Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2025/2026. Awali ya yote, nawapongeza viongozi ambao walipata fursa ya kutuongoza katika kuleta mbele yetu Mapendekezo ya Mpango; Waziri wa Mipango, Waziri wa Fedha, na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bunge inayohusika na Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza na nimepitia maandiko yao, kwa kiasi kikubwa ninaunga mkono mapendekezo yao na kwa sababu, ninayo fursa ya kushauri, ninaomba nishauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mafanikio na mengine yamewekewa picha, nami mafanikio ambayo yameandikwa tu, lakini hayakuwekewa picha, niyaseme. Linalofurahisha ni mafanikio yetu katika kuuzwa nje, tumeweza kuuza nje dola bilioni 14 na yenyewe inapaswa kuwa bolded.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kusimamia vizuri, sifurahi kwamba, tumeagiza nje bidhaa za dola bilioni 16 na kupunguza nakisi kufikia dola bilioni 2.4, ambayo inatupeleka kule tulikokuwa mwaka 2019/2020, tulipokuwa na dola bilioni 1.3. Hayo ni mafanikio niliyoyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio mengine ambayo nachukua fursa hii kuwapongeza wakulima wa nchi hii ni kwamba, wakulima wa Tanzania wale wadogo wa jembe la mkono wameweza kuzalisha chakula tani milioni 22, ambayo ni asilimia moja ya 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Mipango, popote tuendapo tukikutana tunakunywa ile kahawa yetu, anieleze, hawa watu wanaozalisha chakula hiki, hao wa jembe la mkono, miaka 30, miaka 60, watakuwa na hali gani? Kwa sababu, tulikuwa nao miaka 60 iliyopita, hatuwezi kuwaacha, tunakwenda nao vipi? Nao mafanikio yao tumeyaona. Pia, wakusanya mapato wana mikiki yao, na hesabu zinaonesha wameweza kukusanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mafanikio ninapenda niliseme, ni pato la Taifa. Pato la Taifa limeongezeka mpaka shilingi trilioni 148 kutoka shilingi trilioni 141.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nipite kwenye michango. Eneo ambalo nataka kupendekeza mahususi, ni kwenye mapendekezo ya mwaka 2025/2026, yale ya miaka mingine sitashughulika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzungumza hali ya dunia tumezungumza mazingira, lakini jambo moja, hatukwenda mahususi kuliangalia ni hali inayowahusu watu wa SADC, suala la ukame wa Zimbabwe na ukame wa Zambia. Wenzetu wana ukame mkubwa, lakini imedokezwa kwenye hotuba hapa kwamba, nasi kuna hatari ya mazingira, kama wanavyosema wataalamu wa hali ya hewa, na kwetu hali ya mvua siyo nzuri, tunajipangaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshauri, ninakushukuru Mtumishi wa Bwana ninamwona pale, tufanye haraka twende kumwagilia. Tujenge mifumo ya kumwagilia Kanda ya Ziwa ambako already kuna maji. Twende kule kumwagilia kwa sababu, kilichompata mwenzetu Zimbabwe, kikampata Zambia, Mungu apishe mbali kinaweza kutupata, lakini ndugu zangu wa Bunda, ndugu zangu wa Geita, ndugu zangu wa Muleba wana maji, Mungu kawapa. Tukimbilie kule, kwa sababu mkono umpigao mwenzio unamfundisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, narudi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na wenzake. Wamezungumzia dhana ya kununua mafuta na kuyahifadhi yakiwa na bei ndogo kwa kuotea kwamba, yakipanda bei wataweza kuuza. Nakubaliana na suala hilo, lakini linahitaji uangalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Nishati wakitaka kuzungumza jambo hilo, mimi ni old model, waniite wanieleze wanaweza kufanya mchezo huo namna gani? Kwa sababu, tunakwenda mbele haturudi nyuma, ninaishauri Serikali ianze kuwafundisha na kuwaelimisha wataalamu mahususi katika sekta hii. Siyo rahisi sekta hii kuingia na kufanya, inahitaji ujuzi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo ya Kamati ya Bajeti, kuna mambo yamependekezwa. Mojawapo wamependekeza kwamba, tuboreshe zao la nazi ambalo Tanzania tunaongoza Afrika na katika kumi bora tumo. Nakubaliana kwamba, tuongeze zao la nazi, lakini pamoja na hilo, nina mazao mengine tuwekeze nguvu za ziada. Nakubaliana na mpango wa Wizara katika kufanya irrigation. Tanzania tunakwenda vizuri ingawa watu wengine hawajaona. Tulikuwa kwenye tani milioni mbili, tumekwenda kwenye tani milioni nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalamu wanasema sisi tunaweza kufika kwenye tani milioni 10 na Afrika inaagiza nje tani milioni 16. Kwa hiyo, kuna uwezekano, Tanzania, kama tukichukua fursa hii kwa mwaka mmoja tu, haya ni mazao, ninazungumza bajeti ya mwaka 2025/2026, tunaweza kupata potential ya ku-export katika Afrika na tukaweza kupata kipato cha takribani dola bilioni tatu. Dola bilioni tatu kutoka kwenye mpunga! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine lenye fursa, nimewahi kumweleza Waziri wa Kilimo, nimekuwa niki-share naye kinachoendelea Uganda. Zao la kahawa limebadilika, limekuwa na demand kubwa. Uganda Kaskazini wameingia kwa nguvu wakiongeza maeneo ya kilimo, waki-target hilo zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo siri, Mheshimiwa Rais alipokwenda China alipata deal ya kuweza kuuza kahawa China na hakuna mtu anakula kama Mchina. Mchina akiamua kununua korosho yetu, tumepita. Sasa ameamua kununua kahawa. Tuongeze kilimo cha kahawa. Kwetu Kagera, Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Fatma amejasiria, Wilaya ya Muleba unaulizwa unalima wapi ulime kahawa? Ninalisemea suala la kahawa; haya mazao pamoja na nazi mliyosema, sawa, ninaunga mkono, lakini tuongeze mazao haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine ni eneo lenye matatizo, kuna matunda yanayoning’inia. Tanzania tunayo fursa ya mifugo. Nimewahi kuzungumza hapa kwamba, market ya gulf ni dola bilioni tisa, lakini ninazo taarifa Malaysia wanahitaji nyama kutoka Tanzania tani 100,000. Leo tunauza nyama dola milioni 57. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni soko lililopo linalotusubiri na nimesoma andiko moja wamesema maneno siwezi kuyatamka hapa. Wanasema, ardhi tunayo, mifugo inakubali, lakini tumeangalia tu, yaani ukiisikia kwa Kiingereza ni tusi, yaani eti sisi tumeangalia tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa soko lipo, naomba, na hii ni biashara ya mwaka mmoja, tuwekeze zaidi kwenye sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo, nina imani na Treasurer Registrar Bwana Mchechu, aisimamie NARCO. NARCO wanazo hekta 600,000, msiwaangalie walioko ndani ya NARCO; NARCO wawezeshwe wafanye kazi kwenye business mind. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kwenye Kamati ya Kilimo, wale tuliokuwanao, tulifanya mchakato, tulipitia takwimu tukaona zikiwekezwa shilingi bilioni 400 ndani yake, dola moja ingezaa dola 2.5. Watanzania wengi wanaopewa vitalu NARCO wanapewa vichaka na misitu. Hawajapewa Ranch, vile ni vichaka na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inapaswa iige mfumo wa Zimbabwe, mtengeneze pastures, muwape ng’ombe wa kisasa wawe wa nyama au wa maziwa, watu wanaingia na kuzalisha soko likiwa lipo. Tumefanya kazi, tumepata soko gulf, hilo la Malaysia, tuna contact. Sisi mwaka 2023 tulitaka kupata aibu, walikuja watu wanataka mbuzi hapa, tulikimbizana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta nyingine, nimemsikia Naibu Waziri wa Mifugo, sekta ya kufuga samaki ni aibu ya aibu, huwezi kusema. Katika nchi zinazofanya vizuri kufuga samaki Afrika, Tanzania haimo, Zambia imo. Ile Nchi ya Zambia haina ziwa, ni mabwawa yale. Watu wana mabwawa wanaita maziwa, sisi tunaongoza kwa maji. Maji ya kwetu huwezi kuogelea, huwezi kufanya lolote, twende tukafuge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri wa Mipango, namwona Naibu Waziri ananiangalia. Hatujafanya lolote, hatujatumia maji yetu. Mimi nina square kilometer 7,200 Wilaya ya Muleba; 10,200 Mkoa wa Kagera. Kama nimepewa vizimba, hakuna chochote kimefanyika, tunachezea maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Morocco wanapata dola bilioni moja kutokana na samaki. Misri anatuongoza, anapata billions of monies. Hayo ni mambo ya mwaka mmoja ninayozungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia exports, kwamba viwanda vinaweza ku-export zaidi. Kuna kazi ya kufanyika, the Blueprint Regulated Reform, Mheshimiwa Waziri wa Mipango aende akaipitie tena. Nimeipitia sana, yako makosa, lakini sehemu kubwa iko sawa, ile haiwezi kutekelezwa robo. Waziri ahamasishe viwanda ikiwemo kutekeleza ile Blueprint Regulatory Reform. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kupunguza gharama. Kama alivyosema Mheshimiwa Prof. Manya, tupunguze gharama (the cost of production) hapa, na unaifanya makusudi kwa Cross-subsidize. Bangladesh, kwa nini watu wanakwenda kuzalisha kule Bangladesh?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kukaa tukaangalia namna ya kupunguza kusudi watu waliokuwa wanazalisha Tanzania, wakahamia Zambia, Kongo, na Uganda warudi. Kuna watu walikuwa wanazalisha hapa Tanzania wako Uganda, tunawajua kwa majina. Kuna mzalishaji mmoja alikuwa Tanga, anaondoka kwenda Zambia, aliniaga. Nashukuru Serikali imekuja na mfumo wa kupitia kodi, mpitie kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimekuwepo kilio cha kuiomba Kariakoo irudi Ilala. Kariakoo ilihamia Kampala na Zambia. Bring back our Kariakoo. Tunataka watu waje hapa. Watu wachangamke, wafanye kazi saa 24, kama anavyosema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini lazima mwangalie tax regime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni makusanyo mazuri ya TRA. Ukienda mtaani, watu wa mtaani wanakueleza kwa majina, mabingwa wa kukwepa kodi. Unakuwa na mtu unampa jambo anasema na wewe unafahamiana na mkwepa kodi. Hao wakwepa kodi mwaambie inatosha kwa kodi walizokwepa. Tunahitaji kodi ili kutekeleza mipango yetu ya mwaka kesho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema nazungumzia mpango wa mwaka kesho. Tumefanya kazi nzuri kwenye miradi ya shilingi trilioni 10, na shilingi trilioni sita. Fikiria kama Taifa, kama tutachukua shilingi trilioni 10 tukaziweka kwenye production sector, rafiki yangu Mheshimiwa Waziri wa Mipango, ndiyo unajenga uchumi jumuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia rafiki yangu Mheshimiwa Mwambe, alikuwa ananieleza mradi mmoja. Nikasema unauonaje? Akasema super sana. Nikasema, ulichungulia nje! Alichoniambia ni siri yangu na yeye. Tunataka tuwajumuishe watu, na kuwajumuisha watu ni kuwalazimisha kwenda katika shughuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Kagera anakwambiaje? Watoto wa siku hizi huwezi kuwapeleka kwenye shughuli kama wagagagigikoko. Amekwenda akatafuta excavator Wizara ya Kilimo, wakampa matrekta. Vijana wanalimiwa, wanapelekwa shambani, wanafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaeleza potential ya mpunga, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ahsante umekuja. Tunataka mabonde yote ya Ziwa Victoria yalimwe. Tusije kuyalima baada ya ukame kuwa umetufikia kama Zimbabwe, na hayo ni mambo ya short-term. Tumefanyia kazi mambo marefu ya long-term, tunataka ya short term, ndiyo mpango wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kukopa, Kamati imependekeza kwamba tuache kukopa. Nimemsika Mheshimiwa Dkt. Kimei, sawa, lakini akalegea kidogo alipozungumzia vituo. Mimi nasema, tukae chini kwa akili ya bishara na hesabu. Mradi unaoweza kulipa immediately ukopeshwe, turidhike kwamba hii inakuwepo, unaweka shilingi unapata mbili na nusu, kama nilivyopendekeza kwenye sekta ya mifugo na niko tayari kwenda kwenye Kamati. Muilete kwenye Kamati, sitahamia huko, nitakuja kuwaonesha tulipoishia kusudi mwanzie hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mapendekezo. Naomba tuendelee. (Makofi)