Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mpango wetu wa mwaka mmoja. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Mipango, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Vilevile niipongeze sana Kamati ya Bajeti kwa kutupa maelekezo ambayo kwa kweli yametusaidia sana katika kutuonesha wapi tunakokwenda na vile ambavyo ni vipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza niipongeze Serikali, kuna mabadiliko mengi sana ambayo yamefanyika. Niseme wazi kabisa kwamba Serikali yetu ni Serikali ambayo inajali matatizo ya watu. Mambo mengi sana ambayo yamefanyika kwenye utekelezaji wa Ilani, lakini pia kwenye mipango mingine iliyopita yalijikita kwenye maendeleo ya watu na kutatua changamoto za watu. Kwa hiyo, niipongeze sana Serikali yetu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Baba wa Taifa alisema kwamba, maendeleo ya kweli ni maendeleo yanayojihusisha na watu na sisi Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni Serikali ambayo imekuwa inajihusisha na changamoto za watu. Kwa hiyo, nina kila sababu mimi kama Mbunge kijana kujivunia Serikali yangu kwa kazi kubwa ambayo imeifanya, lakini pia kwa malengo ambayo imekuwa ikiyafanya mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye mambo mawili kwenye kuzungumza. La kwanza litakuwa ni suala la Wizara ya Habari na Mawasiliano, lakini la pili itakuwa ni Wizara ya Nishati, haya mambo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye haya mambo mawili jambo la kwanza ninaanza na Wizara ya Habari na Mawasiliano. Kwanza nimpongeze Waziri wa Habari Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kazi nzuri ambayo anaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeusoma mpango huu na 90% ya kinachozungumzwa humu ndani kinazungumzia uchumi wa kidigitali. Uchumi wa kidigitali ni uchumi ambao unabebwa na Wizara ya Mawasiliano kwenye hatua kubwa na kwenye mambo mengi, kwa maana teknolojia na upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye vipaumbele vya Serikali kuna uchumi wa kidigitali hapa wanauzungumzia lakini pili wanazungumzia kuboresha ukusanyaji wa mapato. Niseme, Mheshimiwa Waziri wa Habari na Mheshimiwa wa Mipango hatuwezi kujadiliana kwenye Taifa hili mipango mingi ya ukusanyaji wa kodi mipango mingi ya kuhakikisha kwamba Taasisi za elimu zinakua na mipango mingi ya kuhakikisha kwamba mifumo ya Serikali inasomana kama tutakuwa hatuna uhakika wa access ya internet kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Access ya internet kwenye Taifa letu ndio msingi wa maendeleo ya sasa; kwa sababu asilimia inazungumzwa hapa zaidi ya watu milioni 36 kwenye Taifa letu wana access ya internet, lakini milioni 12 tu wanatumia 2G siyo 3G wala siyo 4G wala siyo 5G kwa maana kwamba internet yenye speed kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni nini ninachotaka kukizungumza na nini ambao ni ushauri wangu. Nimezungumza hapa na nimesoma kwenye ripoti ya Kamati. Wanasema, kuimarisha mradi wa ujenzi wa minara, lakini pia wanasisitiza sana kuongeza matumizi ya teknolojia ya akili bandi (artificial intelligence) katika Taasisi za Serikali. Hatuwezi kujadiliana artificial intelligence kwenye Taifa ambalo internet iko chini kwa kiwango ambacho mambo mengi ya Serikali yanakwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Watanzania kwenye kukusanya kodi unakwenda kulipia kodi taarifa utakayopewa ni kwamba mtandao upo chini. Utakwenda kusoma kwenye online course utaambiwa leo huna access ya internet lakini pia unaweza ukasafiri kutoka hapa kwenda Dar es Slaam ni maeneo mawili au matatu tu ndiko kutakuwa na uhakika wa kupata internet the rest there is no internet, sasa nini lazima kama Serikali ikifanye? Hatuwezi kujadiliana kwamba tusubiri miaka mitano, hatuwezi kujadiliana kwamba tusubiri miaka mwili. Internet ni kitu ambacho kiko sasa ambacho kinatumika hata dakika hii. Kwa hiyo ni muhimu Serikali ikafanya kazi kubwa kwenye kuimarisha misingi au mifumo ya upatikanaji wa internet nchini na hili niliombe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 90% ya vijana wamejiajiri na wamejiajiri wako mitandaoni wako kwenye maduka ya mitandaoni wanauza vitu. Hawa watu wanapokosa internet wanakuwa wamekosa mambo mengi na baadaye na sisi tunakuwa tumekwamisha shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, kuna mambo kwa mfano aliyazungumza Kamishna wa Ushindani wa Kenya, anaitwa David Kemei alisema: “Ujio wa Star Link ni kwamba utalazimisha kampuni na huduma za mawasiliano katika Nchi ya Kenya kufanya kazi kwa ubunifu. Tunataka kampuni za ndani zitikiswe ili zitoe huduma katika ubora wake”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe hatuzungumzii kwamba lazima twende kule Star Link, tunachotaka ni kuwa na uhakika wa internet kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo wakati Waziri akiwa Mheshimiwa Nape Nnauye, alisema: “TTCL mmejikita kwenye kujenga na kusimika minara, mnapambana na makampuni ya Voda na ya Tigo mmeacha fursa ya kutumia fiber, Mkongo wa Taifa kuusambaza zaidi ili kupatikana kwenye nchi yetu ili internet iwe ya uhakika na Taifa letu liweze kusonga mbele”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana Wizara ya Mipango hili jambo ikaliongelea kwa ukaribu sana na ikachukua hatua za haraka kuhakikisha tuna uhakika wa upatikanaji wa mawasiliano nchini especially kwenye mawasiliano ambayo yamechukua zaidi ya 88% ya Watanzania wanaotumia simu na wana access ya internet. Kwa hiyo, Wizara ya Mipango lazima iliangalie hili jambo kwa haraka, kwa sababu sasa hivi kodi ya Taifa hili inakusanywa kwa kupitia mfumo, lakini Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza mifumo lazima isomane. Tatu, tumekuwa tunafanya hadi operation. Ukisoma ripoti za Muhimbili zinazungumza. Kuna mambo ya operation yanafanyika yanatokea kwenye mataifa mengine kwa kutumia mifumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokosa uhakika wa mifumo kuna vitu vingi vinadondoka na kukwama. Utashindwa kukata tiketi, unataka SGR ifanye kazi, tiketi zinapatikana. Tunataka ATCL ifanye kazi, yote hii ni mitandao. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ya Mipango ikahakikisha kwamba inalifanyia kazi sana hili suala la upatikanaji wa internet kwenye Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mataifa ya jirani yameshatuacha. Kwa hiyo, sisi kwa sababu digital economy yetu imebebwa na internet, ni vema Waziri wa Mipango na Waziri wa Sekta husika wafanye kazi kubwa kuhakikisha kwamba internet inapatikana kwa uhakika kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG amezungumza, moja kati ya changamoto inayoikumba TTCL ni kushindwa kutumia fursa. Fursa waliyonayo ni upatikanaji wa mkongo wa Taifa ambapo wao wana mamlaka nayo. Kwa hiyo, ni vema wangelifanyia kazi hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambapo nataka kushauri kwa niaba ya wananchi wa Makete ni suala la nishati. Ukisoma ripoti ya Kamati na ukisoma mipango ya Serikali, moja kati ya mpango mkubwa ni kuongeza uzalishaji viwandani (bidhaa za viwandani), lakini pili, kwenye uwekezaj; hatuwezi kuimarisha uwekezaji kama nishati itakuwa siyo ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali, naipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa nishati kwenye Taifa letu umekuwa ni mkubwa na inapatikana vizuri. Hata hivyo, tusijisahau, alipokuja Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko pale Makete alisema: “Moja ya changamoto kubwa tuliyokutana nayo kama Taifa, tuli-relax kuongeza vyanzo vingine vya kuzalisha umeme, tukawa tumetulia ndiyo maana baadaye tukapata hii changamoto kubwa ya kukosekana kwa umeme.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, tuna vynazo vya umeme. Ukiangalia ukiwa unatoka Dar es Salaam unaelekea Moshi utakuta vibao vimeandikwa kuna upepo mkali. Serikali lazima itumie fursa ya kuvuna umeme kupitia upepo. Ukienda Singida kuna changamoto hiyo, kwamba tuna mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kwa kutumia upepo, lakini haujafanya kazi hadi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ambaye natoka Makete tuna Bwawa la Rumakali ambapo Serikali inakusudia kwenda kuhakikisha kwamba inazalisha umeme. Naiomba Serikali wakati wowote tuna haja ya kuwa na umeme wa kujitosheleza kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, ninaomba kama tunakwenda kuboresha uzalishaji wa umeme ni vema kwenye yaleyale maeneo kama ni Makete kwenye eneo la Rumakali fidia zilipwe kwa wakati ili miradi ianze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi, kwa jinsi ambavyo Serikali ya Mama Samia imesambaza umeme vijijini kwenye REA tuna haja kubwa sana ya kuwa na umeme wa uhakika, kwa sababu unavyosambaza umeme kwa wingi ndivyo pia ambavyo unatengeneza maendeleo yawe ni makubwa. Mfano mkubwa ni huu, Mgodi wa Geita Gold Mining ni mradi ambao kwa muda mrefu ulikuwa hautumii umeme wetu ndani ya nchi. Ni kwa sababu walikuwa hawana umeme wa uhakika, lakini kwa sasa Serikali yetu imefanikiwa wanatumia umeme wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa mgodi mmoja tu wa Geita ni sawasawa na umeme wa Mikoa miwili ya Njombe na Iringa kwenye matumizi. Kwa hiyo, kama tunaenda kuwekeza kwenye viwanda na kama tunaenda kuwekeza kwenye migodi lazima tuongeze uzalishaji wa umeme kwenye Taifa letu, ni muhimu sana. Niiombe Wizara ya Nishati kwamba kwa sababu tuna miradi mikubwa kama SGR, pia tuna migodi na Mheshimiwa Rais amekuwa akivutia sana wawekezaji kwenye Taifa letu, ukisomo kwenye ukurasa namba 25, ni vema tukawa na umeme wa uhakika ili wananchi wetu waweze kuwa na umeme wa kujitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alisema maendeleo ni maendeleo ya watu. Kwa hiyo, tukijishughulisha na shida za watu mojawapo ni kupatikana umeme wa uhakika kwenye makazi yao. Hayo yalikuwa ni mawazo yangu na naiomba sana Serikali iyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni upatikanaji wa internet ya kujitosheleza kwenye nchi. Pili, nishati ni muhimu sana kupatikana kwenye Taifa letu. Najua kwamba Serikali imekusudia kufanya mambo makubwa; sisi tunaiunga mkono and I am very proud of my country, especially utendaji wa Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais wetu anatufanya mtaani leo tunajivunia na tunatembea tunatamba ni kwa sababu amefanya kazi kubwa kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nawatakia kila la heri watu wa Mipango. Sisi kama Wabunge tuko tayari kuwaunga mkono, ahsante sana. (Makofi)