Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja mbili zilizoletwa na Serikali, lakini vilevile na taarifa yetu ya Kamati ya Bajeti ambayo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu kwa ustadi mkubwa sana Mheshimiwa Mzee Oran Njeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/2026 pamoja na mambo mengine, taarifa hizi mbili zimetoa vipaumbele mahususi 10. Vipaumbele hivi vimejaribu kuonesha namna ambavyo tunakwenda kushughulika na uwekezaji kwenye sekta za uzalishaji. Katika hivi vipaumbele mahususi 10, ninataka nizungumzie kipaumbele kimoja tu, kuongeza wigo wa kinga ya jamii ambapo kimsingi mpango unalenga kuongelea bima ya afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechagua kuongelea kipengele hiki kimoja au kipaumbele hiki kimoja mahususi kwa sababu bima ya afya kwa wote inakwenda kumgusa kila Mtanzania kwa maana ya kwenda kuleta ustawi wa jamii. Vilevile, bima hii ya afya kwa wote inakwenda kuliingiza Taifa kwenye historia ya kila Mtanzania kupata huduma ya afya katika mazingira yanayofanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa tunaongelea bima ya afya kwa wote na kwa maana tunaongelea kipaumbele hiki cha kinga, kuongeza wigo wa kinga ya jamii nataka tutazamie maeneo machache ya eneo la afya ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya yakiwa kama sehemu na tunayahesabu kama sehemu ya maandalizi ya mpango huu wa bima ya afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tuna vituo vya kutolea huduma za afya 12,266. Katika hivyo, vituo vipya ni 1,324. Kazi kubwa sana hii imefanyika. Hivi sasa ninavyozungumza tukielekea kwenye huu mpango wa kuandaa bima ya afya kwa wote, nchi yetu ina digital X-ray 346, ina ultrasound 677, ina CT scan 34 (zote hizi ni kazi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan) na MRI za kutosha kulingana na kanda tulizonazo. Vilevile, Serikali imetoa mtaji wa karibia shilingi bilioni 100 kwa MSD ili kuweza kununua madawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mpango wa bima ya afya kwa wote. Vilevile, Mheshimiwa Rais mwaka jana alitoa kibali cha ajira cha kuajiri watumishi 13,187 wakiwemo watu wa Sekta hii ya Afya. Vilevile, Serikali inasomesha wataalam ndani ya vyuo vyetu, wataalam bingwa nje ya nchi wapatao 1,251; mradi ambao unatugharimu shilingi bilioni tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ikiwa tunataka kwenye mpango wetu huu wa mwakani kujiandaa na jambo hili kubwa la bima ya afya kwa wote, mambo yafuatayo ni muhimu tuyafanye:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tupitie upya vyanzo vya mapato kwa ajili ya bima ya afya kwa wote. Mwaka jana kwenye finance bill tulipitisha vyanzo viwili. Kwanza tulipitisha 100% kwenye ushuru wa ethyl na tulipitisha asilimia mbili kwenye ushuru wa bidhaa za pombe, bidhaa za cosmetics pamoja na bidhaa nyingine. Mpaka sasa kwenye vyanzo hivi viwili tulivyopitisha tumekusanya shilingi bilioni 22 peke yake kwenye lengo la kukusanya karibu shilingi bilioni 173 kwenye vyanzo hivi viwili. Hii inatu-alarm kwamba ni muhimu tukafanya tena tathmini na kuendelea kutafuta vyanzo vingine vipya kwa ajili ya mpango huu kabla hatujaanza kuutekeleza 2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunatakiwa kufanya ni kuanzisha kwa mfuko wa kugharamia wasio na uwezo pamoja na wanawake wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, tuanzishe Mfuko. Ni muhimu sana kuanzisha mfuko hivi sasa kabla ya 2026 kwa sababu, fedha ikiwa Mfuko Mkuu wa Serikali haina rangi. Hamna iliyochorwa kwamba hii ni ya bima ya afya kwa wote. Hata hivi sasa tunavyozungumza ni hatari sana kuwa shilingi bilioni 22 zimekaa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na namwomba Mungu kwamba ziwepo kwamba zipo. Ni muhimu tuanzishe Mfuko ili fedha hizi ziende ziwekwe kule badala ya kukaa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali; ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, sheria ile tuliyoipitisha tulisema Waziri wa Sekta kwa maana ya Waziri wa Afya pamoja na Waziri wa Fedha waweke utaratibu wa namna ya kusimamia Mfuko huo. Kwa sababu, kimsingi fedha hizi kama hatuzitumii hivi sasa as long as tunataka kuzitumia kwa ajili ya bima ya afya kwa wote ni lazima ziwekezwe na sio kuwekwa; zinatakiwa kuwekezwa. Sasa kama hatujawa na hiyo structure kamili ambayo ndiyo tafsiri ya sheria ya bima ya afya tuliyonayo, fedha hizi tutakuta tumezitumia kwenye mambo mengine na hii itakuwa ni jambo baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo lazima tulifanye, kanuni za sheria ile tuliyotunga mwaka 2023 (Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote), si tu kwamba ziwe tayari, lakini zifahamike na kila Mtanzania tukiwemo sisi Wabunge, zifahamike na kila mwajiri, zifahamike na kila mwajiriwa, zifahamike na kila mwananchi. Ndugu zangu, jambo hili la bima ya afya kwa wote, duniani kote wakati wa kuanza limeleta rabsharabsha na purukushani nyingi sana. Mataifa makubwa walivyojaribu hivyo walipata purukushani kubwa sana. Bahati tuliyonayo ni kwamba tumepitisha sheria mapema mwaka 2023, tuitumie muda huu kufika 2026 tuwe tumejipanga kuandaa structure na haya mambo ninayoyashauri pamoja na mambo ambayo Serikali inayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa nchi ya jirani hapa, sitaki kuwataja, mnajua kinachoendelea pale kuhusu bima ya afya kwa wote. Kwa hiyo sisi tutumie muda huu kwamba tumepitisha sheria mapema, tuziandae structures zote mapema zikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tutapaswa kulifanya ni elimu. Wananchi wetu wanapaswa waelimishwe kwa sababu tukishatoka kwenye haya makundi maalum ambayo tumeyalenga: wanawake wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watu wasiojiweza; kitakachofuata baadaye ni kuwa-take on board wananchi wote na yapo mambo pale ambayo wananchi kwa upande wao watatakiwa wayafanye. Kwa hiyo ni vizuri elimu wakaanza kuipata sasa kabla ya 2026; hali kadhalika elimu iwafikie waajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu kufanya, tumekubaliana kwa pamoja mtekelezaji wa jambo hili atakuwa ni NHIF. Ninatambua hoja zote za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu NHIF zilishakuwa cleared. Kwa hiyo udhaifu ule ni kama haupo tena. Kwa hiyo tunatarajia sasa, kuelekea bima ya afya kwa wote, NHIF itakuwa imejipanga. Katika kujipanga kwao wahakikishe wanakuwa na ofisi kwenye kila wilaya ya nchi hii, ikiwezekana kila halmashauri ya nchi hiiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante naomba Mheshimiwa hitimisha, ahsante tunakushukuru.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nihitimishe hoja ya mwisho kwamba, zoezi la utambuzi tusitegemee tu zile takwimu za TASAF kwenye kutambua watu wasiokuwa na uwezo kwenye kupata bima ya afya kwa wote. Lazima tushirikishe mamlaka nyingine kama Serikali za Mitaa, tushirikishe viongozi pale kwenye grassroot.

MWENYEKITI: Ahsante muda umekwisha.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)