Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru sana, kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia machache kwenye hotuba mbili za Bajeti Kuu ya Serikali lakini pia na ile ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ningependa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake hadi leo hii, lakini pia, nikishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi na Serikali yake chini ya Jemedari wetu Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli naomba tu nimhakikishie Mama kule Masasi sisi tumejipanga tupo vizuri na wala asiwe na wasiwasi mimi nipo kule. Niwashukuru pia Wananchi wangu wa Masasi Mjini kwa kuendelea kunivumilia lakini pia kunipa mwongozo na kunisimamia katika kutekeleza majukumu yangu kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo sasa naomba niingie kwenye mchango wangu. Ni bahati mbaya kwamba, muda ambao tunapewa kuchangia ni mdogo. Kimsingi hizi hotuba ni mbili ni Wizara mbili tofauti na tafsiri yake ni kwamba, tunapewa dakika tano tano kila Wizara. Pia, ni Wizara ambazo ndiyo Wizara core za kiuchumi kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, labda tunaweza tukafikiria hapo baadaye tuweze kuona upande wa Mipango iwe na siku yake iwe na mfumo wake wa kujadiliwa na Wizara ya Fedha iwe na siku yake ya kujadiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu zamani ilikuwa ni Wizara ya Fedha na Mipango kwa hiyo, ilionekana kama vile ni Wizara moja tu lakini kwa sasa ni Wizara mbili tofauti. Kwa hiyo, nilikuwa napenda kuleta hili kwenye meza yako ikiwezekana Kamati ya Uongozi muweze kulifikiria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ningetamani sana kushauri kwa wenzangu hapo Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Waziri wa Fedha, ikiwezekana tunayo Jumuiya ya Wachumi Tanzania, hebu bajeti kama hizi zinavyoandaliwa na taarifa kama hizi basi tuzipitishe kwenye vyombo vya fani zile ili tuweze kupata michango mizuri zaidi ikiwezekana tuweze kuboresha na kusaidia mchango wetu kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia baada ya kupitia taarifa hii ningetamani kupata ufafanuzi kidogo kabla sijachangia. Ukienda Ukurasa wa 29 wa Hotuba ya Mipango inaonesha pale mwenendo wa deni la Taifa. Sasa takwimu zake zilizopo pale kuna mkanganyiko kidogo. Kuna takwimu ambazo zinajirudia rudia kwa hiyo inaonekana kama vile kulikuwa na shida wakati wa uandaaji wa hii taarifa. Kwa hiyo, labda wanaweza wakanifafanulia kama ipo hivyo hivyo ili wakati wa kuchangia nijue nitachangia hivyo au kulikuwa na marekebisho kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano deni la ndani Machi, 2017 inaonesha ilikuwa ni trilioni 12.074, deni la nje mwaka huo huo ilikuwa ni kiasi hicho hicho na sasa deni kuu unajumlisha deni la nje na deni la ndani halafu kiasi ni kile kile trilioni 12 kitu ambacho haikiwezekani. Pia ukienda kwenye mwezi Machi mwaka 2021 deni la ndani ni trilioni 16.117, deni la nje trilioni 12.074 lile la 2017 halafu ukijumlisha zote mbili unapata ile ile 12.074. Kwa hiyo, inaonekana kama kuna mkanganyiko kidogo wakati wa uandaaji wa hii taarifa. Sijui kama utaruhusu nijibiwe kwanza hilo ndiyo nichangie au niendelee kuchangia tu kwa kujua kwamba hizo ndiyo takwimu halisi?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Geoffrey Mwambe taratibu inakutaka uoneshe kama kuna mapungufu, Serikali itapata muda wa kujibu wakati ambapo wataitwa na Kiti cha Spika. Kwa hiyo, unaweza tu ukatumia fursa hii kuonesha mapungufu uliyoyaona na ukachangia kwa upande ule unaodhani unafaa halafu Serikali itapata nafasi ya kutafakari na itakuja. Mheshimiwa Mwambe.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa mwongozo wako, basi naomba nikimbie kwa sababu muda wenyewe ni mdogo niainishe maeneo ambayo labda tungeweza kuyaimarisha kidogo ili bajeti zetu na hasa Mpango wetu uweze kukaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza nikubaliane sana na Mheshimiwa Askofu Gwajima, ni vizuri mpango wa bajeti uandaliwe na kujadiliwa kwa kina kabla ya Wizara za Kisekta, kwa sababu tunapojadili hapa tukibaini kwamba kwenye mpango, hiki na kile na kile kirekebishwe na utekelezaji ni Wizara za Kisekta tunafanyaje wakati tumeshapitisha bajeti zao? Kwa hiyo nilikuwa nafikiri hii ilitakiwa ije mapema itengenezwe mwongozo kama framework kwa ajili ya Sectoral Ministries kuweza ku-adopt.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilikuwa natamani sana …
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Geoffrey Mwambe samahani naomba uketi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Profesa.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwa sababu linajirudia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba mpango ambao tumeuawasilisha hapa ni mpango ambao mchakato wake unaanza mapema, mtakumbuka kwamba mwaka jana mwezi Novemba, Bunge hili lilijadili kwa siku saba mapendekezo ya mpango wa taifa wa maendeleo, baada ya hapo tarehe 13 mwezi wa kwanza mwaka huu tumekuja rasmi kwa ajili ya kupokea Mpango wa Taifa. Kwa hivyo, mchakato wake ni mrefu, ni mchakato wa mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari hapa wanachojadili walishajadili mapendekezo yake kwa siku saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa Taarifa.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo Waziri wa Mipango na Uwekezaji. Mheshimiwa Mwambe unapokea taarifa?
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea hiyo taarifa lakini labda tu kumshauri Mheshimiwa Kitila Mkumbo kwamba ule ulikuwa ni mchakato wa kupata maoni lakini alichowasilisha juzi ilikuwa ni hotuba rasmi sasa, ambayo tunasema ingetangulia ili Wizara za Kisekta ziweze kufanya mapping, zijielekeze kwenye kilichoandikwa kwenye mpango ili tusi-miss point. Kwa sababu kama sasa hivi hapa tukisema turekebishe kwenye mpango alichokisema sasa, Wizara ya Kilimo inaweza ikarudi ikarekebisha? Haiwezekani! Wizara ya Miundombinu inaweza ikaja kurekebisha? Haiwezekani! Kwa hiyo labda ni kuona namna tu yaku-improve. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nidokeze maeneo machache ambayo nilitamani niyasikie. Kwa mfano, nilikuwa natamani sana kuona kwenye mpango wa bajeti tunaonesha juhudi na mkakati wa kukuza umri wa kuishi wa Mtanzania.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwambe naomba uhitimishe muda wako unaisha.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Sawa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani sana wenzangu waweze kuonesha namna ambavyo tunaweza tukaimarisha umri wa kuishi lakini pia matumizi ya takwimu za sensa. Tumefanya sensa karibuni ni namna gani tunaweka juhudi za kupunguza kiwango cha umaskini kwenye nchi yetu lakini pia tunaongeza matumizi ya maeneo kama ya nishati kwa mfano SNG, kwa sababu tunataka sasa na hata Mheshimiwa Rais ana-thrive matumzi ya gesi kwa hivyo natamani mpango ujielekeze vizuri.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mwambe, tafadhali ahsante nashukuru.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru sana. (Makofi)