Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kupata nafasi hii na mimi ya kuchangia kama mchangiaji wa mwisho kwa session ya asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza niseme wazi kwamba naunga mkono hoja kwa sababu ya kazi kubwa ambayo imefanyika Jimboni Kasulu Vijijini. Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli mkono wake tunauona mpaka chini hela zinashuka mpaka vijijini na miradi inaonekana inavyotekelezwa wananchi wanaona na sisi viongozi tunaona, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hongera sana sana kaka yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda moja kwa moja kwenye mchango yangu na mchango wa kwanza nataka nigusie kidogo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu namna ya ukusanyaji wa VAT kutoka kwa wafanyabiashara ambao kimsingi ndiyo mawakala wa kukusanya hizo fedha kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu ambapo wafanyabiashara wengi hasa ni suppliers wanavyokuwa wame-suppliers vitu hasa Serikalini kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ili waweze kupeleka madai yao lazima watoe invoice, lakini pia watoe EFD receipt, waambatanishe kwa ajili ya kwenda ku-claim madai yao waweze kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida inatokeaje, mfanyabiashara akishatoa risiti ya EFD, TRA anarekodi kwamba amefanya mauzo, kwa hiyo mwezi ujao tu anaenda kudai hela kwa mfanyabiashara. Wakati mwingine hata hamjawasiliana anapeleka demand notice benki ili wakamate hela ambayo umekusanya VAT wakati kule ambapo Serikalini ame-supply vitu hata hela yenyewe hawajamlipa. Ninyi ni mashahidi na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni shahidi, malipo kwa suppliers wa ndani inaenda mpaka miezi sita, mengine mpaka mwaka mzima lakini TRA ukishatoa tu risiti mwezi ujao wanaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wengi wanafanya general supplying kwa mikopo, mtu amepata kazi, ana-supply kwenye taasisi moja ya Serikali labda tender ya bilioni tano anaenda benki anaomba mkopo, anapewa facility, ana-supply vitu kwa mkopo anategemea umlipe kwa wakati aweze kulipa benki abaki na faida kidogo. Unakuta VAT labda ni bilioni moja, wewe unaenda kukamata bilioni moja ambayo hata kwenye account wengine haipo ana milioni 200 yake au milioni 300 unakamata, hii Hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utaratibu tuweke vizuri kuwepo na communication. Mimi nadai Serikali halafu Serikali inakuja kunidai tena kupitia TRA hela ambayo sijalipwa yaani sijai-collect, hiyo VAT sijalipwa na Serikali, lakini TRA wanataka that money 18%. Kwa hiyo, naomba hilo jambo kidogo kuwepo na mawasiliano tutaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza sana mchango wa mashirika ya umma kwenye pato la Serikali bado haujawa mkubwa, ipo namna ambavyo tunaweza tukafanya, lakini hasa mwarobaini mkubwa ni kurejesha ule Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ambao ulitakiwa uje Bunge lililopita, haukuja. Lazima tuweke utaratibu wa kuwajibisha Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali ili waweze kuwa serious kwenye kufanya majukumu yao, tuwapangie KPIs, tuwawekee malengo waweze kufanya kazi vizuri. Nakuhakikishia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kama ule muswada ukirudi tukaupitisha maana yake ulipita katika Kamati yetu na tukaujadili vizuri, unaenda kuwa mwarobaini wa kuongeza mapato ya Serikali kupitia mashirika ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeshauri pia mambo ya Kitaifa tukitaka kuyazungumza tuyape kipaumbele, nataka niguse kidogo kwenye suala la sukari, sukari tatizo lake ni nini hasa kwenye nchi yetu? Moja ni upatikanaji wake, lakini mbili bei kubwa maana wakati mwingine inauzwa kama bei ni kubwa, lakini inapatikana yaani upatikanaji wa sukari Tanzania hautabiriki kila mwaka utasikia sukari hakuna, sukari haitoshi mpaka wakati mwingine mwenye duka hawezi kukuuzia kilo mbili atakwambia chukua kilo moja mwingine achukue kilo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni bei, sukari inaenda mpaka shilingi 7,000, shilingi 10,000 kwa kilo. Sasa ukiangalia haya yote ni so artificial yaani ni cartel tu fulani hivi, ni watu wachache wanakaa wanakubaliana tuweze kufanya sukari isipatikane moja, lakini mbili tuweze kufanya sukari ipande bei, why? Hii scarcity ni artificial kwa sababu haiwezekani, sukari unaambiwa Tanzania haipo, lakini Kenya ipo, Uganda ipo, Malawi ipo unaambiwa Tanzania haipatikani, tena watu wanapanga foleni. Unajiuliza sisi tupo kisiwani, halafu ukihoji utaambiwa unajua hili jambo ni zito, sukari kuipata duniani ni kazi, haiwezekani kuipata kwa kila mtu, Kenya wameipata wapi, Uganda wanaipata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, they are doing it makusudi kwa sababu wanajua kwenye formula za biashara supply ikiwa ni ndogo price inafanyaje, inakuwa kubwa, wanafanya makusudi. Tuliwahi kukutana nayo Bodi ya Sukari kwenye Kamati, tukahoji kwa nini sukari inakuwa ni ngumu kupatikana, wakatupitisha kwenye utaratibu mzima wa kuagiza sukari tukaona kuna tatizo. Lazima tufanye mabadiliko na sisi tukasema kama Kamati lazima tufanye mabadiliko ya uagizaji wa sukari ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wapo watu wanajenga hoja wanasema tusijikite kwenye kuagiza sukari kwa sababu eti tunavyo viwanda vya ndani, ni uongo mtupu. Kabla ya kufanya maamuzi ya Bodi ya Sukari itoe vibali kiasi gani sukari iagizwe, inakaa technical team ambayo inapiga hesabu inajua gap sugar yaani mahitaji ambayo viwanda haviwezi kuzalisha ni kiasi gani. Baada ya kujua hiyo gap wanashirikishwa wazalishaji, sisi tumeongea na Bodi ya Sukari kwenye Kamati yetu, halafu baadaye wanawapa vibali wale wazalishaji wenyewe waende na wao kwa sababu wanajua wakiagiza sukari siyo kwamba sukari yao itakosa soko yaani ile market portion yao haiguswi kama mahitaji ya sukari ni tani 550,000 nadhani kwa mwaka wao wanataka laki tatu, laki mbili lazima waagize nje. Kwa hiyo, ukileta tani 200,000 haiwezi ikaharibu ili soko la tani 300,000. Hakuna kiwanda kinachouawa hapa, ila ni cartel ambayo inatengenezwa tu ili sukari isipatikane Tanzania, halafu then price iweze kupanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hongereni sana, nimeona kwenye Finance Bill tunaenda kubadilisha utaratibu. Lazima tuweke utaratibu mzuri, hii ni nchi yetu sote, haiwezi nchi ikashindikana kwenye jambo hili. Sukari ni neno ambalo kwa Watanzania ni maumivu makubwa sana na ni kila mwaka miaka yote tangu tukiwa wadogo sukari is a problem kama vile magendo, magendo ni kama dawa za kulevya, no thank you, sukari inapatikana vizuri Brazil, inapatikana nchi mbalimbali, inapatikana Dubai na ndiyo maana intervention ambayo Serikali imefanya last time juzi hapo baada ya hawa wazalishaji kusema kwamba sukari haipatikani Serikali ikaagiza tani zaidi ya 50,000 imepatikana wapi? Maana walisema haipo imepatikana wapi? Na ndiyo ikatuokoa kutoka shilingi 10,000 mpaka sasa hivi imekuwa shilingi 2,800. Sasa anakuja mtu tena bahati mbaya wakati mwingine ameaminiwa na watu, amechaguliwa na wananchi, yaani wewe unataka Kasulu Vijijini wanunue sukari shilingi 10,000? Unataka Jimbo la Kisesa pale Mwanza wanunue sukari shilingi 10,000 kwa kilo? Unataka Mlale wanunue sukari kwa shilingi 10,000? No thank you.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vuma endelea. Mheshimiwa Musukuma ulishapata nafasi ya kuomba Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijatoa, mimi sijatoa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vuma tafadhali.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, haya mabadiliko yatasababisha na yatatusaidia availability ya sukari katika nchi yetu iwe ya uhakika na Watanzania waondokane na hayo maumivu makubwa ambayo wameyapata miaka yote, lakini affordability ili iweze kununuliwa katika bei ambayo haiwaumizi Watanzania wa kawaida hasa ambao kila wakati wanagombanishwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo makundi mbalimbali ikija mwezi Mtukufu Waheshimiwa Mawaziri wote roho juu, Mheshimiwa Rais roho juu, sisi Wana-CCM roho juu sukari itakuwaje, sukari itakuwaje? Kumbe ni maslahi ya watu wachache, we should say no to this and hii lazima ifike mwisho. (Makofi)

Kwa hiyo, hongereni Serikali kwa maamuzi mazuri ambayo mmefanya na tunaamini kwamba itaenda kufanya vizuri, NFRA watafanya kazi yao vizuri lakini pia huo ukiritimba yaani bureaucracy ikikoma, tunaamini Watanzania watakuwa wametuliwa mzigo mzito ambao wameubeba kwa miaka mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)