Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja zilizopo mezani kwa maana Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2025 na Mwongozo wa Bajeti ya mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kwa kusimamia mpango ambao tunaenda kuumaliza wa mwaka mmoja na kuja na mpango mzuri huu ambao unatuonesha mwelekeo wa kuweza kuleta maendeleo zaidi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika Mheshimiwa Rais katika mwaka mmoja huu ambao tunaumaliza amefanya kazi kubwa sana. Sisi ambao tupo majimboni tumeona fedha nyingi zimekuja kutekeleza miradi ambayo ilikuwa kwenye mpango uliopita. Kwa hakika wananchi katika maeneo yote wanampongeza Mheshimiwa Rais na wanamshukuru kwa sababu kuna maendeleo makubwa. Fedha zimekuja nyingi, miradi imekuwepo ya kutosha, miradi ya elimu, afya, barabara, umeme pamoja na aina mbalimbali ya uwezeshaji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili Mheshimiwa Rais amefanya jambo jema na sisi tunampongeza sana kama Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango pamoja na Uwekezaji ambaye kwa kweli wamefanya kazi kubwa kuandaa mpango huu. Pia tumpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kutuletea Mwongozo wa Bajeti ambao Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba pamoja na Waheshimiwa Naibu Mawaziri wao wamefanya kazi kubwa ambayo tumeiona hapa na imetupa mwelekeo mzuri wa kuweza na sisi kuongeza ushauri katika mpango waliotuletea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango huu tumesoma na tumeona kwamba uchumi umekua kwa maana ya Pato la Taifa limekua katika kipindi hiki. Kwa hakika tunajivunia sana kwa sababu mipango ambayo imetekelezwa imesababisha uchumi kukua. Kwa hiyo, kupitia taarifa tuliyosomewa hapa inaonesha mwelekeo wetu ni mzuri na uchumi wetu ni stahimlivu ambao kimsingi tukiendelea kufanya mipango tuliyosomewa leo tunaweza tukaja mwakani na uchumi wa juu zaidi tofauti na mwaka huu ambao tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Ninataka kusema kwamba Pato la Taifa tumeelezwa hapa limekua kwa wastani wa 5.1% ambayo kimsingi ukilinganisha na mwaka ule uliopita wa 4.7%. Haya ni mafanikio makubwa ambayo kwa kweli yanaleta matokeo makubwa ya uchumi wetu. Hili tunaweza kuwapongeza Waheshimiwa Mawazari kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pato la Taifa linategemewa kukua mwaka 2025 kufikia 5.8% lakini mwaka 2026 kufikia 6.1%. Ni jambo kubwa la kupigiwa mfano, tuwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kufanya kazi nzuri pamoja na wataalamu kusimamia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili pato hili limefikia hapa ni baada ya kuwekeza kwenye miundombinu ya nishati na usafirishaji, lakini pia mmeongeza mikopo ya sekta binafsi na jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara katika nchi yetu. Haya ni mambo ambayo mliyafanya, lakini pia utekelezaji wa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo (ASDP II) ambayo tunaendelea kutekeleza mpaka sasa. Kipaumbele cha Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa Miaka Mitano 2021/2022, 2025/2026 ilieleza ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili kama ambavyo tumesema tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini niseme tu kwamba tunayo kazi ya kufanya ya kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu kubwa. Tupongeze sana kwenye hatua ya kuwa na nishati ya uhakika, eneo hili tulikuwa na tatizo kubwa la kukatika umeme, kuwa na mgao nchi nzima. Leo tunapoenda kumaliza ule Mradi wa Mwalimu Nyerere tunaenda kuleta megawati 2,115 kwenye Gridi ya Taifa, ni jambo kubwa katika nchi. Tunategemea kwamba tutakuwa na umeme wetu huu unaotosheleza, lakini tutakuwa tunauza nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili, hiki ni kivutio kikubwa cha uchumi na ni kivutio kikubwa cha uwekezaji. Mwekezaji akija nchini lazima aulize kwanza tunayo nishati ya kutosha? Kwa hiyo, kwenye hili sisi tume-win na ndiyo maana unaona wawekezaji wanakuja, ni kivutio kikubwa. Tunaipongeza sana Serikali, tunaomba muendelee kusimamia vizuri mipango hii. Tumesikia juzi SONGAS mmeshamaliza nao mkataba wa miaka 20, maana yake sasa hatutakuwa na sababu ya kugawa fedha kwenye maeneo mengi. Kwenye hili tuipongeze sana Serikali kwa hatua kubwa ambayo mmeifanya. Tunaenda kuwa na umeme wa uhakika kama ambavyo tulikuwa na ndoto kwamba tutakuwa na umeme wetu na tutauza nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili tupongeze mradi wa SGR, tumeshaona matunda yake. Juzi tumepewa takwimu na Mheshimiwa Waziri husika wa Sekta ya Uchukuzi kwamba tumepata faida kubwa katika muda mfupi ambayo kimsingi pato lile linaenda kuongeza uwezo wa Serikali kuhudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili niombe sana juhudi ziendelee na katika mpango huu tumeona kuna mpango wa kumalizia vipande vingine. Kwa hiyo, niombe juhudi ziendelee, tuendelee kumalizia vipande vilivyobaki kutoka hapa Dodoma kwenda Tabora, kutoka Tabora kwenda Isaka kule Mwanza na baadaye twende mpaka Kigoma kabla hatujaenda nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tukiwa na uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria na bidhaa, tutasaidia kuongeza uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, niombe sana eneo hili kwa sababu tunaboresha bandari yetu, kwa hiyo, SGR itakuwa na jibu la kupeleka mizigo katika nchi za jirani kupitia treni yetu ya mwendokasi ambayo tunaisema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili tumewekeza sana vizuri kwenye eneo la elimu pamoja na afya (huduma za wananchi). Tumefanya kazi kubwa, maeneo mengi tumeona maboresho makubwa. Kwenye Sekta ya Elimu tumejenga madarasa, tumejenga maabara za kutosha, tumejenga maeneo mengi na tumejenga mpaka matundu ya vyoo ambayo ilikuwa ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, leo tuna changamoto kidogo ya mabweni ambayo tunatakiwa tuongeze nguvu sana ili tuweze kujenga mabweni, watoto wetu waweze kuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia. Pia kwenye eneo hili tuhakikishe tunajenga nyumba za walimu. Walimu hawana nyumba za kutosha, katika maeneo mengi walimu wanakaa mbali na eneo la shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana mpango unaokuja uweze kutusaidia kuleta jibu la kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira mazuri ya walimu wetu. Kwenye eneo hili tumejenga barabara vijijini zimefunguka. Maeneo mengi wananchi wanafurahia kuona miundombinu yao, wanasafirisha mazao yao na wanasafiri kwenda hapa na pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili tuongeze nguvu, bado barabara nyingine hatujamaliza, madaraja tumalize ili wananchi wetu waweze kufurahia mipango ya Serikali na kuhakikisha kwamba wanaongeza uchumi wao kwani uchumi huo ambao tunausema wa kuchochea uchumi shindani na shirikishi ni pamoja na kuboresha mazingira kwa wananchi kufanya shughuli zao na zaidi tuongeze kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa mud awa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu muda wako umekwisha.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, niombe sana kwenye eneo la uchumi wa wananchi tuongeze juhudi za kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uchumi wa wananchi mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja iliyopo mezani. (Makofi)