Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu, nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/2026 pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais - Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu - Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu - Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko pamoja na wasaidizi wao wote kwa namna wanavyoshirikiana na kuhakikisha Serikali inafanya kazi kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wetu wa Fedha Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba, pamoja na Naibu Waziri wake na Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Kitila Mkumbo pamoja na Naibu Waziri wake, pia Makatibu Wakuu wao wa Wizara zote mbili kwa ushirikiano mkubwa ambao wametupatia kwenye Kamati yetu ya Bajeti. Naomba waongeze ushirikiano huo kwa Kamati nyinginezo pia pindi wanapohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza na kukamilisha miradi yake mikubwa hasa ya kielelezo na kimkakati. Tumeona mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere sasa liko kwenye kukamilika na hata hivyo, tumeona matunda yake. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR, kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Wananchi tumeona matunda yake na tunayashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ahadi yake alipokuwa ziarani Mkoani Ruvuma ambapo aliahidi atajenga reli ya kutoka Bandari ya Mtwara hadi Bandari ya Mbamba Bay. Ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa mikoa inayopitiwa na ujenzi huo, ikiwemo Mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara, Njombe na maeneo mengine ya jirani. Ujenzi wa reli hiyo utapunguza uharibifu wa barabara unaofanywa na malori ya makaa ya mawe na pia utaondoa uharibifu na msongamano wa magari maeneo ya mijini. Vilevile utapunguza ajali, ikiwemo eneo la Songea Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye eneo la ulipaji wa madeni ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma. Kwenye ukurasa wa 59 wa Taarifa ya Kamati umeeleza, uchambuzi wa Kamati umebaini kwamba hadi Juni, 2023 jumla ya madeni yaliyohakikiwa yalikuwa ni shilingi trilioni 3.3 na kiasi cha madeni ambayo hayajahakikiwa ni shilingi bilioni 64.7. Hata hivyo, Serikali haijabainisha endapo madeni ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma ndio ambayo hayakuhakikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili naomba nilizungumze hivi, ziko baadhi ya taasisi zetu za Serikali, hasa upande wa halmashauri, tuna kawaida ya kuanzisha miradi mipya kila mwaka wa fedha unapoanza, wataalamu pale wanaanza na mradi mpya. Anaangalia faida yake yeye, kamisheni, yaani ten percent mradi mpya unapoanza maana atapata chochote ule mradi ukianza, bila kujali kuna fedha ambayo itasaidia kukamilisha mradi ule au laa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, kama tumeamua kuweka kwenye mwongozo naomba tuzingatie, tuusimamie mwongozo ule. Ni vyema tukakamilisha kwanza madeni yetu ya wakandarasi na watoa huduma wetu wote wa nyuma, tukifanya hivyo, watakuwa na ari mpya ya kuendeleza miradi ile ambayo wameianza. Wakandarasi wengi wameacha kufanya kazi kwa sababu wanaidai Serikali na siyo kwamba Serikali inadaiwa Hapana, ni wataalamu wetu ndiyo wanasababisha haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukijipanga Wakurugenzi hawa ambao wako kwenye zile halmashauri hakuna kuhama mpaka mradi wako ukamilike. Hawatahamishwa, wakikamilisha yale maana yake ndiyo wahamishwe, lakini kama Mkurugenzi atahamishwa pale anaacha mradi kiporo, Mkurugenzi anayekuja anaanza na mradi wake, hiyo siyo sawa. Mipango yetu hatuwezi kwenda nayo kwa mtindo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano kwenye baadhi ya mikoa ambako hata mimi nimeona na nimepitapita. Watalaamu wetu wengi wanapenda kumrubuni Mkurugenzi. Mkurugenzi kuna mradi huu hapa unatarajia kutekelezwa kwa fedha kidogo tu, tutafute fedha, tutapata fedha nyingine, wakati huo analenga faida yake yeye. Hiyo siyo sawa, tunawaumiza wakandarasi wetu. Tumeona wakandarasi wengi wamefilisika, wengine wamekufa kwa kuidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme Serikali hii haidaiwi yenyewe kama Serikali, wanaosababisha ni wataalamu wetu. Naomba wataalamu wetu huko kwenye halmashauri muionee huruma Serikali. Serikali haina fedha ya kuweza kutekeleza miradi kila tunapoibua tu mradi mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kama tumeamua kutekeleza miradi viporo kwa awamu hii, twende na utaratibu huu. Tuanze kulipa madeni yote ya wakandarasi, tukishakamilisha twende kwenye miradi viporo, ile miradi viporo hatuwezi tu kwenda kusema tunatekeleza miradi viporo ni lazima tufanye tathmini. Tathmini ile kama itaundwa kamati kimkoa au kiwilaya ikatambua miradi iliyopo kwenye lile eneo maana yake iainishwe na ipangiwe bajeti yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta kuna miradi mingine kwa mfano, miradi ya barabara, imetekelezwa mwaka juzi wameweka vifusi barabara imejengwa. Haya mvua imepita, barabara imeenda na maji, tunapoenda kukagua au kuhakiki hayo madeni, tukienda kuangalia hiyo barabara tunakuta nyasi zimeota, pale tutakuta barabara? Huyu mzabuni au mkandarasi tutamlipaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali tuwe serious na hili kama tumeamua kulipa madeni ya wakandarasi na watoa huduma. Tulipe hayo madeni na kama tumeamua ku…
(Hapa kipaza sauti kilikata mawasiliano)
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo nimalizie.
MWENYEKITI: Ahsante, naomba u-wind up. Malizia.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeamua kukamilisha hiyo miradi viporo, naomba tukamilishe kweli miradi viporo na baada ya kukamilisha hayo, ndipo tuanze na miradi mipya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nashukuru. (Makofi)