Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi mchana huu kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu ambao ni Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo matatu kimsingi ambayo ningependa niyachangie leo kwa nia ya kutaka kuboresha mpango wetu. Jambo la kwanza kabisa ni suala la Liganga na Mchuchuma, lakini nataka kusema kuhusiana na reli ya kusini pamoja na reli ya kati kwa maana ya SGR. Nitaongea pia kuhusu masuala ya madeni ya wakandarasi kwa nia ya kutaka kuchechemua uchumi wetu, na pia nitatoa ushauri kwenye masuala ya kilimo kwa maana korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi ya peke kabisa, nami niungane na wote waliompongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais na kwamba uzalishaji wa korosho umeongezeka sana. Nampongeza pia na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwapatia pembejeo wananchi wa Mtwara, Lindi, Ruvuma na Mikoa yote inayolima korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho hivi sasa tunapitia changamoto kidogo. Changamoto kubwa iliyopo ni suala la usafirishaji. Serikali ilitoa maelekezo kwamba korosho yote inayozalishwa Mikoa ya Mtwara, Lindi na maeneo mengine ikiwezekana isafirishwe kupitia Bandari ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ninaongea mbele yako mwaka huu tunategemea tutakusanya zaidi ya tani 400,000; ndiyo maana nilisema ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kwamba amepeleka pembejeo za kutosha kwa wakulima wa korosho. Uzalishaji kwa kweli umeongezeka ukilinganisha na miaka yote na kama nilivyosema, ni kazi kubwa pia ya Waziri wa Kilimo na wasimamizi wote wa Sekta ya Kilimo na wa korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyo nayo ni ya usafirishaji. Mpaka sasa hivi korosho zilizokusanywa mpaka mnada wa jana na wa leo MAMCU ni zaidi ya tani 200,000, zinakaribia kufikia tani 220,000; lakini korosho hizi zinasafirishwa pekee kwa kutumia Bandari ya Mtwara. Tumekusanya kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja sasa, lakini korosho ambazo tunategemea kuziondoa karibuni ni tani 400,000 tu kwa kutumia meli iliyoletwa na yenye uwezo wa kubeba makasha 175. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakumbuka kwamba mwaka jana mwezi Februari walibadilisha maamuzi wakaanza kuisafirisha korosho kutumia Bandari ya Dar es Salaam, na ndipo korosho zile zilikwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuhusu ughali wa gharama ya kusafirisha kupitia Bandari ya Mtwara. Hivi sasa kontena la futi 40 kutoa Mtwara kwenda India ni kuanzia dola 1,900 mpaka dola 3,300, lakini kontena hilo hilo kulitoa Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi za India na Vietnam haizidi dola 800 mpaka dola 1,000, zipo hapo between. Sasa tazama gharama hizi zilivyo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute namna ya kufanya ili kuwawezesha wafanyabiashara kupunguza gharama zao za usafirishaji ili iweze kuleta tija kwa mkulima. Kwa hiyo hii ilikuwa sehemu yangu ya ushauri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili alifanyie kazi ili kuweza kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa kwamba kuna suala la madeni ya wakandarasi, tumesikiliza vizuri sana kuhusu mpango na hotuba zote zilizopita mbele yetu. Ukiangalia LAAC na PAC pamoja na ile nyingine, ni kwamba wakandarasi wamekuwa hawalipwi kwa wakati, kitu ambacho kimepunguza sana mzunguko wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nilipata bahati ya kuuliza na nikamuuliza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, kwamba ni lini mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga Barabara ya Lindi – Mtwara – Kibiti ataanza kazi? Anasema Serikali ina mpango wa kutaka kujenga barabara hii upya. Hata hivyo kwa hatua za dharura amepatikana mkandarasi ambaye atakwenda kujenga madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumetoka majimboni hivi karibuni tu. Ninataka niseme kwamba mpaka sasa hivi mkandarasi hajafanya mobilization na wala hajafika site, hivyo, uwezekano wa kuanza kazi hiyo mapema ni mdogo. Kwa hiyo, kuna tishio pia hata kwenye namna ya kusafirisha hizo korosho tunazozitaja hapa kwa sababu barabara ya Mtwara mvua zikianza kunyesha hata wiki moja kuanzia sasa barabara hii itajifunga na kwa hivyo haitaweza tena kupitika, tutalazimika sisi kupita Songea. Hiyo ndiyo hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri apeleke hao wakandarasi, kama anasema Mheshimiwa Rais amekwishatoa fedha basi wapewe advance ili wakaanze kazi hii mapema ili kuweza ku-rescue. Hali ni mbaya, barabara nzima unaweza ukasema almost imekufa. Pamoja na nia njema ya Serikali na kwa sasa ameamua kuanza kutengeneza madaraja, basi kazi hiyo ikafanyike mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mpango ninataka nishauri, kwamba mpango bora wa nchi yoyote, ambao pia ni kama manifest, unakuwa na tarehe mahususi ya ukamilishaji wa miradi ya kimkakati. Mradi wa Liganga na Mchuchuma sasa hivi ni zaidi ya miaka 50 hadi miaka 60. Tangu sisi tukiwa watoto wadogo tunasikia zinaongelewa habari za Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imepigwa hatua kidogo sasa hivi walau wananchi wameanza kulipwa fidia. Tunataka sasa tuone utekelezaji wa mradi huu ili kuweza kutuletea tija. Mheshimiwa Eng. Dkt. Chamuriho hapa alikuwa anaongea na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini pia na Mheshimiwa Profesa Manya nilikuwa ninamsikiliza wakati ule na hata ndugu yetu Mheshimiwa Profesa Kaijage, ambaye naye ni Profesa, kwa namna anavyolishauri Bunge. Tunachotaka kifanyike, cha kwanza, ndiyo, kwamba Serikali ilikuwa na nia njema kabisa ya kutengeneza reli ya kati kwa kiwango cha SGR. Awamu ya pili ya reli ilikuwa ni reli ya Kusini inayoanzia Mbamba Bay itapita huko Songea itakuja mpaka Mtwara bandarini yenye urefu wa kilomita 1,000; lakini kilichopo mpaka sasa kwa sababu mpango huu hauna tarehe mahususi ya ukamilishaji wa miradi hii kuna wakati mwingine Serikali haitimizi wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kipande cha Tabora – Isaka chenye urefu wa kilomita 165 kimetengenezwa kwa asilimia 6.62 tu. Kipande cha Mwanza – Isaka chenye urefu wa kilomita 341 utekelezaji wake ni 60.62%. Sasa ukija kuangalia hapa sasa hivi kipande kinacholeta tija ni cha Dar es Salaam – Dodoma, tena tija yenyewe ni abiria kwa sababu uzalishaji wa hapa Dodoma wa mazao ya kilimo na mengine si mkubwa kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunashauri Reli ya Kati ikamilike kwa wakati uliokusudiwa; mpango wake uoneshe tarehe mahususi ya kukamilisha Reli ya Kati, mpango wake uoneshe tarehe mahususi ya kuhakikisha ule Mradi wa Liganga na Mchuchuma unaanza kutelezwa, ambao pia utajenga na Reli ya Kusini ili kwenda sawa na lile jambo lililokuwa linaitwa Mtwara Corridor. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hakuna mjadala wa Mtwara Corridor kwa sababu components nyingine za Mtwara Corridor hazijatekelezwa. Uchumi wa watu wa Kusini in a way umelala. Huwa tunachangamka wakati wa hizi habari za korosho na habari nyingine, lakini kimsingi kuna mambo ambayo Serikali inatakiwa itumie nguvu kubwa kuyatekeleza ili iweze kuleta tija inayokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa hivi; mwanzoni walikuwa wanasema kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma hauwezi kuanza kwa sababu kulikuwa kuna madini ambayo hayatumiki pale, lakini sasa hivi kuna madini ambayo ni very rare yanayotakiwa huko duniani nayo yapo kwenye Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Kwa nini, Serikali isianze kuutekeleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata wasiwasi kwamba kuna mikono hapa inayozuia utekelezaji wa mradi huu, kwa sababu mkandarasi yupo na mazungumzo yalianza tangu mwaka 2011, lakini mpaka sasa hivi mradi hauendelei na mkandarasi hakuna chochote anachokifanya. Serikali inasema inafanya mazungumzo lakini mazungumzo hayo yanafanyika kwa siri kubwa. Sisi Wabunge tunaotokea kwenye maeneo haya kwa kweli tunasikitika. Tunatamani sana tuone uchumi wetu unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili suala la reli wananchi wa maeneo mengi wameshindwa kuendeleza maeneo yao wakiamini utekelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kusini utaanza karibuni. Sasa tutoe ruhusa kwa sababu hakuna mpango wa kutekeleza ujenzi wa reli hii in the near future. Tunasikia sasa hivi wanataka kuboresha Barabara ya Mtwara – Masasi na anatafutwa mkandarasi. Sisi tulipewa taarifa kwamba barabara hii itaanza kujengwa hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kubadilisha taa zilizopo barabarani eneo la Ndanda, Nanganga na maeneo mengine, kwa sababu taa ziliwekwa zikiwa zina mwanga hafifu, ombi ambalo tumekwishalileta Serikalini. Kwa hiyo, tunategemea hivi karibuni mambo haya yote yatafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la msingi kuliko yote, ili kupunguza matumizi makubwa ya forex kwenye kuagiza chuma kwenye hivi vipande vilivyoanza, basi tunashauri kabla utekelezaji wa Reli ya Kusini haujaanza kama ambavyo mzee wangu hapa amesema, ikiwezekana tutafute hizo electrical furnace kwa sababu tunao umeme wa kutosha. Sisi hatuna haja hivyo vitu wavilete Dar es Salaam. Katika hatua za awali kule kule Songea, kule kule Madaba, kule kule huko Namtumbo na kwingine inawezekana kuweka kiwanda cha kuchenjua chuma hii ili tuanze kujenga Reli yetu ya Kusini kwa kutumia chuma chetu wenyewe kwa gharama nafuu sana tofauti na ambavyo imekuwa SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Reli ya Kusini itaanza kuleta tija mara moja kwa sababu inakwenda kusafirisha makaa ya mawe, Reli ya Kusini itakwenda kusafirisha na bidhaa nyingine zilizopo eneo lile na kujipatia fedha; si kwa lengo la abiria pekee yake. Kwa hiyo, hilo tuombe na tushauri; na ndipo tutakapokwenda kuonesha ile tija ya Mtwara Corridor, lakini na matumizi mazuri ya Bandari ya Mtwara. Siyo kutegemea tu mazao kama korosho na sasa tunaona hapa uzalishaji wa korosho umeongezeka, lakini bandari inashindwa kuhudumia korosho hizi. Ndani ya mwezi mmoja tumeondoa tani 4,000 kati ya tani 2,000 zilizozalishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la NLG. Miaka miwili iliyopita sisi Wabunge wote wa Mikoa ya Mtwara na Lindi tulikuwa tunaimba sana kuhusiana na suala la NLG na tuliaminishwa utekelezaji wake utaanza hivi karibuni ili kuweza kusisimua uchumi wa maeneo hayo. Inasikitisha kuona kwamba tulichokuwa tunaambiwa wakati huo na kilichopo sasa hivi field si vitu vinavyofanana. Hatufahamu mazungumzo yameishia wapi na mradi huu unaanza kutekelezwa lini. Kwa hiyo, nimwombe atakapokuja ku-wind up pamoja na kuwa na timeframe na nimshauri kabisa Mheshimiwa Waziri kwamba, katika miradi yote ya kimkakati kuwe kuna timeframe; hivi vitu visiwe infinity, ni lazima tuseme kufikia tarehe 5 Oktoba, wakati fulani tumalize mazungumzo na mkandarasi ili utekelezaji uanze wakati fulani. Tukiacha tu vikawa vile ambavyo vinafanyika ni ngumu kuvitekeleza na uchumi wetu unazidi kushuka chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono kabisa hotuba hii, lakini pamoja na mpango huo bado ninasisitiza kuhusu kuhakikisha kwamba miradi hii mikubwa ya kimkakati anaiwekea timeframe ili kuweza kuleta tija kwa nchi yetu. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)