Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango. Mimi hawa kwangu mmoja ni mwalimu wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mentor na mwingine ndiyo lifetime teacher wangu wa maisha yangu yote hadi leo niko hapa; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo machache ya kuzungumza. Jambo la kwanza ninaunga mkono hoja. Ninaunga mkono hoja kwa sababu kama Wanamakete tuna kila sababu ya kuunga mkono hoja kwa takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumza kwamba ninaunga mkono hoja? Serikali hii imetufanyia mambo mengi sana Wanamakete. Jambo la kwanza kwenye Sekta ya Maji kwa sasa Makete tunaongoza kitaifa. Tunatoa maji kwa wananchi kwa zaidi ya 92% kwenye sekta ya RUWASA. Ukienda kwenye vituo vya afya, hadi mwaka 2020 tulikuwa na vituo vitatu vya afya, Kituo cha Matamba, Kituo cha Lupila na Kituo cha Ipelele. Ninavyozungumza leo tumejenga vituo vya afya vingine saba ndani ya miaka minne. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuona Serikali imetusaidia na imetuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ninamuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, namuomba sana sisi Makete tuna barabara ya kiuchumi ya kutoka Makete kuelekea Mbeya. Barabara hii ina mkandarasi tayari anajenga kwa kiwango cha lami. Tunakuomba malipo yaende kwa wakati ili mkandarasi aongeze speed ya ujenzi wa barabara ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imebakiza lots mbili; lot ya kutoka Kikondo kuelekea Mbeya – Isyonje na lot ya kutoka Ipelele – Inio kuja maeneo ya Makete. Ni lot mbili zimebakia, kilometa 96 tu. Ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, mkandarasi yuko site, tunaomba alipwe ili ujenzi wa barabara hii uweze kuanza kwa ukamilifu wake na hatimaye Wanamakete waweze kuitumia barabara hii kwa sababu kwetu sisi hii ni oksijeni ya uchumi wa Wilaya ya Makate. Wanamakete wengi wanatumia sana barabara hii kwenda Mbeya kwa ajili ya shughuli za kibiashara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunakutegemea sana kwamba, mtamlipa mkandarasi ili speed ya kujenga barabara iweze kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni kwenye Barabara za TARURA. Makete ndiyo Wilaya ambayo katika Mkoa wa Njombe ina bajeti ndogo sana ya TARURA lakini sisi ndiyo wazalishaji wakubwa wa mazao mengi ambayo watu wa Dodoma na Dar es Salaam wanayatumia. Kuna barabara za kutoka Matamba kuelekea Itundu, barabara ya kimkakati kabisa na kiuchumi lakini hatuna fedha. Barabara ya kutoka Mang’oto kuelekea Ibaga, hatuna fedha na barabara nyingi za TARURA za Makete zina changamoto ya kutokuwa na fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutokana na changamoto ya kutokuwa na fedha, wakandarasi hata wale wanaopatikana wamekuwa wakijenga kwa kilometa chache sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi, taarifa.
TAARIFA
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mchangiaji anayechangia sasa hivi anachangia vizuri sana tena kimkakati. Hasa anapolenga suala zima la kuongeza uchumi katika Nchi yetu lakini nataka nimwambie changamoto ambayo anaiona Makete, changamoto hiyo hiyo ndiyo ambayo iko Songea Mjini kwenye barabara ya TARURA inayotoka Mshangano kwenda Mletele. Sasa na hii barabara ikienda ikajengwa kwa kiwango cha lami itachochea uchumi vizuri sana pamoja na Barabara ya kutoka Majengo kwenda Subira yenye urefu wa kilometa 18. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itakaa vizuri sana, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti...
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Msongozi yupo ndani ya kanuni, hajazidisha dakika mbili. Mheshimiwa Sanga unapokea taarifa ya Mheshimiwa Msongozi?
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokea taarifa yake na ninamuunga mkono kwa sababu anatetea Wananchi wa Ruvuma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Barabara ya Makete ni kubwa na ni mtambuka. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha alifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ambalo ninasimama nalo leo hapa, Waheshimiwa Wabunge, ninaomba sana tusikilizane. Ni suala la mabadiliko ya Sheria ya sukari ambalo Mheshimiwa Waziri amelizungumza hapa. Sheria ya Sukari Na. 6 katika mabadiliko yake kwenye kipengele namba mbili anasema “Kufanya marekebisho kwenye Kanuni ya NFRA kujumuisha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia food security; kwenye sheria yetu food security ina tafsiri hii, “all people at all time have physical, social and economic access to sufficient and safe food to meet their nutrition needs for an active and heathy life.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sukari, wananchi wanatusikiliza huko nje in a very sensitive way. Kwa nini nazungumza hili? Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Mipango nawapongeza sana kwa kuja na huu mkakati. hapa hesabu ni ndogo sana. Watanzania mnaotusikiliza, mlioko nje na mlioko hapa, hesabu ni ndogo sana. Hawa watu kwenye suala la sukari Serikali iliona ni tija iwape wenye viwanda kuagiza sukari nje, sugar gap inapotokea, Serikali iliona inatija. Lakini hawa watu kutokana na imani waliyopewa na Serikali wanapewa vibali waagize sukari; wao wamegeuza mchezo vibali wanakaa navyo na vingine wanaviuza. Wakiviuza vibali hivi sukari inachelewa kutoka nje ili kujaza lile gap na hatimaye sukari ya ndani inapanda bei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuomba, wasije wakaja na hoja kwamba Serikali hailindi viwanda, hakuna wakati ambapo viwanda vya sukari vimejengwa kama kipindi hiki cha Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan. Lakini katika kipindi hiki hiki Serikali tayari ina maeneo, maeneo ya Busega na Iringa ambayo inayaandaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya sukari. Hoja ya kulinda viwanda vya ndani siyo msingi; hoja ni maisha ya Watanzania walioko kule nje ambao sukari ilifika shilingi 7,000, shilingi 11,000. Hatuwezi kuwa na hoja ya kulinda viwanda vya ndani na watu ambao wanaifanyia sabotage Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu tunajua wana nguvu na kuna maneno yamezungumzwa hapa na mwandishi mmoja anasema hivi; “older men declare a war but it is the youth that must fight.” Vijana wa Wizara ya Kilimo wanajitahidi kupambana na jambo la sukari na bahati mbaya sana nimesoma political science, wanasema “The most peripheral countries zinakuwa driven by events.” Watanzania ni wasahaurifu, juzi tu hapa walikuwa wanapiga kelele ya sukari lakini hakuna Mbunge alikuwa anaenda kufanya mkutano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mabadiliko ya sheria...
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sheria haya yana...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga naomba uketi.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilinde... maslahi ya nchi.
MWENYEKITI: Naomba uketi.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Taarifa mzungumzaji.
MWENYEKITI: Hii ni Taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Sanga zisizidi mbili.
TAARIFA
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Taarifa mzungumzaji, ni katika Bunge hili hili Serikali imeongeza bajeti katika Wizara ya Kilimo hususani katika component ya umwagiliaji. Sasa nataka nimpe Taarifa kwamba tunavyoongelea umwagiliaji tunaongelea kupanua mashamba makubwa ya miwa ili tuweze kuzalisha sukari za kutosha ili tuwe na malighafi na tuzalishe hapa nchini. Tutengeneze ajira, tunavyoongelea kununua sukari nje tunaongelea kutengeneza ajira Brazil na maeneo mengine.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga unapokea, Mheshimiwa Sanga naomba uwe na uvumilivu.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hajui anachokizungumza.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga sijakuruhusu.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hajui anachokizungumza.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga uketi tafadhali. Zima microphone, Mheshimiwa Sanga unapokea Taarifa ya Mheshimiwa Anatropia?
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei, kwanini sipokei sisi sukari yetu kwenye hivi viwanda Mheshimiwa Rais analinda kabisa ajira na viwanda vya Watanzania. Nataka nikwambie kinachofanyika simple tu, Kilombero inafanya expansion sasa hivi ni Serikali hii imeruhusu, Kagera imefanya expansion ni Serikali hii inaruhusu na Watanzania wako huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokizungumzia viwanda tulivyonavyo havina utoshelevu wa uzalishaji wa sukari, kwa hiyo, Serikali hii kwenye kupambana huwa inakuwepo na hilo gap sugar inawaruhusu waagize sukari ya nje. Kuwapa kibali waagize sukari nje wale watu wanavificha vibali mfukoni mwisho wa siku bei ya ndani inapanda. Watu kama hao unawaruhusuje waonewe huruma kwenye suala kama hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe jambo moja suala la sukari ni sensitive, ni usalama wa nchi, naipongeza Serikali kuleta mabadiliko ya Sheria lazima tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa hiki anachoenda kukifanya. Hatuwezi kuruhusu monopolization ya soko, hatuwezi kuruhusu monopolization ya soko ya watu saba ambao wanakaa mkakati. Nakupa tu mfano mmoja watu wanaotetea hawa watu walipewa tani 15,000 waagize sukari wameleta tani 2,300 ndani ya miezi sita sukari haipo nchini ili bei ya ndani ipande. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wapo Tunduma wanaona sukari kutoka Zambia inatoka inakuja kwa bei nafuu wapo Kyela wanaona sukari kutoka Malawi inakuja kwa bei nafuu Tanzania tunaumiza watu wetu unaenda kuwatetea kwamba hawa watu wafanye nini? Hii tunaita sukari ilikuwa jela sasa tunataka kuiokoa sukari yetu iweze kwenda kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali na ninalishawishi Bunge yoyote anayepinga mabadiliko ya Sheria maana yake anasema nini? Maana yake anasema sukari iendelee kupanda bei kwa sababu hawa watu tunawaruhusu waendelee kuagiza sukari kidogo ili sukari bei ya ndani iweze kupanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe Bunge, iungeni mkono Serikali kwenye ajenda ya sukari, Mheshimiwa Rais amenuia kuishusha bei ya sukari kwenye Taifa letu. Hatuwezi kukubali watu wachache wa-monopolize.... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sanga.
MHE. FESTO R. SANGA: ...soko na hizi nguvu wanazozitumia huko nje kwenye media, hizo nguvu wanazotumia kushawishi tuzikatae tutetee maslahi ya Taifa letu,...
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sanga.
MHE. FESTO R. SANGA:....tuwatetee Watanzania, ninawatetea wana Makete waliopo Bulongwa waliopo Ipelele waliopo Lupila wanaopambania nchi yao na siyo kitu kingine kile.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nampongeza Mheshimiwa Waziri, nakupongeza Mheshimiwa Waziri wa Mipango songeni mbele tupo tayari kuwakingia kifua na Mheshimiwa Rais amekuwa aki-intervein...
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sanga.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikula dakika zangu dakika ya mwisho.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika ya mwisho, hakuna cha Taarifa hapa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga ahsante, Mheshimiwa Sanga nimekupa muda wa kutosha tafadhali, tafadhali, tafadhali.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na changamoto ya mbolea...