Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe pamoja na Wasaidizi wako kwa maana ya Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mussa Zungu na Wenyeviti wa Bunge hili kwa jinsi ambavyo mmeweza kuendesha mjadala huu kwa umakini, umahiri na uwazi wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya lakini kwa mimi binafsi nimshukuru sana kwa sababu amenipa heshima kubwa ya kuongoza Ofisi yake inayoshughulikiwa Mipango na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika historia ya nchi yetu hii ni mara ya tano nchi yetu kuwa na Wizara ya Mpango kamili. Tulianza mwaka 1965 mpaka 1975 tukawa na Wizara ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo, tukaendelea katikati ikachanganywa. Tukarudi tena mwaka 1980, Wizara ya Mipango na Uchumi, Ofisi ya Rais Mpango na Ubinafsishaji, Mipango na Uchumi tena na imerudi tena mara hii Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kunipa fursa hiyo na amenipa fursa na heshima ya kuingia katika historia ya kusimamia zoezi muhimu la kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya nchi hii, nikiwa Waziri wa pili tu katika historia ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru tena Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya uongozi makini sana wa Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kwa uchambuzi wao makini, maoni na ushauri waliotoa. Nawashukuru siyo tu kwa utaratibu na utamaduni wa Kibunge uliozoeleka wa kushukuriana na kupongezana kama njia ya kutiana moyo. Ukweli ni kwamba nimesoma kurasa zote 82 za Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Tathmini ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2023; Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024; Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024; pamoja na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2024/2025. Kamati imeitendea haki sana Taarifa hii, uchambuzi wao ni wa kiwango cha juu sana cha weledi na maoni na ushauri wao waliotoa ni wa kizalendo sana. Tunawashukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia; jumla ya Wabunge 137 ambao wamechangia moja kwa moja kwa kuongea, tumepokea maoni na ushauri wao. Aidha, tumepokea changamoto ambazo wamezitoa na tunaendelea kuzifanyia kazi. Sisi kama binadamu, kama Viongozi na kama Taasisi siku zote nafasi ya kuboresha na kuwa bora zaidi leo kuliko jana ipo na tunaamini kwamba michango ambayo wametoa itatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nijielekeze sasa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo walizitoa. Kwa ujumla wake katika michango yao kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Wwaka 2024/2025, Waheshimiwa Wabunge, wametoa maoni na ushauri katika maeneo mengi. Naomba nijielekeze katika maeneo mahususi saba na baadaye nitatoa pia maelezo kidogo kwenye maeneo ya jumla matatu hivi.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza, ni kuhusu vipaumbele vya kuzingatia katika mipango yetu ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ikiwemo Dira yetu ya Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wamependekeza maeneo kadhaa ya kuzingatia na wamesisitiza tuweke mkazo katika maeneo ambayo yatasukuma ukuaji wa uchumi kuelekea asilimia nane ambayo ndiyo lengo ambalo lipo katika Mpango wetu wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, wameweka mkazo katika maeneo ya kipaumbele muhimu kama elimu na mafunzo, kilimo, nishati, madini, sayansi, teknolojia, utafiti na maendeleo na maeneo mengine. Nisisitize kama nilivyosema katika hotuba yangu kwamba kipaumbele kikubwa cha Serikali ni kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi ili uchumi huo uweze kupunguza umaskini na kuwezesha watu wetu kuzalisha mali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tufike katika katika eneo hili lazima tujielekeze katika sekta ambazo zinabeba watu walio wengi. Sekta hizi ukiangalia grafu ambayo tuliitoa ni muhimu tujielekeze katika sekta nne muhimu sana. Sekta ya kwanza, sekta ya kilimo, kwa sababu inabeba 65% ya watu wetu na inachukua zaidi ya robo ya Pato letu la Taifa. Kwa sasa kilimo chetu kinakuwa kwa 4.2%, lengo la Serikali ni kuona kwamba ifikapo mwaka 2010 sekta hii ikuwe angalau kwa 10% hili ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ni eneo la viwanda, viwanda ndio vinatarajiwa kuzalisha ajira kwa wingi. Kwa sasa viwanda vinakuwa na sekta hii inakuwa kwa 4.3%. Lengo la Serikali ni kuona kwamba ikue angalau ifike asilimia saba mpaka asilimia nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, muhimu ni biashara, biashara pia inabeba watu wengi na ni eneo ambalo ni muhimu sana katika kuzalisha ajira. Hili na lenyewe linakuwa kwa asilimia 4.2, lakini lengo la Serikali na lenyewe likue lielekee asilimia saba mpaka nane.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho, ni usafirishaji, ni eneo muhimu sana takwimu zinaonesha kwamba linakuwa kwa 4.1% na lenyewe lazima tulisukume liende kwenye asilimia sita mpaka nane.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya ni maeneo ambayo Serikali inayawekeza ili tuone kwamba yakue kwa kiwango angalau kisichopungua asilimia sita mpaka nane na kwa mtindo huo tunaweza tukasogeza uchumi wetu ukuwe mpaka asilimia nane ambayo ipo katika Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelitolea maoni ni haja ya kuimarisha mfumo wa usimamizi wa Mipango ya Maendeleo na hapa tumeeleza Waheshimiwa Wabunge wengi wameunga mkono. Tunakubaliana na maoni yao kwamba tupunguze muda ule wa kutoa taarifa ya Kitaifa badala ya mwaka mmoja iwe ni miezi sita walitoa maoni haya. Kwa hivyo, itasomeka kwamba Waziri atapokea taarifa kila wiki; kila mwezi Wizara itawasilisha kwenye Tume ya Mipango na Tume ya Mipango itaanda taarifa ya Kitaifa mara mbili kwa mwaka (miezi sita sita). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, ilikuwa ni haja ya kufanya tathmini ya rasilimali watu ili kutambua idadi na aina ya watu wanaohitajika katika dunia ya leo. Kama tunavyofahamu kwa mujibu wa Sheria Na. 1 ya Tume ya Mipango ya mwaka 2023 hususani Kifungu 6(2)(a), jukumu la kwanza la Tume ya Mipango ni kutathmini hali ya rasilimali za Taifa na kuishauri Serikali kuhusu matumizi bora ya rasilimali hizo. Kwa kuzingatia jukumu hili katika mpango wake wa kazi wa mwaka ujao wa fedha Tume ya Mipango imejipangia kufanya tafiti kadhaa ikiwemo hii ya kutathmini hali ya rasilimali watu, tukizingatia idadi na aina ya rasilimali ambazo tunazo lakini kuelekeea mbele tunahitaji rasilimali za aina gani katika uchumi wa dunia ya leo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ameeleza hapa kwamba tayari Serikali imeshafanya mapito ya Sera na Mitaala yake ya Elimu. Kwa hivyo, tumeiweka katika kiwango ambacho tunaamini inaenda vizuri na dunia ya leo.

Mheshimiwa Spika, eneo la nne ambalo Waheshimiwa Wabunge walitolea maoni ni haja ya kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini sambamba na kuweka mazingira bora ya kurasmisha sekta isiyo rasmi. Hili ni eneo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamelichangia na tunakubaliana na maoni yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisisitize mambo matatu; La kwanza, tayari pale katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tumeshafungua Kituo cha Kuhudumia Wateja cha Pamoja (One Stop Centre). Kwa hivyo, mwekezaji popote alipo anaingia katika tovuti ya TIC, mule ndani ana uwezo wa kuomba ambacho anahitaji na atapata huduma za taasisi ambazo hazipungi saba kwa kuanzia. Baada ya hapo tunatarajia katika mwaka ujao wa fedha zifike taasisi 14. Kwa hivyo, ukienda pale unapata huduma ya taasisi 14 ikiwemo kusajili kampuni yako. Juzi nimezindua huduma nyingine kwamba unaweza ukafungua mpaka akaunti yako ya fedha pale. Kwa hivyo, hii ni hatua kubwa ambayo wawekezaji wengi sana wameifurahia.

Mheshimiwa Spika, ya pili, tunapoelekea ni kwamba tunataka tozo za mamlaka mbalimbali za uthibiti zilipwe mara moja. Badala ya mwekezaji kuzunguka aende kulipa EWURA, aende kulipa TBS aende kulipa na nyingine. Tunataka mwekezaji alipe tozo mara moja na sisi ndani ya Serikali ndiyo tutakao gawana hela ambayo wamelipa kulikoni mwekezaji kuzunguka leo OSHA, kesho FIRE, kesho EWURA na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, la pili, mwaka huu tunaenda kuweka mfumo wa kutoa cheti kimoja badala ya utitiri wa vyeti. Tunafahamu wote ukiingia kwenye kampuni yoyote ya biashara kwenye ukuta ukiangalia utakutana na vyeti visivyopungua vitano mpaka kumi. Tunataka utaratibu huo tuachane nao, katika ulimwengu wa teknolojia inawezekana ukapata cheti kimoja ambacho ndani yake kuna kila kitu. Hili tunaenda kulifanyia kazi katika mwaka ujao wa fedha katika kurahisisha mazingira ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tano, ni suala la kuweka mkazo katika maendeleo ya vijijini, Waheshimiwa Wabunge walio wengi wameunga mkono lengo la Serikali kuendelea kuweka mkazo katika maendeleo vijijini. Hakuna namna ya kutokomeza umaskini wa watu wetu nje ya kuweka mkazo wa kipekee katika kusimamia maendeleo ya vijijini kama njia sahihi ya kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi na tayari tuna misingi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kupitia TARURA mtandao wa barabara vijijini umeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mfano, kati ya mwaka 2020 na 2024 Serikali kupitia TARURA ilifanikiwa kuongeza kiwango cha barabara cha changarawe kutoka kilometa 24,493 hadi kufikia kilometa 41,107 mwaka 2024 ikiwa ni zaidi ya lengo. Lengo letu lilikuwa ni kupeleka kilometa 35,000 ifikapo mwaka kesho. Tayari tuna mtandao wa barabara kupiti TARURA kilometa 41,107.52. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unafahamu kwenye lengo la kuwezesha watu wetu kupata kipato, kufanya biashara suala barabara vijijini ni muhimu sana. Tukishakuwa na mtandao wa barabara vijijini hii maana yake itasaidia wananchi kuweza kufanya biashara kuweza kusafirisha mazao yao ya mifugo kilimo, uvuvi na kadhalika kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kujipatia kipato. Vilevile, kiwango cha barabara za lami kupitia TARURA kimeongezeka kutoka kilometa 2,205, mwaka 2020 mpaka kilometa 3,224 mwaka 2024 na kwa miradi inayoendelea tunaamini kwamba hatua kubwa zaidi itaongezeka.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, muhimu sana kwa vijijini suala la maji, tumepiga hatua kubwa sana katika eneo hili. Wakati tunaanza utekelezaji wa Dira ya sasa coverage ya maji vijijini ilikuwa 32%. Sasa hivi tunazungumzia 78%, hii ni hatua kubwa sana na ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wetu wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, ambalo tumelisema wote hapa ni suala la umeme, hili tumepiga hatua kubwa zaidi ya 96% ya vijiji vyetu vina umeme. Hii ni hatua kubwa ambayo Serikali imeifanya na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa uongozi wake makini.

Mheshimiwa Spika, bila shaka vilevile mtandao wa barabara kwa ujumla kwa kutumia, kwa mfano, TANROADS umeongezeka sana wakati mwingine tunajisahau. Mwaka 2000 TANROADS mtandao wao wote ilikuwa ni kilometa 4,179, leo tunazungumzia kilometa 11,966. Wakati mwingine takwimu siyo muhimu hali halisi. Wale wanaotoka Singida kama mimi na mikoa mingine ya magharibi wanafahamu walikuwa wakisafiri Mwanza, Shinyanga na Singida; kutoka Singida wakifika Nala ilikuwa gari linasimama ubadilishe nguo ukung’ute vumbi ili kuelekea Dar es Saalam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka kufika pale Nala ilikuwa ni vumbi tupu, hali ilikuwa mbaya, lakini wengi wanafahamu wanakumbuka miaka michache iliyopita kwenda Mwanza ilibidi upitie Nairobi lakini leo mtandao wa barabara kutoka Mtwara mpaka Mwanza ni barabara za lami, kwa hivyo hatua kubwa imepigwa sana katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, eneo la sita ni haja ya kuimarisha mashirika ya umma. Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza na kushauri kuwa Serikali ifanye tathmini ya kina kubaini mashirika ya umma ambayo yanafanya biashara na yaweze kufanya biashara na yatoe mchango kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali kama mnavyofahamu ipo katika hatua za kufanyia maboresho na marekebisho makubwa sana mashirika ya umma ili mashirika haya yaweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi na hususani mashirika yale ambayo wanapaswa kujiendesha kibiashara. Katika sheria ambayo tunaipendekeza ambayo itakuja kusomwa mara ya pili tunasisitiza mambo mengi lakini mambo mawili muhimu.

Mheshimiwa Spika, moja ni kuwa na mfuko wa uwekezaji ili taasisi zetu ambazo zinafanya biashara ziwe na uhakika wa vyanzo vya kuweza kuwekeza. Pili, tunataka mashirika haya yaweze kumilikiwa na wananchi kwa hivyo yajisajili kwenye soko letu la hisa la Dar es Salaam na kwa njia hiyo wananchi wanaweza wakanunua hisa katika mashirika haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la saba ni maandalizi ya Dira mpya ya taifa ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza sana, ushirikishwaji lakini pia kuzingatia vipaumbele ambavyo nimevieleza awali. Niendelee kusisitiza kwamba zoezi hili lina ushirikishwaji wa kutosha na mpaka mwezi Mei zaidi ya watu laki nane walishatoa maoni kwa njia mbalimbali ikiwemo mahojiano katika ngazi ya kaya, wametoa maoni kupitia simu, kupitia tovuti lakini pia kupitia makundi mbalimbali ya kijamii na mahojiano ya viongozi mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo linafurahisha ni kwamba asilimia 80 ya wananchi waliotoa maoni kwa njia ya simu na tovuti ni vijana kati ya miaka 15 na miaka 35. Kwa hiyo vijana wamechangamkia sana eneo hili. Eneo la pili ambalo walisisitiza kwenye upande dira Waheshimiwa Wabunge wameshauri kwamba ni muhimu sana tukajifunza kutoka nchi ambazo zimepiga hatua kimaendeleo(Makofi).

Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa tu kwamba timu yetu kuu ya wataalam imeshabaini angalau nchi kumi ambazo zina mazingira kama ya kwetu ya kihistoria na ambazo zimepiga hatua kubwa ambazo tunaende kujifunza nchini pamoja na India kwa mfano, Indonesia, China, Singapore, Korea Kusini, Vietnam, Botswana, Maurtius, Norway na zingine, kwa hivyo ushauri huu utazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la saba la mwisho katika maoni mahsusi ni eneo la mpango na bajeti. Waheshimiwa Wabunge wamesema kwamba ni muhimu sana mpango uje mapema ili uweze ku-inform bajeti. Maoni haya ni mazuri na yatazingatiwa ni suala pia la kikanuni kwa Mheshimiwa Spika hili pia lipo mezani kwako lakini niseme kwamba kimsingi hivi ndivyo ambavyo imekuwa ikifanyika kwa kiasi kikubwa kwa sababu kama mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge mwaka jana tarehe sita mpaka tarehe kumi Novemba tulikaa hapa Wabunge kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Kitaifa. Kwa hiyo, hili linazingatiwa lakini pia Machi tarehe 11 mwaka huu 2024 nilisoma, nilileta hapa mpango wa maendeleo ya Taifa, kwa hivyo njia hizi zinashirikishwa lakini nadhani fursa na nafasi ya kuboresha ipo, sisi wenyewe Wabunge ndiyo tunatunga kanuni zetu kama tukiamua kubadilisha ni suala la sisi kufanya uamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kufafanua nimalizie kutoa ufafanuzi katika maeneo ya jumla matatu. Eneo la kwanza nataka kusisitiza kwamba pamoja na mambo mengine mpango wa maendeleo ambao niliuwasilisha hapa pamoja na hatua za kikodi ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha alizitangaza, zinalenga katika mambo makubwa matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kuchochea uzalishaji wa bidhaa zitakazoifanya nchi yetu ijitosheleze katika mahitaji ya bidhaa muhimu nchini na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje. Wote tunafahamu kwamba kuna bidhaa ambazo tunazitumia sana ni muhimu katika maisha yetu lakini tunaziagiza kutoka nje na tumekuwa tukipiga kelele hapa. Bidhaa hizi ni pamoja na chakula mfano mafuta ya kula, sukari, ngano, mazao ya chakula, madawa, mavazi na kadhalika. Ni katika msingi huu tutaendelea kulinda uwekezaji unaolenga kuchochea viwanda vinavyozalisha bidhaa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezungumza suala la sukari hapa, kwa upande wa sukari kwa mfano, mahitaji yetu kwa mwaka tunakadiria kuwa takribani tani laki sita elfu Hamsini, mwaka jana kwa kweli kabla ya mvua za El-Nino tulishapiga hatua kubwa, tulienda mpaka tani 460,000 kwa mwaka lakini kutokana na mvua za El-Nino hizi uzalishaji viwandani ukayumba, ukashuka mpaka tani 392,724 lakini tunaamini kwa uwekezaji ambao unaendelea na kama hapatajitokeza tena changamoto za El-Nino tunatarajia ifikapo julai mwaka kesho tufike angalau tani 520,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kwamba ifikapo mwaka 2025/2026 tuzalishe tani 700,000. Kwa hivyo, nisisitize hapa kwamba lengo la Serikali kuendelea kulinda uwekezaji katika viwanda vya sukari lipo pale pale, na tuwaambie wenye viwanda ambao tunafanya nao kazi kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba sekta hii sukari inakua, tufike mahala tujitegemee lakini muhimu zaidi tuweze kuuza sukari nje ya nchi kwa sababu nchi nyingi jirani zetu hawana sukari.

Mheshimiwa Spika, nisisitize Serikali inafanya nini? Tunafanya uwekezaji mkubwa sana katika uendelezaji wa sekta ya uzalishaji wa ndani. Kwa mfano, Serikali imewekeza shilingi bilioni 7.2 kuzalisha mbegu bora za sukari. Serikali imewekeza bilioni 12.5 kwenye miundombinu ya umwagiliaji ya miwa especially kwenye bonde la Kilimanjaro. Sasa hivi tunayo kampuni ya saba kutoka Ethiopia ambayo inafanya visibility study kwenye bonde zima la Kilombero lengo tukuze umwagiliaji katika eneo hilo na hii itakuwa ni hatua kubwa sana kwenye kuongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumegawa kitalu kipya hekta 400 bure za mbegu kwa wakulima ili waweze kulima, kwa hivyo mtu anayesema kwamba hatua zote ambazo tumezichukua hivi karibuni lengo lake ni kukatisha tamaa wawekezaji katika sekta ya sukari hajui alisemalo, Serikali inawekeza sana.

Mheshimiwa Spika, ukiacha yote hayo Serikali imesamehe kodi takribani shilingi bilioni 244 kwenye viwanda hivi ili kuweka mazingira rahisi ya wao kuwekeza. Tungekuwa hatuna nia ya kulinda uwekezaji isingewezekana tusamehe kodi yote hiyo, tufanye uwekezaji wote huo. Kwa hiyo, hili ni jambo la muhimu ambalo nataka tulisisitize kwamba lengo la Serikali lipo pale pale, tujitosheleze kwa malengo katika sekta ya sukari na tuachane na mambo ya sugar gap na sisi tunaamini kwamba kwa jitihada hii ifikapo mwaka kesho suala la sugar gap katika nchi hii litakuwa ni suala la historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo linahusiana na hilo, lazima Serikali ihakikishe pamoja na kwamba tunalinda viwanda na uzalishaji lakini lazima kuhakikisha kwamba bidhaa muhimu zinapatikana nchini muda wote na kwa bei nzuri kwa walaji. Ni katika mazingira haya ilikuwa ni muhimu kwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuchukuwa hatua za dharura katika kuhakikisha kuwa bidhaa muhimu ya sukari inaendelea kupatikana nchi na kwa bei nzuri. Kutokana na mafunzo tuliyoyapata, mafunzo ambayo tumejifunza, kila siku tunajifunza, huko nyuma tuliona kwamba ni muhimu wapewe watu fulani kuagiza sukari ili kuondoa uholela wa soko ndiyo tukawapa wenye viwanda, lakini tumejifunza mwaka jana kwamba hii nayo ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, pale ambapo bidhaa muhimu zinakosekana katika soko atakayelaumiwa kwa vyovyote vile ni Serikali. Kwa hivyo lazima Serikali yoyote makini ichukue hatua za kulinda walaji katika mazingira ya soko huria. Kwa hivyo, hii ni muhimu sana kuizingatia wakati wote. Kwa hiyo, hatua hizi nisisitize tena, hazilengi kudhoofisha uwekezaji katika sekta ya sukari bali Serikali inachukuwa jukumu lake la msingi la kulinda wananchi dhidi ya mabavu ya soko huria. Serikali ni mwekezaji muhimu kama nilivyosema katika sekta ya sukari nchini na isingewezekana ijihujumu yenyewe. Hili ni jambo la muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika viwanda vyote vya sukari nchini unakadiriwa kuwa takriban trilioni 4.2. huu ni uwekezaji mkubwa ambao kama Serikali lazima tuendelee kuulinda. Eneo la tatu ni kuchochea mauzo ya bidhaa ambazo zimeongezewa thamani nje ya nchi. Pili, nizungumzie pia haja ya kuwa na mipango ya muda mrefu na ulinzi dhidi ya maono ya kitaifa. Jambo hili limezungumzwa kwa upana na Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Askofu Gwajima amekuwa akilirejea mara kwa mara ni muhimu sana, ni hoja ya msingi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ipo dhana ambayo kwa kweli imekuwa ikijirudia kwamba nchi yetu na pengine nchi zingine za Kiafrika zinakwama kwa kuwa hatuna maono na mipango ya Taifa ya muda mrefu. Hii ni hoja ambayo imezungumzwa kwa upana. Pamoja na umuhimu wa hoja hii, kwa lengo la kuweka kumbukumbu sahihi, nchi yetu hii ya Tanzania imekuwa na mipango katika historia yake yote. Katika Bunge la kwanza kabisa la wakati huo la Tanganyika na Mkutano wa Tano na Kikao cha Kwanza kilichofanyika tarehe 10 Disemba mwaka 1962, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa ndiyo amechukua Urais wa Jamhuri alikaribishwa kuhutubia Bunge kwa mara ya kwanza kama Rais wa Jamhuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku hiyo pamoja na mambo mengine alitangaza kuanzisha idara mpya akaiita Idara ya Mipango ya Maendeleo, aliiweka chini ya ofisi yake. Jambo hili limekuja kujirudia tena mwaka 2023 pale ambapo Mheshimiwa Rais aliunda Ofisi ya Rais Mpango akaiweka chini ya ofisi yake. Lakini limefanyika jambo la ziada, Tume ya Mipango imekuwepo huko nyuma lakini safari hii imetungiwa sheria. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ya kulinda maono ya Taifa hili ni hatua ya kulinda taasisi ambayo inasimamia mipango. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tumeanzisha taasisi ya Tume ya Mipango, tumeipa majukumu 20 na taasisi hii sasa mtu hawezi tu hapa akakurupuka akaifuta, lazima alete katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere wakati anaanzisha alisema na naomba kunukuu “nakusudia kuanzisha idara mpya, Idara ya mipango ya maendeleo, idara hiyo itakuwa chini yangu mwenyewe na itajitahidi kadri iwezekanavyo kutayarisha mipango hususan ya vijijini kwa nchi nzima”. Kwa hiyo, tangu tupate uhuru hatua yetu ya kwanza kabisa chini ya Rais wetu wa kwanza ilikuwa ni kuanzisha Idara ya Mipango na kazi ya kwanza ya idara hii ilikuwa ni kuandaa mpango wa kwanza wa maendeleo wa muda mrefu na mipango ya maendeleo ya miaka mitano mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango wa kwanza wa muda mrefu wa nchi ulikuwa ni wa mwaka 1964 - 1980, miaka 16. Mpango huo ulilenga kuongeza pato la mtu kutoka dola za kimarekani 55 wakati huo pato la Mtanzania ilikuwa dola za kimarekani 55 na tulisema ifikapo mwaka 1980 ziwe zimefika dola za Kimarekani 165. Leo tupo dola 1,222 kwa hivyo hata kwa takwimu hii tu mtu anayesema hatupigi hatua anatuonea sana, na ililenga kuinua umri wa kuishi kutoka miaka 35 wakati ule uende mpaka miaka 50 leo tupo miaka 66. Kwa hivyo, tangu mwanzo mpango ulikuwepo (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango mwingine maarufu sana ambao tunaufahamu ni wa mwaka 1975-1995 ambao ulilenga mahsusi kabisa kwenye viwanda, ulikuwa unaitwa basic industry strategy, mpango pia ulikuwepo. Kwa hivyo miaka yote hii tumekuwa na mipango hiyo, lakini kwa mara ya kwanza mwaka 1998 nchi yetu ilianzisha mchakato wa kuandika dira ya taifa ya maendeleo ambayo ilianza kutekelezwa rasmi mwaka 2000 awamu ya tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaweza kujadiliana kuhusu utekelezaji wa mipango yetu na mikakati yake lakini kwamba nchi hii imekuwa haina mipango haiwezi kuwa kweli. Hata Azimio la Arusha la 1967 mpaka miaka ya 2000 ilikuwa ni mpango wa maendeleo wa muda mrefu na kwa kweli ilikuwa ni dira ya taifa. Tunaweza kujadiliana kuhusu ufanisi wa utekelezaji, kwamba tumekuwa hatuna mipango haiwezi kuwa kweli sana. Kwa hiyo, hilo nilitaka nilitolee maoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho katika eneo hili imezungumzwa hapa kwamba uteuzi wa viongozi wa Serikali na taasisi zake uzingatie sifa za kitaaluma na weledi na maadili. Ni jambo la msingi na ni muhimu sana katika ulimwengu wa leo. Ulimwengu wa leo ni ulimwengu wanaita wa kiuwedi (meritocracy) kwa hiyo hatuwezi kupingana nalo.

Mheshimiwa Spika, of course baadhi ya Wajumbe katika michango yao ndani na nje hata ya Bunge kwa njia moja au nyingine wanatilia shaka hata sifa na weledi wa baadhi ya wateuliwa. hili ni muhimu kama nilivyosema, tunasisitiza mambo matatu, weledi ni muhimu, maadili ni muhimu lakini of course kufanya kazi kwa bidii ni nyenzo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge na hata Watanzania kwamba teuzi zetu ambazo zinafanywa na viongozi wetu zinazingatia sana vigezo hivi kwa maana ya sifa za kitaaluma, sifa za kiuweledi, sifa za kufanya kazi kwa bidiii na hata sifa za kimaadili. Wengi hapa jana mmepongeza hata Baraza la Mawaziri hapa kwamba tunachapa kazi kwa bidii. Ukiangalia kwa mfano wateule wa kwanza kabisa wa Mheshimiwa Rais ni Baraza lako hili la Mawaziri pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na siamini kwamba kuna mtu anatilia shaka sifa za wajumbe hawa 25 wa Baraza la Mawaziri pamoja na Manaibu wao. Mawaziri wanatoka wapi? Mawaziri wanatoka miongoni mwa Wabunge na mimi ninaamini hakuna mtu anayetilia shaka juu ya sifa za Wabunge wa Bunge hili la 12. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia muundo wa Bunge, nimefanya kauchambuzi kidogo, muundo wa Bunge hili la 12 unaonesha kuwa kitaaluma kwa mfano na kiuweledi asilimia 9 ya Wabunge wana Shahada za Uzamivu (PhD) Bunge lako akiwemo Spika mwenyewe. Ukiangalia asilimia 34 wana Shahada za Uzamili (Master’s Degree). Kwa hiyo, ukijumlisha tu Masters na PhD unazungumzia asilimia 41. Asilimia 21 wana Shahada ya Kwanza, asilimia 32 wana ama Diploma, Kidato cha Sita ama Kidato cha nne. Asilimi 4 peke yake ndiyo darasa la saba katika Bunge lako hili. Sasa utahoji vipi juu ya sifa za kitaaluma kitaalamu na kiweledi wa Bunge hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimfanya fanya uchambuzi, ni moja ya Mabunge ambayo sifa hizo hapa Afrika zipo juu sana wakiongozwa na Spika wake. Sasa utatilia shaka juu ya weledi wa Spika huyu kitaaluma, integrity, bidii! Tafadhali sana! Sasa ukisogea katika Wajumbe 25 wa Baraza la Mawaziri ambao wanatokana na Bunge hili, asilimia 28 wana Shahada za Uzamivu, asilimia 36 wana Shahada ya Pili (master’s) yaani Baraza hili asilimia 61 takribani theluthi mbili wana master’s na PhD, asilimia nane wana Shahada ya Kwanza, wameishia hapo. Utatilia vipi shaka juu ya weledi na sifa za kitaaluma za Baraza hili la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? Kwa hiyo, tunaweza kukosoana kwenye mambo mengine lakini siyo juu ya sifa za kitaaluma, za kitaalamu na za kiweledi, sifa hizi katika Bunge hili na katika Baraza hili zipo za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachopaswa kuimarisha ni mifumo yetu ya uwajibikaji na kuendelea kujenga uwezo wa watu wetu katika utumishi wa umma. Hatuwezi kukata mwembe wote kwa sababu tu ya kuoza kwa maembe wawili, hapana. Kama kuna maembe mawili ambayo yameoza ndani ya utumishi wetu wa umma tutashughulika nayo, lakini hatuwezi kukata mwembe mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie; a bit personal lakini nitoe hizi takwimu zifuatazo kwenye sekta ya kilimo. Moja, kwa maono yangu sasa hivi kuna clarity kubwa sana juu ya nini tunafanya katika sekta ya kilimo. Mambo manne; mbegu bora, matumizi ya mbolea, kilimo cha umwagiliaji na zana za kisasa (mechanization). Ndiyo mambo ambayo tunayafanya ili yatusaidie kuongeza tija, na yote hayo ukiangalia yanakwenda juu. Mbegu bora zinaongezeka, matumizi ya mbolea yanaongezeka, eneo la kilimo cha umwagiliaji linaongezeka na matumizi ya zana za kisasa za kilimo yanaongezeka, na matokeo yake ni kwamba uzalishaji umeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazao 84 yanayosimamiwa na Wizara ya Kilimo uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 30.6 mwaka 2021 mpaka tani milioni 36.4. Kitu gani kimetokea pia? Utoshelevu wa chakula umeongezeka kutoka chini ya asilimia 100 mwaka 2010 na leo tunazungumzia asilimia 124. Lengo letu mwaka kesho tufike asilimia 130. Muhimu zaidi uzalishaji wa mazao ya viwandani umeongezeka toka laki tisa mpaka tani milioni 1.1. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya kilimo, tumetoka wapi? Mwaka 2021 ulikuwa asilimia 2.7, mwaka 2022, asilimia 3.3, mwaka 2023 asilimia 4.2. Lengo letu ni kwamba sekta hii ikue kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Kwa jitihada hizi ninaamini kwamba tutafika na tukapata mapema. Ninayasema haya kwa sababu kilimo ni sekta muhimu. Haya ni mafanikio makubwa sana katika sekta ya kilimo katika muda mfupi uliopita. Mafanikio haya hajileti yenyewe, wapo watu nyuma yake; yupo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii tuna tabia na utamaduni wa kutokuaminiana. Ulifanyika utafiti mwaka 2014 ukaonesha kwamba katika watu 10 Watanzania saba hawaaminiani, wanashukiana; na kwa sababu hiyo tumekuwa na tabia mtu anayefanya vizuri huamini kwamba amefanya vizuri kwa nia nje, unaamini kuna kitu tu siyo bure. Tumekuwa tukifanya hivyo na tunawakatisha tamaa watu ambao wanafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe. Mafanikio yote haya ambayo nimeyasoma hapa ni kwa sababu kuna usimamizi imara wa sekta husika. Waheshimiwa Wabunge, ni muhimu kuwatia moyo watu wanaofanya vizuri, tusiwakatishe tamaa. Tusipokuwa makini tutakuwa tunakwenda mbele hatua 10 na tunarudi nyuma hatua 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima mtu anayefanya kazi kwa bidii atafanya makosa, muhimu ni kwamba ajue na arekebishe lakini siyo kumkatisha tamaa. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii, mimi kama Waziri wa Mipango siwezi kusoma mafanikio ya mipango yangu bila sekta ya kilimo. Mheshimiwa Bashe tunakushukuru sana kwa kusimamia sekta hii vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalize kwa kunukuu maneno kuntu sana ya Mzee John Samuel Malecela, aliyoyatoa mwaka 2010 wakati anawasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo lake wakati huo la Mtera. Alisema maneno haya; “Tangu kale hakijatokea chama chochote cha siasa au mfumo wa utawala ambao umekuwa na utaratibu wa kuwatajirisha watu wachache. Badala yake Chama chochote cha siasa kunachotaka kuheshimika kimetetea utoaji wa fursa sawa katika umiliki wa rasilimali za nchi; na ndiyo sababu vyama vyote vya siasa vinavyotaka kuheshimika vimekuwa vinajitahidi kusimama imara, kupambana na umasikini na kuwatetea wanyonge. Haya ndiyo yanyofanywa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na ndiyo maana kinaheshimika duniani.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie nukuu hapa ya mwisho anasema, siyo mimi ni Mzee Malecela anasema, “Haya ndiyo yanayofanywa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na ndiyo maana kinaheshimika dunia.” Ninaamini maneno haya yanaishi hadi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, ninakushukuru tena kwa fursa uliyonipa. Niwashukuru sana wasaidizi ambao tunafanya nao kazi; Mheshimiwa Naibu Waziri, Stanslaus Nyongo na ninamshukuru sana kwa sababu kaingia katikati lakini tayari ameshai-capture sekta vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu wetu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, na ninawashukuru sana Ndugu Laurance Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kwa jinsi ambavyo ameweza kuisimamisha tume hii ndani ya mwaka mmoja taasisi imekamilika na juzi amepata wasaidizi wake; Makatibu watendaji wasaidizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwatoe wasiwasi baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ikiwemo Kamati yetu ambayo ilisema tuanzishe mamlaka ya usimamizi wa ufuatiliaji. Sasa Waheshimiwa Wabunge kama mlivyotunga hii sheria, kimsingi Tume ya Mipango ndiyo imepewa jukumu hilo na tunaye Naibu Katibu Mtendaji wa Tume anayeshughulikia tu suala la ufuatiliaji na tathimini ya maendeleo ya Taifa. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Ndugu Nehemiah Mchechu ambaye ni Msajiri wa Hazina kwa usimamizi mzuri wa mashirika ya umma. Mdogo wangu Gilead Teri, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji, anafanya kazi nzuri sana na anasifiwa, Ndugu yangu Charles Tembe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa EPZA na watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Tume ya Mipango pamoja na taasisi nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kumshukuru sana ndugu yangu na mdogo wangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye Ofisi hiyo ambayo unaiongoza ilimegwa upande mmoja kutoka kwake na kipande kimoja kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji. Alinikaribisha vizuri, tumeshirikiana na amenipa ushirikiano mzuri sana. Muhimu zaidi ni kwamba fedha zote ambazo zilihitajika kuanzisha taasisi chini ya ofisi hii amezitoa kwa haraka sana. Mungu akubariki sana; na tunaendelea kushirikiana vizuri katika majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, ninaomba kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)