Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameturuzuku uhai huu ambao tuko nao na tunapata fursa ya kuchangia mpango huu ili kuboresha na hatimaye kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kuyafanya maisha ya Watanzania yaendelee kuwa bora. Jambo ambalo wananchi wanatutarajia kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia mambo machache ya kushauri. Kwanza ni kuhusu vyanzo vya mapato na ni pili baadhi ya maeneo ya vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama zingefuatiliwa taarifa zangu za kuchangia mpango ambapo hii ninachangia ni mara ya tatu, mara zote nimeshauri kuhusu uongezaji wa mapato kwa kutafuta vyanzo visivyo vya kodi. Moja ya chanzo ambacho nimekizungumza sana ni chanzo cha biashara ya carbon au hewa ya ukaa. Nimekuwa nikichangia chanzo hiki na nikachukua muda wa kujiridhisha umuhimu wake na namna ambavyo kinaweza kikaboresha mapato na kupunguza vyanzo vingine vya kikodi ambavyo vinawaumiza Watanzania na nitajaribu kutoa mifano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hudumu katika Kamati ya TAMISEMI na ziko halmashauri ambazo tayari zimeingia kwenye biashara ya carbon. Nitatoa mfano wa Wilaya ya Tanganyika ambayo mwaka jana imepata shilingi bilioni 14 kupitia biashara ya carbon kwenye misitu yake. Ipo mikoa ambayo mapato yake ya ndani hayafiki shilingi bilioni 14, lakini Tanganyika siyo peke yake ambayo ina mapato na ina misitu inayoweza kusajiliwa na kuingia katika biashara ya carbon.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara ya TAMISEMI. Nimekuwa nikifuatilia ushauri ambao Kamati imekuwa ikiutoa, nimeona wakianza kutoa semina na mafunzo kwa Halmashauri, ili ziweze kuingia kwenye biashara hii. Sasa kama halmashauri zetu zikipata chanzo kikubwa cha mapato ya ndani ambacho siyo cha kikodi. Mfano, mapato yake yakawa ni shilingi bilioni tano, bilioni 10, bilioni 12, kama hivi tunavyoona maana yake ni kwamba, tunawapunguzia Watanzania mzigo wa vyanzo ambavyo ni vya kikodi na kwa hiyo, uchumi wao utakuwa kwa sababu, tumepata mbadala ambao si chanzo cha kikodi. Hili jambo linawezekana
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hapa nimezungumzia Wilaya ya Tanganyika ambayo inafanya biashara ya carbon kwenye eneo la misitu, lakini turudi kwenye vyanzo vingine vinavyoweza kufanyika kwenye biashara ya carbon. Hapa tujiulize, kwa mfano, faida za SGR ni pamoja na kupunguza idadi ya mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuja Dodoma, kile kiasi cha carbon kilichokuwa kinazalishwa na yale mabasi, sisi kama nchi tunaweza kusajili kama mradi na tukapata mapato. Mapato yake yanaweza kuwa makubwa kuliko nauli ambazo Watanzania wanalipa. Swali la kujiuliza ni je, tayari TRC wamesajili? TRC–SGR kama moja ya miradi ya carbon?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishashauri kwa mfano, Mradi wa Mwendokasi, DART, pale Dar es Salaam, kwamba, kwa sababu, tulipunguza mabasi katika Jiji la Dar es Salaam maana yake ni kwamba, idadi ya mabasi madogo tuliyopunguza ile carbon iliyokuwa inazalishwa tungeweza kufanya kuwa mradi ukaingiza mapato katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam. Je, DART walisajili ule kama mradi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachokosekana ni weledi na utaalam katika kusajili miradi hii na kupata mapato. Tuombe ndugu zetu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji kuangalia fursa hii kwa sababu, mara zote tumesema fursa hii siyo ya muda wote, upo wakati itapotea na sisi kama nchi tutakuwa tumepoteza fursa ya mapato yasiyo ya kikodi ambayo yangeweza kupunguza utegemezi wa mapato ya kikodi ambayo kwa vyovyote vile yanawaumiza Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nirudie kusema kwamba, hatua zinaonekana. Kituo kinachosajili kipo pale Chuo cha Kilimo Sokoine, kinafanya vizuri, kinasajili miradi, lakini bado Serikali inatakiwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa kufanya maeneo husika, hasa Serikali za Mitaa na Halmashauri, kuelewa umuhimu wa kusajili miradi na kuhakikisha kwamba, tunapata mapato ambayo siyo ya kikodi. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kushauri ni kuhusu sekta ya kilimo na hapa nirudie ambalo wengi wamesema. Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kutegemea kilimo cha kutegemea mvua, bado tunahitaji kuwekeza kwenye umwagiliaji. Niipongeze Wizara ya Kilimo kwa sababu, ukiangalia tulipewa takwimu na Kamati ya Bajeti kwamba, lengo ilikuwa tufikie hekta milioni 1.2, lakini hadi sasa tuko hekta 727,000 siyo padogo ni hatua kubwa sana tumefikia na hii ni 60%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mpango wetu unaelekea mwishoni, lakini kuvuka 60%, kama ni mtihani nadhani tayari tuko kwenye C. Bado kidogo mpaka mwaka huu uishe, kama ni matokeo tunaweza kupata B, lakini ushauri wangu ni kwamba, bado tunahitaji miradi ambayo bado haijakamilika ikamilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mabwawa 18 ni mabwawa matatu ndiyo taarifa inasema yamekamilika kabisa. Maana yake ni kwamba kuna haja ya kuwekeza fedha, ili haya mabwawa mengine yaliyosalia kukamilika yakamilishwe na kama tunataka kujiridhisha tunaweza kujifunza kwenye maeneo ambayo haya mabwawa yamekamilika ni jinsi gani hali ya uchumi wa wananchi kwenye haya maeneo inabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi na ni dhahiri kwamba, hamna namna wala hamna njia nyingine ambayo tunaweza kusonga mbele kama hatutoi kipaumbele katika uboreshaji wa kilimo. Kwa kweli, Wizara ya Kilimo inafanya kazi nzuri sana, integration ni kitu muhimu, haya mabwawa yakishakamilika ndiyo sasa tutajua ni aina gani ya mbolea, mbegu, viuatilifu vinahitajika na kuwekewa ruzuku ili kukuza kilimo kwenye hilo eneo, tukifanya hivi tutaona kabisa uchumi unakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo inabidi tuliangalie kwa sababu hakuna namna tunaweza kukwepa kukuza uchumi wa nchi yetu bila kuangalia ukuaji wa Sekta ya Kilimo, pia hatuwezi kuangalia Sekta ya Kilimo nje ya kuangalia Sekta ya Umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuongeza jambo hili, katika kufanya kilimo vizuri, kwenye mipango yenu angalieni vizuri jinsi ambavyo halmashauri zinavyotenga bajeti kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo. Wote wanategemea mapato mengi kutokana na kilimo, lakini hata vitabu vitakatifu vinasema huwezi ukavuna mahali ambapo hukupanda! Sasa wao wanategemea mapato makubwa kutoka kwenye kilimo ambacho asilimia ya bajeti yake ni ndogo sana, maana sisi tunazipitia mara kwa mara hizi bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja ya kuweka kiwango cha bajeti ya ya kilimo na yako maazimio haya ya Kimataifa yamewekwa, nchi inatakiwa itumie asilimia fulani, hivyo hivyo, maazimio haya yashuke kwenye halmashauri kwamba, kwenye Sekta ya Kilimo ni lazima tuweke asilimia fulani kwa sababu ndiko tunakotegemea mapato makubwa, kama huwekezi kwenye kilimo mapato yatakuwaje? Sasa ndiyo pale unaweza kuanza kutafuta vyanzo vya mapato na hupati kwa sababu uwekezaji wako kwenye kilimo ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko haja pia ya Wizara ya Kilimo kuangalia namna ya kuzielekeza vizuri Halmashauri kuhakikisha kwamba huo upangaji wa bajeti unalenga katika maeneo ambayo yatakuwa na tija katika kukuza uchumi ili mapato ya Halmashauri yaweze kukua pia uzalishaji wa mazao kwa wananchi uweze kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kushauri leo ni kuhusu mpango mzuri wa matumizi ya fedha hasa pale ambapo zinakuwa zimekusanywa. Katika maeneo ambayo tathmini na majadiliano mbalimbali tunayoyafanya tumeona hayo maeneo yanahitaji attention kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni ukarabati wa shule kongwe za msingi. Shule nyingi za msingi zilijengwa miaka ya 1970 na 1980 kidogo, kwa hiyo shule nyingi zimechakaa. Pia, miradi mbalimbali inajenga shule mpya. Kwa hiyo, zile shule mpya zinakosa uwiano au kufanana na hizi shule ambao zimechakaa. Ni eneo ambalo pia Serikali inaweza ikazielekeza Serikali za Mitaa -halmashauri kujenga shule kongwe vizuri. Kwa hiyo, wanaweza kuwaelekeza kwamba, kipaumbele kiwe kwenye hilo eneo ila lazima kupeleka fedha nyingi, hata kama watapeleka, lakini hata utengaji wa fedha kwenye halmashauri ulenge kwenye maeneo yenye matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni ujenzi wa hostel za wasichana na hostel za wavulana kwa sababu kumejitokeza kusahau kwamba hata watoto wa kiume nao ni watoto, siyo kwa sababu ni wa kiume basi ni mkubwa, ndiyo maana ukifuatilia takwimu sasa hivi, ujenzi wa hostel nyingi za wasichana umesababisha wasichana wengi wanamaliza, lakini watoto wengi wa kiume wanaacha shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, udahili unakuwa mwingi, lakini umalizaji unakuwa mdogo! Hivyo, kwa sababu sasa hivi kupitia miradi mbalimbali shule nyingi za sekondari zimejengwa kwenye maeneo mbalimbali, lazima tujielekeze kwenye kuhakikisha kwamba, kwa sababu ya umbali sasa Halmashauri na Serikali kuananza kuwekeza kwenye ujenzi wa hostel kwa sababu ya kufuta ule umbali. Hiyo itasababisha performance ya wote, watoto wa kike na watoto wa kiume kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyo sasa, ambapo ule umbali wa kutembea unakuwa mrefu na hivyo inakuwa ni changamoto kubwa crosscutting kwa nchi nzima na kwamba kila unapokwenda, ukiacha maeneo machache ya mjini, watoto wanatembea umbali mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninawapongeza wote ambao wanaendelea kuandika na kupata maoni yetu. Ahsante sana. (Makofi)