Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu Benki ya Wananchi wa Mufindi (MUCOBA) kuchukuliwa fedha zake shilingi milioni 681 na TRA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango huu wa maandishi naomba Waheshimiwa Mawaziri warejee mchango wangu kuhusu Benki ya Wananchi Mufindi (Mufindi Community Bank-MUCOBA).
Mheshimiwa Spika, benki hii ni benki ya kwanza ya wananchi hapa nchini, kama nilivyoeleza katika mchango wangu. Benki hii ilipitia kipindi kigumu sana kiasi kwamba BOT ilitishia kuifunga kama ilivyotokea katika baadhi ya Benki za Wananchi. Benki hii ni mkombozi wa wananchi wa Mufindi hasa katika mikopo ya masharti nafuu. Benki hii imesaidia kwa miaka mingi kuchangia uchumi wa wananchi wa Mufindi kuanzia kutoa ajira na kutoa support kwa wafanyabiashara wadogo hususani wafanyabiashara wa sekta ya mazao ya misitu, vikundi vya wajasiriamali vya vijana na wanawake. Ni benki ambayo ni mkombozi wa wananchi wa Mufindi na Iringa kwa sababu benki ilijitanua mpaka kufungua Tawi Iringa Mjini, Ilula na kufungua Ofisi za Mawakala katika maeneo ya Igowole mpaka Madibira ambako ni Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. MUCOBA ni nembo ya Mufindi.
Mheshimiwa Spika, ilikuwa ni matarajio yetu wana Mufindi kuona kuwa baada ya kupitia kipindi kigumu hata kufikia Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ kuongeza mtaji, Serikali ingekuwa mlezi mwema wa kuhakikisha kuwa benki inastawi na kushamiri kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi. Kiuwekezaji benki hii imesaidia wawekezaji wengi wa ndani ya Mkoa wa Iringa kwa kuwapa mikopo na huduma mbalimbali za kifedha. Katika nyakati ambazo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuunda Wizara ya Mipango na Uwekezaji, ni matarajio yetu Wana-Mufindi kuwa uwekezaji wa taasisi local za wananchi unapaswa kulindwa na kulelewa ipasavyo. Huu ni mfano halisi wa local content katika sekta ya kibenki. Benki hii ni mfano wa nguvu ya wananchi siyo tu kushiriki bali kumiliki uchumi wao.
Mheshimiwa Spika, haikuwa kazi rahisi kwa benki hii kusimama tulifanya jitihada kubwa sana na vikao visivyokuwa na hesabu mpaka kufikia hatua ya wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukubali Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ kuingiza mtaji wake. Tulikaa vikao vya kutosha kati yetu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, sisi tukiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mufindi Mzee Yassin Daud ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Mzee Mizengo Pinda - Waziri Mkuu Mstaafu akiwa wakati huo mlezi wa CCM wa Mkoa wa Iringa alishirikiana nasi katika kuhakikisha kuwa benki hii inajikwamua kutoka hatari ya kufungwa na BOT.
Mheshimiwa Spika, vikao hivyo na majadiliano ya mara kwa mara na Maafisa wa BOT ambao walifikia hatua ya kuweka afisa mahususi kushirikiana na benki isifilisike, vilizaa matunda kwa Benki ya Watu wa Zanzibar kuona potential iliyopo ndani ya MUCOBA na kuamua kuongeza mtaji.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo hatua za TRA kuchukua fedha kiasi cha shilingi milioni 681 kwa nguvu imeturudisha nyuma sana kama benki na kama wananchi wa Mufindi na kwa ufupi, pamoja na kuwa mimi siyo mchumi, inashangaza benki ambayo inasuasua kiuchumi, haitengenezi faida, inawezaje kuwa na malimbikizo ya kodi ya shilingi milioni 681?
Mheshimiwa Spika, shida ilianza pale ambapo TRA ilipokadiria kodi kama vile hii ni benki kubwa za kiwango cha NMB au CRDB, hii ni benki ndogo isiyozidi mtaji wa shilingi tano, matokeo yake PBZ wameondoa fedha zao na sasa benki inakaribia kushindwa kufikisha ile minimum requirement ya BOT, hili jambo limewashangaza hata wenzetu wa PBZ kwamba wao wameweka fedha kama mtaji, sisi (TRA) tunatoa fedha za mtaji shilingi milioni 681.
Mheshimiwa Spika, athari za hatua hii ni kuwarejesha wananchi kwenye mikopo tunayoita kausha damu, yawezekana siyo wote wanapata mikopo MUCOBA, lakini hata hao waliokuwa wanapata hivi sasa hawapati, hakuna gawio kwa wanahisa, lakini zaidi ya yote linafifisha jitihada za benki kuendelea kupanua wigo wa kukua, mwisho PBZ imeamua kuondoa mtaji wake na matokeo yake hata kisiasa hili suala litaathiri sana Chama Cha Mapinduzi kwa sababu hii ni benki ya wananchi ambayo sehemu ya mtaji wake ulitoka kwa wananchi kupitia michango yao ya kukatwa kiasi fulani cha fedha kupitia IMUCU na pia halmashauri zote mbili za Mufindi na Mafinga ni wanahisa na wananchi walinunua hisa.
Mheshimiwa Spika, je, hatuoni kuwa tunatengeneza chuki kwa Serikali? Sina maana kwamba sheria zisifuatwe, hapana, naomba tuangalie kiasi hiko cha shilingi milioni 681, ni kiwango sahihi, je, tunaenda nyuma au tunaenda mbele?
Mheshimiwa Spika, kwangu mimi na kwa wananchi wa Mufindi na Iringa kwa ujumla tunawarudisha nyuma kijamii, kiuchumi hata kisiasa wanakuwa na hasira na Serikali. Haiwezekani wananchi hawapati gawio, hawapati mikopo, utarajie wawe na furaha. Tutafakari suala hili kwa umakini na hekima ya Mungu ituongoze.
Mheshimiwa Spika, ushauri/ombi, ninashauri Serikali kwa maana ya Wizara, BOT na TRA kuona uhalali wa jambo hili na kulitafakari upya sio tu kwa mustakabali wa MUCOBA, bali sekta nzima ya benki. Nasema hivi kwa sababu sisi Mufindi tumekuwa shule kwa benki nyingine zote za wananchi (community banks).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili lilikuwa bado katika majadiliano, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mamlaka aliyonayo, aamuru TRA irejeshe fedha hizo ili benki iendelee kuzungusha mpaka hapo mwafaka utakapofikia, kwangu mimi ni ubabe kwa Serikali/TRA kuchukua fedha katika jambo ambalo liko kwenye majadiliano.
Mheshimiwa Spika, ninaamini Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake wa Wizara, BOT na TRA mtaona kilio hiki cha Wana-Mufindi na kama kuna mapungufu yoyote ninyi kama walezi mnaweza kuona namna njema ya kulifanyia kazi suala hili kuliko hali ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28, Mji wa Mafinga ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo ndani ya Serikali ilikubalika kuwa kwa kuwa fedha za mkopo nafuu kutoka India USD milioni 500 hazitaweza ku-cover miji yote 28 iliamriwa kuwa miji minne ikiwemo Mafinga itagharamiwa kwa fedha za ndani, lakini kwa nia njema ibaki ikitambulika kuwa ni mradi wa miji 28. Mradi huu sisi Wabunge na viongozi wa chama kutoka maeneo ambayo ni wanufaika wa mradi tulialikwa kwenye signing ceremonies pale Ikulu mbele ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Juni, 2022.
Mheshimiwa Spika, Jandu Plumbers ni kampuni inayotekeleza mradi huu, hata hivyo ikiwa imebaki miezi minne muda wa miezi 20 ukamilike mradi umefikia only 22%, shida kubwa ni fedha, mpaka sasa mkandarasi ametoa certificates nne hajalipwa, matokeo yake amewaondoa wafanyakazi site. Ninawaomba sana kama sehemu ya kumheshimisha Mheshimiwa Rais tutoe fedha ili mradi huu ukamilike, shida kubwa ni fedha, isije ikaonekana sisi ambao mradi unatekelezwa kwa fedha za ndani ni kama tumefanya dhambi maana miji 28 mambo yanaenda vizuri, najua hali ya fedha ilivyo kutokana na miradi mikubwa, hata hivyo ninaomba mtuangalie Mafinga kwa macho mawili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Mafinga - Mgololo kwa Mfumo wa EPC+F, suala hili limeleta mkanganyiko sana ndani ya Bunge na ndani ya nchi, siyo tu kwa sababu ya mfumo wenyewe, bali kutokana na shauku ya uhitaji wa kuwa na barabara kwa ajili ya kuchochea shughuli za uzalishaji na uchumi kwa ujumla. Barabara ya Mafinga - Mgololo ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa mazao ya misitu, mazao ya chai, mazao ya chakula na shughuli nyingine za kiuchumi. Ni catalyst kwa uchumi wa Mufindi, Iringa na Taifa zima.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, nawaomba Serikali kwa namna yoyote itakayofaa, ujenzi uanze katika Barabara ya Mafinga - Mgololo na nina hakika takwimu ziko wazi hasa katika suala zima la mchango wa Mufindi katika pato la Taifa. Takwimu za TRA za larger taxpayers mtaona, hoja yangu.
Mheshimiwa Spika, kujengwa kwa barabara hii kutasaidia na kupanua wigo wa mchango wa Mufindi katika pato la Taifa, nawaomba sana fursa hii isipotee ili Mufindi tuendelee kuwa na mchango madhubuti katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.