Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na ninaomba anisimamie katika mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa imara na mwanamke ambaye hajatikisika kuhakikisha anaendelea kuliongoza Taifa hili. Vilevile nikupongeze Mheshimiwa Mwigulu, kaka yangu na Mheshimiwa Mkumbo kwa namna ambavyo mnaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ndiyo tunakwenda kuhitimisha Bajeti Kuu na kwa bahati nzuri kwa utaratibu mzuri ambao tumejiwekea ni kuwa, hata kama bajeti za kisekta tumeshazipitisha, mchakato huu unapata kutuongoza pale tunapoona kuna mapungufu na maboresho tunaweza kwenda kushauri kuhakikisha sasa bajeti yetu inakuwa na tija kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake hapa aliongea kwa masikitiko makubwa sana, aliongea kwa uchungu mkubwa sana na aligusa mioyo na mimi alinigusa sana pale ambapo alionekana akisema tunapoteza Watanzania wengi kwa vitu ambavyo tunaweza kuvi-control, vipo ndani ya uwezo wetu. Nami naungana na wewe Mheshimiwa Waziri, na mimi nasikitishwa sana, pale kama taifa tunakuwa na uwezo wa kuzuia vifo vya Watanzania na hatufanyi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunapoteza zaidi ya Watanzania 1,500 ndani ya miaka mitano tumepoteza Watanzania zaidi ya 6,000 hadi 7,000. Naomba nitumie fursa hii kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo iliona jambo hili na walisikitishwa na jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 mpaka 2015 walichukua juhudi za maksudi wakatenga milioni zaidi ya 48 za Kimarekani, pesa za walipa kodi, pesa za watu maskini wakajenga kiwanda pale Kibaha, Kiwanda cha Viuadudu kuhakikisha tutazalisha dawa na kuzipeleka kwenye maeneo yetu kuhakikisha tunatokomeza malaria nchini. Kiwanda hiki ni cha kipekee, tuna viwanda kama hivi vitatu tu duniani, Japan, Tanzania na Cuba, kiwanda hiki kinatumia bio technology ambayo bidhaa hii haina madhara kwa binadamu, haina madhara kwa wanyama, haina madhara kwa mimea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema nasikitishwa na NIMR walitoa hati kuwa dawa inayozalishwa pale Kibaha ni salama na safi kwa matumizi ya binadamu. Kitu cha kushangaza kwa taarifa iliyokuja hapa wiki iliyopita, toka mwaka 2017 mpaka 2024 tumenunua lita laki moja na tisini tu ndani ya miaka sita! Uwezo wa kiwanda hiki ni kuzalisha lita milioni sita, wakati tunajiwekea mikakati tulisema ndani ya miaka mitano maana yake lita milioni 30 tungezalisha pale na kutokomeza malaria kwenye Taifa hili. Tungeokoa maisha ya watoto, tungeokoa maisha ya akinamama na nguvu kazi ambayo ingekuja kufanya kazi kupandisha Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naungana na wewe, hatuna sababu ya kuona Watanzania wakiendelea kuteketea, tume-invest zaidi ya dola bilioni 48, this ball is in your hands Mheshimiwa Waziri. Kama ambavyo umekasirishwa na vifo vinavyotokana na ajali ndivyo hivyo tukahakikishe kupambana kuhakikisha tunaokoa maisha ya Watanzania yanayopotea kwa sababu tu hatujatekeleza majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kwa unyenyekevu mkubwa sana. Kila mwaka tunatumia zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye kununua net, kufanya makongamano na kufanya semina. Sasa najiuliza kwa nini pesa hizi... (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Chumi. Mheshimiwa Chumi, tafadhali.
TAARIFA
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa dada yangu Mheshimiwa Rose, napenda pia kumuongezea taarifa kwamba dawa zinazotengenezwa na kiwanda kile moja wapo wa wateja wakubwa ni Nchi ya Angola. Kwa hiyo, pamoja na sisi dawa ile pia ingeweza kutuongezea kuwa chanzo cha mapato ya fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Angola wameamini dawa hiyo na mimi nilishiriki wakati wa uzinduzi wa kile kiwanda, alikuja Makamu wa Rais wa Cuba. Kwa hiyo kama Angola wameamini kwa nini sisi kama Taifa tunashindwa kuamini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimuongezee taarifa Mheshimiwa Dada Rose. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Rose Tweve, unapokea taarifa?
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya Mheshimiwa kaka yangu Chumi na yeye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatokomeza malaria kwenye Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu. Nilikuwa nahoji na ninajiuliza na nimejaribu kuuliza watu wengi; if we are spending shilingi bilioni 100 kwenye semina, ununuzi wa net na kufanya makongamano, kwa nini nguvu hiyo hiyo tusitumie kwenda kununua dawa ya viuadudu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakuja hapa mnatuambia ndani ya miaka mitano hadi sita tumenunua tu lita 200,000 na nchi zingine wanakuja kununua dawa kwenye kutokomeza malaria kwenye nchi yao. Mheshimiwa Waziri, ndiyo maana nimesema mazungumzo tuliyonayo hapa bado tuna room. Naiomba Serikali twende tukakae Kamati ya Bajeti, Wizara ya Afya na TAMISEMI; twende kuokoa maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Bajeti ya Afya, wametaja malaria mara 57 lakini hakuna kifungu kinachosema tutaenda kununua dawa na kwenda kutokomeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi kwa nini tunatumia hata neno “mapambano dhidi ya malaria,” tunapambana na nini Mheshimiwa Waziri? Kiwanda kipo pale ni kununua dawa na kunyunyizia, hayo mapambano tuyapeleke huko kwingine tukapambane na magonjwa ambayo yanashindwa kutibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili tutafanya historia. Mheshimiwa Waziri utaleta historia kwa nchi hii kuwa ndani ya miaka mitano ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeweza kutokomeza malaria kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, as long as...
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuwa kwenye Bunge hili, asubuhi, mchana na jioni nitaimba malaria kuhakikisha tuna...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose...
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ooh, thank you. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Stella, samahani muda umeisha. (Makofi/Kicheko)
TAARIFA
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na kwamba muda umeisha nilipenda kumpongeza kiongozi wa mbio za mwenge kwa kuungana na haya maneno aliyoongea Mheshimiwa Rose sasa hivi, kwamba Serikali za mitaa halmashauri zote zinapaswa kwenda kununua dawa zile ikiwemo Halmashauri yangu ya Nyasa. (Makofi)
MWENYEKITI: Kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za Bunge sawa sawa Mheshimiwa Rose Tweve unapokea taarifa ya Mheshimiwa Mbunge?
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Pia naomba unilindie muda wangu nina point za kumalizia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose, muda wako umeisha, ahsante sana.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja.
MWENYEKITI: Naomba hitimisha, ninakupa dakika moja.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini nisipopata majibu ya kuridhisha, Mheshimiwa Kaka nyangu Dkt. Mwigulu anajua how much I am proud of him, nitashika shilingi kuhakikisha Tanzania sasa inakuwa malaria free country. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)