Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

Hon. Ally Mohamed Kassinge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja ya Kamati yetu ya Sheria Ndogo na nianze moja kwa moja kwa kuunga mkono hoja ya Kamati kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uchambuzi wa Sheria Ndogo mbalimbali zilizowasilishwa mbele ya Kamati yetu, lakini pia kupitia Maazimio ya Mkutano wa Bunge wa Kumi na Nne, baadhi ya mapungufu ambayo tumeyabaini sisi katika Kamati pamoja na mengine ni pamoja na uandishi wa Kanuni usiozingatia taratibu za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa niseme tu kwamba sheria ni eneo la kiweledi, kanuni ni zao la sheria, hivyo basi kanuni hizi au sheria ndogo hizi zikiwemo rules, bylaws na zinginezo zisipoandikwa kwa mujibu wa taratibu na matakwa ya kisheria zinapunguza ubora wake, zinapunguza ufasaha wa kueleweka lakini pia zinaleta mkanganyiko katika utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitatoa baadhi tu ya mifano ambayo kwenye Kamati tumebaini ambayo kimsingi imekiuka taratibu za uandishi wa kisheria. Kwa mfano, Wizara ya Fedha, ina sheria yake ya The Accountants and Auditors Registration Act, Cap. 286 ambayo imetungiwa kanuni kwa Tangazo la Serikali Na.1 la tarehe 5 Januari, 2024 inayojulikana kama Rules and The Accountants and Auditors Appeals Board 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya kanuni hii ni kwamba Form A katika Jedwali la kwanza ambayo inahusu notice ya kusudio la kukata rufaa imekuwa na changamoto ya kiuandishi kwa kurejea kuanzishwa kwake, imerejea Kanuni ya 8(2)(a) badala ya Kanuni ya 7 kama ambavyo ndivyo ipo kwenye kanuni husika. Mkanganyiko kama huu, tafsiri ya kisheria maana yake ni kwamba tumetunga kanuni ambayo haiendi kutekelezeka kwa sababu kifungu hicho hakipo kwenye kanuni iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika Wizara ya Uchukuzi, ina sheria yake ya Civil Aviation Act, Cap. 80 ambayo na yenyewe imetungiwa kanuni kwa Tangazo la Serikali Na.5 la tarehe 5 Januari, 2024 ambayo ni Regulation under the Civil Aviation Certification, Licensing and Registration of Air Drones 2024. Changamoto ya uandishi wa Kikanuni katika kanuni hii tunaibaini katika Kanuni ya 64(3) ambayo inamtaka mhusika aliyepewa notice ya kusitishwa cheti, leseni au usajili kuwasilisha utetezi wake kwa mamlaka ndani ya siku 14, lakini imefanya makosa kwa kurejea kanuni ndogo ya (2) ambayo haipo katika kanuni iliyotungwa. Hii kadhalika inafanana na kanuni ile ya mwanzo ambayo nimeitolea mfano. Tafsiri yake ni kwamba kanuni hii haitaenda kutekelezeka kwa sababu wamerejea kifungu ambacho hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni hizi ambazo zimebainishwa na Kamati yetu ambazo zina mapungufu ya uandishi wa kikanuni au wa kisheria ni nyingi; lakini nimalizie na Sheria Ndogo ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifugo ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya Mwaka 2024 ambayo imetungwa kwa Tangazo la Serikali Namba 38 la tarehe 19 Januari, 2024. Katika sheria ndogo hii Kifungu cha 3 kimeweka tafsiri ya neno Mkurugenzi, lakini katika ufafanuzi wa tafsiri ya Mkurugenzi sheria ndogo hii imetafsiri Mkurugenzi kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Moshi, kule ndani unapochimba katika kanuni. Kule juu katika tafsiri sheria au kanuni au sheria ndogo hii imetafsiri Mkurugenzi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kanuni hiyo hiyo moja au sheria ndogo hiyo hiyo moja juu kule unapotafsiri Mkurugenzi unatafsiri kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, lakini ndani kule unapokuja kumtaja Mkurugenzi kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Moshi, hii kisheria maana yake ni kwamba haitaweza kutekelezeka kwa sababu kuna legal technicality ndani yake. Hivyo, basi kwa sababu madhumuni ya kanuni hizi ni kwenda kutekelezwa na kuleta tija kwa jamii yetu, tutoe rai sisi kama Kamati, kwamba mapungufu haya ya uandishi wa kikanuni ni vizuri Wizara husika ziende kuyarekebisha ili kanuni hizi ziendane na matakwa ya uandishi wa kisheria, lakini pia ziweze kutekelezwa bila kuathiri taratibu za mkanganyiko katika kutafsiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)