Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo kwa ajili ya mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa Maendeleo nilikuwa ninaangalia katika eneo ambalo linanigusa, naona ni namba 2, 3 na 6 kitu kama hicho. Hili eneo lilikuwa linazungumzia maisha ya watu na hali ya umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikiri kwamba Mheshimiwa Profesa Mkumbo ni mwalimu wangu, kwa hiyo, pamoja na kuandaa kilichoandaliwa na mwalimu wako na hasa alinifundisha katika eneo hilo hilo la watu, umaskini, pamoja na siasa na namna ya kuwaondoa watu katika umaskini. Hili somo ni kwamba Profesa alinifundisha na mimi ninalifanyia kazi. Sasa siwezi ku-doubt chochote hapo kuhusiana na mwalimu, ila ninataka kumkumbusha tu mwalimu wangu kwamba katika hili kuna maeneo ambayo ameyasahau hasa ya wananchi maskini walioko vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kutengeneza furaha ya wananchi wa Tanzania, ni kwamba lazima uwaangalie wananchi maskini walioko vijijini, hali zao na watatoka vipi katika zile hali. Kwa hiyo, katika mpango wako na katika jambo hili, kule vijijini maisha ni magumu sana na ni maisha yao ya kila siku. Mheshimiwa Profesa pamoja na Waziri wa Fedha, bahati nzuri ninyi nyote ni watoto wa maskini, mmefika katika hatua hii, mnajua kilichoko kule kijijini hususani katika Jimbo la Iramba mnajua kabisa kwamba magulio ni sehemu ya maisha ya wananchi kwa kila siku. Liangalieni Gulio la Shelui na Ndago, haya ni magulio tu ambayo nawapeni mfano wake yalivyo, lakini angalie Gulio la Kinampanda wananchi wanategemea kuendesha maisha yao na kuhudumia familia zao kutokana na gulio. Kwa hiyo, gulioni wanakwenda kuuza na kununua vyakula vya kutumia. Watatunza vyakula vyao mpaka gulio lingine tena labda Jumamosi au Ijumaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika Mpango wenu wa Maendeleo, sijaona kabisa kwamba hawa wananchi wa namna hiyo mnawasaidia kwa namna gani, kwa sababu kule ndiko ziliko biashara ndogo ndogo zinazowafanya wananchi sasa waweze kutoka katika umaskini na wanapata pato lao la wiki na pato la mwezi linategemea kutokana na magulio. Hali ya magulio nchini siyo nzuri. Magulio yetu hayana vyoo, hayana mabanda ya kujikinga na mvua pale mvua zinaponyesha wakati watu wanafanya biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya magulio kuna minada. Iko minada mikubwa kwenye nchi hii, ukitembea kila mkoa na kila wilaya minada hii ipo. Hata hivyo, kwenye hiyo minada na yenyewe haijawekwa kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mizani; Waziri, Mheshimiwa Ulega alituahidi hapa kwamba atagawa mizani katika halmashauri ili iweze kuwekwa katika minada yetu. Watu wanafuga ng’ombe wao na mbuzi wao, wanakaa nao kwa muda mrefu (miaka mitatu), lakini anakwenda sokoni, anakwenda kupunjwa. Bei ya nyama sasa hivi zinaanzia shilingi 10,000, lakini mfugaji amekaa na ng’ombe wake anakwenda kumuuza kwa gharama ya chini. Hata hivyo, mizani ikiwepo, anaweza kumpitisha kwenye mizani na akajua hali aliyonayo. Hili halijawekwa kwenye Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuomba sana Profesa hili jambo utusaidie sana kuliingiza ili kuangalia magulio yetu na wananchi watapataje mitaji ili kuweza kujiondoa katika umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la umeme, kwa mfano sisi pale Sengerema tunapokea umeme kutoka Mpomvu – Geita na tunapokea umeme kutoka Nyakato - Mwanza. Wakati tunatengeneza lile daraja (walipokuwa wanafanya upembuzi na usanifu), wakati wanafanya kazi ya kuchoronga kuangalia miamba chini, walikata ule waya na bahati nzuri wakati ule Waziri wa Nishati alikuwepo hapa Mheshimiwa January Makamba, alituahidi kabisa kwamba baada ya daraja kukamilika watapitisha waya darajani. Hili jambo halijafanyika na Mungu akijalia mwaka kesho daraja linafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba katika mpango tujue ile cable itarudishwa au haitarudishwi ili wananchi wa Sengerema sasa tujue nini cha kufanya kwa sababu Sengerema tuna tatizo la umeme kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la leseni ya mgodi wetu sisi, (Leseni ya Mgodi wa Nyanzaga). Mheshimiwa Profesa tulikwenda na wewe mpaka pale Nyanzaga, tumekwenda Nyanzaga kwa wale wamiliki wa awali wa mgodi ule wa Sotta Mining, tumepiga mikutano tuko na wewe na tumetembelea ile milima yote. Pia wakati wanakusomea taarifa walisema kwamba watapunguza kwenye leseni zao shilingi 225 na watatoa leseni 50 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo kwa Wilaya ya Sengerema na Mkoa wa Mwanza. Lile jambo mpaka sasa hivi hawajafanya na mwaka 2025 Mungu akijalia wanaanza kujenga mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka kujua kwamba leseni hizo zitatolewa? Kwa sababu ilikuwa ni ahadi za mkutano wa hadhara na juzi amekuja kule Mheshimiwa Mavunde, amekuja kuwauliza na wao wakasema kwamba wao hawakutamka maneno hayo. Wewe ulikuwa ni Waziri wa Uwekezaji na uko hapa, tayari kuna mgogoro mwingine Sengerema wa kimaslahi kwa sababu tumesema hali ya umaskini na watu, hatuwezi kuwa na mgodi wananchi wanakaa wanauangalia. Pia mmeona migodi mingine yote (Nyamongo na wapi) mnaona fujo zinazotokea katika migodi. Sasa hili jambo tunaomba sana katika mpango wenu mliweke mara moja ili tuweze kuondokana na hali hii ya umaskini na kuwaondoa wananchi wetu wa Wilaya ya Sengerema katika hali ya umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni miradi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tabasam…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie hapo kidogo tu.
MWENYEKITI: Malizia.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni wakandarasi wetu wa ndani, tunaomba wakandarasi wa ndani wawepo katika mpango wa kulipwa madeni yao. Tunao makandarasi hali zao ni mbaya, wakandarasi wanauziwa nyumba zao na hivi tunavyozungumza wazabuni hali zao ni mbaya. Tunaomba kwenye mpango tuone tunawasaida kwa namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)