Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia mchakato wa kutengeneza mapendekezo na mwongozo huu ambao tunaujadili siku ya leo, maono yake na maelekezo yake ambayo ninaamini yamesheheni kwenye maandiko ambayo tumepokea ya mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, nawapongeza pia Mawaziri wanaohusika kwa sababu ninaamini kusema kweli wamechakata vizuri yale maelekezo waliyopewa na Mheshimiwa Rais. Vilevile, nazipongeza na timu zao kwenye Wizara hizi mbili zinazohusika na Tume ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma maandiko yanayohusiana na hali ya uchumi ambayo wameeleza vizuri sana kwenye Mpango na Mwongozo utahitimisha kwamba, uchumi wa dunia, uchumi wa kanda na uchumi wa Tanzania sasa unaelekeza kwenye hali iliyokuwepo kabla ya UVIKO-19, utaona kwamba, hali ya uchumi kwenye nchi zote duniani kwa mfano, ongezeko la pato limefikia kwenye 3.3% na kwenye nchi hizi ambazo zimeendelea utaona ongezeko la pato lao linakwenda kwenye 1.7% mpaka asilimia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hivyo ilivyo kwa nchi zilizoendelea, haziwezi kuendelea kukuza uchumi wao kwa kiasi kikubwa kwa sababu resources zinakuwa almost fully employed na hawana uwezo wa kukuza sana mapato yao kama sisi tunavyostahili kukuza kwenye asilimia tano mpaka 10%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, utaona kwamba mfumko wa bei duniani umepungua kutoka 8.1% umefikia kwenye 5.9% katika kipindi cha mwaka huu tulionao. Kwa hiyo, naona kwamba maendeleo haya tunaona mwelekeo unatupatia fursa nyingi. Kwa mfano, ikiwa mfumko wa bei umeshuka; na ninyi mtakumbuka kwamba nchi zinazoendelea ikiwemo Marekani zilianza kutekeleza Sera ya Kubana Money Supply (Ujazi wa fedha) kwa kuongeza riba mara tu, inflation ilivyokuwa juu sana. Sasa, inflation imeshuka kwenye two digit, sasa hivi ipo kwenye 5.9% kwa wastani na kwenye nchi nyingine inashuka. Kwa mfano, wanaita secure overnight financing rates (SOFR) ambayo imekaa badala ya LIBOR. Sasa hivi ipo kwenye 3.5%. Hii inasema nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasema kwamba, nchi ya Marekani inaelekea sasa kulegeza ile Sera ya Fedha ya Kubana na kwa hiyo, riba zitashuka na itatupatia fursa sasa ya kuweza kukopa kwa gharama nafuu sana ukilinganisha na zile ambazo tumekopea mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ni kwamba hii SOFR ni inasema ndiyo benchmark ambayo unaongeza kwenye ile grace premium ambayo mmekubaliana. Kila wakati ikipanda ina maana na gharama zako zinapanda hata kwa mikopo ya nyuma. Kwa hiyo, ninaamini kwamba gharama za ku-service mikopo zitapungua na kuchukua mikopo mingine zitapungua na ninaamini Serikali itakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mazuri sana yametokea kwenye nchi zilizo kwenye Kanda yetu ya East Africa na SADC, inflation imepanda sana. Kuna nchi kwa mfano Burundi, inflation yao ni takribani 20%; ukienda South Sudan, inflation ni 40.2% na ukija hata kwenye nchi nyingine za East Africa zinakuwa zina inflation kubwa kuliko ya kwetu ambayo ni asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya hizi inflation kwenda juu ni upungufu wa vyakula, lakini sisi tuna vyakula na tuna-reserve kwenye NFRA. Kwa hiyo, naamini kwamba sasa tunaweza tukafaidi na tukaruhusu wananchi wetu wakanufaika kwa kuwawezesha kuuza chakula kile karibia na msimu mwingine unaingia kwa bei nzuri, lakini siyo tu chakula, na bidhaa nyingine ambazo zinazalishwa kwenye viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa bajeti yenyewe utaona kwamba bajeti ya mwaka huu imepanga kutumia shilingi trilioni 55.1. Sasa hilo ni ongezeko la 16.2%, ni ongezeko kubwa sana. Ongezeko la mapato ni 12.6% kutoka trilioni 34.6 hadi 38.46. Kwa hiyo, utaona kwamba matumizi yanakua kwa kasi kubwa sana ukilinganisha na mapato. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kuangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba bahati mbaya kwenye matumizi, bajeti ya maendeleo sasa inapungua kwa uwiano wa bajeti yote. Inapungua, inakwenda kwenye 29.9%. Kwa miaka ya nyuma hii mitatu iliyoisha, bajeti ya maendeleo ilikuwa inachukua 33.7% ya bajeti yote. Mimi ninaamini kwamba tulikuwa tumejiwekea some sort of indicative parameter kwamba, bajeti ya maendeleo isipungue chini ya 30%, lakini naona kwa mwaka huu inakuwa ngumu kidogo kwa sababu pengine kuna uchaguzi, gharama zinakuwepo za ziada na tunafungua vitu vingi vipya kwenye miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuongeze matumizi ya kawaida, lakini tuangalie vizuri tusiondoke kwenye benchmark ya 30%. Tujaribu kwenda kwenye hilo. Niseme kwamba bajeti hiyo kwa namba imeongezeka kwa 7.4%, lakini bado uwiano wake kwa bajeti nzima siyo mzuri. Ubaya mmoja wa ongezeko kubwa la namna hii, halafu tunaweka kwenye ukomo, tunaunda pipeline kubwa ya miradi ambayo haitekelezeki ikamalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kinachotokea ni kwamba ile bajeti ya kawaida inakuwa disbursed, lakini bajeti ya maendeleo inabakia kuwa Mawaziri wameshapewa ukomo, kwa hiyo, Julai wana-contract ile miradi yote bila kujali kwamba, je, fedha itapatikana? Tunazungumzia cash budget, lakini inakuwa siyo cash budget.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi imeshakuwa contracted, wameshapewa advance payment, kwa hiyo, unakuta ile miradi inaanza kukaa kwenye pipeline, fedha haiwi disbursed kwenye ile miradi. Hii ndiyo chanzo cha tatizo hilo unaloona la kusema kwamba, jamani sasa mbona hawalipi? Mbona wameondoka kwenye miradi! Wakandarasi hawafanyi kazi, wanaondoka, wanakimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba kwa sababu pipeline ipo na inakuwa carried forward from a year to a year. Ukiangalia deficit tunayopata kwenye makusanyo ni five percent, yaani kwa miaka mitano ukichukua tumefanya hesabu hizo ni five percent tuna-miss kila mwaka. Sasa, kila mwaka uki-miss five percent kwenye 40 trillion ina maana kwa five years unakuwa umeshaunda pipeline ya vitu ambavyo havijalipika kwa sababu ya makusanyo, 10 trillion. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama hiyo ni ya kweli, lakini ukweli ninaamini kwamba kwenye pipeline Wizara ya Fedha ikiangalia vizuri itakuta kuna vitu vya kulipa. Wakandarasi wa kuwalipa na hawa wa chakula shuleni kama 10 trillion it is a lot of money.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hivi, Serikali sasa iwaagize Maafisa Masuuli waweke line item kabisa ya kulipa madeni haya na ninashukuru kwamba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu alivyo-present alisema kwamba mwaka huu hawataingia kwenye miradi mipya. Nafikiri that is nice and it is a very good stance. Wafanye ili waweze kuweka ile line walipe madeni ya zamani, halafu ndiyo tuanze sasa kuwekeza, lakini ile ya vituo vya afya vya kimkakati msituache solemba na msitutoe, acha ikae tu tutekeleze. Bwana asifiwe! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, niseme hilo ni tatizo ambalo tumeliunda wenyewe na ni tatizo ambalo lazima tu-deal nalo. Ukiangalia vizuri sasa kwenye mambo mengine ya kimkakati utaona kwamba, kitu kitakachotutoa kwenye hali hii ya makusanyo na Serikali yenyewe inasema ni private sector kuweza kuwekeza. Miradi hii ya kimkakati imeingia kwenye stream sasa inazalisha, lakini private sector bado hawajahamasika kuanza kuwekeza na kuzalisha, wale wa nje na hapa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, naomba hivi, ili tujiridhishe kwamba kweli hakuna tatizo ambalo linasumbua watu kuwekeza, tutengeneze international competitiveness index yetu wenyewe. Tujiulize, watu wa nje wanatu-rank hivi, lakini tuchukue vile vigezo vichache tutengeneze kwamba, sisi bei yetu ipo hivi na tuweze kuiuza kwa wawekezaji kwamba kweli hii nchi yetu wanavyosema siyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna bwawa, umeme una-stabilize, reli na yenyewe itakuja i-stream na vitu vyote hivyo, ili kuanza kuuza hii nchi yetu vizuri zaidi na sisi tujiridhishe kweli tunakidhi mahitaji kwa sababu competitiveness yetu kulingana na nchi nyingine hapa Afrika ipo juu. Naamini tukitengeneza na tukifuatilia walikuwa wameanza hapo nyuma kidogo, walikuwa wanakaa Makatibu Wakuu wanaorodhesha mambo ambayo ni ya msingi ili kuweza ku-boost business indicator yetu, lakini Mheshimiwa Waziri ninaona siku hizi hiyo haipo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme cha mwisho kwamba, nafikiri tumefanya makubwa, na Bwawa la Nyerere limeleta mambo mazito. Baada ya kuleta mambo mazito sasa ni kwamba, yaani hakuna kitu muhimu kama umeme wa uhakika kwenye nchi. Nchi zote hizi hapa kwetu, nyuma huku, ukienda huko SADC, umeme ni matatizo. Sasa, hapa kwetu tunaanza kupata umeme wa uhakika, ni Mungu ametuletea hiki kitu, ni bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutumie hilo na pia, tusibweteke, ila tuwaombe TANESCO wawe flexible katika kuingiza watu binafsi kuzalisha umeme. Tatizo la watu binafsi kuingia kuzalisha umeme, kwa mfano kule Ruhuji na Rumatali watu binafsi wangewekeza fedha, hata wa nje wangewekeza kwa sababu, umeme unauzika anywhere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, issue ni kwamba, tatizo ni pricing model ya TANESCO. Pricing model, sisi umeme wetu bei yake ni ya chini, kwa hiyo, mtu ukiwekeza kwa bei hii ya chini ambayo umeme unapatikana hapa kwetu, mwekezaji binafsi hawezi kupata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuwe flexible, tujue kwamba, tutafanyaje ili watu binafsi wawekeze, hata kama watapata subside kidogo kupunguza yale makali. Wawekeze halafu tuone namna gani tuta-price ule umeme wetu. Tusiongeze bei, lakini kwa sababu unakuwa mwingi, basi inaweza ikawa rahisi ku-manage, lakini tusizinyime private sector kuingia kuzalisha, siyo tu umeme wa maji, ila hata geothermal sasa ndiyo umekuwa umeme ambao una tija sana. Wenzetu hapa majirani wameingiza umeme mwingi wa geothermal ambao ni umeme unaozalishwa kwa namna ambayo inatunza mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nawaomba wenzangu wote wakubaliane na mapendekezo haya ili tuweze kuendelea mbele. Ahsanteni sana. (Makofi)