Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninakushukuru na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Kama siku nyingine, ninashukuru kwa Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia chochote katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninatoka kidogo, siyo mbali sana na walivyochangia wenzangu, lakini ni kwa sababu ya kujenga. Kama tunavyojua sote tunajenga nyumba hii, hatuna sababu ya kugombea fito.

MWENYEKITI: Samahani, Mheshimiwa Mchungahela, baada ya Mheshimiwa Mchungahela atafuata Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege na Mheshimiwa Zaytun Seif Swai ajiandae. Mheshimiwa, ninaomba uendelee.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyozungumza, kwamba nitajaribu kuchangia kwa lengo la kutengeneza mtangamano wa mpango huu, kwa sababu huu mpango ndiyo msingi mkubwa wa bajeti yetu inayokuja hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona mgonjwa anaendelea kuumwa licha ya kuwa amepewa dawa, tafsiri yake ni nini? Kwamba, dawa aliyopewa siyo sahihi, lakini hii inaashiria nini? Kuna mambo mawili yanaweza yakajitokeza hapo. Jambo la kwanza, inawezekana maabara haijafanya uchunguzi sahihi wa changamoto ya mgonjwa, pia inaweza ikawa daktari ameshindwa kupata tafsiri sahihi ya ripoti ya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kesi yetu sisi hapa, ni moja kwa moja kwamba, maabara imeshindwa kutoa majibu sahihi ya tatizo la mgonjwa. Kwa nini? Kwa sababu, daktari wetu sisi ni mahiri sana, Daktari wetu kwa maana ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mahiri. Amefanya jitihada nyingi za kutaka kutibu mgonjwa huyu kwa kwenda huku na huku akijaribu kutafuta jinsi gani ya kumtibu. Ni vema kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini bado pia tunahitaji kufanya zaidi kwa sababu tumechelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya fununu ya kushuka kwa mfumko wa bei, lakini bado taarifa hizi zimekuwa siyo njema au hazina tija katika uchumi wetu. Bado kumekuwa na changamoto ya shilingi yetu kuwa dhaifu dhidi ya pesa za kigeni na hali hii inasababisha deni letu la Serikali kuongezeka kwa kasi siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuwa, tumekuwa na mkakati mzuri sana wa kukopa, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukijielekeza kukopa katika kiwango ambacho kwamba deni hili liwe himilivu, lakini pamoja na mkakati na umahiri huo, bado deni hili limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa na sababu kubwa ni kwamba bado hatuja-interact baadhi ya factor ambazo ni muhimu kwa ajili ya kufanya pesa yetu iimarike, kwa nini? Kutokuimarika kwa pesa hii, kunasababisha impact kubwa sana ya exchange rate kwenye deni hili. Ukiangalia hili Deni la Taifa, Deni la Serikali utakuta kwamba eneo kubwa la kukua kwake kunategemeana na rate ya exchange na riba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokikopa siyo kikubwa ukilinganisha na hali halisi ya deni lenyewe. Sasa kutokana na hali hiyo bado tumeona kwamba jitihada kubwa zinazofanyika hazina impact hasa katika eneo hili la kuimarisha pesa ya shilingi, kuimarisha uchumi kwa ujumla na kufanya uchumi wetu uwe wenye manufaa na tija kwa society yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia mjengeko wa riba kwenye mfumo wa pesa, unaweza ukakuta viashiria vya haya mambo ninayoyasema. Kwenye riba ya kibenki, imepungua riba kati ya benki na benki na riba ya kibiashara ni kama bado imebaki palepale, iko juu. Ukienda kwenye riba ya dhamana za Serikali unakuta imekwenda mara dufu, hali ambayo inasababisha na kushawishi wawekezaji kuacha kuwekeza katika production activities kwa maana uzalishaji wa bidhaa ambazo ndiyo muhimili mkubwa wa usafirishaji kwenda nje na wanafanya kazi ya kununua dhamana hizi kwa maana ya kuwekeza kusudi kuwapatia pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata role ya benki ambayo inatakiwa ifanyike unakuta haifanyi sawasawa, benki nao wame-concentrate katika kukopesha Serikali, hali kadhalika, kukopesha wawekezaji au watu ambao tayari wamepevuka wana uwezo wa kupata capital kutoka katika vyanzo vingine. Unakuta benki imejielekeza huko haitaki yaani imekosa uthubutu kabisa, benki imekuwa na uwoga, benki imeshindwa hata kutoa fursa kwa wananchi wa kawaida katika ku-enjoy mikopo katika maeneo hayo kwa kisingizio cha risk (hatari).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali hii kwa sababu ukizingatia kwamba hawa wananchi ndio wengi lazima athari yake ya kiuchumi utaiona pale kwamba watakosa pesa za kuwekeza na mwisho wa siku hakutakuwa na kitu chochote ambacho kitakuwa kimefanyika kwa ubora wake. Mipango ambayo tunayo, mipango mingi sana imekuwa haiendani na uhalisia na changamoto tulizokuwa nazo kama nchi kwa uchumi wa nchi hii. Mipango mingi imekuwa ikienda nusunusu tunakwenda sehemu tunagota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa hali jinsi ilivyo hii mikoa ya kusini hii mikoa imekaa kimkakati Mkoa wa Mtwara, Lindi, Ruvuma na Iringa ni mikoa ambayo imekaa kimkakati, lakini ni mikoa tajiri sana kwa uzalishaji wa chakula, pia ni tajiri katika masuala ya utalii, hali kadhalika ni tajiri kwa sababu ya mipaka iliyokuwa nayo. Inapakana na nchi ambapo nchi hizo ni tegemezi katika mikoa hii, lakini licha ya kuwa na hiyo hali bado hakuna mkakati mkubwa wa waziwazi kabisa wa kuonesha kwamba mikoa hii ina utajiri huo. Bado imeachiwa yenyewe ikihangaika katika kufanya uwekezaji mdogomdogo wa mtu binafsi. Tunahitaji uwekezaji mkakati katika mikoa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninategemea katika Mpango huu nione Reli ya Standard Guage ikitoka Mtwara kuelekea Mchuchuma mpaka Mbamba Bay, kwa ajili ya nini? Maeneo hayo yana uzalishaji wa Chuma cha Liganga, lakini pia na makaa ya mawe ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa Tanzania pamoja na uchumi wa dunia kwa sasa hivi kwa maana ya nishati ya makaa ya mawe. Hali kadhalika, chuma ambacho sasa hivi dunia nzima imekuwa kikipatikana kwa kiasi kidogo sana kwa hiyo kama tungejikita katika maeneo haya bila shaka hii gap inayotokana na masuala ya exchange rate, lakini na pia kutokukua kwa uchumi, yangepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda ninaona niunge mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)