Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana! Nami nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu wa maoni kwenye hizi Taarifa tatu za Kamati ya PAC, PIC na LAAC ambazo zimewasilisha leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwanza kwa kuomba radhi Bunge kutokana na tukio la leo asubuhi la kukatiza Siwa. Halijawahi kutokea hilo tukio tangu niingie Bungeni mwaka 2015, ila limetokea leo kwa sababu nilikuwa nimetegesha wakati wa swali namba 20 ndiyo ningezunguka kule nyuma halafu nije nisogee pale kwenye podium.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lilipoahirishwa hilo swali na kutolewa, ghafla Mheshimiwa Spika, alisimama nami ikabidi niendelee kukaa hapahapa. Kwa hiyo, nilipoitwa nikakosa muda wa haraka wa kukimbia na ndiyo maana nikakatiza, naomba radhi sana kwa kosa hilo na halitojirudia tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nizungumzie maeneo machache; nianze na suala la madeni, taasisi za umma ambazo ni taasisi za Serikali zinadaiana. Kwa mfano, unakuta TPDC inaidai TANESCO, TANESCO inadai Mamlaka za Maji, Taasisi za Serikali zinadaiwa na Mamlaka za Maji, hili limekuwa ni tatizo la muda mrefu na madeni ni makubwa ambapo kwa haraka haraka ukisema uyalipe yote kwa mara moja, inaweza ikawa ni shida kwa hizi taasisi za Serikali vilevile. Kwa hiyo, naomba kuwe na central commitment kama ambavyo tumependekeza. Hata hivyo, hii central commitment itokee kwenye ngazi za juu kabisa, hasa kwenye Baraza la Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafahamu kwamba ziko ankara ambazo zinabishaniwa, basi hizi ankara ambazo zinabishaniwa, taasisi zikae kwa pamoja zifanye reconciliation, wakubaliane ni madeni gani ambayo ni halali, halafu wapate jumla. Ikiwezekana, hii mipango ya malipo inayoitwa payment schedules iandaliwe kwa taasisi zote. Kwa kweli hata kama utakuwa na payment schedules nzuri za namna gani, taasisi moja moja kulipa haya madeni itakuwa ni vigumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2002, nilikuwa Afisa wa Serikali, wakati Baraza la Mawaziri lilipitisha uamuzi ambao naamini hata sasa hivi unaweza ukachukuliwa. Nilikuwa Afisa, Mheshimiwa Lukuvi, akiwa Mbunge anakumbuka; walipitisha maamuzi mahususi kwamba, madeni yote ambayo Taasisi za Serikali wanadaiana, yote yajumlishwe na yalipwe centrally na Wizara ya Fedha kupitia central budget, halafu baada ya hapo kama kutakuwa na madeni mapya, basi madeni hayo yawe yanaingizwa kwenye bajeti za kila taasisi na kila Wizara kwa kila mwaka ili madeni yawe yanalipwa internally, badala ya kulimbikiza madeni ambayo baadaye yanakuja kuisumbua Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uamuzi ule ulifanyiwa kazi na mwaka 2003 nadhani ililipwa hundi ya karibu shilingi bilioni 68 na baada ya hapo madeni mapya hayakuibuka tena, mpaka baada ya mwaka 2007 ndiyo yakaanza kuibuka tena madeni ya taasisi za Serikali kudaiana. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ule uamuzi wa mwaka 2002 wa Serikali kupitia Baraza la Mawaziri, ungerejewa ili kusudi madeni haya makubwa yaliyopo sasa hivi yaratibiwe na Wizara ya Fedha na yalipwe yote, ili madeni mapya sasa yawe yanaingizwa kwenye bajeti za kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nami ningependa kulizungumzia, ni mifumo ya kielektroniki; observation hizi hata Mheshimiwa Rais ameshazitoa kuhusu mifumo ya kielektroniki inayosomana hasa hasa across government na taasisi zake kama TRA na taasisi nyingine. Kwa kweli mapendekezo kwenye eneo hili yako mengi na yameshatolewa sana, kwa mfano kwenye Kitambulisho cha NIDA. Naishukuru Serikali sana iko kwenye mpango wa kuunganisha NIDA na RITA, hiyo ni hatua muhimu sana ya kuboresha eneo hili la utambuzi. Nami nategemea kwamba, tuwe na utambuzi kama uliopo Marekani, Mmarekani ambaye ana personal identification number, taarifa zake zote za kuzaliwa, kazi, biashara na kila kitu anachokifanya, ziko kwenye personal identification number.
Mheshimiwa Spika, hapa Tanzania kama tutafaulu kuweka taarifa zote za Mtanzania kwenye personal identification number ambayo ndiyo inabeba Kitambulisho cha NIDA, basi inawezekana tukafaulu kutatua matatizo mengi sana yakiwemo matatizo ya kodi na matatizo mengine mengi sana. Kwa hiyo, haya mapendekezo ambayo yako kwenye taarifa zetu, naomba yafanyiwe kazi kwa kina. Siyo kusoma tu pendekezo kama lilivyo, hapana, Serikali iende kwa kina ifanye mapitio ya kina ili kuboresha kila maeneo ambayo yamependekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeona linahitaji kuangaliwa kwa kina, ni haya madai ya hospitali ambayo yanakwama kule NHIF. Nadhani napo kinachohitajika ni checklist tu, checklist ya vigezo na masharti kama itaandaliwa vizuri na ikakubalika kwenye mkutano wa wataalam wa hospitali pamoja na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), inawezekana hiyo ika-solve matatizo mengi sana, kwa sababu kila hospitali itakuwa na checklist inayofahamika kwamba, kuna moja, mbili, tatu, nne tano na vigezo na masharti ni moja, mbili, tatu, nne, tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yule anayeandaa pale hospitalini atazingatia hiyo checklist na yule anayepelekewa pale NHIF na yeye ataangalia ile checklist. Kwa hiyo, itapunguza matatizo ya kukataliwa kwa maombi ya malipo ya hospitali mbalimbali. Kwa kweli mengine mengi yaliyopendekezwa ni mazuri, ninaomba Bunge lako Tukufu lizingatie mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati hizi tatu ili kuboresha utendaji wetu na mifumo yetu ya uendeshaji wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)