Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia na kutoa maoni yangu kwenye mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2025/2026. Kwanza ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto nyingi za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilipata fursa ya kuchambua Taarifa zote mbili zilizopo Mezani hapa, Mapendekezo ya Mpango pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na tuliweza kutoa maoni yetu na maoni mengi yameingizwa kwenye Taarifa hiyo ya Kamati na ninaunga mkono hoja maoni yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye masuala machache ili basi niweze kushauri jinsi gani tutaweza kuboresha Mpango yetu kwa kiasi kikubwa. Jambo la kwanza ni katika utekelezaji wa miradi yetu ya kimkakati na kwenye hili tumeona mara nyingi kwamba miradi ya kimkakati na mikubwa inachelewa kwa sababu ya kutokuwa na coordination nzuri ndani ya Serikali. Tumeona Wizara zetu bado hazisomani, lakini taasisi za umma ndani ya Serikali hazisomani na hivyo kuchelewesha miradi mikubwa ya kimkakati kutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilipata fursa ya kukutana na wenzetu wa Shirika la Mandeleo ya Taifa (NDC) na walitueleza changamoto mbalimbali ambazo wao wenyewe wanakutana nazo ambazo zinawakwamisha kutekeleza miradi hii ya kimkakati kwa haraka. Wenzangu wameongelea hapa sana mradi mkubwa huu wa Liganga na Mchuchuma na tumeona kwamba kama Taifa ni jinsi gani tunachelewa kunufaika na faida za mradi ule kwa sababu ya kuchelewa kutekeleza kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye mradi mmoja wa Magadi Soda wa Engaruka. Mradi huu wa Engaruka wa Magadi Soda umeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu wa Miaka Mitano na ni mradi ambao unaonesha dhahiri kwamba ukitekelezwa kwa haraka, basi kama Taifa tutaweza kunufaika na faida nyingi kupitia mradi huu. Mradi huu cha kwanza utachochea ajira nyingi za Watanzania, lakini pia utachochea uanzishwaji wa viwanda vipya. Malighafi ya magadi soda inatumika na viwanda vingi ikiwemo viwanda vya kemikali, viwanda vya kutengeneza kioo, lakini pia kwenye kilimo wanatumia sana magadi soda kwenye kutengeneza mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu tutaweza kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. Pia, tutaokoa fedha nyingi za kigeni ambazo ni takribani dola milioni 120 na zaidi ambazo kwa sasa zinatumika kwenye kuagiza malighafi hii ya magadi soda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na manufaa haya utaona kabisa ni dhahiri kwamba mradi huu ukitekelezwa kwa haraka, basi tutaweza kupata manufaa mengi katika nchi yetu. Pamoja na manufaa haya Shirika letu la Maendeleo ya Taifa (NDC) walituambia wana changamoto kubwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini wanatakiwa walipe leseni ya uchimbaji wa madini ambayo ni takribani dola 153,000 na NDC wamekwama wameshindwa kulipa dola hizi na hivyo kuzuia na kuchelewesha mradi huu kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hii unaona kabisa kwamba ni dhahiri ndani ya Serikali wenyewe kwa wenyewe pia tunajichelewesha kwenye kutekeleza miradi hii muhimu na ya kimkakati. Kamati imeshauri vizuri sana kwamba kwa miradi ile ambayo inatekelezwa na taasisi za umma ndani ya Serikali basi tuweze kuwa na utaratibu wa msamaha wa kodi au tozo mbalimbali ili kuweza kufanya miradi hii inatekelezwa kwa haraka na Taifa liweze kunufaika na faida zinazotokana na miradi kama hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo mwenzetu wa NDC walituambia ambayo inafanya mradi huu usitekelezwe kwa wakati ni ukosefu wa miundombinu sahihi ambayo inaelekea kwenye mradi. Kwenye Mradi huu wa Engaruka kuna barabara za kimkakati, barabara kutoka Mto wa Mbu kwenda Selala lakini kuna Daraja ambalo linaelekea pia kwenye mradi Daraja la Mto wa Athumani ambapo miundombinu hii haijapewa kipaumbele ijapokuwa inaenda kwenye mradi wa kimkakati kama huu. Ninashauri pia Serikali iweze kutoa kipaumbele kwenye miundombinu yote ambayo inaelekea kwenye miradi ya kimkakati kama hii ili basi utekelezaji wa miradi kama hii uweze kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye Sekta ya Utalii, mara nyingi tumeona kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa malazi ya kulaza wageni wetu, Kamati ya Bajeti mara kwa mara imekuwa ikishauri Serikali iweze kufanyia kazi na ichukue hatua kwenye suala hili bado suala la malazi ni changamoto kubwa. Pamoja na jitihada kubwa ambazo anafanya Mheshimiwa Rais wetu, jitihada za kukuza sekta hii ya utalii, ninashauri Wizara yetu ya Mpango basi iweze kuweka mikakati thabiti ya kuendana na jitihada hizo ili basi tuweze kupata wawekezaji mahiri na wa uhakika wa kuwekeza katika sekta yetu hii ya utalii na kujenga hoteli yenye hadhi ya kulaza wageni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali wa utalii na wametueleza changamoto ambazo zinasababisha wawekezaji wengi kusita kuwekeza kwenye sekta hii muhimu ya utalii kwa ujenzi wa hoteli. Moja ya sababu kubwa waliyotueleza ni mikataba mibovu ya uwekezaji ambayo inaweka ukomo kwenye uwekezaji wa hoteli, ukomo wa miaka 15. Vilevile, mikataba hiyo haielezi wazi kwamba, kama mwekezaji hajarudisha faida yake ule uwekezaji utabaki kuwa wa nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kwamba, wawekezaji wale hawapewi hati ya maeneo ambayo wanawekeza na hii ni changamoto kubwa. Hii changamoto kwanza inawafanya wawekezaji waogope kuwekeza kwenye yale maeneo kwa sababu, siyo ya kwao, lakini vilevile changamoto hii inawazuia wawekezaji wetu wasiende kukopa kwenye taasisi za fedha. Hivyo, naomba sana Wizara ya Mipango na Uwekezaji wakishirikiana na Wizara ya Kisekta waweze kuangalia kwa kina hizi changamoto, ili basi waweke sheria na kanuni ambazo haziwabani wawekezaji kuwekeza kwenye sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu, naomba niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkoa wetu wa Arusha ametuletea miradi mingi ya maendeleo na kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Septemba, 2024 tumepokea zaidi ya shilingi trilioni 2.7 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Mkoa wetu wa Arusha unachangia takribani asilimia 4.7 kwenye Pato la Taifa na kuipa nafasi ya sita Kitaifa. Bado Mkoa wa Arusha una nafasi kubwa sana ya kuwekeza kwenye rasilimali zake na ninaamini kwamba, Wizara ya Mipango na Uwekezaji ikiangalia kwa jicho lingine Mkoa wa Arusha wanaweza wakaongeza zaidi uwekezaji kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia; kuna viwanda kama vya General Tire na Kiltex ambavyo hapo awali vilikuwa vinachangia sana kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Mipango na Uwekezaji iangalie ni jinsi gani itaweza kuvifufua viwanda hivi, ili basi viweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)