Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa ambao umewasilishwa Mezani. Naomba nikubaliane na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango ambaye alisema, na naomba nimnukuu kwamba, furaha ya wananchi, furaha ya Watanzania imeongezeka baada ya Serikali yao kukamilisha miradi mikubwa ya SGR. Yeye alisema na DP World, lakini mimi naomba niweke na Bwawa la Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa wale ambao wamesafiri na SGR wote wanafurahia maamuzi, utashi na utekelezaji wa Serikali yao wa kufanikisha miradi mikubwa. Kwa jinsi hiyo, ni kweli kwamba inadhihirisha kwamba kumbe Serikali ikiamua, ikapanga vyema, inaweza kufanya mambo makubwa ambayo yanaongeza furaha ya wananchi na kwa kweli hili Serikali heko sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu SGR imerahisisha usafirishaji. Kila mtu sasa hivi anatamani kusafiri kupitia SGR ili apunguze masaa mengi ya kusafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Saalam. Tunaiomba Serikali yetu, kwa kweli vile vipande vya kutoka hapa Dodoma kuelekea Mwanza na vyenyewe vifanywe haraka kwa umahiri huo huo ili tuweze kurahisiha usafirishaji. Pia, ni kweli kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere limeongeza nishati, umeme umekuwa mwingi na mgao umepungua na hilo nalo limeongeza furaha ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa utashi huo huo ambao Serikali imeweza kufanikisha miradi hii mikubwa, furaha ya Watanzania itakuwa maradufu iwapo miradi ambayo imeendelea kuwa inatajwa mwaka hadi mwaka na yenyewe ikatekelezwa mapema kwa kadiri ya inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano, Mradi wa Kusindika na Kuchakata Gesi (LNG), Mradi huu ukikamilika au ukianza mapema ni kichocheo cha viwanda vya mbolea na viwanda vya kemikali, vyote ambavyo kwa sasa tunapoongea BRT tunaagiza mbolea nje. Kumbe kama LNG ingeanza mapema na baada ya hapo tunakapata viwanda vinavyotokana na LNG vya mbolea, maana yake tuta-save fedha nyingi inayotumika kuagiza mbolea, kumbe ikapatikana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa pili, Mradi wa Chuma na Vanadium wa Liganga, mradi ambao umeendelea kuwa unahuishwa mwaka hadi mwaka katika mipango na hotuba za Bajeti za Serikali, tunajenga reli kwa kutumia chuma kingi sana. Ingekuwa ni habari gani kwamba tungezalisha chuma chetu wenyewe na hivyo kikasaidia kutokutumia chuma ambacho hakitokani na viwanda vyetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja yangu hapa ni kwamba, kwa utashi ambao Serikali imefanikisha miradi mikubwa, basi miradi hii mingine nayo ambayo imeendelea kuwa inaongelewa mwaka hadi mwaka, mimi ningetamani rafiki yangu Mheshimiwa Prof. Mkumbo, Mpango useme lini? Tusiendelee kusema tu, yaani LNG tunasema tunapanga, tunapanga, tunapanda, tuseme ni lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vihatarishi ambavyo mimi ninaviona katika hili ni kwamba majadiliano yanachukua muda mrefu. Tumeendelea kuwa tunajadili, lakini hatuweki ukomo. Ningetamani ili tuweze kupata manufaa ya kazi na miradi mikubwa inayoendelea, tuangalie kwamba majadiliano yafupishwe ili ifikie mahali miradi hii ianze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunaongea habari ya bajeti na kubana matumizi, lazima tunapofanya majadiliano ya mambo haya makubwa kwa mfano, LNG na taasisi za kimataifa, tuzingatie kwamba watu wawekeze weledi mkubwa katika majadiliano ili Serikali isiendelee kupoteza fedha za kutoingia katika mikataba ambayo ni ya maslahi kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana tumeendelea mwaka hadi mwaka kulipa mabilioni ya fedha kwa sababu ya mikataba, kwa sababu tupo katika level ya majadiliano, basi tuweke weledi hapo na uzalendo wa kutosha ili tunapoingia mikataba tupate fedha na siyo tena tuhamishe fedha ndani kupeleka kuwalipa ambao ni wadau wetu wa nje na hatimaye Serikali ikapoteza fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia katika mpango, napenda kutambua kwamba, mojawapo ya mambo ya msingi katika utekelezaji wa bajeti ni kubana matumizi ya fedha za uendeshaji (fedha za utawala) na badala yake kuwekeza fedha nyingi katika shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ni kuwepo kwa utendaji wa pamoja. Nilitafuta neno hili kwa Kiswahili sikulipata vizuri, lakini ni synergy baina ya Wizara na Wizara, taasisi na taasisi katika Serikali. Hili jambo ninaamini linaleta tija na matokeo na mwisho wake ni huduma bora kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano ambao napenda kuuweka mezani asubuhi ya leo. Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji, Mamlaka za Maji nchini zimeendelea kuwa zinatumia gharama kubwa sana katika uzalishaji wa maji. TANESCO imeendelea kuwa inatoza gharama kubwa hizi ikihusisha gharama za KwH, KvA na VAT na gharama ya kuanzisha mtambo. Yaani zote hizi zinawekwa mteja anapotumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, DAWASA Dar es Salaam na Pwani wanatumia shilingi bilioni 2.5 kwa mwezi kwa ajili ya kuzalisha maji wakiilipa TANESCO. Arusha wanatumia shilingi bilioni moja; KASHWASA (Kahama na Shinyanga) shilingi bilioni 670; DUWASA hapa Dodoma tunapokaa wanatumia shilingi milioni 700 kwa mwezi kuzalisha maji kwa ajili ya kutoa huduma ya maji. Kwa nini napendekeza jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunao umeme ambao unaonekana unatosheleza mahitaji, unaotokana na ukamilishaji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, pendekezo langu ni kwamba, kwa sababu tunao umeme wa kutosha, badala ya Watanzania kuomba tupunguziwe bei ya umeme, Mamlaka za Maji zipewe special tariff ya umeme. Kupewa special tariff ya umeme maana yake ni kwamba watapunguziwa gharama ili waweze kuzalisha maji kwa bei ndogo na hatimaye hayo yanayotokea kwa kupunguziwa tariff wananchi waweze kupata maji kwa gharama nafuu. Pia, Mamlaka za Maji ziweze kuweka miundombinu nyingine mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba umeme umepunguzwa kwa section moja ya Serikali, siyo kwa wananchi wote, lakini kwa kuipeleka katika mamlaka za Serikali ukaipa special tariff maana yake ni kwamba, kila kitu huko ambacho kinakwenda kwa mwananchi, kinakwenda kikiwa katika gharama nafuu ambayo mwananchi anaweza kuimudu. Kwa hiyo, katika mpango huu, siyo jambo ambalo nimeliona katika Mpango, lakini napendekeza kwamba Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji waweze kukaa pamoja halafu washushe tariff kwa hizi mamlaka za maji. Kwa mfano, kwenye VAT, Maji ni huduma, lakini unatoza VAT Taasisi ya Serikali na Serikali. Maji ni huduma, unatoza gharama ya kuanzisha mtambo KvA, kwa hiyo, gharama inakuwa kubwa unnecessarily. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pendekezo langu ni kwamba, naomba kuwe na special tariff. Mheshimiwa Prof. Mkumbo rafiki yangu ninaziombea mamlaka za maji special tariffs, bei iliyoshuka ya umeme kwa Mamlaka za Maji tupate maji kwa bei nafuu halafu Mamlaka za Maji ziweze kusambaza maji mengi kwa wananchi. Ninaamini pamoja na hayo, furaha ya wananchi itaendelea kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi. Nakushukuru sana. (Makofi)