Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya Mpango wa Taifa. Mpango huu una vipaumbele vyake na vipaumbele hivi wamechagua vichache ambavyo ni muhimu; kuchochea uchumi, kuimarisha uwezo wa viwanda, kukuza uwekezaji wa biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza ujuzi (elimu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha mpango huo ni lazima tuwe na programu ya Kitaifa. Napendekeza programu hiyo ianze na chakula. Chakula ni kitu muhimu sana. Kwa hiyo, kuwa na chakula cha kutosha cha kuwatosheleza Watanzania wote kwa kutumia kilimo chetu wenyewe halafu kinachobaki tuuze nje kupata fedha za kigeni ni jambo la muhimu sana katika mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha umwagiliaji, tuna bahati sana kumpata Waziri Bashe. Kwanza, yeye mwenyewe anafanya kilimo cha umwagiliaji, ameanzisha mpango mzuri. Pia, ameng’ang’ania kuanzisha mabwawa ya umwagiliaji; haya yataleta uchumi mkubwa sana. Wakulima wakiweza kulima zaidi ya mara tatu au mara mbili kwa mwaka italeta tija ya ukuzaji wa chakula katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo la ardhi. Sasa hivi ni tabu sana. Ukisema upate uwekezaji wa ekari 1,000 au 2,000 za kulima shamba, hakuna. Serikali itenge ardhi ya kilimo na ijulikane kwamba ardhi ya kilimo iko hapa na anayetaka kuwekeza awekeze hapa na ijulikane na itunzwe kama tunavyotunza hifadhi za wanyama; iwepo ardhi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la nishati, amesema Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa kwamba umeme mkubwa utakaotoka Bwawa la Mwalimu Nyerere. Sasa naambiwa mashine mbili au tatu zimewashwa. Zile mashine tisa zikiwashwa zote kutakuwa na umeme mwingi sana. Tusiutumie kuwasha taa na kuuza wenyewe kama rejereja au chukuchuku. Umeme ule kuanzishwe viwanda vikubwa vya uchakataji wa kibiashara ili tuweze kuzalisha mali ambayo tutauza nje tupate fedha za kigeni. Suala la kupoteza dola moja moja hapa nchini na kwa mkasa mkubwa litaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika mpango huu kuna kitu kinaitwa ufuatiliaji, uthamini au tathmini na vihatarishi, lakini. sikuona mahali palipoandikwa research and development (R and D); lazima kuwe na utafiti na uendelezaji. Mataifa yote yaliyo juu kabisa kiteknolojia na yamepita vikwazo vingi vya uchumi yanafanya research and development. Bila kufanya hilo katika mpango huu tutajikanyaga. Lazima kuwe na mpango ambao unaonekana kwamba tunafanya utafiti na uendelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, nina furaha sana elimu tulipofikia siyo pabaya, lakini tunaifanya juu juu mno. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea hela nyingi tumejenga madarasa na mabweni, lakini limetokea tatizo la makazi ya walimu na walimu hakuna. Vijijini anapelekwa Mwalimu, lori la halmashauri linampeleka darasani; umefika saa 12 jioni teremka; hapa ndipo umeletwa, hakuna nyumba ya Mwalimu na hakuna chochote. Asubuhi yake Mwalimu anapaki mizigo anaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule tunazo ila hazina walimu. Nashauri bajeti ya elimu iongezwe ili kuwepo na miundombinu na huduma za walimu ziwepo shuleni. Tunasema elimu ni ufunguo wa maisha na ufunguo uko shuleni. Kama huko shuleni ni jalala, hauwezi kuwa ufunguo mzuri. Ni lazima iwe shule inayotambuliwa kwamba ni shule ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, liko tatizo moja, nami naumia sana, Bunge linakaa kujadili choo, matundu ya vyoo mpaka tunaomba msaada wa matundu ya vyoo. Hebu mpango huu uondoe suala la matundu ya vyoo katika msamiati wa Hazina na bajeti yetu. Vyoo vya watoto wa shule ni jambo baya sana, tuongelee madawati kwa sababu watoto wameongezeka, tumejenga shule, madawati sawa, tatizo la matundu ya vyoo linaweza kuondoka kabisa kama tuko serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji ni jambo kubwa sana kuleta maendeleo kwa wananchi, wananchi wanazurura kutafuta maji maana hayana mbadala. Itakuwa jambo zuri sana kama mpango huu utakazana kuleta maji kama ambavyo ipo na kukuza kiasi cha maji yanayopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafurahia sana miradi iliyokamilika kama SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, madaraja, meli zilizojengwa, Daraja la Magufuli. Ninampongeza sana Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, amejikita katika kuendeleza kufanya mambo yaonekane, hili litatusaidia sana, lakini nina jambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii TRC liwe corporate shirika pale juu, liwe na kampuni mbili, ya SGR na MTR, itaenda vizuri kuliko sasa, shirika limekuwa moja linaendesha reli mbili. Itakuwa jambo la maana sana kama kutakuwa na mashirika mawili ya kuendesha shirika letu la reli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mashirika, taasisi au sekta zinazotoa huduma, ni sekta muhimu, lakini Serikali haioni umuhimu wake. Sekta ya ulinzi binafsi nchini ina miaka 44 leo tangu ianzishwe haina kanuni wala sheria, wana uwezo si mnawaona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, polisi ni wachache askari zaidi ya 560,000 nchi nzima na kampuni zaidi ya 3,000 yapo, yanakusanya hela kiasi gani? Hakuna mfumo wowote, polisi wanatoa vibali mwisho leo polisi wenyewe wamejianzishia kampuni ya ulinzi, tazama sasa, si conflict of interest? Italeta mgongano wa maslahi maana polisi wanatoa vibali vya kampuni za ulinzi, leo na wenyewe wamejipa kibali. Lazima sheria ya sekta ya ulinzi nchini itungwe, ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote duniani kuna sheria ya sekta ya ulinzi katika nchi husika. Sasa hivi inashindikana, kampuni zote za security Tanzania hazina viwango kwa sababu hakuna mamlaka ya ku-certify kwamba kampuni hii ni group gani na hii ni daraja gani. Matokeo yake kazi zote za kimataifa kampuni za Tanzania marufuku, hazina viwango na vipimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nami ninafurahi sana na hii Sekta ya Afya inavyojengwa na Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuanzia hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati pia. Ninaomba, ninasali, vitendea kazi vyote katika hospitali hizi na zahanati viwepo kama ambavyo tumekusudia. Itafanya watu wawe na afya nzuri, watibiwe vizuri na wataipenda Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa muda huu na ninaunga mkono hoja. (Makofi)