Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi na mimi nichukue fursa hii kwanza kabisa kuwapongeza sana watoa hoja kwa hoja zao mbili ambazo kwa kiwango kikubwa zimegusa maisha ya Watanzania na hasa kwenye sekta ya madini. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali ambayo wameitoa ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kati ya maeneo ambayo yamesemwa sana ni kuhusu madini mkakati na kila Mbunge ameonesha ya kwamba lazima Serikali ichukue hatua kuyalinda madini haya, lakini vilevile na nchi yetu iweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, tunayo maelezo mahususi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba tunatengeneza mkakati wa namna ya kushughulika na madini mkakati. Katika eneo hili, katika mkakati wetu, moja ya eneo kubwa ambalo tumelipa kipaumbele ni uongezaji wa thamani wa madini mkakati hapa nchini ili kuongeza ajira kwa Watanzania na vilevile kuongeza mapato kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mkakati wetu huu, moja ya jambo ambalo pia nilisema hapa Bungeni wakati wa bajeti yangu ni kwamba tumedhamiria, hivi sasa hatutatoa tena leseni kubwa ya uchimbaji mpaka yule mwombaji atakapotudhihirishia kwa ushahidi kwamba atafanya investment kubwa katika kuongeza thamani madini mkakati ili nchi yetu iweze kunufaika na madini haya. Huo ndiyo mkakati wetu kuhakikisha kwamba nchi yetu inanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mahitaji ya madini mkakati duniani ni tani milioni kumi, inategemewa ifikapo mwaka 2050 mahitaji haya yatafika mpaka tani milioni 150, kama nchi tumejipanga kuhakikisha kwamba tunanufaika na rasilimali hii.
Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ambao tunao hivi sasa katika eneo letu la Buzwagi ambalo lilikuwa ni Mgodi wa Buzwagi ambao unafungwa hivi sasa, pale tumelitenga kuwa ni Special Economic Zone ambapo tuna ekari 1331 na tumeanza kutoa leseni kwa viwanda vya kuongeza thamani.

Mheshimiwa Spika, tunayo Kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited ambao wao wanafanya investment pale ya dola milioni 500 kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kusafisha madini na leseni imekwisha kutoka, muda wowote wataanza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo limesemwa sana hapa ni eneo la utafiti wa kina, ni kweli nchi yetu ya Tanzania eneo ambalo linafanyiwa utafiti wa kina katika utafutaji wa madini ni 16% tu na tumebaki na eneo kubwa ambalo halijafanyiwa kazi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, katika bajeti yetu ya Wizara ya Madini tumeongezewa fedha mpaka kufikia shilingi bilioni 231 na moja kati ya mkakati wetu katika eneo hili ni kuhakikisha kwamba tunaongeza eneo la utafiti wa kina zaidi ili nchi yetu iweze kunufaika na pia tuwaongoze vizuri wachimbaji wadogo ambao wanachimba kwa kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika fedha hizi pia tutanunua helikopta ambayo tutaifunga vifaa maalumu kwa ajili ya kufanya utafiti nchi nzima ili tuweze kubaini eneo kubwa zaidi lenye madini na kuwaongoza vizuri Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuna mradi ambao ni wa Serikali ya Hispania ambao tunategemea katika mradi huu zaidi ya eneo la square kilometre 165,724 litafanyiwa utafiti wa kina na hivyo kuongeza eneo kubwa zaidi ambalo tutakuwa tumelifanyia utafiti wa kina na kufikia 18%. Hivyo, ukijumlisha 18% na 16% mpaka mwakani tutakuwa tumeshafikia eneo la zaidi ya 34% ya nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, haya yatakuwa ni maeneo mazuri ya kuongoza vizuri wachimbaji wadogo, ili mwisho wa siku wasiendelee kuchimba kwa kubahatisha na mradi huo tunategemea kuuanza Mwezi wa Saba mapema kabisa katika mwaka wa fedha unaokuja. La mwisho ni, imezungumzwa hoja ya kuwawezesha Watanzania, kwa ajili ya kununua madini, hasa ya dhahabu kwa sababu, Watanzania wengi mitaji yao mingi inatoka nje ya nchi na hivyo, kusababisha madini mengi kuuzwa nje ya nchi kwa sababu wanao watu waliowapatia fedha awali.

Mheshimiwa Spika, katika kuisaidia Benki yetu Kuu kupata madini ya dhahabu tumekaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha tumekubaliana. Pale Wizara ya Fedha wana kitu wanakiita Export Credit Guarantee Scheme ambapo hivi sasa tutawawezesha wachimbaji wetu wadogo na wafanyabiashara wa madini waweze kupatiwa mikopo, ili waifanye biashara hii ndani ya nchi tuweze kutunza shilingi yetu na vilevile tupate fedha ambayo itatusaidia kuendesha shughuli mbalimbali na hasa wachimbaji wadogo ambao wanamchango mkubwa sana katika uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ambalo limezungumzwa hapa ni namna ya kuiboresha Tume yetu ya Madini kuendelea kukusanya maduhuli ya kutosha, ili yatoe mchango mkubwa katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)