Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai na kusimama hapa mbele yenu. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa miradi yote ya maendeleo ambayo imekamilika na kwa miradi ambayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Profesa Kitila pamoja na Mheshimiwa Dkt. Nchemba kwa mambo yote wanayoyafanya pamoja na Wizara zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kupongeza kwa upande wa mambo ya vipaumbele. Vipaumbele vingi ambavyo wameviweka na mpango uliotimilika kweli ni mzuri, hata hivyo nitaweza kuongea kwa kiasi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naongea kuhusiana na kipaumbele cha miundombinu pamoja na usafirishaji. Hapa nitaongelea hasa kwenye upande wa reli hii ya mwendokasi ambayo tayari inafanya kazi kwa kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro kilometa 300 na kuanzia Morogoro mpaka Dodoma ambapo Waheshimiwa Wabunge na watu wengi wanasifia na wote tunaitumia kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande ambacho kitawekwa kwenye mpango ambacho kinaendelea kujengwa ni kipande cha kuanzia hapa Makutupora kuendelea mpaka Tabora na kipande cha awamu ya pili ni kuanzia Tabora kwenda mpaka Kigoma mpaka Kalema. Kwa hiyo, mpango huo uwekwe na huo mradi uweze kukamilika kwa wakati kama utakavyokuwa umepangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye mpango huu, ninaomba uhusishe treni ya mizigo kwa sababu treni ya mizigo ya SGR itasaidia sana. Ninasema hivi kwa sababu tumejenga barabara, lakini zinaharibika kutokana na mizigo mikubwa ambayo inabebwa na malori. Kwa hiyo, kwa tutumie treni ya mizigo kwamba ninashauri iwekwe kwenye mpango, ionekane, itekelezwe na iweze kufanya kazi kwa wakati. Hiyo itakuwa imesaidia sana kwa upande wa usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara, ninaungana pamoja na mpango kuwa barabara ziunganishe mikoa kwa mikoa na barabara za mikakati. Hapa ninaongelea kwa Mkoa wangu wa Morogoro ambao ninashukuru na kuipongeza Serikali ambayo imeanza matengenezo ya barabara inayoanzia Kidatu kwenda mpaka Namtumbo – Songea. Pia kwenye mpango huu ninashauri kuwa iweze kuwekwa vizuri ili kuweza kukamilika kwa wakati kwa sababu inasaidia kwa pande mbili za Ruvuma pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa kukuza uchumi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye upande wa vipaumbele ninakwenda kwenye sekta ya uzalishaji. Ninashukuru kwenye mpango wameweka sekta za uzalishaji, lakini ninaomba ikaziwe kabisa hasa kwenye upande wa kilimo, mifugo pamoja na uvuvi ambao unaleta uchumi na kuongeza Pato la Taifa pamoja na la mkulima na kumwezesha mkulima huyo kuwa na hela kwenye mifuko yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, ninashauri mpango uweke na msisitizo sana kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, ukija kwenye central corridor (Ukanda wa Kati) unakuta kuwa mara kwa mara ni kame. Kwa hiyo, hii mipango ihusishe sana uchimbaji wa mabwawa ili waweze kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninapongeza kwa upande wa Mkoa wangu wa Morogoro kwa kuwa tuna maji ya kutosha, lakini ninashauri schemes za umwagiliaji ziweze kuendelea. Hii ni kwa sababu Mkoa wetu wa Morogoro tunaweza tukalisha nchi nzima kwa kuwa ni mkoa ambao una udongo mzuri na una maji ya kutosha. Hata hivyo kilimo cha umwagiliaji ndicho kinachoweza kikaturudisha wananchi nyuma kwa ujumla. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kuwa iweze kuendelea hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru na kuipongeza Serikali na mpango mzima. Ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kutoa ruzuku ya mbolea na ruzuku ya mbegu ambazo sasa hivi inasaidia wananchi kwa sababu wanapata mbolea pamoja na mbegu kwa upande wa ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza hivyo na tukipata maji kwa ajili ya umwagiliaji, mbolea pamoja na mbegu ajira itapanda, Pato la Taifa litaongezeka na pato la mwananchi litaongezeka. Kwa hiyo, mpango huu ukazie sana kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee upande wa viwanda na kuthamanisha vyakula. Ninaomba sana kodi iangaliwe kwenye viwanda, utitiri wa kodi, ukubwa wa kodi na ongezeko la kodi. Unakuta viwanda vingine vinashindwa kujiendesha kwa sababu kodi zinakuwa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mpango huu uweze kuendeleza na kujenga viwanda huku tukiwa tunaongeza viwanda, tuweze kuona viwanda hivi hasa vitakavyoanzishwa hapa na kuweka mazingira mazuri ya wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye viwanda hasa katika kuongeza thamani ya vyakula kwa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini. Kwa namna hii tutaweza kuongeza ajira pamoja na kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vilivyokufa, kwa hiyo, ninashauri mpango huu uangalie kwamba je, viwanda vilivyokufa, vinafufuliwaje na vinaendeleaje? Hapa naweza kuipongeza Serikali kwa mpango uliopo wa kukifufua na kukiendeleza Kiwanda cha Mang’ula Kilombero ambacho kitafufuliwa na kitandelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuendelea kuongea kuhusu mpango wa miradi ambayo haijakamilika. Hapa pia ninamaanisha na miradi ya maji ambayo haijakamilika, maboma ya madarasa pamoja na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuanzisha mipango mipya mpango huu ujikite kwenye kumalizia mipango viporo ambayo bado hajamalizika. Hapo ninagusia pia Mradi wa Liganga na Mchuchuma, ni mradi wa miaka mingi sana, nilianza kuusikia Mradi wa Linganga na Mchuchuma kwa miaka mingi na mimi mwenyewe nimetembelea huko miaka ya nyuma. Kwa hiyo, ninaomba mradi huu umalizike ili tuweze kupata chuma cha kutengeneza mambo yetu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuitilie maanani Liganga na Mchuchuma kwenye mpango huu ili mradi uweze kukamilika. Kama tatizo ni mkandarasi aweze kuangaliwa. Kama tatizo ni mipango iangaliwe ili kusudi nayo iwe historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere; Bwawa la Mwalimu Nyerere linaenda vizuri, ninashukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu umeme sasa unaanza kutoka na unaendelea vizuri ingawa ni lots chache, lakini ikifikia lots tisa zote ninaamini tutapata umeme wa kutosha, tutaweza kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na pia tutaweza kuuza nje na kupata fedha za kigeni kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie upande wa maliasili, mazingira na tabianchi. Hapa ninaomba kwenye mpango wetu tuiweke kuwa huu mfuko ambao tunausemea uweze kuona kuwa kama Serikali tunaiongezeaje hela na ni mikakati gani tuchukue kwa ajili ya kutunza mazingira yetu. Kwa sababu hili ni janga kubwa la Taifa kama tutaacha mazingira yetu yakaharibika. Tutapata joto la kutosha na tutakosa mvua, yaani kwa kweli itakuwa ni disaster kubwa sana. Kwa hiyo, tuweke kwenye mpango jinsi ya kutunza mazingira, jinsi ya kupanda miti na jinsi ya kuiendeleza nayo itakuwa imekuwa nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazabuni, wakandarasi pamoja na watoa huduma, ni kweli kwenye mpango wanasema kuwa wamelipwa, lakini siyo wote. Ninaomba huo mpango uangaliwe ili wale ambao hawajalipwa wawekwe kwenye mpango ili waweze kulipwa kwa sababu kama hatutawalipa, tunachelewesha ile miradi kukamilika kwa sababu huyo mzabuni, mkandarasi hawezi kuendelea bila kupata hela ya kulipwa. Kwa hiyo, ninaomba sana hiyo nayo tuiangalie. Huo ni ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naongelea kuhusu maji. Maji ni maji na kila mmoja anataka maji. Kwa hiyo, mipango ya maji naomba tuiangalie, vile vijiji vyote ambavyo havijapata maji wananchi waweze kupata maji na fidia ziweze kufidiwa. Kwa mfano, wakulima wangu na wananchi wangu wanaozunguka Bwawa la Mindu hawajalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namalizia kuwa umeme upelekwe vijijini na kwenye vitongoji ambao hawajapata. Ahsante sana kwa kunipa nafasi na ubarikiwe na Mwenyezi Mungu. (Makofi)