Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia katika mapendekezo ya mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuiongoza nchi vizuri ili mipango hii ambayo tunakuja kujadili hapa iweze kutekelezeka kwa utulivu na ukamilifu wake kama ulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapenda kumpongeza kwa utekelezaji wake katika utafutaji na upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kutekeleza mipango hii. Vilevile ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, kwa mpango mzuri ambao ametuletea ambao nitauelezea hivi karibuni, vilevile na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa ajili ya mapendekezo au mwongozo aliyotupa kwa ajili ya bajeti inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao umependekezwa ni wa mwisho katika ile mipango ya miaka mitano ambao unaishia 2025/2026 na tunampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa sababu umeendelea kuweka misingi ya Tanzania tunayoitaka. Tunasema hivyo kwa sababu gani? Kwa sababu ameendelea kujenga juu ya sehemu ambayo tumefikia, hakuanzisha mambo mapya. Kwa hiyo, ina maana mipango hii ni endelevu, hivyo tunakwenda vizuri katika eneo la mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika ukurasa wa nne wa mpango wake, malengo mahususi mengi yanaelezea kuendeleaza au kukamilisha. Kwa hiyo, ina maana ni mwendelezo wa yale ambayo yalikuwa yamepangwa hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tukiangalia vipaumbele vyake, ametuwekea vipaumbele sita ambavyo nitajikita katika kimojawapo katika mchango wangu, vipaumbele vyake ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi; pili, ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ambacho ndipo nitakachochangia zaidi hapo, tatu, ni kukuza uwekezaji na biashara. Vilevile ameweka kipaumbele cha kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza ujuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, nitajikita zaidi katika viwanda vya malighafi au rasilimali za ujenzi. Ukiangalia malengo mahsusi ya mpango yapo saba. Nikiangalia lengo namba nne ambalo ni kukamilisha miradi ya kielelezo na kimkakati yenye matokeo makubwa ya uchumi linakuja swali, tujiulize, baada ya kuikamilisha nini kinafuata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo ningependa kuiangalia zaidi kwamba baada ya kuikamilisha nini kinafuata? Ni miradi ya bwawa la umeme, vilevile hata usafirishaji kama SGR. Tuangalie wenzetu walifanyaje walipokuwa na vitu kama au hali kama ambayo tumekutana nayo hivi sasa? Tuangalie mfano wa Msumbiji.

Mheshiiwa Mwenyekiti, katika mwaka 1979 wenzetu wa Msumbiji walikamilisha Bwawa la Cabora Bassa ambalo lilitoa Megawatt 2,075, wao walichokifanya wenzetu walichukua 45% ya umeme wote huo ukaelekezwa katika kiwanda kimoja cha uzalishaji wa aluminium, walivyoweza kuzalisha aluminium yote katika Kiwanda cha Mozal ambacho kinatoa tani 580,000 za aluminium kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini matokeo yake? Wamejikuta kwamba ule umeme wao 90% ya aluminium inayozalishwa Msumbiji yote wanapeleka Ulaya. Kwa hiyo, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba unapata fedha ya kigeni kutokana na mradi wako wa mkakati, lakini vilevile ukiangalia nini kimetokea baada ya kuweka kiwanda hicho ambacho kinazalisha aluminium kwa wingi, kimekuwa ndiyo kiwanda kikuu mwajiri wa nchi hiyo. Kimeweza kuzalisha ajira nyingi, kimeweza kuwapatia fedha za kigeni na kimeweza vilevile kuokoa pesa yao ya kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nini mapendekezo yangu kwa hilo? Mapendekezo yangu ni kwamba katika umeme wetu huu ambao na sisi baada ya kuzalisha umeonekana ni mwingi kuliko mahitaji yetu ya sasa hivi, ina maana tusipange kuuwashia taa tu, tulenge viwanda vya kimkakati. Kwa kusema hivyo tuangalie ni viwanda vipi ambavyo vinaweza kuwa vikatuokoa na sisi kama ambavyo viliwaokoa Msumbiji katika hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jirani yake hapo, kuna siyo machimbo maana hawajaanza kuchimba, kuna akiba kubwa ya chuma katika eneo la Liganga na ukiangalia chuma katika ulimwenguu huu haijawahi kutosheleza. Vilevile chuma katika uchakataji wake upo wa aina mbalimbali. Chuma bora zaidi ni kile ambacho kinachakatwa kwa umeme. Kwa hiyo, tukiweza kupata vile vinu vya awali vya kuchakata chuma ambavyo wanaviita blast furnished, lakini baada ya hapo tukawa na vinu vya kuchakata chuma kwa umeme (electrical furnish) ambavyo vitaweza kutupatia chuma bora ambacho ndicho kinaweza kikatupatia manufaa ya haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia chuma ambacho kimetumika katika reli ya SGR, chote kinatoka Japani kwa sababu ni nchi chache sana ambazo zinatengeneza chuma cha ubora huo, lakini siri ni kwamba wamefanya hivyo kwa sababu wana vinu vya kuchakatia hivyo ambavyo vinahitaji nishati kubwa na sasa nishati kubwa tunayo, hivyo tunaweza kujielekeza huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kwenye sehemu nyingine vilevile ya vifaa vya ujenzi ambavyo ni malighafi ya saruji maarufu kama clinker. Ukienda bandarini pale Dar es Salaam au Tanga utagundua kwamba kuna uagizaji mkubwa sana wa hii bidhaa clinker kwa ajili ya matumizi yetu ya ndani, na hata kwa matumizi ya nchi za nje vile vile ambao ni jirani zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ina maana kwamba hii ni fursa. Pia ukiangalia nini ambacho kinatuzuia sisi kutengeneza clinker hapa nchini kwa wingi? Ni kwa sababu malighafi tunayo, lakini nishati. Sasa suala la nishati ya kutengenezea clinker ni gesi na umeme. Tukijikita kuwekeza katika kutengeneza viwanda ambavyo vinaweza vikazalisha clinker ambavyo vipo vinavyotengeneza cement, vikipewa uwezo au vikirahisishiwa kupata umeme wa bei nafuu, vikirahisishiwa kupata gesi ya bei nafuu, maana yake ni kwamba hii clinker ambayo ilikuwa inaagizwa kutoka nje itakuwa sasa inatengenezewa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia hapa, ni wapi tunaagiza Klinker kwa takwimu za mwaka 2023 kutoka UAE tunaagiza tani milioni 196, kutoka Saudi Arabia, tunaagiza tani 146 kutoka Pakstani, tunaagiza tani 99 kutoka Kenya, tunaagiza tani 19 na kutoka China, tunaagiza tani moja. Sasa zote hizi tunaweza tukazitengeneza hapa nchini kwa kutumia viwanda vyetu na rasilimali yetu wenyewe kwa sababu tunayo; udongo tunao, limestone tunayo, chokaa tunayo, kilichokuwa kinapungua ni nishati. Sasa baada ya kukamilisha hivi viwanda vya mkakati maana yake ni kwamba tuvitumie katika kutengeneza viwanda hivi ambavyo vitarahisisha upatikanaji wa malighafi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda zaidi, vilevile nchi hii udongo wa kutosha tunao, tunaweza kabisa kutengeneza vigae vya kwetu wenyewe na matofali ya kuchoma yenye kiwango kikubwa. Matofali ya kuchoma tuliyonayo hivi sasa, hivi viwango vyake ni vidogo lakini tukichoma matofali ya kiwango kikubwa sana, matofali hayo huwa yanakuwa ghali sana maana ndiyo yanayotumika katika kuweka matanuri ya kutengenezea clinker na kadhalika, yote yale tunaagiza kutoka nje lakini material yote tunayo hapa. Je, hatuwezi kutumia nishati yetu nafuu sasa kutengeneza hayo matofali ambayo tutayatumia wenyewe na kuweza kupeleka nchi za nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia katika kuongeza ajira, itatusaidia katika kuongeza fedha za kigeni na vilevile itatupunguzia mahitaji yetu ya fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda unanitupa mkono. naunga mkono hoja. (Makofi)