Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii na ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa uhai na kupata nafasi ya kuchangia kwenye Mpango na Mwongozo wa 2025/2026. Vilevile, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ili nchi hii iwe na utawala bora na kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zimeonyeshwa kama mafanikio kwenye nyaraka hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Mawaziri wote wawili ambao wametuwasilishia Mpango na Mwongozo. Nimeipitia nimegundua kabisa kwamba ipo katika mazingira ambayo inatakiwa kuungwa mkono. Ninawapongeza wataalam, kwa maana ya Makatibu Wakuu, Naibu Mawaziri na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Mipango. Ninaamini kabisa ushirikiano wa pamoja ndiyo umetuletea nyaraka hizi ambazo sasa tunazijadili na kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyaraka hizi labda nianze na mafanikio kadhaa ambayo nimeyaona. Yapo mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka 2023, kwamba katika bajeti tuliyokuwa tumeipitisha mwaka 2023 ambayo matokeo yake sasa tunayaona huku na mpango tuliokuwa tumepitisha tunaona kabisa kuna habari ya SGR, kilometa 722 sasa inapitika na mimi nimebahatika kuwa msafiri ndani ya treni hiyo. Kwa hiyo, nina ushahidi wa kutosha kwamba sasa tunaweza kusafiri kwenye SGR kwa muda mfupi na shughuli zetu za kiuchumi zikafanyika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika mpango huu wa sasa SGR isiendelee kuonekana kama ni sehemu ya kutusafirisha sisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini ianze kushughulikia namna gani ya kusafirisha mizigo kwenye SGR ili tushughulike na suala letu la mapato na uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna umeme umeanza kuzalishwa kwenye Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, nimepata bahati ya kufika pale, kuna kazi kubwa imefanyika. Pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kuna kitu cha kufanya hapa. Hili Bwawa la Mwalimu Nyerere lisitupe furaha tu, furaha ni kwamba lazima watu wetu wa maendeleo ya jamii waende sasa kule vijijini kwa ajili ya kuwaelimisha watu ni namna gani watatumia kuanzisha miradi ili litumike kiuchumi zaidi badala ya kuendelea kutumika kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna idara yetu ya maendeleo ya jamii ukienda kwenye mikutano vijijini unauliza hapa mna vikundi mlivyounda kwa ajili ya uzalishaji? Wanakwambia hatujawahi kumwona. Kwa hiyo, ninaomba sana watu wa maendeleo ya jamii wafike huko. Umeme huu unaotegemea kuzalishwa kwa wingi uwe kwa manufaa ya kuinua uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote mtakumbuka kwamba ili tuonekane sasa tuna uzalishaji mzuri wa umeme, tunafikiria baada ya miaka mitano huenda tukahitaji megawatt 10,000. Hizi kidogo kama 4,000 tulizonazo mpango huu uanze kufikiria namna gani utatupeleka kwenye nafasi ya megawatt 10,000 ili tusiendelee kufurahia mafanikio haya baadaye tukakuta umeme hautoshi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna habari ya vijiji vyetu vingi sasa kuwa na umeme, baada ya vijiji vyote au asilimia kubwa kuwa na umeme mpango huu sasa ujikite kupeleka umeme kwenye vitongoji vyetu. Umeme huu usionekane tu umefika kwenye vijiji ikaonekana tayari ni access, lakini wananchi wanashindwa kuupata kwenye vitongoji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kukuta kijiji kimoja tu ndiyo kina umeme, vitongoji sita havina umeme. Sasa, mpango huu ujikite kuhakikisha kwamba umeme huu sasa unaingia kwa wananchi wetu kule kwenye vitongoji ili waweze kuutumia kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna habari ya maji vijijini ambayo nayo imeonekana hapa, ninataka kutaja vitu vichache tu. Mheshimiwa Waziri wa Maji atakumbuka kwamba Katoro ilikuwa haina maji lakini kwa shilingi bilioni 6.2 maji yamefika pale na sasa wameanza kutumia maji na visima vingi vinachimbwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ni ombi langu, mpango huu tunaokuja nao sasa ukahakikishe kwamba wananchi wetu wanapata maji na kiwango kile cha upatikanaji wa maji vijijini ambacho ni 79.6 kiongezeke kiende hata 81 au 82 ili mwaka kesho tukija kuzungumza tuzungumze figure nyingine ya maji kwamba imepatikana kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vipaumbele vya mpango huu ambavyo tunauzungumzia leo, kwamba, tulitakiwa tuchochee uchumi shindani na shirikishi, hapa, ndiyo naona bado tuna changamoto. Anayetakiwa kushirikishwa ni nani? Anayetakiwa kushirikishwa ni mwananchi wa kawaida, sasa anashirikishwaje? Tukienda kwenye sekta zetu, ili tuweze kumshirikisha mwananchi lazima sekta za uzalishaji zifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba tukienda kwenye kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua, niliomba scheme za umwagiliaji katika maeneo ya Busanda kule Lake Victoria ambako maji yanapatikana siyo mabwawa tena, lakini bado hatujafanya kitu chochote kule. Kwa hiyo inanionesha wazi kwamba wale wananchi wa kule Busanda hawatashirikishwa na ninataka washirikishwe ili taxbase ambayo tunaizungumzia hii, tuwe tumeitengeneza. Huwezi kuwa unavuna kodi mahali ambapo hujapaanzisha, tupaanzishe wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa ndugu zangu wa Mifugo na Uvuvi, tuna Ziwa Victoria kule ninakotoka mimi, kwenye jimbo langu sasa nina vizimba saba, kwa hiyo jimbo zima la watu 700,000 lina vizimba saba. Hoja yetu kubwa hapa tunataka tuwashirikishe, uchumi uwe shindani, lakini uwe shirikishi. Ninaomba sana, kwenye Mpango huu sasa Serikali ijikite kuhakikisha kwamba vizimba vingi vinakwenda kwenye maeneo yetu ili wananchi hawa sasa wazalishe na kodi yao itapatikana, uchumi wetu huu tunaouzungumzia leo, utapanda na pato letu la Taifa litakua kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo yako maeneo mengi ambayo tunataka wananchi washirikishwe. Bahati mbaya sana ushirikishi wetu umekuwa siyo mkubwa sana. Tuna vijana wengi Taifa hili sasa hivi hawana ajira, tunawapaje ajira? Siyo lazima tuwatafutie kazi ofisini, tukipeleka fedha kwenye maeneo hayo ya sekta za uzalishaji wataajiriwa huko na hii nafasi ya kutoajiriwa watu itapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, katika vipaumbele vilivyooneshwa ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji. Sasa hapa uwezo wa uzalishaji ndiyo napata changamoto. Wazalishaji wanaonekana hawajawezeshwa kule, tunaimarishaje uwezo wa uzalishaji. Kwa hiyo hoja yangu bado ni ileile ya shirikishi kwamba Serikali itenge na ifanye mipango ambayo itawashirikisha watu wengi ili tuimarishe uwezo wetu wa uzalishaji. Jirani yangu hapa Mheshimiwa Mwijage asubuhi alipokuwa anachangia alisema kwamba ana eneo karibu la hekta 7,000 au 8,000 huko (square kilometres 7,000) liko kwenye maji, lakini bado ushirikishwaji wake ili tuimarishe sekta ya uzalishaji bado siyo mkubwa sana. Kwa hiyo Mpango huu tunaouzungumzia leo, hebu utusaidie kwenye hilo

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia maeneo mahsusi yaliyolengwa na Mpango huu, la kwanza ilikuwa ni uendelezaji wa miundombinu hapa napo tuna changamoto. Mwenyekiti wa Kamati wakati anasoma Taarifa yake, alionesha miundombinu ya madarasa inahitaji takribani shilingi 267,000,000,000 ambazo halmashauri haiwezi kuzipata. Madarasa na maeneo ya vituo vya afya au zahanati ambazo zilianzishwa na akatoa ushauri kabisa kwamba Serikali iangalie uwezekano wa namna gani itawezesha hayo maboma ili yaweze kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mheshimiwa Mbunge humu ndani ukimuuliza, ana maboma ambayo hayajakamilishwa. Kwa hiyo tuombe Mpango huu ambao leo tunauchangia na kutoa ushauri wetu, ufanye hili. Tukiendelea kusubiri halmashauri maana yake maboma haya hayatafanyiwa kazi na tutaendelea kuyaona kila siku, yatakuwa na maswali lakini hayakamiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miundombinu iliyotajwa hapa ambayo inaonekana kwamba lazima tuijenge, kuna barabara. Nina mfano mmoja mdogo Mheshimiwa Waziri wetu wa Ujenzi atakumbuka kwamba tunatakiwa kujenga barabara, nilikuwa naiomba kila siku hii Barabara ya kutoka Mpomvu – Nyarugusu – Kakola lakini haijengwi. Hoja yetu kubwa tunataka barabara ile ijengwe kwa sababu wachimbaji wengi wako kwenye barabara hiyo, wanatakiwa kusomba mawe yao kupeleka kwenye CIP ambazo walizijenga siku nyingi ili wakazalishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaweza mkajua Sekta ya Madini inavyofanya, imefanya vizuri kwa sababu wale watu wanazalisha, bahati mbaya barabara ile haijengwi. Nitatumia neno gumu tu ashakumu si matusi, tusiendelee kuwekeza mahali ambapo tunajua panaweza pasituzalishie sana, tukawa tunatengeneza miundombinu ambayo ni kwa ajili ya kwenda kusalimiana. Tutengeneze miundombinu ambayo itakwenda kwenye uzalishaji, baadaye tutajenga hiyo mingine ambayo siyo ya kwenda kusalimiana. Tuhakikishe kwamba tunajenga miundombinu inayoenda kufanya uzalishaji, lakini tukiendelea kufanya hivi tunavyofanya na Mpango huu ukaenda tena usijenge barabara hizo, tutaendelea kupiga marktime muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata nafasi ya kwenda China katika semina moja, naona kuna mtu mmoja hapa tulikuwa naye kwenye semina hiyo, huwa hasemi. Tuliambiwa wao mwaka 1978 walianza na viwanda vya chuma, wakapambana kuwa na chuma cha kwao na baadaye wakajenga reli, wakajenga vitu vingine. Leo tuna Liganga na Mchuchuma hapa, mpaka leo yuko kwenye mazungumzo, sijajua mazungumzo yatakwisha lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokuwa na chuma yetu, kila tunachokijenga tutaagiza chuma kutoka nje. Mfano mzuri ni huu, leo tumejenga daraja kama lile la Kigongo – Busisi, chuma tumetoa wapi na tunapokwenda kushughulika na reli yetu ya SGR, chuma tunatoa wapi? Kwa nini tusianze kidogokidogo tukawa na chuma cha kwetu ambayo itatufanya tufanye miradi mingi kwa sababu tunaendelea kujenga SGR. Kwa hiyo kuna kitu cha kufanya hapa, tufanye maamuzi ili twende kwenye mafanikio makubwa kama inavyotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nataka kuzungumzia tena hapa ni ile gap ya kutokuwa tegemezi…

(Hapa kengele ililia kuashira kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Magessa, muda wako ulishaisha. Unaweza ukahitimisha tafadhali.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sekunde tano hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono hoja, nilitaka tushughulike na lile gap ambalo sisi tumekuwa tegemezi. Mpango wa mwaka jana ulikuwa na 29.3% ambao tunaomba mikopo na vitu vingine na Mpango wa mwaka huu una value ileile kwamba tuna 70.7 ambayo tunaweza kuitafuta ndani, lakini nyingine tunaitafuta nje. Tuangalie namna gani tunaweza kuiondoa hiyo 29.3%, kwenye Mpango huu tuje na wazo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)