Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na niwapongeze Kamati zote tatu kwa taarifa ambazo zimewasilishwa hapa. Nitagusa Kamati mbili, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ambayo mimi ndiyo Mjumbe pamoja na LAAC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati kwa namna ambavyo amewasilisha taarifa ambayo Wajumbe kwa kweli tulitumia muda wetu mwingi, tukatimiza wajibu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo malengo ya Kamati yetu ni kutamani tunavyomaliza Bunge kipindi hiki, basi kuwe na mabadiliko makubwa kwenye taasisi hizi. Bado changamoto ni nyingi sana, naomba nianze na taasisi ambazo bado zinategemea ruzuku kutoka Serikalini. Taasisi hizi zote si kwamba hazijui kwamba Serikali inapowekeza wanatakiwa waanze kupunguza utegemezi mwaka hadi mwaka. Nitatolea mfano wa taasisi hizo ambazo bado zimekuwa zikitegemea ruzuku ya Serikalini; TIB, TTCL, CPB na UDART, hizo ni chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miaka mitatu mfululizo kumekuwa na ongezeko la utegemezi. Yaani badala ya wao sasa tuseme wamekuwa ili na watu wengine waendelee kuwezeshwa, lakini miaka mitatu mfululizo utegemezi umeendelea kuongezeka. Hiyo miaka mitatu kutoka bilioni 13.234 imeongezeka mpaka bilioni 17.456. Nini kitatokea, kuna shida ya management pamoja na bodi zilizopo huko. Kama shida ni management ni lazima tuanze kufikiri upya namna ya kupata watu hawa wanavyoweza kuleta mapinduzi kwenye taasisi hizi. Tofauti na hapo tutarudi kule kule tu. Jambo la kwanza ambalo lazima tulifanye lazima Msajili wa Hazina aongezewe nguvu ili waweze kuwajibika watu hawa kwa sababu shida ni uwajibikaji kwenye hizi taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna utegemezi mkubwa lakini kuna mashirika 63 ambayo yanapata mapato makubwa kutokana na shughuli ambazo wanazifanya ambazo ni zaidi ya ruzuku wanazozipata Serikalini lakini bado wanahitaji ruzuku kutoka Serikalini. Sasa hili jambo halikubaliki. Kwa hiyo kuna haja sasa ya kupitia upya usimamizi wa hizi taasisi. Kama kuna shida kwenye bodi angalau mfumo ubadilike wa kuwapata wasimamizi wa hizi bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mashirika 35 ambayo yanajiendesha kibishara, mashirika 17 bado yanapokea ruzuku kutoka Serikalini, halafu tunasema ni mashirika ambayo yanajiendesha kibiashara, sasa ambayo hayajiendeshi kibiashara itakuwaje? Ni changamoto. Pamoja na changamoto hiyo bado kuna ongezeko la mishahara na matumizi kwa miaka mitatu mfululizo kwenye mashirika hayo, kutoka bilioni 793.58 hadi trilioni 1.33. Badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma na sababu ni kwamba kuna shida kwenye mfumo na upatikanaji wa management ya hizi taasisi. Kama ongezeko hilo la 40.64% kusipokuwa na mabadiliko ya kimfumo hatutasonga mbele, tutabaki hapa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kuna haja ya kupitia upya menejimenti ya taasisi hizi pamoja na bodi zenyewe ndipo tutapata mabadiliko kwenye hizi taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mashirika ya umma yamepata hasara kwa miaka mitatu mfululuzo; TANOIL, TPDC, TTCL, TCB na Shirika la Masoko la Kariakoo. Sasa yaani ukiangalia dude kama la TTCL, ukiangalia fedha ambazo zimewekezwa pale? Kwa nini wanapata hasara, ni kwa sababu kuna shida ya uendeshaji, kuna shida ya menejimenti. Kwa hiyo ni lazima kuwe na mabadiliko makubwa kwenye hizi taasisi tofauti na hapo hatuwezi kufika popote tutacheza hapo hapo siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna hiyo changamoto, pia kumekuwa na shida hata mikataba ambayo wao wanaingia; na jambo hili tumekuwa tunalizungumza mara kadhaa kwenye hizi taasisi. Nini kinatokea kama wanajua kabisa kwamba taasisi hizi tunahitaji kuwekeza ili tupate matokeo chanya. Shida inapokuwa kwenye menejimenti ni lazima hata katika mikataba mtaingia mikataba ya hovyo na mwisho wa siku mtasababisha hasara kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inapelekea, kwa sababu kuna shida ya menejimenti na kwenye bodi kunakuwa na changamoto ya ufanisi wa hizi taasisi na ufanisi hauwezi kuwepo kama shida ni mfumo. Nchi hii shida siyo sheria, shida siyo kanuni, kuna shida kwenye mfumo wenyewe, kwanza upatikanaji wa hizi taasisi zenyewe, vilevile na kwenye menejimenti zinazokwenda kuendesha hizi taasisi. Hatuwezi kufika popote kama hatutafanya mabadiliko makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na mazingira ambayo yamejitokeza, Kamati tumeshauri mambo kadhaa. Jambo la kwanza, ni vizuri Serikali ipitie upya na kutoa elimu kwa taasisi hizi wajue majukumu yao, vilevile waendelee kupimwa na wawekewe malengo ili wale ambao hawajafikia malengo waweze kuondolewa waingie watu wengine wenye sifa; na inawezekana hata wanaoingia sifa zao pia zina changamoto. Kwa hiyo ni vizuri kubadilisha mfumo wa upatikanaji wa hao watu ambao wanaweza wakasimamia taasisi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwa sababu nimezungumzia hiyo changamoto ya menejimenti, kunakuwa na shida, hata vyanzo vilivyopo kuvisimamia kikamilifu ni changamoto na vilevile wanakosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na ndiyo maana watakuwa tegemezi miaka yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nirudi kwenye miradi ambayo haikamiliki kwa wakati, changamoto ni ile ile, ya mfumo pamoja na usimamizi uliopo. Nchi hii ukiangalia uwekezaji ambao umefanywa na Serikali na return ambayo inapatikana ni vitu viwili tofauti. Ni kwa nini? Ni kwa sababu kuna shida hiyo ambayo ninaizungumza ya mfumo. Kuna miradi ambayo imefanyika kwenye taasisi hizi nilizozitaja hapo. Miaka sita miradi haijakamilika, mkandarasi anapata kazi ndani ya mwaka mmoja amefanya kazi kidogo eti anasema amefilisika; ni kwa nini, ni namna ya upatikanaji wa hao wakandarasi, hakuna uadilifu, hatimaye Serikali inapata hasara, tunapata kazi ya kumwambia CAG sijui ukafanye ukaguzi, shida ni mfumo wa nchi hii, lazima tubadilishe upatikanaji wa menejimenti kwenye hizi taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida nyingine ni vipaumbele, ni lazima tuwe na vipaumbele, yaani kama hatuna vipaumbele, ni vigumu sana kufikia malengo. Leo utaamka na hili, kesho utaamka na lile, mwisho wa siku huwezi kufikia malengo ambayo mmejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niguse kidogo suala la 10%. Niwapongeze sana Kamati, wamefanya uchambuzi mkubwa sana na si mara ya kwanza jambo hili linazungumzwa hapa. Kuna haja ya kuwa na ufuatiliaji maalum juu ya maagizo lakini na yale ambayo Bunge linaazimia kwa sababu hatuwezi kuwa tunarudia haya mambo kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata taarifa kwamba wanapokwenda kurudisha hiyo 10% wanataka kuwepo na kamati sijui wilayani, mkoani. Hivi ni nani alisema kwamba shida ya 10% ilikuwa ni kamati? Tunataka tunaporudi kwenye hiyo 10% tuangalie tulikosea wapi, turekebishe ili tujue tunatokaje hapa tulipo. Halafu unapeleka huko mkoani na wilayani, Mheshimiwa Mbunge hajui, diwani hayupo, mnawapelekea watu gani wakasimamie hivi vitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kwenye hii mikopo inayotolewa kuna makundi ambayo yanatajwa kwenye kata fulani kwa mfano Kata ya Namanyele, Kijiji cha Mkangale, Diwani tu wa Kata hiyo hakijui hicho kikundi, unafikiri nani anakitengeneza? Shida siyo kamati shida hapa ni uadilifu na usimamizi wa hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa leo asubuhi kwenye swali la msingi. Leo kama halmashauri zinajua sheria inawataka wapeleke kiasi gani kwenye mapato ya ndani kwa nini wasianze kuwajibishwa ambao wanashindwa kusimamia hiyo sheria kwa sababu shida ni usimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza, kuna haja ya kufuatilia kwa kina, tulikosea wapi tujue tunabadilisha nini ili tunapokwenda kwenye mabadiliko, tusiende kwenye mabadiliko ya nadharia twende kwenye mabadiliko ambayo tunajua tumefanya tafiti za kina na tunakwenda kuboresha makosa yetu tuliyoyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madeni amelizungumza sana Dada yangu Mheshimiwa Ester Bulaya hapa na siyo mara moja. Yaani madeni yanaanzia kule kwa watoto wenu kwenye halmashauri kule mpaka huku juu. Hivi leo mamalishe aliyekopa fedha benki, amepeleka chakula halmashauri, kule benki kila mwezi asiporejesha kuna riba. Halmashauri imekaa na fedha ya mamalishe kwa zaidi ya miaka mitano, kwa nini na wao wasilipe kwa riba kama ambavyo yeye anatakiwa akalipe kule? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo limekuwa na mazoea kwa sababu wanaoonewa ni watu wetu wa chini. Sisi kazi yetu kama Bunge lazima tusimamie hili jambo. Wanapoingia na tutawashauri wananchi wetu, kwenye makubaliano yoyote yale iwe ni kwa maandishi na kuwe na riba kama watakosa kulipa kama walivyokubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunawalaumu wakandarasi, hivi huyu mkandarasi anafanyaje kazi kwa uadilifu? Yaani madai anadai Serikali mpaka unashangaa halafu mwisho wa siku mnasema, wakandarasi wa ndani siyo waaminifu, siyo waaminifu vipi wakati fedha hamuwapatii, mnataka wafanye nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)