Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya jioni hii ya kuchangia katika Taarifa za Kamati ya PAC, LAAC pamoja na PIC. Kabla ya yote nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utashi mwema wa kuweka mazingira mazuri ya Ofisi ya CAG ikafanya kazi vizuri kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana pia Mheshimiwa CAG pamoja na wataalam wake ambao kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi kwa weledi na utashi kwa maslahi mapana ya nchi yetu, ndiyo maana tunapata taarifa kama hizi mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisiposhukuru na kupongeza Kamati ya LAAC chini ya Mwenyekiti Halima Mdee na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Mabula, pamoja na wajumbe wa Kamati. Tuko floor moja, wamekuwa wakifanya kazi mpaka usiku ili kuhakikisha kwamba, hizo halmashauri 55 ambazo wameziita mbele ya Kamati, wamepitia kwa ufasaha na kujiridhisha na utendaji kazi na ndio maana tunaona taarifa kama hizi. Mwisho na kwa umuhimu, napongeza Bunge lako Tukufu kwa kutoa mazingira mazuri kwa Kamati hizo zote ili kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nina machache, lakini mengi itakuwa ni kuishauri Serikali, CAG amepewa hadidu za rejea, Sheria na Katiba ya Nchi imwongoze katika utumishi wa kufanya kazi na ndiyo maana anafanya kazi nzuri. Hata hivyo, kuna baadhi ya mazingira ambayo Serikali inatakiwa iangalie kwa jicho la pekee ili sisi wenyewe tusifanye vitabu vyetu vya Serikali yetu kila siku kuwa na mapungufu ambayo yangeweza kuzuilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikupe mfano, nimesoma ukurasa wa 15 Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe haijakusanya fedha takribani bilioni sita kutoka kwa Yapi Merkezi. Nitoe ushuhuda wa eneo hili, nami nilikuwa Mkurugenzi, eneo hili nimelifuatilia kwa kina nikiwa Wilaya ya Kisarawe, Wilaya ya Kibaha, Mvomero ambayo nilikuwa naisimamia, nikiwa Kilosa ambapo wote tulikuwa tunafuatilia fedha ambazo ni za ushuru wa huduma waliokuwa wanatakiwa kulipa Yapi Merkezi na tulifanya vikao vikubwa. Hapa, Mheshimiwa Chamriho alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, akaja akawa Katibu Mkuu wa Madini, tukaenda Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, lakini yote ambayo tulifanya kama wakurugenzi enzi hizo, kwa kweli yote yaliishia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hizi halmashauri wamesema wamechukua sample, lakini wakienda katika wilaya hizo watakuta madai mengine hayo hayo ya Yapi Merkezi ambapo baadaye yalitolewa maelekezo kwamba, “hatuwezi kutoa fedha mfuko huu tukarudisha huku.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni nini? Sasa hii taarifa ikiwa kwenye vitabu vya CAG inaendelea kuonesha kwamba, bado kuna madeni makubwa ambayo kimsingi hayatekelezeki. Ninaomba kutoa ushauri wangu kwa Serikali, niiombe kunapokuwa na miradi mizuri kama hii ya kimkakati ambayo ni faida kwa Taifa letu, basi Serikali inapoona mazingira ambayo hizi sheria zetu tulizozitunga haziwezi kutekelezwa, ni kiasi cha kutoa utaratibu ambao utafuatwa ili isiendelee kuonekana katika vitabu vyetu na kuchafua au kuweka taswira inayoonekana kwamba Serikali haifanyi kazi vizuri au halmashauri haifanyi kazi kwa niaba ya Serikali. Hili likitibiwa naamini tutakaa vizuri na vitabu vitakaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo sheria ni ngumu kidogo, ni Sheria ya Madeni ya Mifuko. Najiuliza, adhabu ya faini ya 1000% ya kutoza halmashauri au taasisi ambayo haijapeleka makusanyo ya mtumishi kwa muda, inatoka wapi? Nani ambaye aliitunga? Unaona hapa makusanyo ya Mifuko ya bilioni nne, adhabu yake ni bilioni 32. Hii ni Sheria ambayo kwa kweli Serikali inatakiwa kukaa na kuiangalia kwa kina na kuitafakari. Kwa sababu unapokuwa unajikatisha tamaa, au unapokuwa unadai madai ndani ya Serikali hiyo hiyo, kwamba halmashauri ipigwe faini ya bilioni nne, zije bilioni 32, siamini kama tunakuwa tunajenga, sana sana hapa tutakuwa tunatishana na mwisho wa siku haya madeni yatashindikana kulipwa, mwisho wa siku yanabaki kwenye vitabu vyetu, inaonekana vitabu siyo visafi. Kwa hiyo, niiombe Serikali yetu iangalie maeneo mengine ambayo inaweza kuyaboresha ili isionekane kila dakika kwamba tuna mahesabu kwenye vitabu ambayo hayaendi sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, kama Hazina inalipa mishahara kwa watumishi wetu, kwa nini isije na mkakati wa kutoa haya mafao ya watumishi wote yakawa yanapelekwa moja kwa moja kwenye hii Mifuko na tukaondoa hili ombwe ambalo hela zikija huku hazipelekwi kwa wakati, halmashauri inaanza kuchafuka na madeni yanakuwa hayalipwi? Ni ngumu sana kuisemea halmashauri, lakini sisi sote ni mashuhuda, kule chini wakati mwingine halmashauri wanajitoa kwa moyo ili kuhakikisha kwamba shughuli za halmashauri zinakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata maeneo mengine sisi wote humu ni mashuhuda, Serikali imepeleka fedha nyingi za miradi, leo tunapiga makofi na kupongeza kwa kazi nzima ya Mheshimiwa Rais na sisi wasimamizi, kazi imefanywa na halmashauri hizo hizo. Leo tukiulizana, hivi unaweza ukajenga darasa kwa shilingi 12,500,000 na madawati ndani yake? Unaweza ukajenga tundu la choo kwa shilingi 1,100,000 ukaweka na vifaa vyote mle ndani? Kwa hiyo, kuna wakati mwingine wakurugenzi wanajifunga mikanda ili kuhakikisha kwamba kazi za Serikali zinakamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hatutetei kwamba wakurugenzi hawafanyi baadhi ya maeneo na kuna mapungufu, hapana. Hata hivyo, kuna maeneo mengine lazima tuyaangalie kwa kina na tufanye tathmini ya kweli ili tukipeleka fedha kule, zisaidie kuendesha miradi na ziwe zinatosha na hawa watu watashindwa kuchafuka kwa sababu pesa zitakuwa zinatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo lingine ambalo nataka nishauri kulingana na Taarifa ya LAAC, page 12. Tumeona kuna halmashauri ambazo zimekusanya mapato chini ya malengo. Serikali imeendelea kufanya kazi nzuri ya kuzilea halmashauri zetu, nakumbuka miaka mitatu nyuma, Halmashauri ya Kakonko ilikuwa ni halmashauri ambayo mapato yake ilikuwa ni milioni 200 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini halmashauri hiyo structure yake ni sawa na halmashauri nyingine zote nchini. Kwa hiyo, hata uendeshaji wa halmashauri hiyo ilikuwa ni changamoto. Hata hivyo, baadaye kwa uwekezaji wa Serikali na kuendelea kuiwezesha kiuchumi, kuwekeza kwa miradi ya kimkakati, Halmashauri ya Kakonko ikatoka kwenye milioni 200, ikaja milioni 700 na leo tunaongelea bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri nyingine ilikuwa ni Halmashauri ya Gairo ambayo ilikuwa haiwezi kukusanya zaidi ya milioni 400, lakini leo tunaiona Gairo imekwenda na mpaka sasa hivi ina bajeti ya kukusanya bilioni 1.7 kwa sababu ya uwekezaji wa miradi ya kimkakati ndani ya halmashauri hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu hapa ni kuishauri Serikali, tulikuwa na jambo zuri la miradi ya kimkakati na hasa katika zile halmashauri ambazo kwa kweli vyanzo vya mapato ni adimu kulingana na jiografia ilipowekwa halmashauri. Kwa hiyo, nami niendelee kuiomba Serikali, zile halmashauri ambazo tunaona kwamba makusanyo hayakwenda vizuri, tusiende kuwahukumu, ila, tuangalie kwa undani kwamba, sababu ya msingi ni ipi ambayo imefanya halmashauri hiyo isifanye vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni suala la ubadhirifu, basi hatua zichukuliwe, lakini kama ni sababu ya jiografia na maeneo ambayo hayawezi ku-favor halmashauri kukusanya, basi turudi kwenye ule utaratibu wetu uliokuwepo, tuweze kuwekeza katika miradi ya kimkakati ili kuinua mapato ya halmashauri hizo. Naamini baada ya muda, hizo halmashauri zote zitakusanya fedha kulingana na kiwango ambacho kinatakiwa. La sivyo, kwa sasa halmashauri zitaogopa kuji-stretch kuweka bajeti kubwa ya kukusanya ili kuogopa kutofikia malengo, suala ambalo litakuwa siyo zuri kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine wa mwisho ni ushuru wa huduma, tunaona katika Taarifa yetu ukurasa wa 15, imeonekana kwamba ushuru wa huduma unakusanywa kwa shida kidogo na sheria yetu inaruhusu halmashauri zikusanye 0.3% ya mauzo ghafi baada ya kupunguza VAT na ushuru wa bidhaa, lakini makusanyo hayo yasipopelekwa kwa wakati, maana yake 1.5% ndio penalty ya zile fedha, ambazo ni kama wamekwenda zaidi ya 500% ya ile Sheria ya 0.3 percent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niiombe Serikali yetu Tukufu, katika maeneo kama haya unapokusanya ushuru wa huduma wa halmashauri wa mapato ghafi, yaani kwa kweli kwa wafanyabiashara ni kazi ambayo ni ngumu kidogo. Hii kwa kweli imeleta shida sana kwa sababu huyo huyo mfanyabiashara analipa corporate tax ya TRA, yeye ni agent wa kukusanya VAT, atalipa OSHA, leseni, fire na atalipa fedha za kukusanya taka. (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hili tuliangalie, kwa kweli hili limekuwa ni suala ambalo utekelezaji wake kwa wafanyabiashara hata ukienda kwenye majiji yote, nenda pale Jamhuri, nenda Kariakoo kuna ugumu. Kukusanya 0.3% kutoka kwenye mapato ghafi ya service levy kwa kweli bado ni kitendawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niiombe Serikali, kwa sababu inawapenda wafanyabiashara wake na inataka iwakuze kimtaji ili waweze kukua, iliiangalie suala hili kwa undani zaidi. Ni bora kutathmini na kuweka malengo, kukadiria kiasi ambacho mfanyabiashara anaweza kulipa, lakini ukipigia kwenye percentage ya malipo ghafi, kidogo inakuwa inamuumiza mfanyabiashara na ninaamini inakuwa ni ngumu sana katika kutekeleza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi hoja zinaweza zikaendelea kuonekana kwenye vitabu vyetu kwa sababu tunahitaji kuangalia kwa kina, kufanya tathmini na kuangalia namna gani ya kuboresha na kuweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara wetu ili waweze kulipa bila kusita kokote, lakini na Serikali yetu iendelee kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niiombe sana Serikali, halmashauri zetu zinafanya kazi vizuri na ukitaka kuujua utamu wa ngoma uingie ucheze. Bahati mbaya, halmashauri zimekuwa zikionekana kwamba hazifanyi kazi vizuri hasa katika haya makusanyo na taarifa za CAG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kwa usimamizi mzuri wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia, Ofisi yetu ya Rais, TAMISEMI, niombe kuwe na utaratibu wa kwenda kufanya tathmini ndani ya halmashauri zetu, jinsi gani ya kuboresha upatikanaji wa mapato, lakini na yale yanayowasibu wao na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya, baada ya kufanya hivyo, tutawapa mazingira mazuri ya kufanya kazi, makusanyo yatakuwepo, lakini na hizi hoja za Serikali kama siyo kwisha, basi zitaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kuliko sasa hivi. Maana yake kila halmashauri inaonekana kuna wizi, kuna ukwapuaji, lakini mazingira ni magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano, tunapopeleka shilingi 12,500,000 darasa limaliziwe, lakini unakuta kinachotakiwa pale ni milioni 17 au 18. Hakuna room ambayo mkurugenzi atarudi kwa mleta fedha kumwambia kwamba, zimepungua naomba uniongezee. Haya, niambie hizo fedha nyingine alizitoa wapi? Lazima ajifunge mkanda ili kuhakikisha mradi huo umekamilika na watoto wetu wameingia darasani. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa nia njema, iendelee kuboresha mazingira mazuri, halmashauri zetu zinafanya kazi vizuri na sisi sote ni mashuhuda, miradi imetekelezwa vizuri, ili sasa CAG akienda kule akute mambo yako sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, naunga mkono hoja na nashukuru kwa nafasi. (Makofi)