Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nami fursa hii. Ninaomba kwanza nami nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Profesa Kitila Mkumbo na Dkt. Mwigulu na Naibu Waziri Mheshimiwa Nyongo na watendaji wao wote wa Wizara zao zote mbili kwa kuandaa vizuri mpango huu na pia kwa mwongozo wa bajeti 2025. Tunawashukuru sana na hongera sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaipongeza sana Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Pamoja na changamoto zilizopo duniani huko, lakini pato la Taifa limeendelea kukua kwa 5.1% mwaka 2023. Kwa taarifa hii tuliyosomewa hapa pato la Taifa kuanzia Januari hadi Juni limekua kwa wastani wa asilimia 5.4, lakini kwenye ripoti ya Tanzania Economic Outlooks inasema kwamba real GDP 2024 itakuwa 5.8. Kwa hiyo hongera sana kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa zao pia wamesema kwamba tunatarajia pato la Taifa kukua kwa mwaka 2025 wastani wa 5.8 mpaka 6.1 ambayo itakuwa 2026. Ukuaji huu wameeleza kwamba unategemea utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati; na miradi hii kimkakati wameeleza kuwa ni ya ni miundombinu ya nishati, miundombinu ya barabara, kuongeza mikopo sekta binafsi na kuendeleza sekta zingine na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuzungumzia kuhusiana na kuendeleza miundombinu ya nishati na barabara. Ni kweli kwamba wameuona umuhimu wake na ili uchumi uendelee na pato la Taifa liendelee kukua hatuna budi kuimarisha maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nilizungumza hapa, niliuliza swali kuhusiana na mradi wa umeme wa njia kubwa ambao unatoka Songea – Namtumbo – Tunduru – Masasi unaenda mpaka huko kwingine Mtwara; kwamba ni kwa nini umesimama. Hili walilolisema hapa, kwamba ukuaji wa uchumi unategemea pia miundombinu hii ya umeme; lakini mradi ule sasa hivi umesimama kwa sababu hawajalipwa fedha, lakini pia watu ambao wamepitiwa na mradi ule nao hawajalipwa fidia. Vilevile, mradi huu watu wenyewe wanaopitiwa kutoka Songea mpaka Masasi fidia yake ni bilioni mbili tu na milioni mia nne; na wamebaki wako na taharuki, kwamba mwaka huu wakalime wapi. Walitegemea wakilipwa hizo hela waende wakatafute maeneo mengine wakakate pori lingine ili waweze kulima; sasa mpaka leo hazina haijawalipa hela. Kwa hiyo tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapochelewesha miradi kama hii pia wanawachelewesha watu kiuchumi na pia tutachelewesha ukuaji wa pato la Taifa kama wenyewe walivyosema hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka 2025/2026. Serikali wamesema hapa kwamba inatarajia kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote vya jumla ya trilioni 55 na bilioni 61 huku mapato ya ndani yatakuwa ni trilioni 38.962. Dhamira hii ni kuhakikisha kwamba mapato ya ndani yanagharamia bajeti kiasi cha 70%. Ninaipongeza sana Serikali kwa sababu projection hizi ni nzuri, lakini pia kugharamia bajeti ya Serikali kwa 70% ni jambo kubwa sana; tumetoka mbali. Ninakumbuka wakati tunaingia hapa Bungeni na akina Mzee Mkuchika na akina Mzee Ole-Sendeka, Serikali ilikuwa na uwezo wa kugharamia 27% mpaka thelathini na kitu, lakini leo wanazungumza kwamba Serikali itaenda kugharamia bajeti mapato ya ndani zaidi ya 70%, hii ni pongezi kubwa sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye fedha hizo, jumla ya kiasi hicho trilioni 65, kama tulivyosema, makusanyo ya ndani trilioni 38, lakini kati ya hizo trilioni 38 za makusanyo ya ndani wamepanga kwamba zitatumika hizo trilioni 38 kwenye matumizi ya kawaida halafu matumizi ya maendeleo ni trilioni 16. Sasa ukitazama hapa utaona kabisa kwamba zile trilioni 16 ni zile ambazo tunaenda kukopa zote kwenye mikopo nafuu na mikopo ile ya ghali pamoja na misaada kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba lazima wataalam tuangalie hapa; uchumi duniani umebadilika, kwa maana ya kwamba kuna inflation kubwa sana huko juu na wenzetu sera yao kubwa ya kupunguza inflation ni kuongeza riba ya mikopo kiasi kwamba sasa hivi mikopo ina riba ya juu sana. Sisi hapa tunategemea kwenda kukopa huko takribani trilioni 15 kwenda 16 ya bajeti yetu, maana yake ni nini? Tunakwenda kukopa kwenye riba kubwa. Kwa hiyo, tuangalie hizi hela za ndani matumizi yake yawe ambayo yanastahili ambayo yatawezesha kupunguza gharama ya kuendesha Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara za kisekta watu wa mipango waangalie Wizara za kisekta zinapokwenda kupanga matumizi ya fedha za bajeti zao, wapunguze gharama zisizokuwa za msingi ili kuhakikisha kwamba tunapunguza mzigo wa Serikali wa kwenda kukopa ili fedha zingine hizi ziweze kusaidia katika miradi ya maendeleo ya ndani. Kwa sababu hapa inaonesha kwamba hela nyingi za mapato ya ndani tutakwenda kutumia kwenye matumizi ya kawaida. Ndiyo, utaniambia matumizi ya kawaida, ni kweli, inalipa kwanza mikopo, inatoa mishahara na pia inagharamia shughuli za Serikali. Sasa hapo inapogharamia shughuli za Serikali matumizi yake katika mpango huu ni lazima yaangaliwe ni ya aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine ni kwenye makusanyo; mtazamo pia wa revenue reforms. Tunashukuru sana Mheshimiwa Rais alivyounda Tume hii ya kuchukua maoni kwa wananchi mbalimbali, kwa walipakodi mbalimbali pia na kwa wasiolipa kodi. Ninaamini kabisa kwamba Tume hii itatufanyia kazi nzuri sana; ni hatua nzuri sana kwa sasa hivi. Ninaomba tuiunge mkono ili ifanye kazi yake vizuri, ije na matokeo chanya ya kuongeza wigo wa kukusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine pia ni eneo la miamala ya fedha katika simu zetu au katika mobile money transactions. Kuna ongezeko kubwa sana la miamala ya fedha katika simu; eneo hili linaonyesha linafanya kazi vizuri sana. Katika muda huu tu wa mwezi Agosti miamala milioni 310 ya fedha kwa kutumia simu imefanyika. Kwa hiyo eneo hili tunatakiwa tuliangalie vizuri sana na kiutalaam. Hili ni eneo zuri sana la kukusanya fedha. Kwa mfano, ukikusanya average shilingi 1,000 kwa muamala mmoja ni bilioni 310. Kwa hiyo eneo hili nalo lazima tuliangalie sana katika kuongeza mapato ya Serikali, tusilionee haya, tusiliache hivi hivi, eneo hili lina transaction nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatumia sana simu, ukiweka hela kwenye simu mara imekwisha. Kwa hiyo ni lazima Serikali iangalie kitaalam hasa katika eneo hili, kukusanya fedha ili kuweza kuongeza mapato kwa Serikali. Kwenye eneo hili mobile money account zimekua kwa asilimia 116. Mwaka 2019 tulikuwa na account milioni 25.8, lakini tunapozungumza hapa leo tuna account 55.8. Kwa hiyo hili ni ongezeko kubwa sana la account kwenye eneo hili, hili eneo tuliangalie kwa maana ya kuchukua pato letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwamba, ni lazima tuangalie sana kuwaendeleza wananchi wetu vijijini katika uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha mic basi naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)