Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwanza kabisa kulipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye jukumu la kutunga sheria. Nalipongeza kwa sababu kwa namna tunavyokwenda na hasa session hii ya utunzi wa sheria tumeona usimamizi umekuwa mzuri na kazi inafanyika kiuhalisia kweli na sheria zinazotungwa zinatungwa kwa umakini hasa. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kukipongeza kiti chako lakini kumpongeza sana Mheshimiwa Spika kwa usimamizi huu mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Kamati hii ya Sheria Ndogo. Jukumu hili ni zito na kama unavyojua sheria ni nyingi kweli kweli, lakini chini ya Kamati hii na chini ya uongozi hodari wa Mheshimiwa Rweikiza Kamati hii imejitoa na kufanya kazi kubwa kweli kuhakikisha dosari zinazokuwa kwenye hizi Sheria Ndogo zinafanyiwa kazi. Kwa hiyo naipongeza sana Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, niipongeze Serikali hususani Serikali hii ya Awamu ya Sita. Serikali hii kwa wakati tofauti imekuwa ikitekeleza maazimio mengi ambayo Bunge lako Tukufu inayatoa, imekuwa ikitekeleza maelekezo mengi ambayo Kamati inayatoa na hivyo sasa tunaona Kanuni nyingi zinazotungwa zimepungua sana changamoto. Changamoto hizi hazipungui hivi hivi, zinapungua baada ya Serikali kutimiza wajibu wa kutekeleza maazimio ya Bunge. Kwa hiyo ninaipongeza sana hii Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kuipongeza Serikali kwa namna inavyotokeza, inavyo-appear kwenye Kamati na hapa niombe sana Waheshimiwa Mawaziri na Taasisi zao pale wanapoitwa na Kamati wasipuuzie, wajitokeze kwenye Kamati, kwa sababu tunapokaa kujadiliana ndipo tunapopunguza matatizo, tunapopunguza sheria zenye dosari ambazo zinawaumiza wananchi na ndipo tunapopata sheria nzuri baada ya mashauriano upande wa Kamati lakini pia na upande wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana na wale ambao pengine na wakati mwingine wanaitwa hawajitokezi wajirekebishe kwa sababu waone umuhimu wa kujitokeza kwenye Kamati ili kupunguza haya matatizo. Kwa nini? Wakati mwingine Serikali inaweza kulegea kidogo kujitokeza kwenye Kamati tofauti na maeneo mengine sisi katika utaratibu tuliojiwekea Serikali inatunga kanuni hizi inazipeleka kwenye matumizi kabla ya Kamati kuzipitia. Kwa hiyo, wakati fulani na mahali fulani sheria hizi zinawaumiza wananchi, lakini wanapojitokeza tunafanya majadiliano, tunafanya marekebisho, tunapata sheria nzuri ambayo inatumika bila manung’uniko na bila bugudha kwa wananchi. Kwa hiyo, niombe sana na nitumie nafasi hii kuiomba Serikali na taasisi zake kujitokeza pale zinapoitwa kwenye Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo niongelee upande mwingine, upande wa halmashauri. Serikali, Wizara na Taasisi huwa zinajitokeza lakini kwa upande wa Halmashauri mara nyingi wanaojitokeza ni Waziri pamoja na wataalam ngazi ya Wizara, lakini ingependeza sana kama waliotunga hizi sheria kwa maana ya Halmashauri husika wangekuwa wanajitokeza kwenye Kamati kutoa ufafanuzi ili wa-feel facial expression ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sawa, lakini ingependeza sana kama wale waliotunga hizi sheria, kwa maana ya halmashauri husika, wangekuwa wanajitokeza kwenye Kamati kutoa ufafanuzi ili wa-feel the deminer na facial expression ya Kamati inapoelezea kwa nini ulitunga kanuni hii, kwa nini ulitunga sheria hii na kwa nini isiwe hivi, iwe hivi. Kwa hiyo ingekuwa inafaa sana halmashauri zikaambatana na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri kuja kwenye Kamati kutoa ufafanuzi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo ninaipongeza Serikali, dosari nyingi zimepungua kama alivyosema mzungumzaji aliyetangulia, ambaye ni makamu wangu. Ni kweli dosari nyingi zimepungua kwa sababu hizo ambazo nimezisema hapa, lakini zipo dosari ndogo zimeendelea kuwepo kama Mheshimiwa Mwenyekiti wetu alivyowasilisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, dosari ambazo bado zipo zinaonekana, ambazo ni pamoja na kutunga sheria ambazo zinakosa uhalisia. Naomba sana wanaotunga hizi sheria; na tukumbuke kwamba wajibu wa utunzi wa sheria ni wa Bunge. Wahusika huku wamepewa dhamana tu au wamekasimiwa tu. Kwa hiyo, wanapotunga hizi sheria, watunge sheria zenye uhalisia. Kwa mfano, Sheria Na. 217, ambayo ilitengeneza ada ya ushuru katika Manispaa ya Mtwara kwenye kipengele cha sehemu ya majedwali iliweka viwango vya ushuru wa malori kuingia kwenye mji, kwamba, malori yakiingia kwenye mji, unaweka kiasi kikubwa cha ushuru; lengo likiwa kuzuia malori yasiingie kwenye mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uhalisia ukoje hapo, unazuia lori moja kuingia kwenye mji kwa kuhofia kwamba litaleta msongamano. Lori moja hili limebeba labda tani 30. Badala ya kuingia lori moja kwenye mji unaweka kodi kubwa ili yaingie malori madogo madogo, kwenye tani 30 utaingiza malori matatu au manne. Sasa hapo unapunguza msongamano au unaongeza?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hii Mtwara; twende kwenye uhalisia kabisa. Pale Mtwara ndipo kwenye bandari. Hivi malori yatakayoenda kuchukua mizigo na kupeleka mizigo kwenye bandari ni malori ya namna gani? Ni lori dogo au lori kubwa? Kwa hiyo, unaweza kuona sheria hii kwa kweli haikuwa na uhalisia. Kwa hiyo, wahusika waangalie mazingira waliyokuwa nayo ili watunge sheria zenye uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna sheria Tangazo la Serikali Namba 219, Kifungu cha 11 cha Sheria ya Kilimo na Usalama wa Chakula, kimeweka masharti kwamba afisa muidhiniwa anaruhusiwa kuingia kwenye kaya au ghala kufanya ukaguzi. Hakikusema muda gani afisa huyu muidhiniwa aingine kwenye kaya au ghala. Tunaweza tukawa na afisa muidhiniwa mzuri anayetimiza wajibu wake, lakini anaweza akaja afisa muidhiniwa wa hovyo, yeye akawa anataka kufanya kazi usiku tu wa manane. Yeye saa saba za usiku ndiyo anagonga nyumba ya mtu, ngo, ngo, ngo! Watu wamelala. Kwa hiyo, sheria kama hizi zinakuwa hazina uhalisia, lakini kiujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mifano hii michache, niseme tu kwamba, Serikali imekuwa ikisikiliza maelekezo na imekuwa ikitekeleza maazimio ambayo tunayatoa hapa Bungeni. Niombe sana Waheshimiwa Mawaziri na wataalam wao, ku-appear ili mashauriano yanapofanyika tuweze kutengeneza sheria ambazo hazileti kero kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapinga, hilo ombi lako lipo katika maazimio yenu? Hiyo ku-appear kwenye Kamati yenu lipo kwenye azimio? Hicho unachoomba; umeomba hapa wahusika ku-appear kwenye Kamati yenu, iko kwenye azimio?

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijafuatilia yote, lakini wakati tunajadiliana ni mambo ambayo tulikuwa tunajadiliana kusisitiza wawe wana-appear kwenye Kamati.