Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na mwenzake katika kuhakikisha kwamba wametuwasilishia Taarifa ya Bajeti na Taarifa ya Mpango ambayo imesheheni mambo mazuri na sasa inakwenda kuwa mkombozi kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikoa ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua ambazo zimeendelea ni Mkoa wa Lindi. Mkoa wa Lindi mvua imenyesha zaidi ya miezi mitano mfululizo. Kwa hiyo, hali ya miundombinu katika Mkoa wetu wa Lindi ni mbaya sana. Madaraja yamekatika, hakuna mawasiliano kati ya kijiji na kijiji, hakuna mawasiliano mazuri kutoka wilaya moja kwenda nyingine ni shida tupu katika barabara zetu za Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Waziri wa Fedha azingatie. Ninajua kwamba Mheshimiwa Rais ana mapenzi makubwa na ametenga fedha nyingi ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kuboresha barabara zetu ili sisi Watanzania tuendelee na maisha mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana fedha hizi zitakapopatikana mara moja zije Lindi kufanya kazi ya kuhakikisha kwamba tunarejesha miundombinu yetu ya barabara ili Wananchi wa Mkoa wa Lindi waendelee kufanya kazi zao kwa amani lakini waendelee kufanya kazi zao za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri Bashungwa kwa sababu alikuja kwa haraka kuja kusaidia ili walau kuwafanya Wana-Lindi waendelee kupata huduma mbalimbali. Sisi Wana-Lindi hatuna bandari, hatuna ndege ambayo tunaona tukishindwa kusafiri kwenye barabara yetu tutasafiri kwa njia nyingine. Kwa hiyo, njia tunayoitegemea ni barabara peke yake. Kwa hiyo, barabara ina umuhimu mkubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi. Kwa hiyo, ujumbe huu Mheshimiwa Waziri wangu wa Fedha aupokee kwa sababu Mheshimiwa Bashungwa hana neno, yeye akipelekewa fedha mambo yanakwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wizara ya Fedha, mmesimama vizuri katika kuhakikisha kwamba mnaendelea kusimamia mapato ya nchi yetu. Tunajua kwamba tunajimwambafai (kujitutumua/kujisifu) humu ndani kuelezea mafanikio, lakini kwa sababu ya fedha ambazo nyie mmezisimamia kuzitafuta. Tunawashukuru sana Mungu awabariki. Hata hivyo, nitumie nafasi hii kuwapongeza ndugu zetu wa TRA kwa kazi kubwa wanayofanya, lakini bado wanatakiwa kuongeza jitihada kubwa ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo yanayoendelea ambayo siyo mazuri sana. Tunajua kwamba nchi yetu tuna wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi lakini niseme tu kwamba wananchi wengi wamewekeza katika biashara ndogondogo. Vilevile, zipo changamoto ambazo zinaendelea katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulipa kodi siyo vita bali kulipa kodi ni uzalendo. Pia kila Mtanzania anayeshiriki katika kufanya shughuli za kiuchumi na shughuli za kiuzalishaji ni muhimu sana na ni wajibu wake kulipa kodi. Niseme tu kwamba, mambo ambayo ndugu zetu TRA wanaendelea kuyafanya wanataka kuturudisha nyuma. Sisi tunasonga mbele wao wanataka turudi nyuma na ndiyo maana nasema kwamba kulipa kodi siyo vita, ni suala la watumishi wa TRA kukaa na kutoa elimu kwa wafanyabiashara ya namna ya kuweza kushiriki kulipa kodi bila kutozwa faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba zipo mashine za EFD ambazo zinatumika lakini wakati mwingine zinaharibika na maeneo ya kwenda kutengeneza kwa haraka hakuna. Kwa hiyo, huduma hiyo inawezekana ikakosekana kwa wiki moja au wiki mbili. Sasa kodi inayokuja ambayo anakadiriwa mfanyabiashara yawezekana anakadiriwa kiwango kikubwa tofauti na mauzo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yanayoendelea siyo mazuri sana kwa sababu wafanyabiashara wengi wamekuwa na malalamiko. Hakuna mahusiano mazuri kati ya watumishi wa TRA na wafanyabiashara. Nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa sababu alifanya kikao na wafanyabiashara pale Dar es Salaam na anajua changamoto mbalimbali ambazo wamemwelekeza na sasa wanasubiri kuelekea kwenye utekelezaji wa kupunguza zile changamoto za wafanyabiashara ili wafanyabiashara wa Tanzania waweze kufanya biashara zao kwa amani na waweze kulipa kodi bila kushurutishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kuna suala la uwekezaji wa Mradi wa LNG. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu, kwa sababu Mradi huu umekuwa wa muda mrefu lakini Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha kwamba anatamani mradi huu utekelezwe. Ninajua kwamba Serikali iko katika hatua mbalimbali ya utekelezaji wa mradi huu lakini Serikali nayo kupitia Wizara ya Nishati mmekaa muda mrefu hamjasema chochote kinachoendelea. Wananchi wa Tanzania na Wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara wanatamani kusikia juu ya utekelezaji huu wa LNG. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapo-windup atueleze ni kwa namna gani tunakwenda katika utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu amewekeza fedha nyingi katika Mkoa wetu wa Lindi na amewekeza fedha nyingi katika eneo langu la Lindi Mjini. Miradi mingi imetekelezwa, leo tuna shule za sekondari za kutosha, vituo vya afya na hospitali za wilaya. Sasa niiombe tu Serikali kwamba kwa sababu mpango huu tumetoka nao katika mwaka huu wa 2023/2024, miradi ambayo haijatekelezwa niiombe Serikali sasa ni wakati wa kutoa fedha ili wananchi wetu wa Lindi waweze kupata huduma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu tunayo changamoto katika miradi ya maji. Miradi mingi ya maji haijakamilika na sasa tunakwenda kwenye robo ya mwisho ya mwaka. Niliomba kupitia Wizara ya Maji mtuletee fedha tukamilishe miradi ya maji ili wananchi wetu waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mji wetu wa Lindi uliathiriwa sana mvua nyingi, ninapoongea hapa leo kuna mgonjwa mmoja ana shida ya kipindupindu pale Lindi Mjini kwa sababu ya kukosa maji safi na salama. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba fedha za miradi ya maji zinakuja Lindi Mjini kwa ajili ya kutekeleza miradi ili wananchi wetu waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niwatakie kila la kheri Wizara ya Fedha katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa changamoto ni nyingi na mahitaji ya Watanzania ni mengi. Nikushukuru sana, ahsante sana.