Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye Kamati yetu hii ya Sheria Ndogo. Ninaomba nitoe shukrani zangu za dhati kwanza kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inastawi na inakuwa na maendeleo makubwa, kwa kweli jambo la Kumshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninaomba niishukuru sana ofisi yako hasa kwenye kitengo hiki cha utungaji wa sheria, kwa kweli wanaturudisha darasani. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa jinsi anavyohakikisha kwamba Sheria zetu tunazotunga zinakuwa sahihi na hana haraka kwa jambo hili. Kwa jambo hili Mheshimiwa Spika tunawashukuru sana meza yote inayofanya kazi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kwa upande wetu sisi nawashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, hasa Mwanasheria Mkuu mwenyewe, ni kipindi kifupi amefika, lakini sisi ni mashahidi ameonesha jinsi gani yupo committed na shughuli hii, amejifunza kwa haraka na tupo naye sambamba, namshukuru sana. Naishukuru sana ofisi yake ambayo kwa kweli inaratibu shughuli nzima za Utungaji wa Sheria na Uandishi, vijana wake wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichangie katika maeneo yafuatayo ya hizi dosari ambazo zinakosa uhalisia. Sisi tumepitia dosari mbalimbali zinazokosa uhalisia. Kwa mfano, kwenye Tangazo la Serikali Namba 96, Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Halmashauri ya Wilaya ya Magu imetunga Sheria, imetunga Kanuni ya kuzuia watu kulima kwenye miteremko. Kanuni ile ukiiangalia inakosa uhalisia, unamzuiaje mtu kulima katika maeneo yenye miteremko. Sisi wote tumesoma hapa kuna kilimo cha tambarare, kuna kilimo cha miteremko na kuna vilimo vya aina mbalimbali, kwa hiyo Sheria hii imetungwa kuwazuia wananchi kustawi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitarajia Sheria hii itoe mbadala kama unamzuia mtu asilime kwenye mteremko alime nini endapo yeye anaishi kwenye miteremko? Jambo lipo wazi, lipo wazi na tumejifunza wengine tumesoma shule za kilimo, tunajua ukiwa kwenye miteremko unatakiwa ulime kilimo cha aina gani. Sheria za namna hii kwa kweli zinawarudisha nyuma wananchi na zinawaongezea katika umaskini. Ni matarajio yangu kwamba Sheria hii maadamu ni moja mapendekezo yetu Halmashauri ya Wilaya ya Magu wataifanyia marekebisho haraka ili tarehe 27 mwezi Septemba iletwe na marekebisho haya tunayozungumza yawe yamefanyika na kuwasaidia wananchi wetu kustawi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, dosari nyingine ipo kwenye Tangazo la Serikali Namba 219, Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga. Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga wameleta Kanuni, Kanuni ya kwanza ambayo inawataka wenye vyombo vya usafiri wa umma kusimama kwenye vituo vilivyowekwa isiwe zaidi ya dakika tano. Sheria hii ina ukakasi, mtu unaambiwa usiongeze zaidi ya dakika tano, sasa sheria haisemi ninapopata dharura je, siwezi kuongeza zaidi ya dakika tano? Maana yake wote wanawachukulia kwamba ninyi ni wakosaji, kwa hiyo hata gari kama limesimama zaidi ya dakika tano, lakini lina uharibifu au lina changamoto basi wewe unachukuliwa kama ni mkosaji. Kwa kweli Sheria hii tumeigundua kabisa kwamba haina uhalisia na utekelezaji wake na ni kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwamba Halmashauri hii ya Mafinga imetengeneza Kanuni ambazo endapo mtu atapaki kwenye maeneo yasiyoruhusiwa basi Halmashauri ya Mafinga ina uwezo wa kuja kukichukua chombo chako na kukipeleka kule kunakotakiwa kwenda kuhifadhiwa kwa gharama zako. Jambo ambalo Sheria hii inaonyesha mapungufu, kama watachukua chombo chako hicho na wakakiharibu wakati wa kukichukua sheria hii haisemi kwamba wao wapo liable kulipa hiyo gari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka sheria ambazo zisiwe za kimabavu, umekuta chombo nimeweka wrong parking sawa, umekichukua, hakikisha unakichukua kwa utaratibu na ukikiharibu wewe ukigharamie uharibifu ule. Sheria hii tumeiona kwamba ina mapungufu na tunaipenda ndugu zetu wa Mafinga waifanyie marekebisho ili kama kuna uharibifu utakaojitokeza basi Halmashauri ya Mafinga iwajibike na uharibifu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria tangazo la Serikali Namba 217 ambalo wenzangu pia wamelielezea kwa sababu mimi natokea Mtwara, nina interest na hii Namba 217 inayohusu ushuru wa uvuvi, ada na muda wa kukusanya ushuru. Ushuru huu najua Halmashauri hii ya Manispaa ya Mtwara inajaribu kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato lakini wamekwenda kwa kweli katika maeneo ambayo watatengeneza kero zaidi kwa watu wetu. Wanakwenda kumchaji mtu ambaye anapaa samaki, ndugu zangu kwa ninyi ambao hamjui kupaa ni wale wanaosafisha samaki! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli tumefikia hatua leo tunakwenda kuwachaji ushuru watu wanaopaa samaki, unategemea kupata shilingi ngapi. Wameandika hapa mpaa samaki anatakiwa alipe shilingi 200, mwenye boti analipa ushuru, wavuvi wanalipa ushuru, kwenye mnada pale wanalipa ushuru, mtu ukichukuwa wale samaki ukianza kuwapaa wanakwambia ulipe ushuru, sasa hii tena imekuwa too much, hii Hapana! Hii tunawatengenezea kero. Hawa vijana, vijana wetu wameamua kujiajiri badala ya kwenda kukabana wanafanya hizi shughuli ndogo ndogo. Hebu tuwaache vijana wetu wahangaike na hizi shughuli ndogondogo ili waweze kujipatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hawapati zaidi ya shilingi 1,000, kwa hiyo nasema Halmashauri huu ushuru najua mna shida sana ya mapato, lakini kwa vijana hawa kwa kweli imefika muwaachie ili waweze kufanya shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni muda wa kukusanya ushuru, huu muda waliouweka kutoka saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni, kwa hiyo baada ya saa 12 wale wote watakaotumia muda kwa sababu wameshajua kwamba halmashauri hii muda wa kukusanya ushuru kisheria ni saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni, baada ya hapo hautokusanywa ushuru, kwa hiyo kuna watu wanaweza wakatumia nafasi hii kukwepa ushuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi miji yetu inafanya kazi masaa 24, vyombo vya usafiri vinasafiri masaa 24, kwa nini wanaji-limit wao kufanya kazi muda huu, huu muda mwingine wanalala wanamwachia nani? Halmashauri iweke utaratibu wa overtime baadhi ya watumishi wa muda wa kazi wafanye ili waweze kukusanya mapato 24 hours. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mchango wangu hizi dosari ndogo ndogo ambazo zimejionesha zikimalizika nina imani kwamba wananchi wetu tutakuwa tunawapunguzia kero na wanaweza wakafanya shughuli zao kwa amani. Ahsante sana. (Makofi)