Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Awali ya yote ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye Mpango wa Serikali wa mwaka 2025/2026. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ambayo leo nimeipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye Jimbo langu la Bunda Mjini ambapo zaidi ya miaka 30 iliyopita wananchi wangu wa Kata ya Nyatwali wamekuwa wakiishi katika maisha ambayo walikuwa hawawezi kujua mwanzo wao na mwisho wao. Hata hivyo, changamoto hiyo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameitatua kwa sababu hawa wananchi muda wote wameambiwa kwamba maeneo yale wanayoishi wangetakiwa kuhama. Kwa hiyo, zaidi ya miaka 30 iliyopita walikuwa hawawezi kujifanyia maendeleo yao ya msingi kwa sababu wana mambo mawili, ama wanaweza kuondoka kwenye eneo hili, ama inawezekana wakaendelea kuishi kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo hili lilikuwa linawaletea watu umaskini mkubwa kwa sababu walikuwa hawawezi kupanga mipango yao ya miaka ijayo, kwa sababu wanahisi tu muda wowote kwa chochote watakachokifanya pale wanaweza kuondolewa. Hata hivyo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake, imelipa zaidi ya shilingi bilioni 60 kwenye Kata ile ya Nyatwali na kuwafanya wale wananchi wetu waweze kwenda kupata mahali pao papya pa maisha yao mazuri ambayo na wao itawafanya wafanye mipango yao endelevu kwa ajili ya wao wenyewe na vizazi vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilikuwa ni kero kubwa katika Jimbo la Halmashauri ya Bunda Mjini. Kwa hiyo, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa aliyoifanya, lakini pia ninamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo alitupatia msaada mkubwa kwenye jambo hili ili kuhakikisha kwamba jambo hili linafikia mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru pia Waziri wa Fedha, Mkuu wangu wa Mkoa wa Mara pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bunda kwa namna ambavyo tumeshirikiana kwenye jambo hili. Wananchi wetu wale wameishi katika kadhia kubwa kwa muda mrefu. Hawawezi kuvuna, kujenga wala kufanya chochote kwa sababu tu wanaambiwa kwamba muda wowote wanaweza kuhama. Sasa kwa sababu Serikali imetatua tatizo hili, imewafanya wananchi wetu waweze kupata mwelekeo mpya na mpango mpya wa maisha yao huko wanakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninasema ahsante sana kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi hiyo kubwa ambayo wameifanya kwa ajili ya wale wananchi wetu wa Jimbo la Bunda Mjini hasa ile Kata ya Nyatwali, kwa kuwafanya sasa na wao waweze kupanga mipango yao mizuri katika maisha yao. Pia ninaamini huko ambako wao wamekwenda, watakwenda kufanya vizuri kwa sababu Serikali imewalipa fedha zao vizuri, ingawa bado kuna changamoto ndogo ndogo ambazo ninaamini tu kwamba bado Serikali inazishughulikia na itazitatua changamoto hizo zikaisha vizuri, ili wale wananchi wetu waweze kuishi vizuri katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika Mpango huu, ni kuiomba Serikali kuhakikisha kwamba Mpango huu unachukua jambo kubwa ambalo wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wanalitegemea. Kumekuwepo na ule Mradi wa TACTIC ambao kwa muda mrefu wananchi wetu wameahidiwa na bado jambo hili halijafanyiwa kazi. Pia ndilo deni kubwa ambalo limebaki katika Halmashauri ya Mji wa Bunda. Niombe katika mipango hii, jambo hili nalo liingizwe ndani ili utekelezaji utakapoanza mradi huu uweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la maji; mpango huu ujikite pia katika kutatua changamoto za maji kwa wananchi wetu. Huko tunakokwenda maeneo yanazidi kuongezeka, idadi ya Watanzania inazidi kuongezeka. Kwa hiyo, tatizo la maji bado litaendelea kuwepo. Kwa hiyo, lazima mpango useme kwa muda mrefu kuwa tatizo la maji litatatuliwa vipi kwa wananchi wetu, kwa sababu kila leo tunapokamilisha na kusema mfumo wa maji umefikia hapa na wananchi walikuwa wanaishia hapa, baada ya mwaka mmoja wananchi wameongezeka na eneo limepanuka zaidi. Kwa hiyo, tatizo la maji linazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la umeme, kwa sababu Serikali yetu imekamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linatusambazia umeme kwenye nchi yetu, kwa sasa Serikali inakwenda kusambaza umeme kwenye vitongoji, na vitongoji ndiyo mahali pa mwisho ambapo wananchi wetu wanaishi hasa wale ambao ni wakulima na wafugaji ambao pia siyo wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilidhani mpango pia ungesema kwamba hawa wananchi badala ya kuwaambia watoe fedha za kuunganishiwa kwenye umeme, wao waruhusiwe na Serikali iwaunganishie umeme kwenye maeneo yao. Baada ya kuwaunganishia umeme, hawa wananchi walipe ile gharama ya kuunganishiwa umeme kupitia bili zao. Kwa nini? Kwa sababu hawa ni wakulima, wafugaji na ni wale watu ambao wanaishi katika hali ya maisha ya chini kabisa. Pia kwa sababu sasa hivi umeme katika nchi yetu unazalishwa kwa kiasi kikubwa, mimi ninadhani Serikali itengeneze mpango wa kwamba hawa wananchi na wao waunganishiwe umeme ili na wao wanufaike na jambo la umeme kama vile Watanzania wengine wanavyonufaika na umeme. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maboto, kengele ya pili, ninaomba unga mkono hoja.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)