Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kabisa Serikali iliamua kuweka maeneo ya EPZ kwa ajili ya maendeleo na kuhakikisha kwamba uchumi unakua kwa kasi. Katika maeneo 17 ambayo yalitengwa, ni mawili tu ambayo ni pale Benjamin Mkapa na Bagamoyo ndiyo ambayo yameweza kufanya kazi na mengine yote bado fidia na vitu kama hivyo vinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwamba shilingi bilioni 9.9 imeanza kulipwa kwenye fidia, lakini maeneo ya Nala hapa Dodoma na kule Songea, bado. Tunafikiri kwamba tunapokuwa na mipango na tunapoenda kufanyia, kazi basi tuongeze speed na ndiyo maana wenzangu wametoka kusema hapa, watu wanaachia maeneo kwa ajili ya kupisha Serikali ifanye maendeleo, lakini Serikali inakaa muda mrefu sana bila kuwalipa fidia ili kusudi watu waendelee na maisha yao na kwamba ile mipango ambayo Serikali imepanga basi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninatambua kwamba hiyo shilingi bilioni 9.9 ni ndogo, watu wengine bado wanadai. Kama nilivyosema hapa Dodoma tumesema ndiyo jiji na ndiyo katikati ya nchi na ni makao makuu, basi walipe pale Nala na kule Ruvuma ambapo tayari ndugu zetu wameachia maeneo kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kabisa ili kujenga mpango wa mbali ni lazima nguvu ya kiuchumi ya wananchi iendelee kuwepo. Leo hii tuna Mfuko wa Barabara, tunapopata hela katika mfuko ule basi pesa zitoke mapema ili kurekebisha maeneo yaliyoharibika au kujenga barabara zingine. Tunaomba Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Mwigulu nafahamu yeye anajua, tusipofanya hivyo basi barabara ambayo inabeba hayo mazao ambayo watu wetu wanalima huko inaweza ikaleta bei ya mazao kuwa kubwa zaidi kwa sababu ya usafirishaji kuwa mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua SGR imefanya vizuri, TAZARA najua sasa hivi wana mazungumzo kwamba angalau wenzetu wa China walioitengeneza warudi na kuisimamia. Kwa sababu TAZARA ilikuwa inasaidia sana Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kubeba mazao na pia kusaidia usafirishaji, basi tunaomba mazungumzo hayo yafanyike haraka na TAZARA irudi kwenye nafasi yake ya awali ili watu wa Nyanda za Juu Kusini tuweze kufanikiwa tukitambua kabisa kwamba sisi ndiyo wazalishaji wakuu na mazao mengi yanatoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia habari ya TEHAMA; TEHAMA ni kitu muhimu sana kwa sababu Tanzania haijajitenga. Tunaamini kwamba tusipokuwa na mifumo ya kitaalamu kama hiyo basi tunafanya watu wetu kurudi nyuma hasa katika mambo ya kiteknolojia. Tunaomba fedha iongezwe kwa hawa ndugu zetu wanaoshughulikia TEHAMA ili tupate wataalamu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba kuna akili bandia ambazo zinatakiwa kuongezeka vyuoni kwa ajili ya kusaidia ufundishaji wa wataalamu mbalimbali. Basi tunaomba tuwekeze huko ili na sisi twende kwa speed kubwa sana ya kimaendeleo, kwa maana ya TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunazungumzia habari ya minara. Tumesema hapa na tumesikia kwenye bajeti zilizopita kwamba tunahitaji kuwa na minara zaidi ya 758, lakini mpaka sasa ni minara 295 tu iliyojengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba tunapokuwa na teknolojia ya habari au kupata simu kwa watu wa vijijini ni kitu muhimu sana katika kuleta maendeleo. Leo hii wakulima wanatafuta masoko kwa kutumia simu. Pamoja na hayo, Maafisa Ugani ni wachache, kwa hiyo, wanaweza wakatumia teknolojia ya simu kuweza kuendeleza wakulima wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba minara vijijini iongezeke, kuna maeneo mengi sana, kwa sababu kati ya minara 758 iliyojengwa ni minara 295, kwa hiyo haijafika nusu. Tunaomba speed iongezeke ili tuweze kuwa na usikivu mzuri sana wa simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tunaomba tufanye angalau bundle na gharama za simu zishuke kidogo. Hii itasidia watu wa vijijini hususani wanawake kuweza kuwa na mawasiliano na wakaingia katika mambo ya simu kwa kuwa itakuwa ni bei rahisi kudogo, lakini tunapokuwa na bundle, unaweka bundle limeisha na hatujui limeishaje na kampuni za simu lazima zidhibitiwe ili tuweze kuona watu wetu wakifanikiwa katika uanzishwaji wa simu na kuongeza idadi ya watumiaji wa simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba ili tuweze kuendelea, bado ile kauli ya kwamba kilimo ni uti wa mgongo, mimi nniaamini bado inaendelea. Ninajua kwamba Mheshimiwa Kitila anayafahamu mambo haya. Sasa basi, watu wengi ambao wako kwenye kilimo, ni kweli bajeti imeongozeka kwenye kilimo, tumetoka mbali na sasa tuna 1.2 billion kwenye bajeti yao, tunawashukuru kwa kuongeza, lakini bado lazima tusimamie kilimo kwa sababu watu zaidi ya 70% wako kwenye kilimo. Tunajua kabisa kuwa mbolea inatoka, lakini je, inatoka kwa wakati? Wale wanaopewa dhamana ya kuendeleza mbolea za ruzuku ni waaminifu? Usimamizi lazima uwepo na ni lazima tuwekeze kwenye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Chuo cha Kilimo Uyole kwa muda mrefu sana hakipati fedha za utafiti. Tutapataje mitambo mizuri tusipowekeza kwenye watafiti? Tunawezaje kuwa na mbolea ya kufaa bila kuweka watafiti wa kujua kwamba mbolea hii itafaa. Tunafahamu kabisa leo hii kumekuwa kuna watu wanauza mbegu fake, tunahitaji watafiti ambao wataisaidia Serikali kusema kwamba mbegu hizi hazifai, tunahitaji mbegu hii. Tunaomba sana sana muongeze jitihada katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa tunavuna, leo hii tuna parachichi ambayo tunaiita ni dhahabu ya kijani. Ni kweli imepanda katika soko la nje, lakini tunahitaji kuongeza nguvu ya bei ya parachichi na kuwaondoa madalali wanaowaumiza wakulima. Leo hii mkulima analima parachichi halafu anakuja dalali anasema parachichi hii ni reject.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuongeze wataalamu kule chini ambao wataweza kuwasaidia wakulima waweze kuuza parachichi zao. Kwa sababu yanakuwa reject kwa macho ya nani? Anasema reject halafu anayachukua, halafu yeye anakwenda kuyauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali isimamie hilo na tunapoendelea na mipango hii ni lazima tuwalinde wakulima hawa kwa sababu zao la parachichi haliishi leo. Tumeona kwamba parachichi siyo tu chakula, ila inatengeneza pia dawa pamoja kusaidia mambo tofauti. Kwa hiyo, mimi ninaomba katika mpango wa kilimo tuhakikishe tunatumia muda mrefu sana, kuweza kulilinda zao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakwenda sambamba na zao la chai. Tunafahamu kwamba chai inanyweka dunia nzima. Leo hii wanasema kwamba soko la chai limeshuka, siyo kweli. Kati yetu hapa wote tunakunywa chai na dunia nzima inatumia chai. Basi tupambane kwenye soko la dunia ili chai yetu iweze kusonga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wawekezaji wanaotoka nje ni lazima tuwangalie kwa jicho la forensic. Haiwezekani mwekezaji anatoka nchi za East Africa hapa, nchini kwake analima chai na wala kiwanda hakifi, lakini akija kununua kiwanda na kuwekeza hapa Tanzania, anafunga kile kiwanda anasema chai haina soko, lakini hapo jirani tu anapotoka yeye huyo mwekezaji chai inaendelea. Kwa hiyo, tunawaomba watu wa usalama wasimamie, wahakikishe chai ya Tanzania inapata bei kama ambavyo East Africa wanauza kwa bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kuwa ili uwe na mpango mkubwa wa muda mrefu na mzuri basi watoto wetu tuwapatie elimu nzuri na kwamba tuhakikishe kuwa wanakuwa na elimu ambayo inaeleweka. Tunaomba Wizara ya Elimu ihakikishe kuwa mitaala yetu haichezewi wala kubadilika badilika kila wakati. Tuhakikishe kuwa watoto wetu wanapo-stick kwenye elimu fulani ambayo Bunge na wananchi kwa pamoja tumepitisha, basi iende hivyo. Isiwe kwamba leo GPA, kesho wanatoa na kufanya kitu kingine, huko ni kuyumbisha wanafunzi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja na ninaamini tutatoa mpango ambao ni mzuri wa kulisaidia Taifa letu, ahsante. (Makofi)