Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii ya Serikali tunapohitimisha Bajeti Kuu ya mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze pia kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa wasilisho zuri na bajeti nzuri ambayo Wabunge wenzangu waliochangia kabla yangu wameonesha sehemu nyingi ambazo wameridhishwa nazo. Vilevile, niipongeze sana Serikali kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri ya utekelezaji wa Bajeti iliyopita. Tunapokwenda kuhitimisha bajeti hii kwa utekelezaji wake mwezi huu wa sita na kuanza bajeti mpya, tunaamini kasi ile ile itaendelea na tutaendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kulikumbusha Bunge lako Tukufu juu ya mchango ambao niliwahi kuutoa na nitaurudia tena juu ya kufananisha au kutoa mfano wa familia ya Kisukuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baba yangu Mheshimiwa Kiswaga na Mheshimiwa Njalu watanielewa ninaposema, ukiwa na watoto wengi kwenye familia ya Kisukuma ndiyo unaonekana tajiri zaidi. Hii ni kwa sababu watu ni mali. Ukiwa na watoto wengi maana yake ng’ombe wako watajaliwa kwa wakati, utalima eneo kubwa zaidi kwa wakati, utavuna kwa haraka na kwa wakati. Kwa maana yake wingi wa watu ni asset.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii takwimu za mwaka 2022 za sensa zinaonyesha kwamba Taifa hili bado ninaweza nikasema ni Taifa kijana kwa sababu zaidi ya 70% ya Watanzania kwa maana ya wananchi wa nchi hii ni vijana, kwa hiyo Taifa letu bado ni changa kwa hiyo tuna uwezo wa kutumia uwingi huu kama asset kuipeleka mbele nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Itakushangaza wewe na Bunge hili Tukufu kwamba bado tunajadili changamoto ya ajira wakati duniani wanapomaliza kujadili changamoto ya climate change, mabadiliko ya tabia nchi changamoto ya pili wanayoijadili ni global labor shortage. Kuna changamoto ya ukosefu wa watumishi duniani, lakini Tanzania tunaongelea ukosefu wa ajira, tena changamoto hii ni kubwa kiasi cha kwamba tayari mataifa yanakutana kuanza kujadili namna gani tunakwenda kuongeza zaidi matumizi ya Sayansi na Teknolojia ili kupunguza changamoto hii, lakini sisi tuna watu tumekaa huku tunawaelimisha, tena niipongeze sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi katika juhudi zake za kufuta ujinga, ujinga umefutika watu wana elimu na wana ujuzi lakini lazima tuangalie kwenye mipango yetu, tunapangaje kutumia changamoto iliko duniani ya global labor shortage kama fursa kwetu sisi kupunguza changamoto yetu ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mdogo, USA imeanza kuwa na changamoto hii ya global labor shortage kuanzia miaka ya early 2000 na kila mwaka wana-register pungufu ya asilimia tatu kwenye watu wake wanaondoka kazini. As we speak, kwa mfano kwenye sekta ya afya, wana upungufu wa zaidi ya manesi milioni kumi lakini wamesha-register manesi zaidi ya laki sita ambao wanategemewa kuacha kazi ifikapo 2027, hiyo ni kwenye healthcare peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye manufacturing globally kuna upungufu wa watu zaidi ya milioni nane wanaohitajika na hizo ni sekta mbili tu nilizozitolea mfano. Sisi huku tuna workforce ya kutosha, vijana wenye nguvu, wana ari na uwezo wa kufanya kazi, Balozi zetu zinatumia vipi Diplomasia ya Uchumi anayoijenda Dkt. Samia Suluhu Hassan kila siku duniani kuhakikisha tunaondoa changamoto hii? Nadhani kuna jambo la kufanya (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ng'wasi Damas Kamani.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza mzungumzaji aliye….
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sijakukaribisha. Mheshimiwa Getere.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampongeza mzungumzaji anaongea vizuri lakini pia naomba na mimi nitoe tu kwa mchango wake kwamba sasa hivi Dunia ajenda kuu kama siyo kuu lakini ya kati ni ajira Ulaya, ni ajira Afrika. Kwa hiyo, watumishi upungufu wa ajira katika dunia ni mkubwa na upungufu wa ajira Afrika ni mkubwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kamani umemsikia au nimruhusu arejee tena?
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia.
MWENYEKITI: Unapokea Taarifa ya Mheshimiwa Boniphace Getere?
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana siipokei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozunguza taarifa ninazozitoa hapa ni za kitakwimu na ni takwimu ambazo zimethibitishwa na nchi husika kila mwaka zinatoa ripoti za kuonesha ni namna gani zina upungufu mkubwa sana wa watumishi kwenye maeneo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitumia fursa hii hatutapunguza tu changamoto ya ajira kwa vijana kwenye nchi yetu lakini tutaongeza mapato kwa njia ya remittance. Profesa Kitila utanielewa kwamba kuna nchi sasa hivi Afrika hii ya kwetu zinaingiza zaidi ya dola bilioni 20 za mapato kwa mwaka kama remittance, kama fedha zinazotumwa na watu wake walioko nje kuwatumia familia zao na watu wao walioko kwenye nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake tutaongeza fedha za kigeni kwenye nchi zetu, tutapunguza utegemezi na mzigo mkubwa kwa Serikali kuhudumia watu ambao hawa-produce chochote. Hili mimi naomba sana Profesa Kitila anapokuwa kwenye utaratibu wake wa kutengeneza sasa mpango wa mpaka 2050 tuangalie namna gani tunatumia diplomasia ya kiuchumi. Mtaji mkubwa sana ambao ametutengenezea Dkt. Samia Suluhu Hassan kupunguza changamoto hii lakini kuongeza mapato na fedha za kigeni kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili nitauelekeza kwenye bajeti yetu ya Serikali ambayo tunayo hapa mezani. Pamoja na kuipongeza sana Serikali kwa makusanyo yake mazuri ambayo kwenye graph zake inaonekana inapanda kila mwaka, kwa namna ambavyo TRA inakusanya mapato kutoka kwa wafanyabiashara na watu mbalimbali lakini bado hatujafikia viwango ambavyo vinastahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba kwa developing countries kima cha chini au average ambayo mara nyingi tunakusanya kama mapato ya ndani kwa watu wetu ni 15%. Leo hii sisi japokuwa tumetoka mwaka uliopita tuna 12.6% na mwaka huu tunatazamia kukusanya 12.9% kama mapato ya ndani, lakini bado hatujafika hata ile average ambayo inaweza ikatusaidia sasa kutoa huduma Serikali kwa watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitakwimu ili Serikali iweze kuhudumia watu wake vizuri kwa kutumia fedha na mapato yake ya ndani kwa kujitegemea, lazima TRA ianze kukusanya kuanzia 40%. Sasa research zimeshafanyika hasa kwa nchi ambazo zilikuwa na hali mbaya kabisa za single digit za makusanyo yake mpaka wamefika zaidi ya 40% wamechukua hatua kadhaa na mimi niishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kupunguza wingi wa kodi. Tuangalie namna ya kupunguza wingi wa kodi na punguzo hili tutakwenda kuli compensate kwa kuongeza wingi wa walipakodi. Tunapopunguza wingi wa kodi tunaondoka kero kwa wananchi na kuongeza hamu yao ya kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine World Bank imeonesha kwamba ni muhimu Serikali ikajenga uaminifu kwa watu wake, sisi kwwenye nchi zetu zinazoendelea watu wengi wanafanya kazi za nguvu sana ili kupata vipato vyao. Watu hawana shida na kulipa kodi, shida ni kutaka kujua kwamba matumizi ya fedha wanazolipa kuingia Serikalini zinakwenda sehemu sahihi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitatoa tu reference ndogo kwa ripoti ya CAG ya mwaka jana ambayo amewasilisha Machi mwaka jana, ripoti inasema; “vyanzo vya mapato ambavyo havikukusanywa bilioni 61, ushuru wa huduma usiokusanywa bilioni 4.1 kutowasilishwa kwa makusanyo na mawakala waliokusanya bilioni 5.6 ushuru wa mazao usiokusanywa bilioni 5.2 lakini ukusanyaji usioridhisha katika vyanzo vikubwa bilioni 6.8.” Hizi ni chache tu ambazo nimezinukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini? Tukipunguza upotevu au kutokukusanywa huku kwa fedha kunaongeza imani ya watu kulipa na hivyo kutaongeza makusanyo, suluhu pekee ni kuhakikisha tunaondokana na cash economy. Lazima tuondoe fedha za makaratasi kwenye mzunguko wetu, na ni lazima pia Serikali itoe elimu kwa watu kwamba kuwa na mashine ya kukusanyia haimaanishi kwamba ndio unakatwa kodi, kama wewe kisheria hustahili kukatwa kodi utaonesha zero, lakini kule Serikali itasoma kwamba kuna transaction fulani zimefanyika. Tujenge utamaduni wa kuondoa fedha za makaratasi kwenye mizunguko yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali imeweza na niipongeze kugawa pikipiki kwa Maafisa Ugani wote nchi nzima, tunatenga bajeti za kugawa fedha za magari kwa Halmashauri zetu na Mikoa yote nchi nzima, ninaiomba na kuishauri Serikali iangalie namna kila anayefungua biashara wapewe vile vifaa vya kukusanyia malipo yao kwa kadi, watoe vile vifaa bure, hiyo itakuwa ni investment ya kutusaidia sisi kutoka kwenye 12% tulizonazo leo kwenda kwenye 40% ikiwezekana 50%. Fedha ambazo zinalipwa leo hii na Serikali haijui zimelipwa ni nyingi kuliko kawaida zaidi ya 80% ya transaction kwenye nchi hii zinafanyika na Serikali haijui zimefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya transaction zote ziwe zinapita kwenye mashine, mabenki yapunguze viwango vya makato ili kila mtu anayelipa alipe kutumia kadi. Kwenye nchi za wenzetu kadi ni kitu cha kawaida na mtu ukitoa fedha kulipia kitu unaonekana wa ajabu, kwamba huyu mtu anatoaje fedha? Kadi ni kitu cha kawaida na Serikali haipati shida kukusanya kodi zake kwa sababu inajua transaction zote zinazofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iangalie hii kama investment, itafute hivyo vifaa kugawa kwa kila mtu benki zetu wawe wadau wakubwa wa maendeleo watoe kadi kwa kila mtu ili hata anayelipia hata kama ni 1,000 lipa kwa kadi kusiwepo na gharama za makato, Serikali itajikuta inakusanya kodi kadri inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia takwimu zinaonesha hata fedha zinazokuwa-printed na Serikali….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru dakika moja.
MWENYEKITI: Naomba hitimisha.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazokuwa printed na Serikali na ndiyo sababu pia na Serikali huwa inabadilisha fedha kila baada ya muda, kwa sababu inapo-print fedha baada ya muda fedha hazionekani kwenye mfumo, watu wanatunza fedha ndani lakini tukiondoa cash economy hakuna fedha itakayobaki ndani, Serikali itaona fedha zake zote 100% zilipo, tutakusanya mapato na nchi hii itaweza kuhudumia huduma zote bila kutegemea vyanzo vingine isipokuwa vyanzo vya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)