Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu na kuweza kuchangia. Pia, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo nchini na Nyang’hwale ikiwa ni miongoni mwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale Mama hatumdai; yeye anatudai na tunasema tunaenda na mama 2025. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa sana kwenye Jimbo la Nyang’hwale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla kuingia kwenye mchango wangu na ushauri naomba angalau niyaseme machache ya kumpongeza mama. Kwa nini sisi Wananyang’hwale tunampongeza? Mama ameweza kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo. Fedha hizi zimeenda kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo kwenye Sekta za Elimu, Maji, Barabara, Afya, Umeme, Mawasiliano ya Simu, TASAF, Ujenzi wa VETA, Kilimo, Madini pia mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana pamoja na wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja kubwa sana ambalo ni kama miujiza ametufanyia sisi Wananyang’hwale. Ameweza kutenga fedha kwa ajili ya kutujengea daraja ambalo lilibomoka zaidi ya miaka 40 iliyopita. Mama Samia ameweza kututengea fedha kiasi cha shilingi milioni 573. Daraja hili linaenda kukamilika mwezi wa 12. Baada ya miaka 40 mama ameweza kutoa fedha; Mama hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, ameweza kutujengea kilometa moja ya lami kwenye Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Nyang’hwale kwenye Mji wa Kharumwa. Baada ya kuyasema haya nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Mheshimiwa Professor Kitila Mkumbo, kwa hotuba yake nzuri ya mipango ya maendeleo ya 2025/2050. Ni mipango mizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba kwa mwongozo wake na kwa maelezo mazuri aliyotupa kwa hatua ambayo tumeifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, sasa nijielekeze kwenye mchango wangu kwa kifupi. Mchango wangu huu unaelezea mpango huu. Kuna baadhi ya mambo ambayo mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo nla Nyang’hwale na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna maeneo ambayo nataka nishauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mpango ni mzuri lakini kuna maeneo ambayo nikiyaangalia ukusanyaji wa mapato bado haujawa mzuri kwenye baadhi ya maeneo. Mfano, kuna watu ambao wamepewa majukumu haya kwa ajili ya kuisaidia Serikali kukusanya fedha ikiwa ni watumishi wa TRA na wafanyabiashara. Kumekuwa na ujanja unaofanyika wa kulipotezea Taifa hili mapato makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kweli inabidi tutangulize uzalendo mbele. Tuseme haki japokuwa tutalaumiwa, lakini ukweli lazima tuseme. Kwa nini nasema kwamba kuna uvujaji wa makusanyo ya fedha za Serikali? Leo hii utaona vijana wetu ambao wameaminiwa na Taifa hili hasa wa TRA wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara ambao siyo waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa TRA siyo wote wabaya, lakini wamo ambao ni vijana wameingia mle kwenda kupiga na kujinufaisha wao na siyo kulinufaisha Taifa. Nitatolea mfano kidogo. Utakuta kuna baadhi ya wafanyabiashara wanapofanya biashara zao hawatoi risiti. Vijana wa TRA unawaona wanapita kwenye maeneo hayo na hayo yanafanyika na hawachukui hatua. Kwa hiyo, katika ushauri wangu huu naomba, nitakapofika mwisho wayachukue wayafanyie kazi, kwa sababu nimekuwa nikichangia mara kwa mara na kutoa ushauri huu, lakini sioni kama unafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii unaweza ukaenda dukani ukanunua mali yenye thamani hata ya shilingi laki tano, tajiri mwenye duka au muuzaji anakuuliza, unataka risiti nikupe bei ya risiti au bei ambayo siyo ya risiti? Utakaposema nataka bei ya risiti, wakati wa kutoa risiti, hatoi risiti inayolingana na fedha ambayo umeilipa; umelipa shilingi laki tano, unakatiwa risiti ya shilingi laki mbili. Haya yanafanyika. Je, ndani ya TRA hakuna kitengo cha kufuatilia mambo haya? Kwa hiyo, ili tuweze kuendelea kukusanya pato la Taifa, nashangaa Mheshimiwa juzi hapa anasema tunakusanya fedha nyingi, lakini nikiangalia kuna fedha nyingi bado tunaziacha kule nje. Leo hii TRA inakusanya zaidi ya shilingi trilioni mbili, lakini kuna shilingi trilioni mbili au zaidi tunaziacha kule nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, naomba sana wauchukue. Watengeneze utaratibu ulio mzuri wa kuongeza hii faini ya shilingi milioni mbili/milioni tatu, naona si chochote si lolote, kwa sababu unayemtengenezea sheria ya kumpiga faini shilingi milioni mbili wakati amekuibia shilingi bilioni moja, tofauti yake ni kubwa sana. Naomba sana hili jambo wajaribu kulifuatilia kwa vijana wetu wa TRA, pia, wafanyabiashara wetu wanakuwa siyo waminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nishauri, kwa nini kumekuwa na tofauti kwenye hizi biashara zetu? Tuchunguze ni kwa nini? Leo hii unakuta mimi ni mfanyabiashara, tunatoa mzigo China makontena yetu ni mawili, tumepakia mali inayofanana. Makontena ya 40 feet yote mali iliyomo mle inafanana na tumenunua kiwanda kimoja na tumesafirisha meli moja, tunakuja kufikisha bandarini mzigo huo agent wetu wanaotoa mzigo inakuwa huyu anachukua agent wake na nachukua agent wangu. Unakuta huyu analipa shilingi milioni 40, huyu analipa shilingi milioni 20 kwa mali ileile. Hivi hamlielewi hilo? Hebu jaribuni kufuatilia. Haya yapo yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili linaumiza. Nimeshachangia na kutoa ushauri huu tangu wakati ule wa enzi ya Waziri wa Fedha, Waziri Mpango, nilishalizungumzia hilo lakini sioni kama hatua zinachukuliwa. Madukani huu utaratibu unaendelea. Leo hii nenda kwenye baadhi ya vituo vya mafuta, unafika pale unajaza mafuta anakwambia bwana mashine ni mbovu. Tangu asubuhi anauza ila anasema mashine ni mbovu. Hamlielewi hili kwamba huu ni upotevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wafuatilie kuna maeneo mbalimbali nendeni kwenye vituo vya mabasi na nendeni kwenye magari yanayosafirisha mizigo. Magari yanapakia mizigo hawatoi risiti na wakitoa risiti wanatoa risiti za mkono, kwa nini? Nendeni kwenye mabasi, unaenda kusafirisha mzigo gari linajaa chini mzigo zaidi ya shilingi milioni tano ama sita lakini hawatoi risiti na wakitoa risiti wanatoa za mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, kwa nini Serikali isichukue maamuzi kuagiza mashine za EFD? Mashine hizo ziletwe kwa gharama nafuu, wafanyabiashara wote wakopeshwe walipe kidogokidogo ili wawe na EFD machine. Tuondoshe lile suala la kwamba inatakiwa huyu mwenye shilingi milioni 100 ndiyo awe na mashine na huyu ana shilingi milioni 50 asiwe na mashine. Hii inaleta upotevu wa fedha za Serikali. Walete mashine, wahakikishe mtu yeyote anayekuwa na leseni ya biashara awe na mashine ya EFD ili tuweze kukusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato haya yanapotea. Ukiangalia mfano katika maeneo mbalimbali nchini, nenda maeneo mbalimbali kwenye maduka hawatoi risiti. Hizo pesa zinakwenda kupotea bure. Naiomba Serikali yangu sikivu ichukue ushauri huo wa kuweza kuagiza hizo mashine kutoka kiwandani kwa gharama nafuu na kuwakopesha wafanyabiashara kwa gharama nafuu ili waweze kulipa kidogo kidogo. Pia, wote ambao wana leseni za biashara wasajiliwe kwenye mfumo huo wa ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho naishauri Serikali, kwa nini isipunguze ongezeko la VAT 18% angalau basi turudi kwenye 14% ili watu wengi wawe na hamu ya kuingia kwenye mfumo huu wa VAT? Mwisho, nimewahi kuishi Malaysia, ndugu Waheshimiwa nchi ile hata ukienda kula mishkaki...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba hitimisha muda umeisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kula mishkaki ya shilingi 1,000, itaandikwa 1,000 na shilingi 100 chini pale kodi ya Serikali. Hebu tutenge fedha kwa ajili kutoa elimu, kuwaelimisha wananchi wetu kwa ajili ya kujua nini maana ya kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)