malipo kwa wakandarasi. Mtakumbuka ripoti ya CAG iliyopita Wizara ya Ujenzi, TANROADS walikuwa wanadaiwa bilioni 700. Hizo ni riba tu. Sasa tunaweza kuepuka hii hasara ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaepukaje? Ni lazima sasa tuwe na vipaumbele, kupanga ni kuchagua, kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha, tuchague. Kwa mfano, barabara ina mahitaji makubwa kwa Taifa letu. Ukitoka hapo sekta ya maji ina mahitaji makubwa kwenye Taifa letu. Kwa hiyo, kuna baadhi ya sekta kimsingi tunaweza kuziacha kidogo, lakini sekta hizi muhumu ambazo kimsingi ndiyo uchumi wa Taifa letu zikawekewa mkazo mathalani leo pale Jimboni kwangu kuna barabara ambayo kimsingi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Mheshimiwa Rais kuridhia. Hii barabara sasa inakwenda kuwa na hadhi ya trunk road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ninayoizungumza ni inayounganisha Mikoa ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini, lakini mpaka leo ninavyozungumza, barabara hii imepata kandarasi na hapo namshukuru sana Mheshimiwa Rais. Pamoja na mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais na mapenzi mema ya Serikali katika kuunganisha Mikoa hii ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini, ujenzi wa barabara hii bado unasuasua. Hivyo basi, rai yangu ni kwamba ili tuepukane na kadhia ya riba zinazosababishwa na kucheleweshwa kwa malipo ya wakandarasi, ni muhimu mradi huu nao ukalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mkandarasi amesaini mkataba mwaka jana mwezi wa Novemba mpaka leo amepeleka mitambo site, yuko site hajalipwa fedha na anadai bilioni tisa tu malipo ya awali. Kwa hiyo, huyu kesho atakuja kudai riba, sasa ni hasara ambazo zinaepukika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naishauri Serikali kwamba, hasara za namna hii ambazo zinaepukika, kwanza tuwe na vipaumbele kwenye mikataba yetu. Hatuna sababu ya kuwa na mikataba mingi ambayo hatuwezi kukidhi kulingana na rasilimali fedha. Ni muhimu sana tukafanya tathmini ya kina, tuwe na mikataba ambayo kimsingi Serikali inaweza ku-afford kulipa kandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais kwenye mradi huu ameweza kuruhusu barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami kilometa 100. Kutoka kipande cha kutoka Ifakara mpaka Mbingo pale Mialeijima, kilometa 62.5 mradi wa bilioni 97, mkandarasi anadai bilioni tisa tu advance payment mpaka sasa hajalipwa toka Novemba mwaka jana. Kesho huyu atakuja kudai riba atakwenda kwenye mpango ule ule wa riba ambazo kimsingi tunaweza kuziepuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi wa pili naye amesaini mkataba kipande cha kilometa 37.5 kutoka Mbingo pale Miale kwa maana ya Ijima Miale mpaka kwenda Chita, Kambi ya Jeshi pale Makutano, sasa jambo hili linawezekana. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba ni muhimu kwa Serikali ifanye tathmini ya kina kwenye miradi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie, kwa sababu kwenye uchumi tunasema opportunity cost, you fore gone for the best alternative. Rasilimali fedha ni ndogo kulinganisha na mahitaji. Kwa hiyo, tukiwa na mipango ambayo inaendana na rasilimali fedha kwa uwezo wa Serikali, itatusaidia kama Taifa kuepukana na malipo ya riba ambazo zinasababishwa na kutolipa wakandarasi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ahsante sana na Mungu atubariki. (Makofi)