Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza jioni ya leo niweze kuchangia hoja mbili zilizoko mbele yetu. Kwanza kabisa naanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyofanya kazi kwa kweli, sisi Watanzania tunasema mama anatutendea haki, zaidi tunamuombea mama aendelee kuchapa kazi na tunamtia moyo kwamba, kazi anaiweza na Watanzania tutaendelea kumuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango pamoja na wasaidizi wao wote wa Wizara husika kwa namna walivyowasilisha hoja za Wizara hizo hapa mbele yetu. Kwa kweli, hotuba zao zilikuwa nzuri, zilizoshiba na mimi naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kuchangia kwamba, sisi Watanzania tunategemea kilimo kama uti wa mgongo. Watanzania wengi ni wakulima na tunategemea kilimo kwa kila kitu, unapozungumzia kilimo kwa Watanzania maeneo mengi, hasa wakulima wadogowadogo wanategemea kilimo kwa kila kitu. Mkulima anategemea kilimo, kwa ajili ya kusomesha, mkulima anategemea kilimo, kwa ajili ya mahitaji yake ya nyumbani na mkulima anategemea kilimo anapoumwa, ataenda hospitali kwa kutumia kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki ndio wakulima wanavuna, lakini jambo la kusikitisha ni wakulima wanalia kwa sababu, bei ya mazao iko chini sana. Katika maeneo yetu leo gunia la kilo mia moja linauzwa shilingi 35,000 mpaka 50,000, kitu ambacho ni kilio kwa mkulima yeyote kwa sababu, gharama tunayotumia katika kilimo ni kubwa ukilinganisha na gharama ya kwenda kufanya mauzo. Kwa hiyo, mkulima anapata hasara badala ya kupata faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilituahidi hapa wakati wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwamba, watakwenda kufungua vituo vyetu vya NFRA. Mimi naomba jambo hili liende kwa haraka sana kwa sababu, mwaka jana wakulima walipata faida kwa kuuza mazao yao kwa kuanzia shilingi elfu themanini na sita mpaka elfu tisini na nane kwa sababu, waliuza kwenye vituo vyetu vya NFRA, lakini kwa sasahivi hali ni mbaya. Mkulima anapoenda kuuza gunia shilingi elfu hamsini, hela haitoshi hata kwenda kulimia kwa jembe moja la kwanza. Kwa hiyo, unaona ni kwa namna gani wakulima wanaendelea kurudishwa nyuma. Kwa hiyo, mimi naomba Serikali itupie jicho suala hili, hasa kwa wakulima wadogowadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilisoma Bajeti ya Wizara ya Fedha, ukurasa ule wa 126, Waziri amesema kwamba, watatoa unafuu kwenye ushuru wa forodha katika zao la ngano. Ni jambo jema kwamba, ushuru unapungua kutoka 35% kwenda kwenye 10%, sio jambo baya, lakini tuangalie wakulima wetu wa ndani hali yao itakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu, mwaka jana wakulima walipata hasara sana, hasa wakulima wa ngano. Wapo wakulima kama Ngano Limited aliteketeza tani elfu tano kwa kukosa soko, zao lile liliharibika. Sasa tukienda kwa style hii kwamba, wanaoleta zao kutoka nje automatically watauza kwa bei ya chini na huyu wa ndani amelima kwa gharama kubwa anapoenda kuuza kwa bei ile ya chini atapata hasara. Kwa hiyo, yeye atataka kuuza kwa bei ya juu ili apate faida, sasa zao lake litanunuliwa na nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba kwa mpango huu wa Wizara mliokujanao waende kuwaangalia pia wakulima wetu wa ndani, ili na wenyewe waweze kujinyanyua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa makusanyo mazuri ya kodi, lakini pia, naweka angalizo, ukusanyaji wa kodi kwa sasa ulivyo hauna uwiano. Leo walipaji wazuri wa kodi ni watumishi, asilimia mia moja watumishi wanalipa kodi, hakuna namna wanaweza kukwepa, lakini wako wafanyabiashara hawalipi kodi na ukiangalia hakuna uwiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mtumishi wa Serikali ameajiriwa, analipwa shilingi 400,000 kwa mwezi analipa kodi vizuri, lakini wapo wafanyabiashara kwa siku ana uwezo wa kuingiza shilingi elfu ishirini, huyo kwa mwezi tunakadiria kwamba ana uwezo wa kupata shilingi laki tano, halipi kodi. Kwa hiyo, nasema tu kwamba, Wizara iangalie namna ambayo itaweza ku-balance kwamba kila Mtanzania anaweza kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke utaratibu mzuri wa kurahisisha ukusanyaji wa kodi. Sasahivi tunategemea ukusanyaji wa kodi kwamba, wale wafanyabiashara ambao wanatakiwa kukusanya kodi wanategemea mashine ya EFD, zile mashine, hata hapa Bungeni tukitaka tufanye utafiti, twende kwenye maduka kumi, maduka saba utakuta wanakwambia mashine zimeharibika, maduka matatu ndio unakuta wanatoa risiti. Tunadai risiti, lakini mashine zimeharibika, mtandao uko chini, hao wote ni wakwepaji wa kodi. Wakati mwingine huwa tunaenda kuwaonea wafanyabiashara, mashine zinaharibika kweli. Je, wanapata service wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, ndani ya Mkoa wangu mimi, unatoka Wilaya ya Kiteto, Wilaya ya Babati, Wilaya ya Hanang mpaka Wilaya ya Karatu unaambiwa mashine ikiharibika service anaenda kufanyia Arusha. Huyu mfanyabiashara afunge duka atoke Kiteto aende mpaka Arusha akafanye service, ametumia shilingi ngapi kwenda? Amekula wapi? Amelala wapi? Kwa hiyo, naomba Wizara irahisishe upatikanaji wa huduma za mashine ya EFD kama kweli, tuko serious katika kukusanya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hilo halitoshi wafanyabiashara hawa wanapotumia zile mashine za EFD wakati mwingine wanapata changamoto, hata upatikanaji wa zile mashine ni wa shida kwa hiyo, mimi naomba Wizara ibuni namna nyingine. Aidha, hata kwa kutumia simu watu walipe kodi, watumie printer kulipa kodi. Sasahivi mambo ya kutoa risiti, ukienda super market kubwa hapa nchini hakuna namna unaweza kudai risiti, risiti wanatoa bila hata kudai, lakini kwenye maduka yetu hawatoi kwa sababu, utaratibu wa kulipa kodi haujawa uzalendo kwa kila Mtanzania. Kwamba, mtu anakupa risiti pale unapomdai, usipomdai hakupi, huo ni utamaduni ambao Watanzania bado hatujajijengea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iangalie namna ya kuharakisha kuona hizi mashine za EFD zinapatikana maeneo yote kwa urahisi. Hata zile kampuni ambazo zina-supply hizi mashine ziwafuate wafanyabishara kwenye maeneo yao, lakini gharama zile za utengenezaji na service ziondolewe, ili zinapoharibika zitengenezwe badala ya mfanyabiashara kuona uchungu kwamba, anaenda kutengeneza mashine kwa shilingi 80,000. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iliangalie hili, ili walau ulipaji kodi uwe rahisi kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nilisoma kwamba, kuna faini imeongezeka kutoka shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni 15. Mimi naomba hii Wizara iliangalie upya kwa sababu, kiuhalisia ni jambo gumu sana kulitekeleza. Mfano, leo unataka kuniambia mtu ambaye hajatoa risiti anatakiwa kulipa shilingi milioni kumi na tano kwa kosa la kutotoa risiti. Mfanyabiashara huyo unakuta duka lake lina thamani ya shilingi milioni 10 tu halafu wewe unamdai shilingi milioni 15 kama faini, hili jambo muliangalie kwa sababu, halina uhalisia. Tuweke faini ambayo kila Mtanzania anapofanya kosa anakuwa na uwezo wa kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishukuru Serikali yangu, naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitutengea shilingi bilioni 5.4, kwa ajili ya kujenga soko la kisasa la Tanzanite. Nasema masikitiko yangu mpaka sasa ni ujenzi wa lile soko unasuasua kwa sababu fedha hazijapelekwa mpaka sasa, tumepewa shilingi bilioni 3.3, kwa ajili ya kujenga lile soko. Kwa hiyo, naomba Serikali itupelekee fedha ili kukamilisha huu ujenzi wa soko kwa sababu wafanyabiashara wetu wa Tanzanite wamekosa imani, wamepata hofu, hawana amani tena kwa sababu wanajua soko lile haliendi kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, point ya mwisho ni suala la umeme. Sisi kule Mkoa wa Manyara umeme umekuwa na tatizo kubwa, hasa kwa Wilaya ya Hanang ambao wanatumia line moja.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua dakika zimeisha kwa hiyo, naiomba sana Serikali itupelekee substation pale Hanang kwa sababu, umeme ukikatika Babati line unakatika mpaka Hanang, vijiji vyote vinakuwa havina umeme mpaka Mbulu. Kwa hiyo, naomba sana substation ikajengwe pale, ili Watanzania na wananchi wote wa Hanang waendelee kupata huduma za umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa muda. (Makofi)