Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Mpango huu wa mwaka 2025/2026. Nimejaribu kusoma Mpango huu, hotuba zote nimeona ni nzuri na zinatupeleka pale ambapo Watanzania wengi watakuwa na matumaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye vipaumbele kuna vipaumbele vitano ambavyo ni kuendeleza miundombinu, kusimamia huduma za jamii, mazingira na tabianchi, usimamizi wa utawala bora na kugharamia uchaguzi wa mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa ningetamani ingekuwepo pia kusimamia na kuimarisha biashara za ndani na nje, sikuiona katika kipaumbele, hayo ndiyo maisha ya watu. Tumeona kwamba hizi zote zinakwenda katika Serikali, katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ni jambo jema sana, lakini biashara ndiyo ambazo zinawafanya wananchi wanakuwa na fedha mifukoni ambazo zinawasababisha kuwa na umaliziaji wa mahitaji yao kama chakula na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nilitamani sana liwepo katika kipaumbele chetu katika mpango huu. Sasa tukisema biashara, nilitamani kwamba sehemu zetu za Wamachinga hawa zipewe kipaumbele na siyo kama hivi tunavyofanya sasa hivi. Tunawajengea Wamachinga nje ya mji matokeo yake wanakimbia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoa mfano pale Kariakoo, nchi nyingi tunavyokwenda hatukuti vurugu kama zile, lakini katikati ya nchi, katikati ya mji, unakuta kuna mall kubwa sana la Wamachinga peke yao ambalo linaweza kwenda ghorofa kumi na kwa upana, zaidi ya ekari mbili. Utakuta kwamba wameingizana humo wanafanya biashara na watu wanakwenda maalumu kwa ajili ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunawatoa nje, jambo hili nilitamani Serikali ilipe kipaumbele. Mfano mzuri ni pale Kariakoo, sasa hivi tunajenga majumba yale, kwa nini tusichukue nyumba hata 20 tukajenga hiyo mall kubwa wakaingizwa Wamachinga, naamini wasingefanya vurugu na kila mtu angetamani kwenda Kariakoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye suala la kuimarisha TEHAMA kwa ajili ya makusanyo ya nchi. Mimi nilitamani Bodi ya TTB, hawa TTB na watu wa maliasili wawe ndiyo pilot wetu kwa sababu wenyewe kwenye Ripoti ya CAG kule wamesema hawajaanza na wataanza. Sasa wawe pilot kwa sababu mapato makubwa hapa yanapotea, sasa TEHAMA ikaanzie huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kipaumbele cha mwisho, kugharamia uchaguzi wa mwaka 2025. Zanzibar kule kulitokea mauaji kwenye uchaguzi na mwanzo wake ulianzia kwenye gharama za uchaguzi, sababu kubwa ilikuwa ni uchaguzi wa mara mbili. Sasa sisi kama Wazanzibar hatuhitaji uchaguzi wa mara mbili, uchaguzi uwe ni wa pamoja na kwa nini nasema hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliopiga mwanzo walikuwa ni Watendaji wa Sekta za Muungano na kwa hiyo, bila shaka Serikali ya Muungano inahusika na hili. Kwa hiyo, tunahitaji tufanye uchaguzi, usiwe na malalamiko na usiliingizie Taifa hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitachangia kwenye suala la connection ya umeme. Mimi siku zote nimekuwa nikichangia suala la umeme, kutenganisha mijini na vijijini katika connection fees, hili si muumini nalo kwa sababu wananchi hata kule mjini kuna maskini wengi na hawana uwezo, lakini hata connection kwa sehemu za mijini ni rahisi kwa sababu ukiutoa nyumba hii unaingia nyumba hii, lakini vijijini ni lazima unapata nguzo mbili, tatu, gharama ni kubwa. Sasa wanapokuja na mpango wao, wanapokuja kwenye bajeti, wamshauri Mheshimiwa Rais naye alikubali hili kwa sababu yeye ndiye walimweleza, wakamdanganya Mheshimiwa Rais, akakubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunavyohitaji ni kwamba wananchi wote connection fee hii iwe moja, kwa sababu tariff za umeme ndiyo zinaweza kurudisha gharama za connection, siyo hii connection. Wananchi wa mijini sasa hivi hawana umeme, unakuta nyumba tano, sita, ambao gharama zake ni ndogo. Kwa hiyo, ushauri wangu ni huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni suala la afya; suala la afya bado tunalichezea, tumepitisha Sheria hapa ya Bima ya Afya kwa Wote tunaimba, lakini utekelezaji wake haufanyiki, mwisho tunasikia utafanyika mwaka 2026. Wananchi wanaumia, sasa hivi wanakufa, hawaendi hospitali kwa sababu hawamudu gharama za kwenda hospitali. Kila siku tunapiga blabla tu, leo mara unasikia sijui kuna kongamano, kuna nini, lakini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka bima ya afya ya wote na ambayo kila mtu ambaye atakuwa amekata huduma hii, basi apatiwe, siyo kuchagua aina ya magonjwa. Jambo hili si zuri na halikubaliki, tunahitaji anayeumwa kansa atibiwe, anayeumwa figo atibiwe, tuna anayeumwa homa atibiwe, mwisho Watanzania wote wawe na afya njema na bora na wawe wazalishaji mali wanaoipenda nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)