Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa maandalizi ya mapendekezo ya mpango wa mwaka, pamoja na bajeti yake kwa mwaka 2025/2026. Ninaunga mkono kwa sababu wamezingatia vipaumbele vikuu vitatu vya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawakumbusha, kipaumbele kikuu cha kwanza alikitangaza siku alipoapishwa. Alisema, “nikisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, semeni kazi iendelee.” Kwa maana ya kwamba, yeye alikuwa amezamilia kutekeleza miradi yote mikubwa ya kimkakati ambayo ilikuwa imeanzishwa na mtangulizi wake, ndiyo maana akasema kazi iendelee, hivyo hicho ndiyo kipaumbele chake cha kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele chake cha pili alikuja akakitangaza baadaye kwamba, yeye atazingatia zaidi huduma za jamii kwa maana ya Sekta ya Afya, Elimu, Maji halafu baadaye ndio uchumi. kipaumbele kikuu cha tatu alikuja akakiandikia barua kabisa kwa watanzania, kudumisha amani na utulivu wa nchi. Kwa hiyo, niwapongeze kwamba, kwa kweli mmetembea kwenye vipaumbele vikuu vya Mheshimiwa Rais na mmeweza kutupatia dondoo kwamba, vipaumbele hivyo vinazingatiwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipitia kimoja baada ya kingine, miongoni mwa kazi alizozisema Mheshimiwa Rais kazi iendelee, ilikuwa ni mradi wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kufua umeme na kusambaza umeme kwa Watanzania, kwa lengo la kuwa na umeme wa uhakika ndani na ziada ya kuuza nje. Pia, niipongeze Serikali kwamba, kwa hatua ambayo imeripotiwa sasa hivi, tunakwenda vizuri na uwezekano wa kuukamilisha kabisa huo mradi katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 na mwaka ujao 2025/2026 ni mkubwa sana, Watanzania tujipongeze sana kwa mradi huu kwa sababu ni ukombozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza inawezekana tukapata viwanda vikubwa kwa sababu tuna uwezo wa kuvipata umeme. Hilo ni jambo ambalo limetajwa na wataendelea kulikamilisha, hilo ni jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa pili ni Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Viwango vya Kimataifa ambayo treni za mwendokasi zitapita humo. Tayari Watanzania wameanza kusafiri kutoka Dar es Salaam - Dodoma na juzi treni ya mchongoko imeanza kuja kutoka Dar es Salaam - Dodoma na kwa kweli imeleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Hata hivyo, mradi huu bado una vipande vya kuendelea kujengwa, kutoka Makutupora – Tabora; Tabora – Isaka; Isaka – Mwanza; Isaka – Rwanda; Tabora – Kigoma; kutoka Uvinza – Msongati; vilevile Urambo - Mpanda - Kalema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umetajwa kwenye mpango, ninaomba usiishie kutajwa tu Serikali iendelee kutumia mbinu zozote zile ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa muda. Mradi huu una faida kubwa sana kwa nchi, wasije wakashindwa na changamoto halafu wakaishia njiani, naomba niwatie moyo kwamba, endeleeni kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalenga kuongeza usafirishaji wa mizigo kutoka tani 200,000 mpaka tani milioni 10 na zaidi. Hiki ni kitu kikubwa sana. Mradi huu ukikamilika tunalenga kuajiri watu 600,000 ambao watakuwa ni permanent employment, watu zaidi ya milioni nane watasafiri kwa sababu sasa muda wa kusafiri utapungua kutoka saa zaidi ya 40 kutoka Dar es Salaam – Kigoma hadi saa chini ya 10. Kwa hiyo, ni jambo ambalo ni kubwa sana tunalifanya Tanzania naomba sana kutokana na umuhimu wa miradi hii, Serikali ifanye kila mbinu inawezekana kutekeleza miradi hii kwa 100%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna changamoto na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna wakati alilazimika kwenda nchi guarantors, siyo lazima nizitaje, kuhakikisha kwamba mradi huu unaendelea kuondoa changamoto ambazo zinajitokeza ili uweze kuendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Mradi mwingine wa Bomba la Mafuta (EACOP), nao ni mradi muhimu sana ambao inatakiwa waendelee kufanya kazi na Nchi ya Uganda ili kuhakikisha kwamba mradi huu nao unakamilika kwa 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanapoona kwamba miradi hii inachelewa kidogo kidogo wanaanza kujiuliza hivi kama nchi are we serious? Lazima tuhakikishe kwamba hii miradi ya kimkakakti inakamilika. Wito wangu kwa Serikali ni kwamba, watumie mbinu zozote zile ambazo zinawezekana ili miradi hii ikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kumung’unya maneno, kwa sababu tumeiona dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kuendelea kujenga na kukamilisha miradi hii basi mwakani 2025 ile kauli ya “Mitano Tena” itumike ili kusudi aendelee kusimamia miradi hii iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ambayo iliachwa na mtangulizi wake ni kama vile barabara za lami, madaraja makubwa, viwanja vya ndege, bandari, ujenzi wa meli na vivuko na kadhalika ni sehemu ya kipaumbele cha Mheshimiwa Rais cha “Kazi Iendelee”, na tumeona ambavyo utekelezaji unaendelea vizuri. Kipaumbele kikuu cha pili ni cha huduma za jamii, elimu afya na maji. Huyu ni Rais pekee ambaye ametoa fedha nyingi katika kipindi cha miaka mitatu na nusu tu iliyopita kuliko Rais yoyote ukilinganisha takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano, katika Halmashauri ya Wilaya yangu ya Sikonge fedha za elimu pekee imepokea zaidi ya bilioni 19 katika kipindi cha miaka mitatu na nusu, haijawahi kutokea. Ni jambo ambalo Mheshimiwa Rais analitilia mkazo sana. Isipokuwa kuna changamoto zake ambazo ni muhimu sana ziwe kwenye mpango. Kwa mfano, wenzangu wamezungumza kuhusu maboma ya madarasa, mabweni, zahanati na vituo vya afya. Sisi Waheshimiwa Wabunge kwa sababu tunakwenda vijijini tunatembelea wananchi na tunaona jinsi ambavyo wananchi wanakuwa wamejitolea nguvu kwa kweli naomba sana nguvu za wananchi zisipuuzwe kwenye mpango. Ziwepo kwenye mpango na ionekane kabisa kwamba Serikali imedhamiria kukamilisha maboma ambayo yalianzishwa na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha tatu cha Rais ni amani na utulivu. Sitaki kuzungumza sana kwenye eneo hilo kwa sababu inafahamika jinsi ambayo wanaendelea kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za jumla; ajira ni changamoto kubwa sana. Tumejenga madarasa, afya na zahanati, lakini ujenzi wa infrastructures uliofanyika haulingani na watumishi walioko kwenye shule, kwa maana ya walimu katika ngazi zote; msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vya maendeleo ya wananchi (FTC), vyuo vingine vya kati na vyuo vikuu kote kuna shida ya walimu. Maeneo haya yote yanahitaji mkakati kabisa ambao utabuniwa hata kwenye ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa sababu ukimuuliza Waziri wa Fedha atakwambia mimi nalia kwa sababu ya wage bill. Hii wage bill ni lazima watafute njia za kurekebisha ili watu wapate huduma iliyotarajiwa na zile infrastructures ambazo zimejengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya ushauri ni mawili tu; Mpango unazungumzia sana kuhamasisha uwekezaji. Hatuwezi kuhamasisha uwekezaji kama hakuna ardhi ya uwekezaji (land bank) na ardhi ya uwekezaji haiwezi kupatikana kwa sheria ya sasa hivi ya vijiji, ardhi inamilikiwa na vijiji na ardhi ikimilikiwa na kijiji huwezi kupata tittle deed. Ninaomba sana Sheria ya Ardhi ifanyiwe marekebisho ili tuweze kupata ardhi ya uwekezaji (land bank).
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kukamilisha miradi ambayo ilianza kutekelezwa zamani kwa mfano, Barabara yetu ya Mwanza – Tabora - Ipole - Mbeya haijakamilika. Ninaomba Serikali waweke kipaumbele kwenye barabara hiyo ili ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, hili la barabara nitawafuata Waheshimiwa Mawaziri tuongee vizuri. Ninashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)