Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo nimepata ili na mimi niweze kuchangia kwenye mpango wetu huu wa maendeleo wa Taifa. Nami nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Naibu Mawaziri na wataalam wote walioshiriki kuandaa mpango huu, bila kuisahau Kamati nzima ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kabisa kwamba, naunga mkono hoja maana kuna msemaji amesifia vizuri, ametoa mchango wake, amemsifia Rais na akawasifia Mawaziri wanatoka kwake, akashindwa kuunga mkono hoja hii. Nami nikajua ndiyo maana Mawaziri wote wawili wameoa Mkoa wa Kilimanjaro, maana sasa kama huungi mkono hoja kidogo anasababisha waje kule kwetu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kupongeza Serikali kwa namna ambavyo inasimamia mpango huu. Nianze kwa kusema kwamba, kuna maneno ambayo ningetamani sana tuyaone kwenye mpango wetu. Sijayaona moja kwa moja kwenye hotuba na pengine yapo kwenye tafsiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona mahali ambapo tumeonesha nia thabiti ya kwenda kuwa na bajeti ambayo tunaweza kui-fund wenyewe kwa 100%. Sijaona mahali kwenye huu mpango ambapo tunayo nia ya kwenda kuhakikisha bajeti yetu kwa miaka hii ya hivi karibuni, mwaka 2025 tutatoa utegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sasa hivi tuko kwenye 70%, lakini ni lini tutafikia 80%, 90% na 100%? Pia, hata kwenye mapendekezo ya Kamati wamesema na wamelitaja hilo kwamba, ni eneo ambalo na wenyewe wanategemea kuliona, kwamba, angalau sasa katika kila mpango tuseme mpango huu pamoja na mambo yetu yote tuliyoweka, tunategemea utegemezi wa bajeti yetu kwenye mikopo, misaada, mikopo ya nje tutaisogeza kutoka kwenye hii 30%, tutabaki na 10% na kuendelea. Kwa hiyo, hilo nategemea tuanze kuliona kwa siku ambazo zinakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nilitegemea pia kuona ni namna gani mpango huu unakwenda kuongeza tax base. Mheshimiwa Rais wakati anaongea na ile Kamati ya kwenda kumshauri kuhusiana na mambo ya kodi alisema kabisa kwamba, Tanzania wanaolipa kodi moja moja wanaonekana ni milioni mbili tu, sasa nilitegemea kwenye mpango utuoneshe ni namna gani tumekusudia kwenda kuongeza tax base, badala ya kwamba ni watu milioni mbili au taasisi milioni mbili, tunatoka milioni mbili, tunakwenda milioni mbili na laki tano, milioni tatu na kuendelea ili Tax base ikiongezeka, maana yake mzigo wa tax kwa wale wachache ambao wanatambulika utakuwa umepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye miradi ya kimkakati. Ninaipongeza sana Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwamba, miradi hii ya kimkakati imeshaonekana tayari inaleta tija. Leo tunaongelea SGR tayari inafanya kazi, leo tunaongelea bandari, wameelezea mafanikio ambayo yalikuwepo kwenye yale maono na tayari yameshaanza kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea Bwawa la Mwalimu Nyerere, juzi nimeona nadhani wale ni songas, mkataba wao umeisha na wala hatuna haraka wala wasiwasi wa kuwaongezea Mkataba kwa sababu umeme tayari tunajitosheleza. Vilevile, naona jinsi ambavyo shirika letu la ndege linavyoendelea kupambana, kwanza, kutoa usafiri ndani ya nchi, lakini kuendelea kupambana kimataifa. Tumeanza safari za Afrika Kusini, Marekani, Uarabuni na nyingine zinakwenda Zanzibar na kadhalika, kwa maana ya kwamba kutoka nje na kuja Zanzibar moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, juhudi za Serikali kuhakikisha Dodoma kama Makao Makuu inaendelea kuwa ndiyo makao makuu ya nchi, inapendeza na tunaona kabisa Serikali inafanya juhudi. Airport inaendelea na miradi inaendelea, kwa hiyo, ninaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi imetupima sana uwezo wetu wa kutekeleza mambo, ili sasa tuendelee tusikate tamaa na tusiridhike ni vizuri sasa ile miradi mingine ambayo inazungumziwa sana LNG, Liganga na Mchuchuma, tuweke timeframe kwamba, ni lini na hii inaingia kuongeza nguvu katika pato letu la Taifa, miradi mikubwa na kuonesha kwamba uchumi wetu unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la utalii, kwa sababu Moshi Mjini ni moja ya vituo vya utalii katika Kanda ya Kaskazini, ni eneo la muhimu sana. Nimeona nia ya Serikali kuhakikisha kwamba utalii wa mikutano, utalii wa michezo na utalii wa kimatibabu, unakwenda kujumuishwa katika kutangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye takwimu, kwenye yale majedwali pale, naona kama kuna tatizo. Tumesema tunategemea kutoka watalii milioni mbili kwenda milioni tano, lakini mchango wao kwenye Pato la Taifa, milioni mbili kwenda milioni tano ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya watalii tunaowapata. Pia, expenditure ya kila mtalii kutoka dola 230 kwenda dola mia tano hamsini na kitu kwa mwaka 2026, mchango ni kama mara mbili, lakini mchango wake kwenye pato la Taifa tunasema utatoka 17.5% kwenda 18.9%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa wakati watoa hoja wanaenda kuhitimisha hili wanifafanulie vizuri, kwa sababu kimapato tumesema expenditure ya mtalii mmoja itatoka zaidi ya dola 200 na kwenda zaidi ya 500, tumesema idadi ya watalii tunategemea itoke milioni mbili kwenda milioni tano. Sasa inakuwaje kwenye mchango tumesogea asilimia moja tu? Nadhani kuna kitu hapa nitaomba watufafanulie ili na sisi tuweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba, pia kwenye eneo la utalii tuangalie namna ya kuongeza utalii unaotokana na manmade attractions, vitu tunavyovitengeneza. Nilishasema tena Dubai ina utalii maradufu ya sisi na vitu vyao vingi ni man made. Kwa hiyo, tuendelee kuangalia vitu ambavyo ni man made ambavyo vinaweza kutusaidia kwenye utalii wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo lingine, sijaona mahali ambapo wameelezea au tumeonesha namna makusudi kwamba, sasa hivi hawa watalii milioni mbili tulionao, tuna vitanda kiasi gani na tutakapopata watalii milioni tano, tunao uwezo wa kuwa-accommodate? Tunavyo hivyo vitanda? Tuna sera ambayo itasababisha hivyo vitanda vijengwe? Tuwe na hoteli za kutosha na kuwa-accommodate hawa watu ambao ni mara mbili pamoja na miundombinu mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wameelezea vizuri hali ya uchumi kwa regional integration zote. Wameonesha SADC na position yetu, wameonesha East African Community na position yetu. Sijaona mahali ambapo wameonesha uchumi wetu utawezaje kunufaika kwa kuwa kwenye hizi regional integrations, kwamba, ni kitu gani cha kimkakati cha kuhakikisha kwamba tunahakikisha tunakipata mapema. Kwa mfano, tunakuwa supplier wa chakula kwenye regional integration (SADC pamoja na EAC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tuna position gani katika manufacturing katika hizo jumuiya mbili? Ilitakiwa mpango utuelekeze moja kwa moja. Hapa nikumbushe kwamba wakati tunapambana na SGR kwa haraka kuhakikisha inakwenda nchi kama Congo, tukumbuke pia kuna mpango wa kutoa treni kutoa Afrika ya Kusini kuja Angola mpaka Congo. Ni namna gani sisi tutahakikisha ya kwetu inafika mapema na benefits tunaanza kuzipata kabla ya hiyo nyingine haijaja? Kwa sababu dunia ni ushindani, sasa hatuwezi kutengeneza reli yetu taratibu wakati competitor wameanzia kule Afrika Kusini na wakafika kabla yetu. wakifika kabla yetu watakuwa wamesha-cement position yao kwenye hiyo na sisi tutapata shida ya kupata return kwenye uwekezaji wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sekta za muhimu za Kilimo na Uvuvi. Ninaelewa kabisa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha haya maeneo ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu, yanaendelea kuwa imara na yanaendelea kusaidia uchumi. Hata hivyo, kuna eneo ambalo ningetaka kuliona kwenye mpango; kwa mfano, ni namna gani haya mafuriko yanayotokea tunaya-capitalize ili kuhakikisha tunajenga mabwawa ya umwagiliaji yatakayosaidia kilimo, maeneo yote ambayo yana umwagiliaji. Pia, kwa mfano, ni namna gani Sekta ya Ngozi ambayo nimeiongelea juzi kwamba, 95% ya ngozi inayotoka kwetu inauzwa West Africa kama chakula. Kwa hiyo, maana yake bei yake siyo nzuri kama ingeenda kwenye manufacturing. Ni namna gani kwenye uvuvi nako tunahaikisha inakwenda kwenye manufacturing?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pamoja na mambo mengine ambayo nitachangia kwa kuyaandika, niunge mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)