Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naomba nianze kwa kusema ninaunga mkono hoja na ninawapongeza wawasilishaji wote wawili, Waziri anayehusika na Mipango na Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuchangia kwangu nitakuwa ninagusa maeneo yote kwa pamoja na la kwanza, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kupata nafasi hii, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya na kazi kubwa ambayo imefanywa kwenye maeneo mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa ya Mheshimiwa Profesa Kitila, maeneo mengi ambayo tumepata mafanikio makubwa kazi hii imefanyika vizuri katika kipindi cha muda mfupi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika maeneo ambayo yalikuwa yanatiliwa wasiwasi tayari Watanzania wamepata uhakika kwamba yataendelea kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia kuhusu umeme, tumesikia kuhusu reli, tumesikia kuhusu uwekezaji bandarini, naipongeza Serikali kwa kuendelea kusimamia vizuri ahadi ambayo tulitoa kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mafanikio kwenye taarifa hasa ya Kamati kuhusu mafanikio hasa kwenye kilimo kwamba sasa tumefika takribani 700,000 kati ya hekta 1,200,000 zilizokuwa zimepangwa ambayo ni sawa na 60%. Kwa maoni yangu nadhani bado kilimo kama ambavyo tuliazimia kuongeza kutoka bilioni 270 na kitu kwenda trilioni 1.2 tunayo haja ya kuendelea kuboresha kilimo na kukipatia fedha nyingi za kutosha kwa sababu mpaka sasa bado ndiyo mwajiri mkubwa wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili nizungumzie irrigation scheme ambayo tayari mchakato wake ulikwishakamilika ya Ibanda - Igaka. Naipongeza Serikali kwa kukamilisha mchakato ambapo kazi hii ilikamilika tangu mwaka wa fedha ulioisha, lakini utekelezaji wa mradi huo haujaanza. Hii maana yake ni kwamba inawezekana pia Ibanda - Igaka ikawa ndani ya hizi hekta 727,000 ambazo kule kwetu sisi bado hatujaanza. Tunatakiwa kujenga kingio la maji halafu turekebishe lile eneo lenyewe la scheme ili hekta sasa hivi 2000 pale ziweze kuleta uzalishaji wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili kama Watanzania nadhani bado tunahitaji kutumia fursa ambayo tunayo. Tumezungukwa na nchi ambazo nyingine zina hali mbaya ya hewa, lakini tumezungukwa na nchi ndogo ambazo zinatutegemea sana kwenye mazao ya chakula na uzalishaji wetu wa chakula pamoja na kujitosholeza sisi wenyewe ndani unatupa fursa ya kuuza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Serikali kuweka fedha nyingi sana kwenye kilimo na kuzitoa fedha hizo kwenda kwenye miradi iliyokusudiwa. Tunatenga pesa nyingi, lakini zisipoenda ni sawa sawa na kujidanganya sisi wenyewe, tutakapokamilisha masuala ya irrigation na masuala ya uboreshaji wa mifugo ukienda vijijini bado wakulima wetu wanalima kizamani. Bado wakulima wetu productivity yao kwa heka ni ile ile ya mwaka 1960 wakati tunapata uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitoe wito, nadhani ni vema tukaangalia namna ambavyo huduma za ugani zikawa accessible zaidi kuliko hata huduma nyingine. Tulikuwa na maadui wengi, tulikuwa na ujinga, maradhi sijui na nini, ukiangalia vizuri huko tumetoka, sasa tumebakiza umaskini na njia pekee ya kutoka kwenye umaskini ni kwenye kuboresha kilimo, kwa hiyo, nitoe wito kwamba maeneo haya yawekewe fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imesemwa pia kwenye mifugo bado mchango wake ni mdogo, pia kwenye uvuvi bado mchango wake ni mdogo. Hapa kwenye uvuvi ninaipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi kwenye vizimba (cages). Ulikuwa ni ushauri wetu sisi kwamba tuache vizimba tuweke cages, lakini nadhani kuna technical mistake moja imefanyika hapo. Vizimba ni very expensive, lakini running cost ya kizimba kimoja mpaka samaki wakakue tangu kununua vifaranga na kuwanunulia chakula mpaka kukua ni kubwa, sasa Wizara ikaja tena na proposal ikapunguza kodi ya importation ya samaki kutoka nje, sasa matokeo yake hao wenye vizimba hawawezi ku-operate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vizimba nataka nikuhakikishie vyote mlivyogawa ndani ya mwaka mmoja vitabaki kuwa white elephant, kwa sababu vyakula ambavyo vinapelekwa kwenye vizimba vinakuwa imported na vilivyopo Tanzania vinazalishwa kwa gharama kubwa, wakati huo kuna samaki wa bei rahisi sana kutoka nje ya nchi, sasa hili tuliangalie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye madini. Tunaipongeza sana Wizara ya Madini imefanya kazi vizuri hasa imechangia takribani 9% kwenye Pato la Taifa na imechangia kuingiza fedha za kigeni takribani dola bilioni 3.6, hili ni ongezeko kubwa sana.
Sasa Mheshimiwa Waziri wetu wa Mipango hapa nashauri jambo moja tu kubwa kabisa, ukiangalia vizuri mapato kwenye eneo hili makubwa yanatokana na wachimbaji wakubwa ambao wanachangia takribani 60% na wachimbaji wadogo 40%. Wachimbaji wadogo waliochangia 40% ya dola bilioni 3.5 bado asilimia kubwa wanachimba kienyeji. Mwaka jana tulipitisha pesa kwa ajili ya kuiwezesha Wizara kununua mitambo ya uchorongaji na kununua ndege, jambo hili lingefanyika haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, uwezekano wa siku moja tukawa na madini, lakini eneo lenye madini tukalikuta tayari ni vijiji au ni makazi ni mkubwa. Kwa hiyo, upimaji huu usipofanyika haraka na kwa sababu wenye ardhi ni wananchi tutajikuta tunayo madini chini ya ardhi, hatuwezi kuyachimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tu, Dodoma hapa inawezekana kuna gold chini, lakini kwa sababu utafiti haukufanyika na mji unakua, kesho kutwa ukigundua kuna dhahabu ukiwa unaenda kule Mji Mpya wa Serikali, inaaminika kuna dhahabu, lakini tayari kuna mji pale chini. Kwa nini utafiti ulichelewa, watu wamejenga hiyo dhahabu haitachimbwa tena, kwa hiyo, tutakuwa na utajiri hapo chini ya ardhi ambao hauwezi kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaiomba Serikali iharakishe utafiti kwenye eneo hili na utafiti ufanyike tuwe na land bank ya ardhi ambayo imefanyiwa utafiti wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye elimu; nimefanya utafiti tu mdogo nikagundua kwamba tuna tatizo kubwa sana, nadhani la vipaumbele. Miaka michache nyuma tulikuwa tunahamasisha wanafunzi au watoto kusoma sayansi na watu wengi sana wakaenda kwenye sayansi, sasa hivi kijana anamaliza form six anapata division one ya PCB ya point nane mpaka point tisa anakosa chuo cha sayansi cha kwenda kusoma kwa sababu ushindani ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano karibu miaka mitatu yote ama minne. Mwaka juzi vijana wanne walipata division one ya point tisa, walikuwa wanataka kusoma medicine, pharmacy au nursing wakakosa chuo, wakaambiwa wasubirie mwaka unaofuata. Mwaka jana wakaamua kwenda kusoma biashara. Mwaka jana walikuwepo watatu wakakosa chuo, mwaka huu wakaenda kusoma biashara, mwaka huu karibu sita, Waziri wa Elimu anajua nilimwambia akiwa Geita. Huyu amefaulu division one ya PCB ambacho ndicho kipaumbele cha nchi, lakini vyuo hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unashindwa kuelewa, humu tunao maprofesa na madaktari ambao walikwenda university wakiwa na division two na wengine walikuwa na division three wali-upgrade wakaenda. Leo inakuwaje mtu wa division one ya PCB anakosa chuo eti competition ni kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali haioni kwamba si una-project? Ni lazima u-project kwamba unajua form six wapo 120,000 kati yao wanaosoma sayansi ni 60,000, tentatively watakaofaulu ni 45,000, wewe wanafaulu wanapata division one halafu unamwambia huyu aliyehangaika na sayansi tangu form one mpaka form six aende akasome biashara, akasome sheria kwa sababu tu Muhimbili imejaa, UDOM imejaa basi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye enrolment kwa mujibu wa taarifa hii ya TCU ya mwaka 2023 kati ya wanafunzi takribani 40,000 waliochukuliwa zaidi ya 20,000 ni vyuo binafsi. Ninaishauri Serikali hapa, tunapoteza vijana ambao wamepambana huku chini na tena wana uwezo mkubwa kwa kisingizio kwamba ushindani ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imagine mtu aliyepata division two wa Art anapata course yoyote anayoitaka, mtu aliyepata division one wa sayansi anakosa course aliyoikusudia kwa sababu Serikali haijajiandaa. Kwa nini Serikali isiongeze vyuo vya madaktari kama imegundua Muhimbili pamejaa, kama imegundua UDOM pamejaa, kwa nini usipeleke chuo kikubwa katika kila hospitali kubwa ya kanda mkajenga chuo kikubwa cha Serikali cha medicine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwahi kupelekwa na Bunge hili China sehemu moja inaitwa Nanchang, chuo kimoja kina wanafunzi 60,000 na course moja ina wanafunzi 30,000. Hapa sasa hivi wanakuambia chuo kimejaa, ukienda kuna wanafunzi 3,000. Tunawakatisha tamaa watu, sasa wote hawa tunawalazimisha kubadili course aliyokusudia kusoma, anakwenda kusoma course nyingine, matokeo yake hawa waliopo form four wote wana-opt kwenda kusoma diploma, matokeo yake sasa tunakuwaje? Matokeo yake huku mbele tunapokwenda tunaandaa kundi fulani hapa katikati ambalo na lenyewe litakuja na crisis kama tuliyonayo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo tumeshauri hapa sana kwa muda mrefu. Inawezekana mfumo hauna uwezo wa kugundua watu wenye matatizo au wenye shida ya mkopo. Mimi nina watoto ambao baba yake amefariki, cheti ameweka kwenye mfumo. Mama yake ni mama ntilie cheti ameweka kwenye mfumo. Mfumo unam-reject kwa sababu alisoma english medium! Sasa mwenye mkataba wa kuishi milele kwamba kwa sababu ulisomeshwa english medium huku chini au ulisoma form four ya private ni nani humu? Hebu tuambizane. Kila kitu ulichokitaka kwenye mfumo kimewekwa bado mfumo unasema system imem-reject kwa sababu huko zamaniā¦, hebu tuwaambie Watanzania sifa hasa ni ipi ya kumsaidia Mtanzania. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kanyasu muda wako wa kuchangia umeisha na taarifa haiwezi kutolewa muda ukiisha. Naomba u-wind up.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo moja tu. Ni haki ya kila Mtanzania aliyelipa kodi anapoomba mkopo apate mkopo, kama mfumo hauwezi kumgundua mhitaji, hakuna haja ya kuweka sasa standards hapa, tuweke flat rate ili kila Mtanzania mwenye haki ya kusoma apate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)