Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii na ni saada na soud mimi kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu kusimama hapa ili kutoa mapendekezo yangu katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2025/2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mwenyezi Mungu, tunamshukuru Mheshimiwa Rais na tunashukuru watu wote wa Wizara zote mbili kwa maandalizi ya mpango mzuri, kitabu hiki kizuri, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushie mabalaa na majanga haya yaliyokuwepo humu basi yaweze kufanyiwa implementation kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema mara kadhaa kwamba maendeleo ni mchakato na mimi hapa uniruhusu kidogo niseme maana yake nimeona kuna mzee mmoja huko nje anazungumza Bunge hili ni Bunge la kusifia sifia na kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasifia na kupongeza kwa sababu yapo mambo tumeyaona katika mpango wa mwaka jana na mpango wa mwaka juzi katika nchi yetu yametokea. Mara zote tumekuwa tukisema hapa tunalalamika, tunasema mambo ya maendeleo ya watu wetu. Sasa leo tunavyotoa mifano na vitu unavyoviona na Mheshimiwa Rais anavyozunguka, anavyoenda kusema kuhusu vitu hivyo anavyovifungua hatuna budi kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo la Kilombero tumepata Kiwanda cha Sukari karibu shilingi bilioni 700, barabara ya lami shilingi bilioni 150, mradi wa maji shilingi bilioni 41, umeme shilingi bilioni 24, tumejenga shule mpya, tumejenga vituo vya afya, kituo cha polisi na mambo kibao. Haya yote yalikuwa ni changamoto, lakini katika mpango uliopita yametekelezwa na yamefanyika. Sasa anatokeaje mwanasiasa huko mzee mchekea mwezi analalamika lile Bunge mnaliona la kupongeza tu. Kinamkera nini sisi tukiendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zitaendelea kuwepo, tumesema mara kadhaa mpaka mwisho wa dunia, lakini sisi tunampongeza Mheshimiwa Rais wetu kumpa comfort, kumpa nguvu, kumpa moyo zaidi na wasaidizi wake katika kazi kubwa wanayoifanya katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu kidogo niseme changamoto; katika Jimbo letu la Kilombero tuna changamoto ambazo zimetokana na utekelezaji wa mpango wa mwaka jana. Kwa mfano, tumepata kiwanda kipya cha sukari chenye thamani karibu shilingi bilioni 700 na tunaishukuru Serikali, lakini wakulima sasa hivi wana-experience kuchelewa kulipwa na kupungua kwa bei ya sukari, tuna changamoto ya barabara zetu, tumepata mafuriko sisi na Rufiji kuliko mtu mwingine yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba katika utekelezaji wa mpango unaokuja mtatusaidia kata 19 za Ifakara bado zina mashimo na hali ni mbaya, tunaomba mitaro na tunaomba madaraja. Pale Chicago kwa mfano barabara katika Kata ya Kidatu hakuna, kivuko cha Kidatu A kwenda Kidatu Kati, Daraja la Msola stesheni kuunganisha na Kata ya Mang’ula limekatika kabisa. Mji wa Ifakara wenyewe sasa hivi una hali ngumu. Kwa hiyo, hiyo ni changamoto mojawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo hilo la mafuriko na sisi tunajaza kwa 65% Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunaiomba sana Serikali na tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ametusaidia tumeweza kujenga tuta upande mmoja basi tunaomba tupate na tuta upande wa pili ili tuweze kukamilisha maendeleo yetu ya jimbo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha upo hapo na Mheshimiwa Waziri wa Mipango, mimi nataka kusema hili jambo ambalo lipo changamoto katika jimbo langu ili unisaidie na namshukuru sana Mheshimiwa Mkuu wangu wa Wilaya ameweza kulituliza jana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alienda jimboni kwetu, ametuzindulia daraja kubwa la Kidatu ambalo zamani tulikuwa tunapishana kwa magari kwa kusubiriana, ametuzindulia barabara mpya yenye kilometa 67 haijapita mwezi. Hata hivyo, nataka kukwambia sasa hivi ninavyokwambia, mkandarasi yule ameondoa watumishi (vijana wetu wote kazini) na amefungia vifaa ndani kwa sababu hajalipwa na mkandarasi anaitwa Reynolds Construction Company. Amewapa likizo kila mara watumishi wale vijana wetu na tunaenda kwenye Serikali za Mitaa na wengine walikuwa wamekuja Dodoma hapa jana na juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nilikuwa nakusubiri sana nikwambie jambo hili. Nakuomba yule mkandarasi alipwe na TRA anayoidai ama na Serikali mumlipe ili matunda ya ile barabara katika utekelezaji wa mpango uliopita tuweze kuyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu mimi nizungumze kidogo kuhusu kipengele cha malengo mahsusi ya mapendekezo ya mpango. Kipengele cha sita kinasema; “Kuendeleza kuimarisha amani, utulivu wa kisiasa nchini pamoja na usalama wa Watanzania.” Tunaweza tukaongea yote haya, lakini tunajifunza katika nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipolinda amani yetu katika nchi yetu utekelezaji wa mpango huu hatutoupata na tunajifunza katika nchi ya jirani. Ninaona kwenye mitandao, baadhi ya vijana wenzangu wanaona chokochoko kama Watanzania malofa kwa sababu hawaambukizwi na mambo yanayotokea katika nchi za jirani. Nawasihi vijana wenzangu, kuwaasa na kuwaomba tusikubali kusikiliza haya ya mzee mchekea mwezi, tulinde amani yetu kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu nizungumzie sasa vitu vitatu ama vinne kwa haraka haraka, kwanza nataka kuzungumzia population. Tunavyo-calculate maendeleo ya nchi yetu tuna-calculate mapato yetu yote kwa ujumla tunagawanya kwa Watanzania wote bila kujali nani anacho, nani hana na ndiyo tunapata per capita hiyo development. Mheshimiwa Waziri nawaomba sana, ni nani anafuatilia population ya nchi yetu? Tunajua ongezeko la watu linaenda sawa sawa na mahitaji ya labour force, siyo? Cheap labour kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Mawaziri niwaambie, mimi nilienda Mwanza pale na Kamati, juzi tulikuwa Dar es Salam tunaangalia TBC inavyorusha watoto wa Taifa hili wanavyolala kwenye maduka usiku. Watoto wa Taifa hili pale Mwanza tumewakuta, mimi nimewahoji angalia ile video yangu, watoto hawawajui baba, mtoto hajui mama. Sasa kama tunataka kwenda kwenye maendeleo ya kweli na Mheshimiwa Msambatavangu alishawahi kusema hapa siku moja, lazima tujiulize kijana wa kike na wa kiume wakiamua katika starehe zao kuzaa, watawajibika kulea. Hakuna Taifa ambalo tunaweza tukatelekeza watoto barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa na Mheshimiwa tunatoka pale nje tumekuta mama amebeba watoto watatu, kila mtoto na baba yake na wanaume wote wamemkimbia yule mama. Mama yule siku akichoka akitelekeza wale watoto, wanahesabika ni maskini wa Watanzania. Waheshimiwa Mawaziri haikubaliki, taasisi zinazohusika tunaomba sana msimamie population yetu, mui-control vizuri ili iweze kwenda na maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna video moja maarufu sana yule kijana wa Mbeya na mimi namtafuta, anayesimamisha vijana wenzake wa bodaboda anawaambia siyo ujanja kuzaa, kuzalisha wanawake na kupeleka kwa bibi. Anawaambia mimi nalea watoto wangu watatu nyumbani kwangu ni bodaboda, hata Mheshimiwa Hakimu akinihukumu leo anaweza kunipunguzia adhabu kwa sababu nalea mwenyewe. Kawakusanya vijana wenzake anawaambia wewe fulani huo ni ulofa, umezalisha watoto wanne umepeleka kwa bibi. Unazalisha unasema wanawake wanaojileta unazalisha tu. Watoto wanaenda mtaani, watoto yatima wanazidi na sasa hivi tuna utamaduni wa kujenga vituo vya watoto yatima, hatulei watoto yatima katika majumba yetu. Hatuwezi kufikia maendeleo ya kweli kama tunaongeza population ya namna hiyo ya holela holela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nigusie TRA; yote haya ya mpango na utekelezaji yanataka mapato, tulisema katika Taarifa ya PAC hapa. TRA wanataka kuwezeshwa kuwekeza katika mifumo ili wawajue walipakodi wote katika nchi hii. Tunaomba sana mtusaidie, TRA iweze kupatiwa fedha hizo iweze kukusanya mapato, lakini vinginevyo hapa hatutaweza kukamilisha mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni nataka kumalizia kwa kusema mimi naunga mkono hoja. Nasisitiza sana ili tupate maendeleo lazima tuangalie kila Mtanzania, kila kijana wa Kitanzania anayezaliwa anamulikwa katika nchi hii. Akizaliwa tunampa cheti cha kuzaliwa kinakuwa na namba ambayo ndiyo account ya benki yake ya Taifa na ndiyo kitambulisho chake cha Taifa hili na wazazi wake wawajibike kumtazama mtoto yule mpaka anapopata elimu ya msingi na elimu ya ufundi. Vinginevyo hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru. (Makofi)