Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyopo mezani kwetu ambayo ni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo unaokusudia kutekelezwa mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa ushauri wangu kwenye mapendekezo ya mpango huu nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushusha fedha nyingi sana za maendeleo katika Jimbo la Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninavyoongea jimboni kwangu Bukene kuna mradi mkubwa wa kusambaza maji ya Ziwa Victoria ambao una thamani ya shilingi bilioni 29, hii ni dhamira ya dhati kabisa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuondoa tatizo la maji ambalo kwa kipindi kirefu imekuwa ni kero ndani ya Jimbo la Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongea sasa hivi jimbo langu lina mradi mkubwa wa scheme ya umwagiliaji ya shilingi bilioni 40 ambako tunakwenda kumwagilia zaidi ya ekari 4,000 za kilimo cha mpunga na hii inakwenda kuwa mkombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Bukene hasa Kata ya Sigili, lakini tunakwenda kuongeza sana mapato kwa halmashauri kwa maana ya kupata mpunga mwingi sana kutokana na hii scheme kubwa ya shilingi bilioni 40 ndani ya Jimbo la Bukene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wote tunafahamu kwamba mradi mkubwa wa kusambaza umeme vijiji vyote ambao umegharimu shilingi bilioni 27 unakwenda vizuri na sasa tunakwenda hatua ya vitongoji kwa vitongoji. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene tunatoa pongezi na shukrani za dhati sana kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia kwa namna ambavyo ametushushia fedha za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi sasa kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo huu ambao unakusudiwa kutekelezwa mwaka 2025/2026, kimsingi mapendekezo mengi ninakubaliana nayo isipokuwa nina ushauri kwenye maeneo kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo napenda kutoa ushauri, kwanza ninakubaliana na mpango kwamba kuendelea kujenga miundombinu muhimu ikiwemo reli ya kisasa (SGR) kwa sababu kile kipande cha SGR cha kutoka Tabora mpaka Mwanza kinapita katikati ya Jimbo langu la Bukene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu hapa ni kwamba tunapopanga bajeti ya ujenzi wa SGR tuzingatie sana component ya fidia. Sasa hivi kuna tatizo pale jimboni kwangu, nina watu karibu 183 ambao wametoa mashamba yao wamepisha ujenzi wa hii reli ya kisasa, lakini huu ni mwaka wa pili sasa, walishafanyiwa tathmini ikajulikana gharama wanayopaswa kulipwa kama fidia, lakini huu ni mwaka wa pili sasa hawajalipwa. Wananchi wameachia mashamba hivyo hawalimi na fidia hawajapewa na huu ni mwaka wa pili. Kwa hiyo, hii component ya fidia inaleta kero kwa wananchi wetu, mradi ni mzuri, faida za mradi ni nzuri, lakini sasa hii component ya fidia kidogo inaleta changamoto kwenye huo mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi 183 mashamba yao yametwaliwa kupisha tuta la reli, lakini mwaka wa pili sasa hawajalipwa, kwa hiyo, fidia ni jambo ambalo lizingatiwe sana tunapoweka bajeti ya miradi kama hii, otherwise miradi ni mizuri lakini sasa inakuja kuleta kero kama hawa wananchi wangu 183 wa Jimbo la Bukene ambao wanadai fidia mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa rai kwa Serikali kwamba wananchi hawa walipwe mapema sasa hivi hawawezi kulima kwa sababu maeneo yao wametoa kwa ajili ya ujenzi wa reli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kushauri kwenye huu Mpango wa Maendeleo ni kwamba nakubaliana na mpango kuweka kipaumbele cha kuendelea kufanya jitihada za makusudi za kuongeza tija kwenye kilimo. Ajira kuu au shughuli kuu ya wananchi wetu hasa sisi tunaotoka majimbo ya vijijini ni kilimo, kwa hiyo, ukitaka kuinua maisha ya wananchi wetu ambao wanajishughulisha na kilimo hakuna njia nyingine zaidi ya kuongeza tija kwenye kilimo. Sasa tija kwenye kilimo huwezi kukwepa matumizi ya mbegu za kisasa, matumizi ya mbolea za kisasa, matumizi ya huduma za ugani na haya yatawezekana tu kama Serikali itaendelea kuweka ruzuku hasa kwenye mbegu na kwenye mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu na ninapongeza jitihada kubwa za Serikali ambazo zimekwishafanyika kwa sababu maeneo mengi ambayo mbolea ilikuwa ikigharimu karibu shilingi 150,000 baada ya ruzuku ya Serikali imeshuka mpaka shilingi 70,000 lakini jitihada ziendelee kwa sababu maeneo mengi ya kwetu huko ardhi zimechoka, bila matumizi ya mbolea huvuni. Kwa hiyo bado kuna mahitaji makubwa sana ya matumizi ya mbolea na naunga mkono Mapendekezo ya Mpango ya kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu bora ili wakulima wetu waweze kuongeza tija katika kilimo, kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuongeza kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mapendekezo ya Mpango ya kuendelea kujenga scheme za umwagiliaji. Ili kuongeza tija katika kilimo lazima tulime mara mbili, lazima tulime kwa kutumia mvua za kawaida, lakini lazima tuwe na scheme za umwagiliaji ambazo zitatunza maji ili tuweze kulima kwa kipindi ambacho hakuna mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimboni kwangu kule sasa hivi kuna scheme zinaendelea kujengwa, lakini bado jimbo ni kubwa, vijiji vingi, kata nyingi, bado naishauri Serikali kuendelea kutenga fedha za kutosha ili tuwe na scheme nyingi zaidi za umwagiliaji. Kwangu kule na scheme za umwagiliaji za Kamanhalanga, Kasela, Mambali, Itobo, Mwangoye na Chamipulu ambazo zikifufuliwa na kuboreshwa zitatufanya tuweze kulima kwa tija na kuongeza kipato kwa wananchi wetu ambao wengi wao wanategemea kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono Mapendekezo ya Mpango huu katika eneo la kuendelea kuboresha barabara zetu, barabara zetu hasa maeneo ya kijijini ni uchumi. Sasa hivi kuna jitihada kubwa ambayo inaendelea ya kuleta fedha kwa ajili ya barabara za kijijini na niipongeze TARURA kwa kiwango fulani wanajitahidi, lakini bado fedha inatakiwa iongezwe ili tuhakikishe barabara za vijijini zinapitika na mazao kule tunalima mpunga sana, mpunga uweze kubebwa kwa gharama nafuu kwenda kwenye maeneo ya masoko.
Kwa hiyo, naunga mkono eneo la mpango ambalo linasisitiza Serikali kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha barabara hasa za vijijini ili kuongeza tija katika kilimo na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia umeme vijijini kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao (value addition). Hapa ushauri wangu ni Serikali sasa baada ya kueneza umeme vijiji vyote, umeme huu sasa uende ukatumike kuongeza thamani ya mazao na wakulima ambao walikuwa wanauza mpunga, sasa wasiuze mpunga wauze mchele, wakulima ambao walikuwa wanauza alizeti zikiwa ghafi sasa wawe na viwanda vidogo vidogo na wasindike mafuta ya alizeti ili wauze mafuta ya alizeti badala ya kuuza alizeti yenyewe ghafi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ninashauri jitihada za makusudi zifanywe ili vikundi vya wakulima kule maeneo ya vijijini wafundishwe na wapewe mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitaongeza thamani ya mazao kwa makusudi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Bukene kule tuna maembe mengi mno, tunalima maembe mengi. Hakuna sababu yoyote ya wanavikundi eneo la kwangu kule kushindwa kuungana na baadaye Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi wa Taifa kuwasaidia mitaji ili waweze kuwa na viwanda vidogo vidogo vya kusindika matunda kwa kutumia maembe ambayo wanalima kule. Kwa hiyo, kuwe na jitihada za makusudi za Serikali za kuwawezesha hawa wakulima ili sasa waongeze thamani ya mazao yao ili waweze kupata tija kwenye maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)