Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Mwenyekiti wetu kwa kuwasilisha taarifa hii ya Kamati ya Sheria Ndogo, lakini pia niwapongeze Kamati ya Sheria Ndogo kwa kufanya kazi nzuri ya uchambuzi wa sheria pamoja na kanuni ili kufanya shughuli za kila siku za taasisi mbalimbali, Wizara na halmashauri ziweze kutekelezeka kwa ufasaha zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia majukumu yake ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika nchi yetu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo tumejiwekea. Tumeona tumepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inasonga mbele. Pia nimpongeze kwa dhati kabisa Mwanasheria Mkuu, amekuwa msaada mkubwa katika usimamizi na uchambuzi wa sheria hizi na kuharakisha michakato mbalimbali na kufanya sheria hizi ndogo ambazo zinatungwa na kanuni kuelekea katika utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejifunza mengi katika Kamati hii ya Sheria Ndogo na nimeona kwamba mambo yote ya utekelezaji tunayokwenda nayo kila siku ni lazima yazingatie sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo tumejiwekea ili kuharakisha maendeleo, lakini kuleta ustawi wa wananchi wetu, pia kuongeza ajira katika sekta binafsi pamoja na mambo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo halmashauri ambazo zilileta sheria ndogo na tumezipitia na tumeona kuna changamoto mbalimbali. Wasijisikie vibaya ndugu zetu wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara kwa sababu sheria yao tayari ilikuja kwetu na tumeipitia tumeona mapungufu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Sheria Ndogo ya Kilimo na Usalama wa Chakula wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Sheria ya Tangazo la Serikali Namba 219 ukiangalia Kifungu cha 15 kinaweka utaratibu wa namna ya kushughulikia mifugo inayotembea kiholela. Tatizo ambalo tumeliona kimakosa ni utoshelevu wa masharti yanayohusu namna ya kushughulikia hiyo mifugo, maana baada ya mifugo hiyo kushikwa kinachoendelea hapo hakijasemwa na kinaleta utata kwa mwenye mifugo yake ambayo imekamatwa. Kwa sababu halmashauri wanapokamata mifugo na kuweka katika eneo ambalo wanaweka na kumpa mwenye mifugo yake labda siku saba aende akalipe faini, maana yake ni kwamba mfugo ule hakuna mtu anayeutunza kwa kumpa malisho ya chakula, maji pamoja na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inapotokea kukosekana kwa haki ya mwenye mfugo unaokamatwa baada ya mfugo wake kufa anakosa haki kwa sababu sheria haijakaa vizuri. Kwa hiyo, ndugu zetu wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara waendelee kujipanga vizuri kuhakikisha kwamba sheria hii inakuwa wazi na inaweka kipengele hicho wazi kuhakikisha kwamba kila mmoja anakuwa haki; na mwenye mifugo yake pale inapotokea mfugo wake unakufa, basi aweze kupata haki yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona pia mambo mengine katika uandaaji wa majedwali yetu haya. Tunajua kwamba kuna utaratibu wa kisheria wa uandaaji wa majedwali, lakini inapotokea kuwepo kwa typing error, neno tu likibadilika tafsiri yake kwenye utekelezaji wake inaleta shida na inakuwa ngumu sana. Kwa hiyo, niombe waandaaji wa majedwali haya wazingatie tafsiri ya maneno inayoendana na utekelezaji wa jambo lile husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba tumefanya kazi kubwa kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba tunalisaidia Bunge letu kuweka sheria hizi ndogo ziweze kwenda kwenye utekelezaji vizuri na kuendelea kuleta ustawi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)