Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, kipekee nipongeze juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mipango na mikakati mizuri ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote. Mheshimiwa Rais halali usiku wala mchana kwa ajili ya Watanzania, hongera sana Mheshimiwa Rais, tunakupenda, tunakujali na tutaendelea kukujali na tunasema piga kazi mama, tupo nyuma yako mpaka kieleweke na katu haturudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wote waliowasilisha, Naibu Mawaziri na watendaji wote kwa kazi wanazozifanya kwa kuandaa hotuba hizi na kuwasilishwa kwetu kupitia Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naanza na suala la kodi ambapo hotuba imeeleza mabadiliko ya sheria kwa wafanyabiashara wanaokwepa kutoa risiti. Nataka niseme ni kweli kwamba baadhi ya wafanyabiashara pamoja na kwamba Serikali imeweka msisitizo kuhusu matumizi ya EFD wanapouza na kudai risiti pale mtu anaponunua. Hii imechukuliwa tofauti na baadhi ya wafanyabiashara kwa kuleta visingizio vya kuharibika kwa mashine au biashara mpya hawajapata, hawajapata mashine na haya yote ni kuwepa kodi. Isitoshe wafanyabiashara wamekuwa na malalamiko makubwa kuhusu utarabu uliowekwa kisheria kwamba unamuumiza sana mfanyabiashara hasa mdogo na kusema kwamba hili la sasa linaweza likachangia rushwa kwa kiwango kikubwa kwa wafuatiliaji wa makusanyo ya kodi.

Mheshimiwa Spika, kwa nini kabla ya matumizi ya sheria hii Serikali iamue kukutana na wafanyabiashara wote kulingana na maeneo wanayofanyia biashara zao ili kuondoa mkanganyiko wa malalamiko kwa wafanyabiashara kwamba kumekuwa na utitiri wa kodi ambao unaendelea kukwamisha mwenendo wa ukuaji wa biashara zao.

Mheshimiwa Spika, moja, kodi ya jumla wakati mzigo unapoingia nchini na pili, mfanyabishara anapouza likitokea kosa kwa mnunuzi kwa kusahau TIN adhabu inarudi kwa muuzaji na kutakiwa kulipa fidia na tatu, kodi inayotozwa inaangalia kwenye mtaji zaidi wa mfanyabiashara na siyo faida kama ilivyo taratibu.

Mheshimiwa Spika, ifanyike tathmini ya jumla ya kadirio la kodi kuanzia pale mzigo unapofika na pale unapokuwa dukani na kama mfanyabiashara hakutimiza kodi yake hapo ndio Serikali iweke msisitizo wa sheria aweze kulipa fidia kama hakukamilisha kodi yake na hii iweke ulingahisho kutokana na thamani ya biashara husika ili tusiumize wafanyabiashara wadogo. Hii itawafanya wafanyabiashara kuongeza wigo mpana kukamilisha kodi yake ambapo nusu ya kodi ameshalipia mapema.

Mheshimiwa Spika, kuwepo na sheria kwa kufanya ufuatiliaji madhubuti kwa wale wote wanaopita kukusanya kodi kwa wafanyabiashara kwani wengi wao wamejilimbikizia mali na majumba ya kifahari. Ufuatiliaji uanzie mwanzo anapoanza kazi hii ya ufatiliaji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine linahusu Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu TANAPA na NCAA kuhusu sheria inayowataka makusanyo ya kodi yabaki na kuwawezesha kutumia katika miradi ya maendeleo. Katika hotuba ya Wizara haionekani wazi mabadiliko ya sheria hiyo ambapo wataweza kukusanya na kutumia fedha kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi niunge mkono hoja na kuwataka wananchi waone na kuzingatia umuhimu wa kulipa kodi. Lipa kodi kwa maendeleo ya Taifa. Niwaambie wananchi tu kwamba bila kulipa kodi mipango ya Serikali kuhusu huduma za wananchi haiwezi kufikiwa.