Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D.CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kuongelea kuhusu nguzo za umeme kutoka nje. Viwanda vya Sao Hill (Mafinga) na TANWAT (Njombe) waungwe mkono katika suala la tenda ya nguzo hasa kwa ajili ya REA phase III na TANESCO. Nguzo kutoka nje zinapata msamaha wa import duty na pia malipo yanafanyika kwa wakati. Pia Serikali (TANESCO) inawasaidia kwa mfumo wa Letter of Credit (LC). Favour hii inayotolewa kwa kampuni za nje haitolewi kwa wazalishaji wakubwa kama Sao Hill na TANWAT.
Viwanda nilivyovitaja vina uwezo kwa sababu vina misitu, lakini pia hata wananchi wamepanda miti ya kutosha. Nashauri tuunge mkono wazalishaji wa nguzo wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni REA. Pongezi zangu kwa watendaji wa REA, hiki ni chombo cha kupigiwa mfano siyo kwa sababu wanapewa fedha la hasha, bali utendaji bora wa watumishi wote wa REA. Tumeona taasisi ngapi za Serikali zinapewa fedha lakini bado hakuna tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mkubwa kuhusu REA, Serikali ione uwezekano kupitia TAMISEMI/Wizara ya Fedha kuzisaidia Halmashauri gharama za wiring kwenye maeneo ya huduma (shule na zahanati) ambazo REA wamefikisha umeme lakini wananchi (vijijini) wameshindwa kuuingiza kwenye shule, mabweni na zahanati kwa kuwa hawana uwezo. Nafahamu ni jukumu la REA kufikisha umeme na siyo kugharamia kuingiza ndani, hata hivyo Serikali kwa pamoja mnaweza kuona tunawasaidiaje.
Tatu, katika Jimbo langu Mafinga Mjini kuna kijiji kinaitwa Sao Hill huko ambako nguzo za umeme zinazalishwa. Kijiji hicho naomba tukiwekee umeme kuenzi japo mchango wa kijiji hiki katika suala zima la nguzo. Tuwaonee imani yaani wao nguzo zitoke kwao lakini umeme wausikie. Pia vijiji vya Mtule, Matanana, Kisada, Bumilayinga, Ulole, Itimbo, Maduma na Kikombo na pia maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Mafinga, nashauri TANESCO wafunge sub-station maana matumizi yameongezeka kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya kuchana mbao na kukua kwa mji.
Nne ni kuhusu mafuta na gesi. Pamoja na wafanyabiashara kupiga vita EWURA, nashauri Wizara iwe makini na wafanyabiashara wanjanja wanaojenga hoja dhaifu za kuondoa “marker” ili kudhibiti wanaokwepa kodi. Pia tumejipanga vipi kuhakikisha haturudii makosa ya kwenye madini katika suala zima la kuhakikisha kuwa tunanufaika na sekta ya mafuta na gesi?