Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba nzuri kabisa ambazo zimewasilishwa na wenyeviti wetu wa hizi Kamati za LAAC, PIC na PAC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaanzia alikoishia wajina wangu, Mheshimiwa Francis Ndulane, ambaye amegusia jambo ambalo nilitaka niliseme, lakini kwa sababu nilishajipanga nalo nani muhimu tukilisema mara nyingi na wengi nina uhakika Serikali itaona kwamba sasa umefika wakati wa jambo hili kuweza kulifanyia kazi kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la connection fee ya umeme, mara baada ya REA kupeleka umeme kwenye vijiji vyetu na kumaliza kuweka umeme, sasa wale wanaobaki wanatakiwa wajiendeleze kuchukua umeme wanakutana na shida ya connection fee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nilimsikiliza Mheshimiwa Naibu Waziri vizuri akijibu swali, suala la connection fee kwenye vijiji. Hili suala limekuwa gumu kidogo, kwa mfano, katika Jimbo langu la Iramba Mashariki, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, kipo Kijiji cha Iguguno, ni Kijiji lakini kwa sababu kuna vijumba vya bati vya zamani vimekuwa vingi, ukiangalia kwa haraka haraka unaweza ukadhani ni mji. Leo wanaambiwa wa-connect umeme kwa shilingi 320,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumelisema hapa mara nyingi, lakini TANESCO wamekuwa wagumu sana kutekeleza jambo hili, kila wakati ukiwafuatilia wenyewe wanasema michakato inaendelea, tathmini inaendelea nchi nzima kuangalia wapi ni miji. Leo nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba mji mdogo ni ule ambao upo kwa mujibu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtinga, nakuomba radhi kidogo, naomba uketi.

Waheshimiwa Wabunge, mniwie radhi kidogo, nimefuatilia hotuba za Wabunge, najua tuna changamoto mbalimbali kwenye maeneo yetu, lakini madhumuni ya siku hizi mbili ni kujadili taarifa tatu ambazo zimekuja Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mtinga, nakupa nafasi lakini naomba niwaelekeze Waheshimiwa Wabunge waliobaki, tujielekeze kwa sababu Serikali iko hapa ili iweze kuchukua ushauri mahususi kwenye haya maeneo matatu ambayo yamesomewa taarifa zake leo asubuhi na nimefanya consultation na Sekretarieti hapa kuna hiyo changamoto. Kwa hiyo, tafadhali tujielekeze huko ili ku-focus michango yetu na kuiwezesha Serikali kutekeleza kazi yake. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mtinga.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunachangia Kamati lakini tunatoa mifano hai ili hoja zikae vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ku-connect umeme kwa shilingi 320,000 kwenye vijiji ambavyo hata TAMISEMI haitambui kwamba ni mji mdogo, lakini wananchi wanaambiwa watoe shilingi 320,000 linafubaza maendeleo na ninashukuru Kamati ya PIC wameongelea hili jambo.
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Wapi taarifa? Mheshimiwa Mwenyekiti wa PIC, tafadhali, Mheshimiwa Vuma.

TAARIFA

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Francis kuhusu hoja yake ya gharama za kuunganisha umeme katika maeneo ya vijiji-miji, kwamba ni suala ambalo liko valid na kwenye taarifa yangu ya leo ukurasa wa 14 nimelitaja. Kwa hiyo, ni jambo ambalo liko valid kabisa, endelea kushindilia vizuri ili Serikali iweze kutoa tathmini. Tumependekeza maazimio kwamba tuwape miezi sita ili waweze kukamilisha hiyo tathmini na tuweze kutoka kwenye hiyo sintofahamu ambayo tunayo. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa, unapokea taarifa?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili na niombe Kamati wametoa miezi sita lakini jambo hili tumeliongelea muda mrefu sana. Hili ni suala la kutoa tamko tu kwa sababu kama ni miji midogo inajulikana TAMISEMI, kama ni vijiji vinajulikana TAMISEMI. Kwa hiyo, hili suala wala siyo la miezi sita, mimi ningeliomba Bunge lako Kamati ifupishe zaidi katika maazimio, ni tamko tu litolewe kwamba vile ambavyo ni vijiji ambavyo havijawa miji waendelee na connection fee ya shilingi 27,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiombe TANESCO, hii bei ya shilingi 27,000 hata mjini bado inafaa kutumika kwa sababu ukienda kwenye miji mingine nguzo moja inaweza ikahudumia zaidi ya nyumba saba mpaka nane, lakini wanashindwa kuunganisha kwa sababu ya shilingi 320,000. Kama TANESCO wataziunganishia hizo nyumba umeme watapata ile fedha ya malipo ya mtu anatumia umeme, biashara itakuwa kubwa zaidi. Tunapoelekea niombe TANESCO inabidi tufike mahali tugawe nguzo kwa wananchi ili wakitumia umeme walipe ile connection fee hata kama itabidi kulipa kidogo kidogo kwenye bills lakini nguzo zije.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo vijijini umeme umeshaenda, mwananchi anauona kwa jirani lakini anashindwa kupata kwa sababu hakuna nguzo. Kwa hiyo, ningeomba hii TANESCO hata ikibidi lizalishwe shirika lingine ndani yake yawe mawili ili lingine lishughulikie tu kugawa nguzo huko vijijini na lingine lishughulikie mambo mengine kwa sababu ni shirika kubwa ambalo wananchi wanahitaji sana huduma yake, lakini nadhani limelemewa kwa sababu ya ukubwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri na hivi ndiye Naibu Waziri Mkuu waliangalie hili suala la TANESCO kuweza hata kugawanywa yawe mashirika mawili ili ufanisi uwe mkubwa zaidi na ubunifu uongezeke kwa sababu zitakuwepo bodi mbili na menejimenti mbili zaidi. Kwa hiyo mambo mengine makubwa zaidi yanaweza yakafanyika na wananchi wakapata huduma hii ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka, naomba niseme suala la halmashauri kulipa madeni kwa wazabuni wadogo wadogo. Kuna watu wanaumia sana, yaani mtu amejenga madarasa, mtu kajenga bweni halafu mtaji wenyewe alikopa shilingi milioni 40, milioni 30 hawajalipwa zaidi ya miaka 10. Ukienda kule wanakwambia kwa sababu wewe ni Mbunge hebu chukua hata hii barua, nenda kaniangalizie madeni yangu, nenda kamwone Mheshimiwa Waziri, nenda kamwone nani, watu wanalia wanasikitika wakati majengo waliyojenga wanayaona na yanatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe hili suala Serikali iliangalie, ilipe watu wetu wa ndani madeni yao. Mbona haya makampuni makubwa yanayojenga ambayo kuna riba ndani yake mbona hela zinaenda? Mbona madaraja ya Busisi yanaenda, huko kwenye umeme mkubwa unaenda kwa sababu kuna riba kubwa ndani yake, lakini hawa wa kwetu wadogo wadogo hizo shilingi milioni 30, milioni 40 ndiyo mitaji yao na sisi ndiyo maisha yetu kule kijijini yanaenda kwa sababu uchumi unazunguka kwa hizo fedha. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, halmashauri ziangaliwe na haya mashirika mengine SUWASA, GUWASA na mengine ambayo wamehudumiwa hebu walipe hizi fedha. Serikali iangalie fedha ilipwe ili uchumi uendelee kuzunguka kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wetu wanateseka, wanalia sana, wanatuangalia kwa macho ya huruma, mtu anakulilia mpaka unasema hivi wewe nenda huko ukamwambie Waziri, unamwambia kuna taratibu, ukimuuliza document anakwambia walishasema madeni yamehakikiwa kila kitu imebaki kulipwa tu. Hebu tuombe hili suala liangaliwe kwa umakini ili wananchi wetu wapate fedha ambazo zinazunguka huko chini na ndiyo tunazozitegemea fedha hizi katika mzunguko wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kugusia uendeshaji wa mwendokasi. Nchi yetu inatumia fedha nyingi sana kujenga mwendokasi. Mpaka sasa barabara zinajengwa kila kona pale Dar es Salaam, lakini uendeshaji wake, mtu unaenda kwenye kituo unakaa muda mrefu na hii labda kwa sababu ni kampuni moja. Tuiombe Serikali ziwekwe kampuni kadhaa pale, ziwaze kushindana. Yawepo mabasi ya blue pale, mabasi ya njano, mtu unakuwa unaangalia nikisimama hapa likija basi la njano haraka unajua hili basi linafaa nitakata tiketi kwa sababu hawachelewi kufika. Hii kuwa na mtu mmoja tunatumia fedha nyingi kujenga miundombinu mizuri ya kisasa lakini bado huduma zinakuwa mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe hili suala liangaliwe kwa umakini ili haya mashirika yetu yaweze kutoa huduma ambayo wananchi, nchi yetu ni ya kisasa ina SGR ina kila kitu na hii mwendokasi iende vizuri ili tuendelee kutamba katika Afrika Mashariki na kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)