Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Nami naungana na Wabunge wenzangu kupongeza upande wa Serikali kwa maandalizi mazuri ya taarifa hizi na ninaipongeza Kamati yangu ya Bajeti na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Njeza, kwa kutusimamia vizuri kuweza kuishauri vizuri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya. Hata wananchi kule majimboni wanaona jinsi fedha zinavyokwenda na ambavyo miradi inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, liko jambo ambalo nisipolisema wapigakura wangu wataona kwamba, Mbunge wetu namna gani huyu? Hawatanielewa kwa sababu, hata jana nimetoka jimboni, ilikuwa kila unachoeleza wanakukumbusha juu ya barabara, kipande kinachoanzia Itoni mpaka Lusitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali imetujengea barabara nzuri sana ya zege kutoka Lusitu mpaka Mawengi, takribani shilingi bilioni 179 zilitumika. Awamu ya pili wakaja upande wa Njombe, kutoka Lusitu hadi Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa bahati mbaya sana kazi ilianza vizuri sana, wananchi walishangilia sana, lakini kwa mkoa wetu ule wa Njombe mwezi huu ni msimu wa mvua kali sana na mvua ikianza pale wananchi wana hofu ni kwa jinsi gani Mheshimiwa Bashe ataweza kuwapelekea mbolea kule Ludewa? Ni kwa jinsi gani pembejeo nyingine za kilimo zitaweza kwenda? Ni kwa namna gani wananchi wataweza kusafiri kwenda kupata matibabu Ikonda, Hospitali ya Rufaa Njombe na maeneo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla sijaendelea na mchango wangu naiomba sana Serikali iweze kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kipande kile cha Lusitu kwenda Njombe kinaendelea vizuri. Niwe muungwana, ninamshukuru sana Mheshimiwa Bashungwa, haya maeneo ninayoyazungumza alikuja mwenyewe, akayaona. Kwa hiyo, nina imani haya ninayoyasema atakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudi tena kuendelea kuipongeza Serikali kwa Mpango mzuri wa Maendeleo wa Taifa. Naungana na Wabunge wenzangu ambao wameainisha sekta zile ambazo zinaweza kuinua sana pato la mwananchi mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pato la Taifa linakua vizuri sana, lakini pato la mtu mmoja mmoja hata katika Taarifa ya Kamati yetu tumeona bado ni changamoto. Sasa tunajiuliza, je, zile tafiti ambazo zinafanyika za kuandaa pato la mtu mmoja mmoja ni za usahihi? Wanatumia njia gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kukuta pale kwako, Madaba, kuna familia moja ina watoto wengi, lakini wanamudu mahitaji yote ya kila siku, lakini yanategemea jasho lao na namna wanavyozalisha shambani. Kila kitu wanategemea shambani, kitu cha dukani labda chumvi na sukari, lakini vitu vingine vyote ni kule. Watu kama hawa wanafanyiwa vipi tathmini kuweza kujua pato lao kwa mtu mmoja mmoja? Hilo limebakia swali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maeneo ambayo Wabunge wengi wameona yanaweza kusaidia kuinua pato la mtu mmoja mmoja, kwanza ni eneo la kilimo, tukiboresha eneo la kilimo kwa sababu ndiko eneo ambalo Watanzania wengi zaidi wanapata ajira, nasi Wabunge wengi humu ndani tunatokana na wakulima, hasa pale kwangu Ludewa nako wananchi asilimia kubwa shughuli yao ni kilimo. Kilimo kimeajiri zaidi ya 65% hadi 70% ya Watanzania na kinatoa mchango mkubwa sana kwa usalama wa chakula. Vilevile kinachangia vizuri kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kuinua pato la mtu mmoja mmoja, eneo hili la kilimo hasa, tumsaidie mwananchi katika kuongeza tija, kwa hekari pale akitumia mbegu, anaandaa shamba, anakuzia mara moja, mara mbili palizi, zile gharama anazozitumia je, baada ya mauzo mwishoni anapata faida kiasi gani? Je, hiyo shughuli, anapata moyo anavutiwa kuendelea kuifanya kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo hili tukimsaidia mkulima akapata soko la kutosha na hizi ruzuku za mbolea na mbegu, ambazo wanapewa, wananchi watazalisha zaidi kwa sababu watakuwa na uhakika wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa NFRA mwaka huu wamefanya kazi nzuri, wamenunua tani nyingi sana za mahindi na mwanzoni walikuwa wanalipa vizuri sana, lakini hapa mwishoni kuna wananchi wachache ambao kidogo kama mwezi hivi wamecheleweshewa malipo yao na huu ndiyo ulikuwa msimu wa kupeleka watoto vyuo vikuu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aweze kuingilia kati ili wananchi hawa wasivunjike moyo wa kuendelea kuzalisha mazao kwa wingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu wa NFRA, kwa sababu nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na ukame, na zina njaa, wangeweza kutafuta masoko mapema ili yale mazao wanayoyakusanya kule waweze kuyauza nchi jirani ambazo zina uhitaji mkubwa wa chakula. Kwa hiyo, kukiwa na soko zuri wananchi wengi watajituma kwenda shambani, watazalisha zaidi na pato la mtu mmoja mmoja linaweza kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko hili ni pamoja na kuruhusu ile mipaka iwe wazi kwa wafanyabiashara wa mazao ya chakula, wakiruhusiwa, ila tu wananchi wapewe elimu namna ya kuweka chakula akiba kwa ajili ya familia yao mwaka mzima. Kwa hiyo, wananchi wakishakuwa na uhakika soko lipo, kwa kweli watazalisha kwa wingi zaidi kwa sababu watakuwa na uhakika wa kwamba wakizalisha mazao ya chakula wanapata kipato, eneo hili litainua sana pato la mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la kilimo, mwaka huu kumekuwa na changamoto kubwa sana ya maghala, ma-godown au maeneo ya kuhifadhia mazao. Kwa mfano mazao kama mahindi, hapa kuna njia mbili; njia ya kwanza, Serikali itabirike kwamba huu ununuzi wa mahindi unaofanywa na NFRA ufanyike mfululizo miaka mitatu hadi minne. Hii itavutia watu binafsi kwenda kuwekeza kwenye ujenzi wa ma-godown na maghala ili waweze kuyapangisha kwa NFRA, lakini ikiwa mwaka huu wananunua miaka miwili hawanunui, inaweza ikawa changamoto na hii sasa itasababisha kuhitaji Serikali yenyewe iweze kujenga maghala ya kutosha ili wananchi waweze kuzalisha kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la uzalishaji kwenye kilimo ili kuinua pato la mwananchi mmoja mmoja linaenda sambamaba na miundombinu ya barabara za vijijini. Zile barabara za TARURA wanavyozitengeneza wanaweka ukomo kwenye uzito, kwa hiyo wanatengeneza barabara vizuri lakini wanazuia lori tani zaidi ya 10 lisipite pale, lakini maeneo yale ni ukanda wa uzalishaji mkubwa sana, una mazao mengi, unahitaji malori ya tani zaidi na wafanyabiashara kupeleka magari madogo madogo, wanaona ni hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali kuainisha barabara za vijijini zile ambazo zipo kwenye ukanda wa uzalishaji ili ziweze kuwekewa kiwango kikubwa cha changarawe ili magari ya uzito wowote yaweze kuingia mashabani. Kama magari ya mizigo ya uzito mkubwa hayatoruhusiwa, kwa kweli tutarudisha nyuma sana maendeleo ya wakulima na pato la mtu mmoja mmoja linaweza kuathirika kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo linaweza kuinua pato la mwananchi mmoja mmoja ni eneo la uvuvi. Nchi hii imejaliwa kuwa na maziwa, bahari na wananchi wengi wanajishughulisha humo. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni Serikali kuona namna gani tunaweza kuwawezesha wananchi wale wa kando kando ya maziwa, bahari, mito mikubwa, mabwawa, wakawezeshwa kufanya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba. Imefanyika sana Ziwa Victoria lakini yapo maeneo ambayo bado rasilimali ya maji hatujaitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nashauri kwamba eneo hili tulitilie mkazo ili wananchi waweze kufuga samaki kwenye vizimba. Hii itasaidia kutengeneza ajira kwa vijana wengi ambao ni changamoto na hata wakina mama na watu wengine, pia hata usalama wa chakula utakuwa wa kiwango cha juu. Eneo la mifugo pia tukiweza kulizingatia itakuwa nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru Serikali kwa kupiga hatua kwenye eneo la uwekezaji eneo la Liganga. Pale Liganga kuna miradi miwili, kuna ule mradi wa kimataifa ambao Serikali iliingia mkataba na ile Kampuni ya Sichuan Hongda ambao umekwama muda mrefu, lakini upo mradi wa Maganga matitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza eneo la Manganga Matitu kwa hatua iliyofikiwa, hata jana tulikuwa na mwekezaji kule ameshasaini mkataba na anakwenda kuanza ujenzi wa viwanda. Atazalisha tani milioni moja za chuma kwa mwaka. Kwa hiyo zile trilioni 2.9 iliyokuwa inaagizwa nje ya nchi sasa itaagizwa Ludewa. Kwa hiyo, hii ni hatua kubwa sana, na ni jambo la kupongeza na tuwaombe Serikali waongeze speed kwenye ule mradi mwingine mkubwa wa kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile eneo la makaa ya mawe pale Mchuchuma watu wa NDC kuna Mkurugenzi mzuri sana Dkt. Nicolaus. Aongezewe wasaidizi wazuri ambao wanaweza kumsaidia kufuatilia mambo yakaenda haraka na uwekezaji ukaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba na fidia ziweze kulipwa kwa wananchi wachache waliosalia wa Ketewaka na wale wengine wa Maganga Matitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja nashukuru sana kwa kupewa nafasi. (Makofi)