Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninashukuru kwa kupata nafasi niweze kuchangia kwenye mpango huu ambao uko mbele yetu na nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya na kuhakikisha mpango huu unaenda kumkomboa Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imeeleza kwenye kauli yao kwamba mpango wa maendeleo unalenga kuboresha hali ya maisha ya Watanzania na kujenga uchumi imara na shindani na sisi tunataka tuone mpango huu namna ambavyo unaenda kuboresha maisha ya Watanzania, lakini vilevile kuendelea kuboresha uchumi wetu uendelee kuwa imara na ushindani.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mipango ya Serikali imekuwa inapangwa kila mwaka na ile ya miaka mitano, na ile ya miaka 25. Ni mipango mizuri na ambayo utekelezaji wake tunakuwa tumeuona, sisi sote humu na Watanzania wote wamekuwa mashuhuda namna ambavyo miradi mingi na ya kimkakati ambavyo imefanyika ndani ya nchi yetu. Ninaipongeza Serikali, nampongeza Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba hakuna kilichosimama, mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango hii mizuri ambayo ipo kwenye huu mpango wetu, lakini ili utekelezaji wake uweze kwenda vizuri kuna baadhi ya maeneo ya kuweza kushauri ili yaweze kukaa vizuri na utekelezaji wake kweli uweze kumnufaisha huyu Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku juu Tume ya Mipango pamoja na Wizara zinapanga vizuri na upangaji huu upo kwenye level ya huku juu ya Wizara, lakini tunaposhuka huku chini bado kuna changamoto ya hizi taasisi zetu kuweza kuongea lugha moja na kuweza kusomana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, leo kuna barabara zinajengwa na TARURA, barabara za lami au za changarawe, lakini mahali ambapo barabara hizi zinapita, ipo miundombinu mingine ambayo inapita, ipo miundombinu ya maji, umeme na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wa TARURA wanapotengeneza hizi barabara unakuta hawahusishi watu wa maji na matokeo yake wanaharibu miundombinu ya maji pamoja na miundombinu mingine ilhali hawa watu wa maji na miundombinu mingine hawana bajeti ya kuweza kurekebisha hii miundombinu. Matokeo yake, leo barabara zinatengenezwa vizuri, lakini tunaenda kutengeneza changamoto nyingine ya maji na miundombinu baadhi ya maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na nishauri, mipango ambayo inapangwa kuanzia ngazi ya huku juu Wizarani mpaka chini kwenye Serikali za Mitaa tuone namna bora ya kushirikisha hizi taasisi ili tusiwe tunafanya kazi ya kurudia rudia na kuingia gharama mara mbili. Niombe sana mlichukue hili na muweze kwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimeona kwenye mpango hapa wameeleza namna ambavyo Serikali imepanga kutumia zaidi ya shilingi trilioni 16 katika mipango mbalimbali na miradi ya maendeleo. Ni fedha nyingi, lakini kwa namna ambavyo miradi ya nchi hii inavyokwenda bado fedha hizi ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali pamoja na kwamba tunategemea kodi kuweza kupata hizi fedha, misaada pamoja na mikopo mbalimbali, tuone namna ya kuongeza walipa kodi wengine ili fedha hizi ziweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TRA pamoja na Serikali bado tunaendelea kuwakamua walipa kodi walewale Watanzania. Tunazibadilisha kodi kwa majina tofauti, lakini bado walipa kodi ni walewale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali ione namna bora ya kuboresha mazingira ili tuweze kuwatengeneza wafanyabiashara wapya ili waweze kulipa kodi mpya na ili tuweze kuongeza mapato kwenye nchi yetu, hii ndiyo itakuwa namna bora na nzuri ya kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili yake, tuna wafanyabiashara mitaji yao ni midogo, Serikali itumie hii nafasi ya kuona namna nzuri ya kuweza kuwasaidia kuweza kuwainua wao ili tuwatengeneze wafanyabiashara wakubwa pamoja na mabilionea wapya kwenye nchi yetu hii ya Tanzania. Hii itaweza kutusaidia kuboresha mazingira mazuri ya biashara ili wafanyabiashara wetu hawa waweze kufanya biashara katika hali nzuri zaidi, lakini tukiweza kuvutia wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la nishati; kila mmoja hapa ameweza kuzungumza namna ambavyo Serikali yetu imeweza kupambana kuhakikisha Bwawa letu la Mwalimu Nyerere limeweza kukamilika na sasa hivi tuna nishati ya uhakika ya umeme tunao wa kutosha, hii tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo na kuwa na umeme wa uhakika, Serikali sasa iwekeze nguvu kwenda kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa huu umeme. Bado kuna baadhi ya maeneo mengi umeme unakatikakatika, lakini ukiuliza, changamoto ni miundombinu ya umeme ambayo imeshachoka na imeshakuwa dhaifu. Hivyo, Serikali iweze kutumia muda huu kuweza kuboresha hiyo miundombinu ili umeme uweze kupatikana wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, (b) yake; baadhi ya maeneo tunapata umeme mdogo. Nami kule kwangu baadhi ya maeneo, Chunya, Makongorosi na maeneo ya Tarafa ya Kipembawe, umeme umefika, lakini umeme ni mdogo. Hivyo, bado wananchi wanashindwa kunufaika na ule umeme ambao unakuwa umefika kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, ni muda mwafaka wa kujenga substation ili kuweze kupata umeme wa uhakika, wenye nguvu ili wananchi hawa waweze kunufaika na umeme wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, (c) yake; pamoja na kwamba umeme ni huduma Serikali inapeleka, pia umeme ni biashara, pamoja na kwamba umeme ni biashara sasa tutumie nafasi hii kuweza kupeleka umeme kule kwenye uhitaji mkubwa ili wananchi wa Tanzania waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka kule Chunya ambako tuna wachimbaji wengi wadogo wadogo, wana uhitaji mkubwa sana wa umeme. Hivyo, Serikali iweze kuona na kuwekeza nguvu za kutosha ili kuhakikisha kwamba umeme huu unawafikia wachimbaji wengi kwenye maeneo yao ili waweze kuutumia, kuzalisha vya kutosha na waweze kuununua kwa sababu hii ni biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niweze kutoa ushauri, kama bado Serikali inaona kwamba kupeleka umeme kule gharama ni kubwa, iwakopeshe hawa wachimbaji wetu wadogo wadogo ili wanapokuwa wananunua umeme wawe wanalipa kidogo kidogo na ndiyo tutaweza kuwasaidia hawa wachimbaji wetu na wengi wataweza kufikiwa na umeme huo na itaweza kuwasaidia zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo limeelezwa kwenye Mpango ni sekta ya madini. Niishukuru Serikali, sekta ya madini imeweza kufanya kazi vizuri, lakini pia Serikali imeweza kwenda kuboresha mazingira ya madini. Leo imeweza kufikia zaidi ya 9% kwenye mchango wa Pato la Serikali, hii ni hatua kubwa sana. Hata hivyo, pamoja na haya 40% ya pato hilo bado ni kutoka kwa wachimbaji wadogo ili tuweze kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo hawa tunawawekea mazingira mazuri ili waendelee kuzalisha vizuri zaidi. Kubwa zaidi, tuendelee kuwekeza kwenye tafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuwekeza kwenye utafiti kwa wachimbaji wadogo, wataweza kuchimba uchimbaji wao mzuri zaidi na watazalisha vizuri zaidi. Pia tutaweza kupata kipato kikubwa na ile 11% ambayo Serikali iliweza kuipanga, tutaweza kuifikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)