Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa heshima hii. Nitaomba nichangie kwa kifupi sana kwenye mada zote tatu, lakini kila mmoja atachukua la kwake halafu tutaelewana mbele ya safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya Serikali ni chain of command na Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya kuidhinishwa na Bunge kwa kufuata Sheria na Kanuni za Fedha na kiongozi anayestahili kulisimamia hili ni Bunge hili, kwamba Serikali tunairuhusu iende ikafanye matumizi baada ya kupitisha bajeti lakini baadaye tunakuja kuangalia nini kimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nyuma niliwahi kusema kwamba huwa tunakutana muda mrefu hapa tunachagua, tunaamua halafu tuna wapa wenzetu wakatekeleze ila kwa bahati nzuri au kwa bahati mbaya sana inaonekana tunalo tatizo kwenye chain of command. Maana yake ni kwamba Serikali inatoa maelekezo, lakini watendaji nadhani hawaelewi au wanafanya kwa makusudi kutokusikiliza maelekezo ambayo yanatolewa na Serikali ili kuhakikisha kwamba sheria zinafanya kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano hapa na nitaomba ninukuu ili nikae kwenye mstari. Liko tatizo la fedha ambazo hazitakiwi kubaki mwisho wa matumizi au mwisho wa mwaka. Sasa kwenye Waraka Namba moja wa Mwaka 2021/2022 tarehe 7 Juni, 2022 ulitolewa Waraka Namba Moja na Mhasibu Mkuu wa Serikali ambao unaandaa taarifa za mwaka ukiwakumbusha Maafisa Masuuli kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali na kuhakikisha kuwa account ya masurufu haina bakaa mwishoni mwa mwaka wa fedha yaani tarehe 30 Juni, 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni nini kilichobainika? Kilichobainika ni kwamba Taasisi saba zilikuwa na bakaa ya shilingi bilioni 2.45, nini maana yake? Maana yake Serikali inatoa maelekezo, lakini watekelezaji wanaopanga na kuruhusiwa kufanya wanafanya yaleyale kinyume kabisa na maelekezo, maana yake nini? Maana yake huu ni uvunjaji wa Sheria za Fedha na kanuni kwa makusudi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taasisi nyingi hapa nitaomba nitaje chache, kwa mfano Wizara ya Mambo ya Ndani ilibakiza milioni 195, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya milioni 72, Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure milioni 276 na nyingine. Ukifanya majumuisho unapata bilioni 2.45 zimekaa hazina maelekezo. Kwa maana hiyohiyo tunakwenda kwenye taasisi zilizofanya ununuzi nje ya mipango, lakini wakati huohuo ziko taasisi ambazo zimekusanya fedha, kwa mfano halmashauri zetu lakini zimekusanya fedha hazikuwasilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizifanyia hesabu kuna mambo matatu yanafanyika kwa wakati mmoja. Wako wanaokusanya fedha, lakini hawapeleki kwenye Mfuko Mkuu, lakini wako wanaokaa na fedha kwa muda mrefu, lakini wako wanaokaa na fedha ambazo zinatumika nje ya utaratibu. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ukiangalia kwa haraka haraka ni mambo mawili au matatu: la kwanza, hawa wanaopewa maelekezo kwa mujibu wa sheria inawezekana sheria hizi kwa sababu wanazifahamu, lakini wanajua udhaifu wake wameamua kwa makusudi kukiuka maelekezo ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili, lazima Serikali iwe na meno makali, Serikali iache kuchekacheka na kuwachekea hawa kwa sababu wanatuweka kwenye kipindi kigumu, bahati mbaya sana tunaelekea kwenye eneo ambalo tutakwenda kuulizwa. Niliwaambia wenzangu mwaka 2021 tutakwenda kuulizwa na wapigakura na Chama chetu tumefanya nini? Sasa kwa stahili hii maana yake lazima tujipange upya na lazima meno yetu yawe makali kuhakikisha kwamba kila maelekezo tunayoyatoa kwa watendaji wetu lazima wayafuate siyo kwa hiari. Kwa hiyo, mimi ombi langu Serikali iongeze meno, ing’ate na sisi tuone kwamba imeng’ata, isiwachekee hawa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa ujumla fedha ambazo ziliachwa bila ya kutumika kwa harakaharaka tu ni shilingi milioni 409, lakini kule nyuma nimesema ni shilingi bilioni 1.8 zimeachwa tu bila ya kazi, lakini hizohizo zinakwenda kutumika huko bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda hautoshi, ninaomba nichangie kidogo tena kwenye hoja ya ongezeko la deni linalotokana na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha. Ziko taasisi zetu kwa mfano, mimi natokea kwenye Kamati moja ya NUU (Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama) kwenye Kamati hii kuna chombo chetu sisi tunakiita Jeshi la Polisi. Kwa mwaka ule wa 2023 Jeshi letu lilikuwa linadaiwa shilingi bilioni 6.621, deni hili limekaa mpaka tunatakiwa kulipa shilingi bilioni 244.51.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Ni kwa sababu tu tumechelewa kulipa na ni kwa sababu ni fedha za kigeni, kwa hiyo kutoka 114 tunakiwa kulipa 244, nini maana yake? Maana yake ni kwamba tumeongeza zaidi ya mara mbili ya fedha hizi ambazo ni kwa sababu tu mmoja anafanya maamuzi mwingine anatekeleza, lakini hapa katikati hakuna kiungo, kwa hiyo mmoja anaamua lini alipe na nani amlipe. Jambo hili halijakaa sawa kwa sababu hii ni fedha nyingi ya wananchi ambayo tungeweza kuilipa kwa wakati deni hili lisingeweza kutoka 114 mpaka kufika 244 maana yake ni zaidi ya 50%. Sasa hili halikubaliki na halitujengei heshima kama Bunge kwa sababu sisi tunatakiwa tuongeze ukali kuishauri Serikali kwa kuwa mambo haya yanawaumiza sana wananchi na kwa kweli yanatuweka kwenye wakati mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kifupi kabisa niongelee kwenye kutumia fedha nje ya mfumo wa electronic. Sisi tunapofanya bajeti na tukaiidhinisha Serikali ikatumie na Serikali inaweka mifumo maana yake lazima watendaji wetu watekeleze kwa mujibu wa utaratibu. Inakuwaje Serikali inaelekeza, lakini watalaam hawatekelezi na siku zinavyokwenda haya yanaongezeka, linatuweka kwenye kipindi kigumu kama Wabunge, lakini kama Wabunge kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona aibu hata kutaja hapa, lakini niruhusu nitaje kwa heshima kabisa ili wenzetu hawa wajifunze. Ukifanya hesabu ya harakaharaka hizi ni bilioni 149 nje ya mfumo wa electronic, hivi hii guts wanatoa wapi hawa? Ninaomba nirudie kusema bado huu ni mwaka wa nne ninasema bado Bunge letu halijafanya kazi ya kung’ata. Bunge letu lipo halijafanya kazi ya kung’ata ili kila mtu ajue kwamba Bunge lina jukumu la kusimamia na kuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano, Taasisi ya Wakala wa Barabara inazo 82, Shirika la Magereza 6,551, Wizara ya Elimu 51.24, halafu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Musoma 591. Ukiyataja haya unapata kichefuchefu hivi hawa watu hii nguvu wameitoa wapi? Hii Serikali ambayo tumeipa dhamana na sisi kama Bunge tunaisimamia na yenyewe ina sheria za kufanya kazi, hawa watu wamepata wapi guts hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwamba Bunge lako hili lazima lioneshe kwa nguvu zote kwamba hatukubaliani na mchezo huu. Kila siku tunaendelea kuilazimisha Serikali itafute hela, Serikali inatafuta, lakini wanaotekeleza kule wanafanya wanavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ili tuweze kufanya kazi kama Bunge, ili tuweze kufanya kazi kama Wabunge, ili kila mmoja akae kwenye mstari wake, ninaona aibu kuyasoma haya maana yake hayanipi raha. Ninaomba sana nishauri haya na haya sikuyashauri leo niliyashauri mwaka 2021: la kwanza, tuhakikishe kwamba sisi kama Bunge na Kamati zetu zote zinazohusika na mambo ya fedha kwa ujumla zifanye kazi ya kuziita taasisi zote. Wenzetu hapa wamesema wamekagua kwa mfano kwenye halmashauri 30% au 31% ya halmashauri bado. Tulisema kila aliyepewa pesa ya Serikali lazima ziwe accounted for, hilo la kwanza; (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninaomba nirudie wito wangu nilioutoa mwaka 2021 kwamba Bunge linatakiwa kufanya kazi sambamba na Serikali. Bunge hili kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali, sasa kama sisi tumefanya kazi ya kushauri lakini hatuisimamii Serikali maana yake sisi wenyewe hatufanyi kazi ya kutekeleza sheria ambazo tumezitunga wenyewe. Ombi langu, Bunge lichukue nafasi yake ya kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali kwa sababu sisi tunaunda Mhimili mwingine ambao ndiyo Mhimili pekee unaoweza kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru sana. (Makofi)